NGAWAIYA: Watanzania tushirikiane kudhibiti ugaidi nchini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

NGAWAIYA: Watanzania tushirikiane kudhibiti ugaidi nchini

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jun 30, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jun 30, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  [h=1][/h]

  Na Otilia Paulinus, Dar es Salaam
  [​IMG]


  KUNA mambo mengi yanayoweza kuvuruga amani ya nchi, kuanzia yale ambayo chimbuko lake ni ndani ya nchi husika na yale yanayosababishwa na au kuchochewa na maadui kutoka nje.

  Matatizo ya ndani yanayoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi ni pamoja na mambo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kikabila, kidini, vitendo vya ufisadi na mengineyo mengi.

  Kadhalika kuna yale yanayoweza pia kusababishwa au kuchochewa na maadui wa nje pamoja na kwamba pia yanaweza kutokea ndani ya nchi husika pasipo chokochoko kutoka nje.

  Hayo ni mengi lakini tutataja moja tu ambalo si lingine zaidi ya ugaidi, ambalo ndio kusudio la makala haya.

  Ugaidi ambao umeonekana kushamiri zaidi hivi sasa, japokuwa umekuwapo tangu zamani ni msamiati mgeni katika nchi yetu, kwa maana kuwa umeshika chati katika miongo hii.

  Kiuhalisia ugaidi hauna rangi, dini, haujali mipaka na wala kuchagua nchi, ikimaanisha kwamba kila mtu anaweza kuwa mwathirika wa ugaidi, hakuna mwenyewe uhakika wa kutoguswa na matukio au tukio la kigaidi.

  Ni ukweli usiopingika kwamba inahitaji mtu mmoja mmoja, familia, jamii na taifa na jumuia ya kimataifa kwa ujumla wake kuunganisha nguvu na mikakati ya pamoja katika kuukabili.

  Mikakati hiyo ina lengo la kuimarisha usalama na kuhami utalii na uwekezaji na kulinda mafanikio yaliyopo kisiasa, kiuchumi na kijamii pamoja na amani.

  Kwa kuwa magaidi wanaweza kutokea miongoni mwetu, kuna kila sababu ya kudhibiti hali hiyo na umuhimu wa kutoa elimu ya uraia kwa wananchi hususani vijana ambao ndio walengwa hasa wanaohitaji kuelimishwa juu ya madhara ya ugaidi.

  Hakuna dini yoyote duniani au kitabu chochote kitakatifu kinachoruhusu mtu au watu wengine wasio na hatia kuua kama ambavyo kundi la Al-Qaeda na washirika wao wanavyofanya.

  Kutokana na umuhimu huo wa kutoa elimu, taasisi isiyo ya kiserikali inayo shughulika na Demokrasia, Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA) imejidhatiti kutoa elimu kwa wananchi juu ya kupiga vita vitendo vya kigaidi.

  Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi Mtendaji wa CEGODETA, Thomas Ngawaiya, anasema vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote wawe makini dhidi ya mashambulizi ya kigaidi kama yanayotokea katika nchi za wenzetu.

  Anasema, kitendo cha kuuawa kwa kiongozi wa Al-Queda, Osama Bin Laden, aliyeuliwa na makomando wa Marekani nchini Pakistan baada ya msako wa miaka 10 kinafaa kutoa onyo na hadhari pia.

  Anasema kuwa Watanzania wanapaswa kuwa makini kufuatia kauli ya mtandao wa Al-Qaeda kutangaza kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi duniani kote kulipa kisasi cha kuuawa kwa Osama.

  “Lazima tuviepuke vitendo vya kigaidi huku tukiwa na kumbukumbu kuwa tuliwahi kushambuliwa na Al-Qaeda mwaka 1998 wakati magaidi hao waliposhambulia Ubalozi wa Marekani nchini na kugharimu maisha ya Watanzania 12 huku wengine wengi wakijeruhiwa ikiwamo kupata ulemavu wa maisha.

  “Wakati wakiushambulia ubalozi huo pia waliposhambulia Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam, walishambulia pia ule uliopo Nairobi, Kenya na kuua watu zaidi ya 200 kabla ya miaka mitatu baadaye kushambulia miji ya New York na Washington na kuua watu zaidi ya 3000,”anasema Ngawaiya.

  Alikumbushia wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zikifanyika nchini Afrika Kusini, Al- Qaeda kupitia tawi lake la Somalia, Al-Shabab waliishambulia Uganda na kuua watu takribani 100 waliokuwa wakifuatilia mchezo wa fainali hizo kupitia luninga.

  “Ukweli ni kwamba Tanzania bado hatuko salama kutokana na urafiki wetu au ukaribu na Marekani kwani Rais mstaafu wa Marekani George Bush, aliwahi kufanya ziara ya siku nne nchini, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa kiongozi huyo kukaa nchi ya kigeni kwa muda mrefu kiasi hicho.

  “Wasiwasi wetu upo kwa vijana wetu kwani wapo baadhi wanaoshabikia Al-Qaeda. Hawa ni rahisi kushawishiwa na kuingizwa kwenye mtandao huo na baadaye kushiriki kwenye mashambulizi ya kigaidi ndani na au nje ya mipaka yetu kama ilivyotokea huko nyuma,” anasema.

  Iwapo hilo litatokea si tu litatutia hasara bali pia kuchafua taswira yetu kutokana na Watanzania kushiriki ugaidi.

  “CEGODETA imefanya utafiti na kubaini kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaotoa hotuba kwenye nyumba za ibada kushabikia malengo ya Al-Qaeda na kuwapotosha vijana ili washiriki kwenye vitendo vya kigaidi,” anaongeza Ngawaiya.
  Anasema hali hiyo inaweza kudhibitiwa iwapo elimu juu ya ugaidi itatolewa ili watu waogope kujihusisha na masuala kama hayo yatakayopelekea kutoweka kwa amani nchini.

  Anasema kutokana na wasiwasi huo, CEGODETA imeamua kutoa elimu ya uraia nchi nzima kuhusu madhara ya ugaidi.

  Alitoa wito kwa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya habari kushirikiana katika kufanikisha lengo hilo la kutoa elimu.
  Pia ameiomba Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua zinazostahili ili kuepusha mashambulizi ya kigaidi yasije kutokea tena nchini.

  CEGODETA pia imeitaka Serikali iwachukulie hatua kali viongozi wote wa dini wanaochochea vitendo vya kigaidi sambamba na kuwafungulia mashitaka mahakamani ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.

  Anasisitiza kwamba ili nchi iendelee kuwa na amani tunatakiwa kuupinga ugaidi kwa nguvu zote kwa kuwa si utamaduni wetu.

  Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo taifa lolote linategemea nguvu kazi yao hivyo ni wajibu wetu kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili na kujiingiza katika vitendo viovu ikiwamo ugaidi,” anasema Ngawaiya.
   
Loading...