Nguzo Kuu Tano za Maisha: Soma utakapoishia panakutosha

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,883
NGUZO KUU TANO ZA MAISHA

Na, Robert Heriel

Maandishi ya Robert Heriel kwa Lugha ya Kiswahili.


Maisha ni kuishi, na kuishi ndio maisha yenyewe. Hapana shaka ndoto ya kila mwanadamu ni kuishi maisha mazuri na ndio sababu watu wanahangaika kuhakikisha maisha yao yanakuwa mazuri.

watu wengi (mimi nikiwemo) wamekuwa wakijiuliza maisha ni nini? Jibu fupi la swali hilo ni kuwa Maisha ni kuishi na kuishi ndio maisha. Lengo la maisha ni nini? Lengo la maisha ni kuishi. Sasa kama lengo la maisha ni kuishi kwa nini watu wanakufa? kwa nini hawaishi milele? Jibu ni kuwa; watu wanakufa ili wengine waishi, hasa wale wanaotegemea uhai wetu kama nishati ya wao kuendelea kuishi. Wengine kina nani? Hilo ni swali jingine ambalo ni gumu.

Umuhimu wa maisha unaletwa na uwepo wa kifo. Bila kifo pengine maisha yasingekuwa na thamani. Waliokufa hawahitaji sana uhai sana kama wanaoishi. Sisi tunaooishi ndio tunauhitaji uhai zaidi na hii hufanya kifo kuwa kichocheo cha kuishi. Kama mtu aliyelala usingizini asivyohitaji kuamka walakini aliyemacho huhitaji kulala kutokana na nguvu ya usingizi. Ndivyo katika kifo na uzima.

Uzima hauhitaji mtu ila woo ndio unahitajiwa na watu.

Maisha kama yalivyo mambo mengine yana mihimili yake. Yana nguzo zake ambazo hizo ndizo humfanya mtu aishi tena kwa furaha.

Kama nguzo hizi zikiwa imara basi maisha ya mtu huwa ya furaha na amani. Lakini kama moja wapo ya nguzo hizi tano zitaguswa basi ndipo maisha huanza kuwa mabaya.

Uwepo wa Kifo ni matokeo ya nguzo moja kumegwa, kuvunjwa, kupuuzwa, na kuacha. Bila shaka utajionea mwenyewe.

NGUZO KUU TANO ZA MAISHA. (MIHIMILI MKUU MITANO YA MAISHA YA MWANADAMU)

1. MUNGU
2. KAZI
3. MAMA NA BABA
4. MKE AU MUME
5. MAJIRANI

1. MUNGU
Hii ndio nguzo ya kwanza ya maisha. Huyu ndiye aliyejenga mihimili mingine minne iliyobakia. Mungu ndio muumbaji wa maisha na ulimwengu. Mungu ndio uhai, Mungu ndio maisha. Pasipo na Mungu hakuna maisha.

Muhimili huu ni walazima kwa maana pasipo na nguzo hii hakuna maisha. Hasa maisha mema kwa maana kuna maisha mabaya. Moja ya makosa makubwa mwanadamu anayoyafanya ni kuiangusha nguzo hii. Unapoiangusha nguzo hii ambayo ndio imeshikilia jengo zima la maisha. Ni lazima maisha yakae upande au kuanguka kabisa.

Ukishamjua Mungu lazima ujue lengo la Maisha. Kwa maana maisha bila Mungu hayana lengo, kamwe huwezi ona umuhimu wake.

Nguzo hii ilivunjwa na ndio maana watu wanakufa. Kwa maana nguzo hii ndio hutoa uhai, nguvu, uweza, kibali, mamlaka na utawala. Mwanadamu kabla hajaasi alipewa mambo yote. ambayo ni uhai, nguvu, uweza, kibali, mamlaka na utawala. Lakini Mambo hayo sita aliyauza kwa kutaka akili, utashi, maarifa, ujuzi na ufahamu. Hivyo Mungu akamnyang'anya mwanadamu uhai, nguvu, uweza, kibali, na mamlaka lakini Mungu akampa vile alivyotaka ambavyo ni akili, utashi, maarifa, ujuzi na ufahamu kisha akamuongezea na utawala wa dunia.

Ndio maana mwanadamua anatawala dunia lakini hana Mamlaka nayo.
Katika dini tunaona Yesu Kristo akisema; Nimepewa Mamlaka Mbinguni na Duniani.
Kumaanisha Yesu ndiye anamamlaka ya dunia hii na Mbinguni kwa mujibu wa Biblia, lakini duniani wapo watawala ambao huongoza watu.

Binadamu hana mamlaka ndio maana huomba KIBALI iwe kutoka kwa Mungu, au kuomba kibali kwa watu kuwaongoza. Mwenye mamlaka haombi Kibali, yeye hufanya atakavyo na huwezi kumfanya chochote. Si ajabu ndio maana Mungu akiamua kuchukua Roho yake sasa hivi hana muda wa kukuomba ruhusa wewe au ndugu zako, bali hufanya vile apendavyo na hakuna wa kuzuia. Lakini wanadamu waliojaribu kufanya vile watakavyo waliishia kuitwa madikteta na kuuawa na wanadamu wenzao.

Nguzo hii ndio hutoa kibali cha watu kuwepo duniani au kutokuwepo. Nguzo hii ndio hutoa kibali cha mtu kufanikiwa katika jambo fulani. Kuivunja nguzo hii ni kujikosesha kibali. Ingawaje wapo wanaofoji vibali bandia kwa kutumia mashetani, majini, au viumbe wengine wa nguvu za giza. Vibali hivyo ni bandia(fake) ingawaje wakati mwingine huweza kukusaidia kwa muda tuu lakini hautasaidika daima. Vibali bandia humfanya mtu asiishi kwa amani. Maisha huwa mabaya pale unapotumia vibali haramu.

Kabla mwanadamu hujaanza kutafuta maisha ni lazima umtafute aliyeumba hayo maisha. Hiyo ndio iwe nguzo yako ya kwanza. Hakuna aliyeitegemea nguzo hiyo akaanguka.

Nguzo hii inamaelezo mengi lakini tuishie hapa.

2. KAZI
Hii ni nguzo ya Pili katika maisha. Baada ya Mungu kinachofuata ni kazi. Tunaposema kazi tunazungumzia kumtumikia Mungu, tunawezaita Ibada. Kila unayemuona duniani ni mtumishi wa Mungu. Watu wanamtumikia Mungu kulingana na idara. Kazi ndio mtandao unaomuunganisha Mtu na Mungu wake moja kwa moja kuliko jambo lolote. Unapofanya kazi basi fahamu kuwa umejiunganisha na Mungu moja kwa moja. Usipofanya kazi basi jua Mungu yupo mbali na eneo ulilopo.

Zipo kazi za aina nyingi. Kuna kazi za kufanya kwa mikono, miguu, kazi za sauti, kazi za mikono na miguu kwa pamoja,
Mtu yeyote unayemuona anafanya kazi jua anamtumikia Mungu. Mimi namuita Mtumishi wa Mungu.
Mwalimu humtumikia Mungu kwa Kufundisha watu(wanafunzi) Elimu ya duniani.
Tabibu humtumikia Mungu kutibu wagonjwa kwa kutumia malighafi za duniani
Mwanasheria na Hakimu humtumikia Mungu kusuluhisha migogoro, na kuadhibu watu wanaokosea.
Polisi wanamtumikia Mungu kwa kuwalinda raia na mali zao.
Dereva wanamtumikia Mungu kuwasafirisha watu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na mali zao.
Fundi nguo, fundi ujenzi, wapiga debe, Mawaziri, wabunge wote wanamtumikia Mungu kuhudumia watu.

Hakuna kazi bora kuliko kazi nyingine. Kazi zote ni bora na zinaumuhimu. Mtu yeyote anayedharau kazi ya Mtu mwingine yupo hatarini kuangamia.

Mtu anabarikiwa kupitia kazi ile aifanyayo kwa Moyo. Kazi yoyote inayofanywa kwa moyo kwa lengo la kuhudumia watu, kutatua changamoto za watu humfanya mtu kuwa tajiri

Katika kazi ndio kuna wizi na dhuluma. Usimuibie mtu au kumdhulumu mtu kwa kazi aliyokufanyia na mlivyokubaliana. Nawe mtu akija ili umfanyie kazi basi mfanyie kwa ubora kabisa bila kumdhulumu. Usitangulize pesa mbele bali tanguliza huduma bora mbele. Watu wote waliofanya kazi bora hufanikiwa zaidi.

Kama mtu hajaridhika na kazi yako, irudie na kama hataki basi mwambie akulipe nusu ya kazi, na kama amekulipa basi mrudishie nusu ya pesa yake. Mtu asilaumu kazi ya mikono yako.

Kazi ndio utu,
Usichague kazi
Heshimu kazi za watu wengine.

Watu fulani walinipigia simu na kuanza kunikaripia kuwa kwa nini Nilimkemea Askofu Gwajima, je sikujua kuwa ni mtumishi wa Mungu? Mimi ni nani mpaka nimfokee Mtumishi wa Mungu? waliniuliza kwa jazba,

Nilkawauliza swali moja ambalo liliwapa kigugumizi: Nini maana ya Mtumishi wa Mungu? Wakanijibu; ni mtu anayeshughulika na masuala ya Mungu kama vile uchungaji, upadri, uaskofu n.k

Nikawauliza kuwa wanamjua Mfalme Nebukadreza wa Babeli, wakanijibu ndio. Nikawaambia, Mungu alivyomuita Mtumishi wake, je Nebukadreza alikuwa mchungaji, askofu, kuhani au alikuwa anafanya kazi za dini? Wakajibu hapa, bali alikuwa mfalme.
Basi nikawapa somo kama nililotoa hapo juu, kuwa mtu yeyote ni mtumishi wa Mungu ikiwa tuu anahudumia watu wa Mungu kwa njia halali.

Mtu anapoenda kinyume na maadili ya kazi yake lazima akemewe, akaripiwe bila kujali cheo chake.

Ukivunja nguzo hii pia imekula kwako. Kwani unaambiwa asiyefanya kazi kula na asile.

3. WAZAZI (BABA NA MAMA)
Hii ni nguzo ya tatu muhimu ambayo nayo ni muhimili katika maisha. Wazazi ndio wamekuzaa, unaowajibu wa kuwaheshimu, kuwasikiliza, na kufuata mafundisho yao.Mwalimu wa kwanza wa mwanadamu baada ya Mungu ni Mzazi. Mzazi ndiye ameshikilia baraka ya kuishi maisha marefu duniani.

Wazazi waheshimiwe katika mambo mema tuu. Lakini wapo wazazi waliopotoka, wazazi hawa usiwaheshimu(usiwasikilize yale maovu watakayokuagiza) Bali waelekeze kwa upole. Na kama wanashingo ngumu achana nao. Usipende kupita mbele ya uso wao wasije wakakutegemea mitego ukakwazika ukatenda uovu juu yao.

Siku hizi kutokana na maovu kuongezeka nguzo ya wazazi imetetereka, kwani wazazi wengi tunazaa kwa njia haramu na kutelekeza watoto kwa Bibi au ndugu. Hii husababisha nguzo hii kuleta madhara hasa katika mafanikio ya mtoto Kimaadili, kijamii na kiuchumi.

Wazazi hutokana na ndoa halali, kinyume cha hapo husababisha hatari kwa maisha ya watoto. Ndoa ni msingi katika nyumba(maisha ya mwanadamu). Mtoto anapotokea kwenye ndoa isiyohalali, ndoa ya magumashi husababisha maisha ya mtoto kuwa magumu. Watoto wengi(mimi nikiwemo) Tumezaliwa kiholela. Hatulaani lakini haituzuii kusema ukweli tuliouona kuwa watoto wanaozaliwa kiholela(ambao wanazidi kuongezeka kutokana na zinaa kuwa kubwa) maisha yao huyumba kutokana na nguzo ya wazazi kutokuwa imara.

Ni wajibu wa kizazi hiki kujiimarisha kwa kukataa na kuipinga zinaa. Wanawake wasifanye zinaa mpaka ndoa halikadhalika na wanaume. Isipokuwa kwa Makahaba(haipo kisheris katika dini)

Sisi kama wazazi lazima tutambue kuwa sisi ni nguzo muhimu kwa watoto na kizazi kijacho. Tunapogombana na waume/wake zetu tusikimbilie kutoa talaka kwa maana talaka huchukiwa na Mungu.

4. MKE AU MUME
Nguzo ya nne ni Mke au Mume. Hii ni nguzo kubwa na muhimu katika maisha. Nguzo hii ikiyumba basi maisha ya mtu yanayumba. Nguzo hii ikiwa imara, basi maisha ya mtu huwa imara.

Nguzo hii mtu huichagua mwenyewe, sio kama Nguzo ya Mungu, au nguzo ya wazazi ambazo huna uamauzi nazo. Upende usipende umezikuta na ndizo nguzo zako.

Mtu huchagua mke/mume wa kuishi naye. Unapochagua Mke/Mume lazima uelewe kuwa unaenda kuchagua nguzo moja wapo katika ya nguzo tano za maisha,

Nguzo huchagizwa na upendo wa ndani kabisa.

Unapochagua mke/mume jua unaenda kuchagua
> Mtu unayeenda kuanzisha kizazi chenu
> Mtakaoishi pamoja kwa nyakati zote
> Utakaye share mwili pamoja
> Atakaye kufurahisha kwa asilimia 60, 10% utafurahishwa na Mungu, 10% wazazi, 10% marafiki, na 10% kazi uifanyayo. Kumbuka mke/mume ni mwili mmoja. Hivyo 60% mtu hujifurahisha(hufurahishwa na mwenzi wake)

Kama unataka kuzaa watoto wa aina fulani huenda ni warefu au wafupi, weupe au weusi, wanene au wembamba, wenye akili au wajinga, n.k yaani unataka kuanzisha kizazi cha aina fulani basi usidhani anayeamua ni Mungu. Mungu haamui kizazi utakachokileta duniani.

Kama unafurahi kuona watoto weupe na unatamani kuzaa watoto wa aina hiyo basi lazima utafute mume/mke mweupe.
Kama unataka watoto warefu tafuta mwenza mrefu
Kama wataka watoto wafupi, tafuta mwenza mfupi hivyo hivyo.

Usijeukazaa watoto ambao hutawafurahia machoni mwako. Kwa maana hiyo itaathiri maisha ya watoto hao na maisha yako. Jambo lolote usilolifurahia hugeuka kuwa laana na linaweza kukuumiza.

Kikawaida binadamu ni wanafiki, lakini ukweli ni kuwa wapo wazazi wasiowafurahia watoto wao iwe kimaumbile na kiakili. Lakini wengi husahau kuwa makosa walifanya wao, Huwezi oa/olewa na mwenza mwenye kichogo alafu ukasema hupendi watoto wenye kisogo, labda uwe umelogwa

Ndio maana Biblia inasema; Naye atatafuta wa kufanana naye, nao watakuwa mwili mmoja.

Sasa wewe hufanani na mtu mfupi kama mimi Taikon, nimekudanganya na maneno yangu laini ukajaa kingi. Nikakuoa, kumbe mwenzangu hutaki watoto wafupi, sasa vinapozaliwa vi-omolo kama mimi Baba yao unachukia, maisha yako yanaingia dosari kwa ufupi wangu kila ukiwaona watoto wangu walivyo pimbi. Wewe utakuwa mwehu.

Nguzo hii inachangamoto nyingi mno lakini kama utaweza kuzipangua kwa asilimia 70 basi lazima maisha uyaone bwerereee!

Kwenye maisha usijidanganye. Life is real
Usitamani Mke wa jirani yako. Iwe mwiko kutembea na wake za watu. Hiyo ni laana. Ndio maana kuna makahaba wa kununua.

5. MAJIRANI
Nguzo ya mwisho ni majirani au watu wanaokuzunguka.
Ishi na watu vizuri, usitamani mali ya jirani yako, usitamani mke wake, mfanyakazi wake, kazi yake, au jambo lolote. Yaani usiwe na wivu na mambo ya watu wengine. Ishi maisha yako.

Kanuni inasema; Mpende jirani yako kama nafasi yako.

Jamani nimeandika mno. Nafahamu wengi hawapendi makala ndefu. Ila nami siwezi kupunguza. Kila mmoja atakula kwa urefu wa kamba yake.

Soma utakapoishia inatosha.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam
 
Back
Top Bottom