NGELEJA : "Tumefanya kazi kubwa sana tena sisi tulikuwa wawili tu"

fangfangjt

JF-Expert Member
Apr 25, 2008
571
139
Mawaziri waliong'olewa wamsusa JK

MAWAZIRI wapya na manaibu wao, jana waliapishwa na Rais Jakaya Kikwete, huku wale waliong'olewa katika baraza hilo wakisusia sherehe hizo, isipokuwa William Ngeleje, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Ngeleja aliyeonekana mwenye furaha, alisema hana kinyongo na mtu baada ya kuondolewa katika uwaziri, akitamba kuwa miaka mitano aliyokaa si mchezo na hivyo atakuwa mwepesi kutoa ushauri kwa waziri mpya aliyeingia.
"Tumefanya kazi kubwa sana tena sisi tulikuwa wawili tu lakini sasa wamekuwa watatu, hivyo mimi nafurahi kuwa hizi ni mbio za kupokezana vijiti, ngoja na wenzetu wasogeze gurudumu japo," alisema.

Waliong'oka na kushindwa kufika Ikulu jana ni Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Mustafa Mkulo (Fedha), Omar Nundu na naibu wake Athuman Mfutakamba (Uchukuzi), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Dk. Haji Mponda na Dk. Lucy Nkya (Afya).

Hata hivyo, tofauti na sherehe hizo zinavyokuwa miaka yote, jana hali ilikuwa tofauti kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mawaziri hao kwani shamrashamra za kuwapongeza zilitiwa nyongo baada ya Ikulu kuwazuia wasiingie na mashada wala maua.

Mawaziri waliokula kiapo ni 15 na manaibu 16, ambao ni Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk. Fenella Mukangara (Habari na Utamaduni), Dk. William Mgimwa (Fedha), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi), Dk. Hussein Mwinyi (Afya), Prof. Jumanne Maghembe (Maji) na Hawa Ghasia (Tamisemi).

Wamo pia Mathias Chikawe (Katiba na Sheria), George Mkuchika (Utawala Bora), Celina Kombani (Utumishi), Wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Christopher Chiza (Kilimo), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili), Dk. Abdalah Kigoda (Viwanda) na Prof. Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini.

Hata hivyo, waziri asiyekuwa na kazi maalum katika Ofisi ya Rais, Prof. Mark Mwandosya, hakuapishwa na wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu afya yake kwani amekuwa mgonjwa muda mrefu.

Kwa upande wa manaibu waziri walioapishwa ni Adam Malima (Kilimo), Lazaro Nyalandu (Maliasili), Gregory Teu (Viwanda), Pereira Silima (Mambo ya Ndani), Charles Kitwanga (Makamu wa Rais), Gerson Lwenge (Ujenzi), Seif Seleman Rashid (Afya) na Binirithi Mahenge (Maji).

Wengine ni George Simbachawene Na Stepehen Maslle (Nishati na Madini), January Makamba (Sayansi na Teknolojia), Charles Tizeba (Uchukuzi), Amos Makalla (Habari na Utamaduni), Anjela Kairuki (Katiba), Janeth Mbene na Saada Salum Mkuya (Fedha).

Mgimwa alia na mfumuko wa bei
Waziri mpya wa Fedha, Mgimwa, ameahidi kuanza kazi mara moja kwa kushughulikia mfumko wa bei za bidhaa ili kuleta ahueni kwa wananchi wanaokabiliwa na ugumu wa maisha.
"Kwa sasa hali ni mbaya, tunataka watu waone thamni ya fedha yao. Hivyo utofauti wetu utakuwa katika kujituma zaidi, kuwajibika na kushirikiana," alisema.
Alifafanua kuwa kazi kubwa aliyonayo ni kuiboresha wizara ya fedha na kuimarisha utendaji ili uchumi ukue kulingana na hali halisi ya maisha ya wananchi.

Mwakyembe: Tutatanguliza uwazi
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, alisema wizara yake ina changamoto nyingi, hivyo wanahitaji kupewa muda wajipange.
"Sisi sera yetu kubwa itakuwa uwazi mbele. Hapa mjue kila kitu ni kipaumbele katika wizara hii, nchi ina shirika halina ndege inayoruka, reli iko hoi wakati ni mkombozi wa wengi na bandari vile vile tunapaswa kuzipanua," alisema.
Dk. Mwakyembe alisema zaidi ya asilimia 40 ya malori ya mizigo yanaharibu barabara, hivyo lazima uangaliwe uwezekano wa kuiboresha reli haraka ili mizigo yote ipitie huko.

Muhongo ataka mg 500 za haraka
Yeye Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo, alisema ili kukabiliana na hali mbaya ya umeme iliyoko nchini kwa sasa, watahakikishwa kwanza zinapatikana megawati 500 za haraka.
Alisema kuwa kama mtaalam wa jiologia mwenye uzoefu, atahakikisha wanakuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu ili kutumia vyanzo vilivyopo kuzalisha megewati 3000 kwa ajili ya matumizi na kuuza nje.

"Tulipaswa kuwa na megewati 1500 mpaka sasa. Hivyo kazi yetu kubwa itakuwa ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya watu wanaopata umeme inafikia asilimia 75, wenzetu Mauritius wameweza kwa asilimia 95 na Afrika Kusini (75) kwa nini tusiweze?" alihoji.

Kuhusu madini, Waziri Muhongo alifafanua kuwa amefanya kazi sekta hiyo toka mwaka 1990 hivyo anaelewa kuwa hitaji kubwa la wachimbaji wadogo ni mitaji, zana za kisasa na masoko, hivyo kuahidi kuwa atalishughulikia sambamba na kutazama upya mikataba ya wachimbaji wakubwa.

Kagasheki kuwabana wezi wa wanyama
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki, na naibu wake Nyalandu, walisema kuwa wizara hiyo ina changamoto lukuki kwani hata wenzake wote waliopita hawakutoka salama, hivyo wakaapa kufa na mafisadi wanaopora nyara za taifa kama wanyama, meno na pembe za ndovu.
"Huku wako watu wanakula kama mchwa, hivi inaingia akilini mtu anapakia tembo na ukubwa wote na kuondoka naye halafu asikamatwe? Nina pa kuanzia hasa kwenye ripoti za kamati na ile ya CAG," alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Dk. Mwinyi, aliahidi kuanza kushughulikia mgogoro wa madaktari kwa kukutana na kamati yao ili kuona ni madai yapi serikali inaweza kuyatekeleza. Pia aligusia kuongeza kasi ya usambazaji dawa.


Zitto awapa somo mawaziri
Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto, alisema uteuzi wa mawaziri hao umetokana na kazi kubwa ya Bunge.

Alisema kuwa sasa mawaziri wapya watakuwa na hofu ya meno ya Bunge na hivyo wanapaswa kuchapa kazi vinginevyo yatawakuta kama wenzao.

"Kwa sasa tuwape muda wafanye kazi maana wana jukumu kubwa mbele yao ya kuelekea kwenye bajeti, hali ya umeme huenda ikawa mbaya zaidi maana mabwawa yamepungukiwa na maji, hivyo ngoja washughulike," alisema.

Zitto aliongeza kuwa wale mawaziri waliotajwa moja kwa moja na ripoti kama Mkulo na wengine pamoja na watendaji, wachunguzwe haraka na kufikishwa mahakamani mara moja kujibu mashtaka.
 
Back
Top Bottom