NHC wafanya kweli, wavamia hospitali

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
214,635
2,000
KAMPENI ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ya kukusanya madeni yake yanayofikia Sh bilioni tisa, imeanza kwa kasi mkoani Dar es Salaam na kuacha wapangaji wake wakiwa hoi.

Baada ya kujikuta na deni la Sh bilioni tisa linalotokana na malimbikizo, NHC ilitangaza kuwa inatarajia kuwaondoa kwenye nyumba zake wapangaji wasiolipa madeni ya kodi.

Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita hadi sasa, shirika hilo linawadai wapangaji wake Sh bilioni tisa, Sh bilioni saba kati ya hizo ni madeni kwa wapangaji wa Jiji la Dar es Salaam peke yake.

Kuonesha kuwa imedhamiria kuhakikisha inapata fedha zake hizo, jana maofisa wa NHC walivamia hospitali maarufu nchini ya Dk. K. K. Khan ya Dar es Salaam na kuchukua vifaa vyote vilivyokuwamo ndani ya hospitali hiyo kwa lengo la kuviuza ili kufidia limbikizo la deni la pango la Sh milioni 100.

Hatua hiyo iliyosababisha shughuli za hospitali hiyo kusimama na wafanyakazi wake kuhaha kwa mshangao na hasira, ilitekelezwa jana asubuhi kwa ushirikiano wa maofisa wa NHC na wa Kampuni ya Udalali ya Mzizima, ambao kwa pamoja walitoa vifaa vyote nje ya jengo la hospitali hiyo iliyoko katikati ya Jiji.

Licha ya kutopata upinzani wowote kutoka kwa uongozi pamoja na wafanyakazi wake, maofisa hao wa NHC na madalali wa Mzizima, walilalamikiwa na watu waliokusanyika kushuhudia tukio hilo kwa madai ya kushindwa kutafuta njia mbadala ya kutatua tatizo hilo, hasa kutokana na unyeti wa eneo lenyewe.

Akizungumza hospitalini hapo, Meneja Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga alisema hatua hiyo ni halali na inatekelezwa kwa wadeni wote sugu na wenye madeni yasiyolipika kirahisi akiwamo Dk. K.K. Khan.

Mwanasenga alisema hakuna sababu nyingine iliyosababisha kufunga shughuli za hospitali hiyo, bali ni kuokoa fedha nyingi ambazo zingepotea kwa kuruhusu utoaji wa huduma za afya uendelee katika hospitali hiyo iliyoonesha dalili zote za kushindwa kumudu gharama za pango, ambazo ni Sh milioni tano kwa mwezi.

Alisema, waliupa uongozi wa hospitali hiyo muda wa kutosha kulipa deni hilo, lakini walishindwa na kuonesha dalili zote za kutofanya hivyo katika kipindi kifupi kijacho, jambo ambalo lingezidi kuitia NHC hasara.

Hivyo, alisema waliona kuwa njia pekee itakayoweza kusimamisha matumizi ya majengo yao kwa watu wenye madeni makubwa na wasioonekana kuwa na uwezo wa kuyalipa ni kuwaondoa katika majengo hayo na kukamata mali zao, ambazo zinauzwa na kufidia angalau sehemu ya deni husika.

“Tunajua fedha zitakazopatikana baada ya kuuza vifaa hivi ni kidogo na hazitaweza kufikia milioni mia, lakini hatuna jinsi, inabidi tuviuze ili angalau tukusanye kiasi cha pango linalodaiwa, vinginevyo shirika litapata hasara kubwa… dalali wetu Mzizima ndiye atakayesimamia uuzaji huo,” alisema Mwanasenga.

Aidha, alisema hatua hiyo haipaswi kuwashtua wala kuwashangaza wahusika wa hospitali hiyo kwa kuwa walipewa taarifa ya kuwepo kwa kazi hiyo mapema na ndio maana pamekuwa na utulivu wa hali ya juu wakati wa utekelezaji wake, licha ya manung’uniko na maneno ya chini chini yaliyokuwa yakitolewa na watu waliokuwa wakishuhudia, wakiwamo wafanyakazi wa hospitali hiyo na baadhi ya majirani.

Meneja huyo wa Madeni alisema pia kuwa kazi hiyo ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba za NHC na kuuza mali zao ni endelevu na litawakumba wote wanaoangukia katika kundi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Ruth Alice Lembuya alisema kushindwa kwao kulipa deni hilo kumesababishwa na kushuka kwa mapato yao ambako kumechangiwa kwa asilimia kubwa na kuanzishwa kwa huduma ya bima ya afya, pamoja na malipo ya huduma ya matibabu kwa ankara, kutoka kwa wagonjwa wanaodhaminiwa na mashirika wanayoyatumikia au ofisi wanapofanyia kazi.

NHC wafanya kweli, wavamia hospitali

Imeandikwa na Namsembaeli Mduma; Tarehe: 16th December 2010 @ 07:00

Lembuya aliyekuwa ameketi kwenye korido iliyopo mbele ya hospitali hiyo huku akishuhudia vifaa vyake vikitolewa nje, alisema hawajaonewa kwa kufanyiwa kitendo hicho na shirika hilo isipokuwa wanataka muda wa miezi mitatu au sita wa kuendelea na utoaji wa huduma ili wakusanye angalau sehemu ya deni hilo na kulilipa wakati wakisubiri taratibu za ubia walizoanza na mashirika kadhaa ambayo hakuyataja kukamilika.

Kwa maelezo yake, uongozi wa hospitali utakusanya mapato kutoka kwa baadhi ya wateja wa kudumu wanaodaiwa na hospitali hiyo ili kuwalipa wafanyakazi wanaodai mshahara wa Novemba unaofikia kati ya Sh milioni saba na nane, ambao wamekuwa wakimfungia ofisini kwa saa nyingi ili kushinikiza malipo hayo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom