Ngwe ya pili ya awamu ya nne Changamoto nne za Rais Kikwete katika elimu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
NOVEMBA 5 mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Dk Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31.
Kutangazwa huko kuliashiria kuanza kwa ngwe ya pili ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne ambayo pamoja na mambo mengine imekuwa ikiweka msukumo mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Kwa mfano, ongezeko la bajeti katika sekta ya elimu, ujenzi wa shule za sekondari za kata na kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni baadhi tu ya mambo ambayo wadau wa elimu wanakiri kuwa serikali ya Kikwete imekusudia kubadili hali ya mambo katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Hata hivyo wadau hao kama sehemu muhimu katika mchakato wa maendeleo ya elimu, hawajasita pia kutoa dosari zilizopo katika sekta ya elimu kama vile uhaba wa walimu na vifaa kama vitabu.
Jambo linalotia moyo ni kwamba Rais Kikwete amekiri kuwa sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazopaswa kufanyiwa kazi na serikali yake.

Mara kwa mara hususan wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita, Kikwete alinukuliwa akisema kuwa kwa sasa changamoto tete na kubwa katika elimu ni nne. Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu, ukosefu wa vifaa, maabara na nyumba za walimu.
Mikakati ya serikali
Katika hotuba aliyoitoa siku ya ufunguzi wa Bunge Novemba 18 mwaka huu, Rais Kikwete aliweka bayana dhamira ya kuzitafutia mwarobaini changamoto hizi na nyinginezo.
Alisema: “ Tutaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa bajeti ya elimu ili tufundishe na kuajiri walimu wengi zaidi, tupate vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia….tutajenga maabara za sayansi katika sekondari zetu zote.”

“ Katika kipindi hiki pia tutachukua hatua thabiti za kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi ya walimu na watumishi wa sekta ya elimu. Kwa ajili hiyo, tunakamilisha na kuanza kutekeleza mpango kabambe wa kujenga nyumba za walimu kote nchini. Tutahikikisha kuwa mpango huo unatengewa pesa za kutosha.”
Hata kabla ya hotuba hii, serikali ilikwishaanza kutekeleza baadhi ya mikakati ikiwemo uanzishwaji wa vyuo vikuu maalum vya walimu kwa minajili ya kupunguza uhaba wa walimu shuleni,

Wadau wanasemaje?
Pamoja na mikakati ya kumaliza changamoto hizi nne, wadau wa elimu wana msururu mwingine wa matatizo ambayo nayo yanapaswa kufanyiwa kazi
Kwa mfano, wanalia na matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa katika elimu wakidai kiasi kikubwa cha fedha kinatumika katika malipo hewa au kwenye maeneo yasiyo na umuhimu katika maendeleo ya sekta hiyo.
“Usimamizi wa matumizi ya fedha za umma bado ni changamoto. Wizara bado ina matatizo ya kulipa wafanyakazi hewa. …… Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali imebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2008/2009 sekta ya elimu ilipoteza Sh 47 bilioni kwa kulipa wafanyakazi hewa, “ anasema Elizabeth Missokia, Mkurugenzi wa asasi ya HakiElimu.

Mwaka 2002 serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM), ilianzisha utaratibu wa kutoa ruzuku kwa wanafunzi. Wadau wa elimu wanasema ukitoa udogo wa kiwango cha fedha kilichotengwa bado kiasi hicho kidogo aidha hakifiki kwa walengwa au hufika kwa kuchelewa
“Ruzuku kwa wanafunzi ni kipengele muhimu sana kwenye mpango wa MMEM, na imekuwa ikitengewa rasilimali nyingi…… Kiwango halisi cha ruzuku hii kinachopelekwa shuleni ni kidogo zaidi ya kile kilichoidhinishwa kwenye bajeti,’’inasema sehemu ya taarifa iitwayo “Ruzuku ya Wanafunzi kwa ajili ya Elimu iliyotolewa na asasi ya kiraia ya Twaweza.

Aidha, ripoti ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za ruzuku ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2009 inaonyesha kuwa ni wastani wa Sh 4500 tu zilizopokelewa shuleni badala ya Sh10,000.
Matumizi mabaya ya fedha za elimu na udogo wa ruzuku kwa wanafunzi ni changamoto nyingine zinazopaswa kufanyiwa kazi hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya nne imeahidi kuongeza bajeti katika sekta ya elimu.
Kwa upande mwingine, ongezeko la bajeti halitokuwa na maana yoyote ikiwa fedha zinazotengwa zitatumika ndivyo sivyo.

Kwa kuwa rungu la maamuzi analo Rais Kikwete na ndiye aliyeahidi kuzishughulikia kero za elimu wakati ule wa kampeni na katika hotuba bungeni, matarajio ya wadau wa elimu ni kuona muhula wa pili wa serikali yake ikizitafutia dawa mujarabu kero hizi na nyinginezo.
Kukiwepo na nia na kama serikali mpya itajipanga vema kila kitu kinawezekana. Rais Kikwete ana miaka mingine mitano ya kukamilisha kasi aliyoanza nayo ya kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.
Nini kitajiri katika kipindi hicho? Si jambo rahisi kutabiri ila baadhi ya watu wanaamini kuwa hotuba aliyoitoa bungeni, imeonyesha mwanga wa mabadiliko hayo. Tusubiri.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom