Ngawaiya: Nguvu ya umma ilishinda yote Tarime | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ngawaiya: Nguvu ya umma ilishinda yote Tarime

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Habarindiyohiyo, Oct 23, 2008.

 1. H

  Habarindiyohiyo JF-Expert Member

  #1
  Oct 23, 2008
  Joined: Aug 11, 2008
  Messages: 263
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  John Mnyika  MAKALA ya mtazamo wa Thomas Ngawaiya, aliyejitambulisha kama Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA), na kuchapishwa na gazeti hili Oktoba 21, 2008 si ya kupita bila kutolewa mtazamo mbadala.

  Kwa mtazamo wake, Ngawaiya amejenga hoja za ‘vioja’ kadhaa. Mosi, amepotosha umma kuwa CHADEMA ilishikilia Halmashauri ya Tarime kuanzia mwaka 2005. Pili, amepotosha zaidi umma kuwa viongozi wa CHADEMA wanakataza wananchi wasilipe kodi.

  Tatu, amedanganya umma kuwa kutokana na kuongoza huko, Tarime imekosa maendeleo na kwamba miradi ya shule katika wilaya hiyo, imeshindwa kutekelezwa na sasa shule hizo zimekuwa magofu. Nne, ameibua kioja kingine kwa hoja yake kuwa viongozi wa CHADEMA wana sera ya kutaka biashara zipitie njia za panya.

  Tano, ametoa mtazamo wake kuwa mapigano ya koo Tarime yanaletwa na mababa wa vita (warlords) kwa lengo la kujipatia fedha.

  Mwisho, ameibua uzushi wa kuhusisha CHADEMA na hoja ya wananchi kuhusu mbolea ya ruzuku tani 6,000 iliyopelekwa msimu uliopita kutowafikia walengwa.

  Nitaacha kwa muda mjadala wa viti maalumu niliouchangia kwa wiki kadhaa sasa, ili nipate fursa ya kuzijibu hoja hizi za Ngawaiya.

  Awali ya yote ni vyema ikazingatiwa kuwa mwandishi wa mtazamo huu amewahi kuwa mbunge na pia diwani, hivyo anaelewa utendaji wa halmashauri na wa serikali kwa ujumla kupitia uwajibikaji unaofanyika bungeni.

  Hivyo, naamini upotoshaji huo wa hoja sita hapo juu kama nitakavyoeleza, ameufanya si kwa kutokujua, bali kwa kudhamiria kwa lengo la kuendeleza kile nilichowahi kukiita ‘propaganda chafu’.

  Huko nyuma, niliwahi kuandika kwamba katika sanaa na sayansi ya siasa na maendeleo, kuna aina tatu za propaganda: Propaganda nyeupe - huu ni ukweli ambao mimi hupenda kuuita propaganda safi, ni mfumo wa kusambaza ukweli kwa lengo la kujenga imani na kukubalika.

  Aina ya pili ni propaganda za kijivu. Mwenezi au msambazaji huchanganya ukweli na uongo katika sura ambayo kwa uchambuzi wa kawaida si rahisi kujulikana.

  Aina ya tatu ni propaganda nyeusi inayohusisha mahubiri ya uongo. Aina hii hutolewa kishujaa tena kwa uwazi, katika hali ambayo kama mtu haufahamu ukweli, basi huweza kuamini uongo kuwa ukweli na ukweli ukageuzwa kuwa uongo.

  Naandika makala hii nikiwa nimerejea kutoka Tarime ambako nimepata wasaa wa kuzunguka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na kuzungumza na wananchi. Kama ilivyo ada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo, kiliendeleza zile zile mbinu zake za zamani za kutumia maadui, ujinga, umaskini, maradhi na ufisadi katika kutafuta madaraka kwa nguvu!

  Nimeshuhudia CCM ikijaribu kutumia umaskini wa Watanzania kwa kufanya uchaguzi kuwa gulio la kura - kwa kugawa fedha taslimu waziwazi, kununua kadi za kura, kugawa mavazi ili kutafuta ridhaa ya kuongoza. Nimeshuhudia, CCM ikitumia ujinga kutafuta madaraka, ikijaribu kumwaga propaganda chafu badala ya sera safi ili kutafuta madaraka.

  Hakika mkakati huu ulihusisha makada wa upotoshaji, mmojawapo akiwa Thomas Ngawaiya. Katika mikutano yake alikuwa akihubiri hizo hoja sita hapo juu, akijaribu kupotosha kila hali kimtazamo na hatimaye msimamo wa wananchi wa Tarime.

  Katika kundi hilo, wapo pia makada wengine ambao kampeni zao hazikuwa na jipya bali kutusingizia, mimi, viongozi wengine wa CHADEMA pamoja na watu wengine wa pembeni, kwamba tumemuua kwa ‘kumchoma na kisu na kumpiga na nyundo kichwani’ aliyekuwa mbunge wa Tarime Chacha Zakayo Wangwe. (Apumzike kwa Amani).

  Pia nimeshuhudia CCM ikijaribu kutumia maradhi ikiwamo kufadhili na kutuma vikundi vya kiharamia vyenye silaha, kuwadhuru wananchi ili kujenga mazingira ya hofu na vitisho kwa lengo la kupata madaraka.

  Katika kundi hili nilishuhudia pia askari polisi waliotumwa kufanya ‘operesheni demokrasia’ wakiwa wa kwanza kuanzisha ghasia ili kupata sababu ya kuwapiga wananchi, kukamata na wakati huo huo kufanya vitendo vya wizi na unyang’anyi.

  Nilishuhudia CCM ikiwatumia maadui hawa watatu - ujinga, umaskini na maradhi - kwa kumtumia vizuri adui namba nne aliyetangazwa na Mwalimu Nyerere – ufisadi.

  Haya ndiyo niliyoyashuhudia Tarime, chama kinachotawala kikitumia kila aina ya ufisadi kikifadhiliwa na fedha za mafisadi ili kushinda uchaguzi. Moyoni nikasema wakishinda hawa hakuna uadilifu utakaokuwapo zaidi ya kuendeleza ufisadi Tarime, kwa ari, kasi na nguvu mpya. Hivyo, Tarime ilikuwa mpambano kati ya mafisadi na umma.

  Katikati ya mazingira hayo hayo ya kukatisha tamaa, nikashuhudia ‘Tumaini Jipya’. Nikashiriki katika kampeni zilizoongozwa na maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

  Nikashuhudia falsafa ya CHADEMA ya Nguvu ya Umma ikiwa katika maneno na vitendo - katika uhalisia kwenye maisha ya wananchi. Nikashuhudia uongo ukikabiliwa na ukweli; vitisho vikikutana na msimamo wenye amani. Wananchi wakasimamia haki na maendeleo kwa nguvu ya umma.

  Hakuna mabomu ya machozi, vipigo, risasi, rumande, mapanga ya maharamia yaliyoweza kuzima dhamira ya kuchagua viongozi wao na nguvu ya umma iliyohamasishwa miongoni mwa wananchi wa Tarime. Hakuna uongo na propaganda chafu ulioweza kuushinda ukweli. Hakika, wapiga kura waliufahamu ukweli na ukweli ukawapa uhuru wa kuchagua viongozi waliowataka.

  Kuna mengi niliyoyashuhudia Tarime ambayo pekee yanaweza kuandikiwa mfululizo wa makala kadhaa, hususan hatua kwa hatua yaliyotokea tulipokamatwa. Kwa ujumla kampeni zile zilijaa huzuni na furaha huku vijana wakiwa mstari wa mbele kuandika historia. Vituko vya kampeni zile, navyo vinaweza kujaza kurasa.

  Ukweli uliposambaa na kukabiliana na uongo, hata CCM iliamua kuiga mikakati ya kampeni za kisayansi ikiwamo kutumia helikopta - kile chama kilichokuwa kikibeza matumizi ya helikopta kuwa ni anasa, nacho kikaleta helikopta mbili.

  Hata hivyo, kwa nguvu ya ukweli, wale wananchi waliokuwa wakibezwa kuwa ni ‘wahuni’ wanaokwenda kwenye mikutano ya Mbowe ‘kushangaa helikopta’ wakawazomea wao na helikopta yao! Helikopta za CCM zikawa karaha badala ya raha.

  Bila kujiuliza ni kwa nini yote haya yanayokea, CCM ikaendeleza kampeni za kuwatumia makada wake kusambaza propaganda chafu, ikiwamo hizo sita hapo juu zilizokuwa zikipigiwa upatu na Ngawaiya.

  Ukweli katika vichwa vya wananchi ulikuwa ukizijibu hoja hizo sita moja baada ya nyingine, na hukumu ya hoja hizo za uongo ikiwa ni katika sanduku la kura. Sasa naona wameanza kuhamishia hoja hizo kwenye makala za magazeti ili kuwapotosha Watanzania wa maeneo mengine ya nchi.

  Wakati Ngawaiya na wenzake wakisema kuwa CHADEMA imeshikilia halmashauri tangu mwaka 2005, wananchi walikuwa wakiwapuuza kwa kuwa wanajua ukweli kuwa mwaka 2005, CHADEMA ilishinda ubunge na udiwani katika kata kadhaa; halmashauri ilikuwa chini ya CCM.

  Kwa taarifa ya Ngawaiya na wenzake, CHADEMA ilipata halmashuri ya Tarime mwaka 2007 baada ya halmashauri ya awali kugawanywa kuwa mbili - Rorya na Tarime.

  Wakati Ngawaiya na wenzake wakisema kwamba viongozi wa CHADEMA wamewakataza wananchi kulipa kodi na hivyo kukwamisha maendeleo, wananchi wa Tarime walikuwa wanawapuuza. Kwa kuwa wanajua ukweli kuwa hakuna kiongozi aliyekataza wananchi wasilipe kodi. Wananchi wanaelewa wazi hoja ya wabunge wa CHADEMA, akiwemo Chacha Wangwe ilikuwa ni nini.

  Lakini inasikitisha kwamba Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo na Utawala Bora katika mtazamo wake gazetini, anashindwa kuelewa tofauti kati ya michango na kodi. Hakuna kiongozi wa CHADEMA aliyekataza wananchi wasilipe kodi.

  Kodi ni lazima na kukataza mtu kulipa kodi ama kuzuia kodi kukusanywa ni kosa la jinai. Kwa hiyo, Ngawaiya anataka kusema kuwa viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakivunja sheria na serikali ya CCM chini ya Amiri Jeshi Mkuu Rais wa nchi ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, amekuwa akikaa kimya wakati wote? Wananchi wa Tarime wanajua kuwa wanalipa kodi kila wanaponunua bidhaa kama sukari na nyinginezo.

  Wanajua kuwa wote wanalipa kodi, tena kodi kubwa. Viongozi wa CHADEMA wametoa somo kuhusu kodi hadi ‘kimeeleweka’. Wafanyakazi Tarime wanajua kuwa wanalipa kodi. Suala la msingi kule ni je, kodi zao zinatumikaje? Hasa ikizigatiwa kuwa kuna kampuni za madini Tarime ambazo nazo zinalipa kodi.

  Je, haziwanufaishi mafisadi na tabaka la matajiri wachache? Na hapo ndipo inapozaliwa hoja ya michango, ambayo pengine ndiyo ambayo Ngawaiya alitaka kuizungumzia. Ni kweli, viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakikataza wananchi kulipa michango bila kwanza kuelezwa na kuridhika kwamba kodi wanazolipa hazitoshelezi kufanya maendeleo. Na pili, kupewa taarifa za mapato na matumizi ya michango iliyotangulia.

  Na tatu; wamewakataza wananchi kukataa kulipa michango kama endapo itakusanywa kwa njia ambazo zinakiuka haki za binadamu ambazo ni pamoja na kunyang’anywa mali zao. Sasa kwa CCM na makada wake, ambao wamekubali serikali yao ilee ufisadi, itumie kodi za wananchi katika matumizi makubwa ya anasa; somo hili ni mwiba mchungu hususan katika uchaguzi!

  Na hapo ndipo wanapozua vioja vingine, kwamba eti kutokana na uamuzi huo Tarime imekosa maendeleo. Ngawaiya na wenzake wanashindwa kujua kabisa kuwa kwa miaka zaidi ya arobaini tangu tupate uhuru, Halmashuri ya Tarime imekuwa chini ya CCM ikikusanya kodi na kutoza michango lukuki. Cha ajabu maendeleo ya wananchi hao na pengine pengi hapa nchini bado yako nyuma.

  Wanajua kuwa halmashauri zilizotangulia kuchukuliwa na CHADEMA kama Karatu zilionyesha njia kwa kufuta michango ya manyanyaso, lakini bado zikaweza kuleta maendeleo kwenye sekta za maji, elimu nk. Bahati nzuri, wananchi wa Tarime katika uchaguzi ule walikuwa na rekodi za kulinganisha.

  Tuweke pembeni rekodi ya utawala wa giza wa CCM wa zaidi ya miaka 40 tangu uhuru, wananchi walikuwa na fursa ya kulinganisha mwaka mmoja na nusu tangu CCM ichukue halmashuri hiyo mwaka 2005 na mwaka mmoja tangu CHADEMA ichukue halmashauri hiyo mwaka 2007.

  Hapa tofauti ilikuwa bayana. Wakati CCM kwa muda mrefu ilikuwa inapokea mamilioni ya kodi kutoka kwenye migodi iliyomo kwenye halmashuri hiyo, na kuishia kutumika kifisadi na mengine kutumika kwenye matumizi ya anasa ya posho za wakubwa katika halmashauri; CHADEMA ilifanya tofauti.

  Kwa muda mfupi wa uongozi wa CHADEMA, Charles Mwera, akiwa Mwenyekiti wa Halmashuri hiyo, CHADEMA ilipitisha utaratibu kwamba katika milioni 260 zinazopatikana kutoka migodini, milioni 140 zitumike kulipia elimu ya watoto wa Tarime kwa wastani wa milioni saba kwa kila kata.

  Hii ni sera ya CHADEMA iliyoanza kutekelezwa katika kata zote zenye madiwani wa CHADEMA. Watoto wote waliopata nafasi ya kusoma Tarime sasa wanasoma bure kupitia fedha hizi.

  Kwa bahati mbaya, katika kata chache za madiwani wa CCM, wamekataa utaratibu huu na hivyo kukwamisha maendeleo ya vijana na watoto katika kata hizo! Hawa ndio kina Ngawaiya wanaoamini kwamba ili tuendelee ni lazima wananchi wachangishwe kwa wingi zaidi. Tena ni lazima kwenda kuombaomba nje ya nchi. Huu ndiyo utawala bora na maendeleo wanayohubiri.

  Inaelekea Ngawaiya haielewi hali halisi ya Tarime, inaelekea aliishia kwenye majukwaa ya kisiasa alipokuwa kule na hakupata fursa ya kutembelea shule zilizojengwa Tarime tangu mwaka 2005 hadi sasa, ndiyo maana amezuka na kioja kuwa ‘shule zimetelekezwa na kuwa magofu’!

  Badala ya kuinyooshea kidole Tarime, ambayo imeonyesha mfano wa kuwa halmashuri pekee nchini ambayo wanafunzi wanasomeshwa bure, azitazame halmashuri zilizo chini ya chama chake CCM katika mkoa huo huo wa Mara. Aende Bunda akaone shule ambazo hazina vyoo, binafsi nafahamu shule sita katika wilaya hiyo ambazo hazina huduma hiyo muhimu kwa mwanadamu.

  Aende Wilaya ya Mugumu chini ya utawala wa miaka zaidi ya arobaini ya CCM, hakuna barabara ya Lami, halafu alinganishe na Tarime iliyo chini ya CHADEMA. Halafu apitie hesabu za halmashuri hizo kwenye taarifa za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) aione zilivyojaa hati chafu.

  Halafu arudi Tarime akatazame; baada ya miaka mingi ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma yalisababisha hati chafu katika wilaya hiyo, wananchi wakaamua kuichagua CHADEMA kuongoza halmashauri.

  Na katika kipindi kifupi cha kuwa chini ya CHADEMA, halmashauri ikaongozwa kwa uadilifu na kupata hati safi. Ngawaiya na wenzake wafahamu kuwa rangi nyeupe katika bendera ya CHADEMA haipo kama urembo, ni nembo ya kwamba chama hicho kinasimamia uwazi, ukweli na uadilifu katika uongozi wake kwa kupinga aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za taifa.

  Ngawaiya anasema kwamba viongozi wa CHADEMA wanatetea biashara huria na kutaka biashara zipitie njia za panya. Hapa ndipo sanaa na sayansi ya propaganda majivu inapotumika kupotosha umma.

  Wananchi wa Tarime na Watanzania kwa ujumla wanajua kabisa ya kuwa CHADEMA chini ya itikadi yake ya mrengo wa kati, inaunga mkono soko huria bila kupora mamlaka ya umma katika sekta nyeti.

  Lakini CHADEMA imetamka bayana katika katiba yake kuwa haiungi mkono soko holela. Na wakati wote nimekuwa nikisema kwamba serikali ya CCM inayoamini katika ujamaa wa dola kumiliki njia za uzalishaji mali, imerukia sera ya soko huria bila kuwa na misingi ya utekelezaji wake kupitia yale Maamuzi ya Zanzibar yaliyozika Azimio la Arusha. Matokeo yake wameipeleka nchi katika soko holela!

  Ieleweke wazi kuwa chini ya mfumo wa chama cha kina Ngawaiya, ambacho kinahodhi mamlaka ya mambo mengi katika serikali kuu tofauti na mfumo wa majimbo ambao CHADEMA iliupigia upatu katika kampeni za 2005, na inaendelea nao, udhaifu katika mipaka ya Tarime unafanywa na serikali ya CCM na si Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iliyoko chini ya CHADEMA.

  Ikumbukwe kwamba, uhamiaji na askari walioko mipakani wanapokea maagizo na maelekezo kutoka serikali kuu ambayo iko chini ya CCM.

  Serikali ya CCM inashindwa kusimamia mipaka ya nchi, na hata katika njia rasmi kama za Sirari katika wilaya ya Tarime, napo kuna udhaifu mkubwa! Lilipojitokeza suala la uhaba wa mchele nchini Kenya, ambapo wafanyabiashara walikuwa wakipitisha na kuuza katika nchi hiyo kwa bei ya juu kupitia njia za panya; serikali ya CCM badala ya kukabiliana na chanzo cha tatizo, ikaanza kukimbizana na matokeo. Ikaamua kuweka kizuizi cha barabarani katika eneo la Kirumi; mpakani mwa Wilaya ya Musoma na Tarime.

  Walichofanya ni kudhibiti mchele kwenda Kenya hivyo serikali ikaamua kudhibiti mchele kwenda Tarime. Watanzania wakaanza kunyimwa haki ya kula wali kwa uhuru kwa sababu ya Wakenya. Hapo ndipo Wangwe, akiwa mbunge anayewakilisha sauti ya tabaka la chini, akaibua suala hilo bungeni.

  Serikali ya CCM badala ya kushughulika na mzizi wa tatizo, wameendelea na utamaduni wao wa kushughulikia matunda; sasa wamehamishia kizuizi hicho eneo la Rubana mpakani mwa Bunda na Mwanza.

  Ngawaiya ameenda mbele zaidi kwa kuwaita viongozi wa koo zinazokinzana huko Tarime kuwa ni mababa wa vita (warlords) wanaopigana kutafuta fedha. Ni hoja za kutokujua historia ya migogoro ya koo kama hizo ndizo zilizofanya makada wa CCM kina Ngawaiya, Makamba na wengineo kunyimwa kura katika maeneo hayo.

  Bahati nzuri Charles Mwera katika ilani yake ya uchaguzi wakati akigombea kiti cha ubunge kilichoachwa wazi na Wangwe, ameeleza bayana juu ya asili ya matatizo ya koo hizo kuwa ni migogoro ya ardhi.

  Ameweka wazi dhamira yake na ya chama anachotoka ya kuhakikisha kwamba panakuwa na mipaka pamoja na upatanisho. Ni muhimu sasa akapewa ushirikiano na asasi zote za haki za binadamu na za utawala bora kutekeleza azima hiyo.

  Ngawaiya amemalizia mtazamo wake kwa kuibua uzushi wa kuhusisha CHADEMA na hoja ya wananchi kuhusu mbolea ya ruzuku tani 6,000 iliyopelekwa msimu uliopita kutowafikia walengwa.

  Bila kujijua ameibua kashfa kwa chama chake na serikali yake. Pia, ameibua mjadala mkubwa zaidi kwa kuwa huko Kilimanjaro, kwa miaka kadhaa kati ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitajwatajwa katika kashfa za ruzuku za wakulima yeye ni mmoja wao.

  Bahati nzuri wananchi wa Wilaya ya Tarime na Watanzania wa maeneo mengi wanafahamu kwamba mawakala wa kusambaza mbolea hizi wanateuliwa kutoka serikali kuu moja kwa moja. Matokeo ya serikali kuu kuhodhi mamlaka hayo ni kuwapo kwa tuhuma za ufisadi katika uteuzi wa baadhi ya mawakala ambao wengine wameshindwa kufikisha mbolea hizo kwa wananchi, huku wengine wakipandisha bei tofauti ya dhamira ya mpango wa mbolea ya ruzuku.

  Halmashauri za CHADEMA na wabunge wake wamekwishaanza harakati za kufichua ufisadi na/ama matumizi mabaya ya madaraka katika eneo hilo hadi kieleweke! Ngawaiya ameyasema yote hayo, kujenga hoja kwamba Tarime hawakufanya chaguo bora; hii ni baada ya wananchi wa huko kudhihirisha kuwa ‘sauti ya watu ni sauti ya Mungu’. Nguvu ya umma ilishinda yote Tarime.  juu
  Maoni ya Wasomaji
  Maoni yanayotolewa na wasomaji wa safu hii ni ya kwao na sio maoni ya kampuni ya Freemedia Ltd. Aidha sio maoni ya mtunzi au mwandishi wa habari au makala husika hapo juu. Maoni haya hayajahakikiwa wala kuafikiwa na kampuni ya Freemedia Ltd.
  Maoni 14 yameshatolewa. (Nawe toa maoni yako!)
  BRAVO MNYIKA.100/100.OMBI LETU KILIMANJARO,NI KWELI TULIYAPOKEA MAGEUZI KWA MWITIKIO MKUBWA MIAKA YA 90'ILA HALI KWA SASA IMEKUWA TOFAUTI,WANANCHI WAMEBANWA KIMAENDELEO ILI WAPATE MAJUTO KUCHAGUA UPINZANI,WENGI WAMEINGIA WOGA NA KUSHABIKIA MAFISADI KINYUME NA DHAMIRA ZAO. NAOMBA MPITE KILIMANJARO YOTE KUWASHA ARI YA MAGEUZI KUPITIA OPERATION SANGARA'TUKO TAYARI KUWACHANGIA KILE KIDOGO TULICHO NACHO MAPAMBANO YAENDELEE.

  na MU-URU JASIRI - 22.10.08 @ 09:53 | #49815

  Ufafanuzi wako uko bayana.Niliposoma makala ya Ngawaiya na kwa jinsi alivyojaribu kujenga hoja, hakika walio wengi watakuwa waliamini makala ile.Lakini kwa kutoa ufafanuzi ulio wazi basi umempiku.Utaratibu huu uendelee pale inapotokea upotoshaji  na Melissa, Dodoma, - 22.10.08 @ 09:56 | #49818

  Kwa Hali hii kakika Ngawaiya atakuwa amepoteza attention ya Wananchi, hawezi kuaminiwa tena, safi sana Mnyika, Hoja Nzuri imejibu Viroja vya Ngawaiya

  na Pepe, Kusadikika, - 22.10.08 @ 10:06 | #49821

  Bwana Mnyika ni hazina kubwa katika ukombozi wa kifikra kwa Taifa hili linalozama kama Titanic'Wito wangu kwa CHADEMA,fuatilieni sana masuala ya upotoshaji yanayofanywa juu yenu na kupambana nayo kisayansi.Ni kweli nilipatwa hofu jana kuona makala ya mzushi'Ngawaiya kuwa mmewakataza wanatarime kulipa kodi,Sasa nimepata picha Halisi.Kwa kuiongoza Halmashauri na mbunge pia ni wenu:mnaweza kufanya makubwa kwa kuwa'Nguvu ya maamuzi kupitia vikao vya halmashauri iko mikononi mwenu!Sasa kodi inayokusanywa ili kusukuma maendeleo,isimamieni vizuri kwa kuwa Mafisadi CCM watataka kuonesha wanatarime wamerudi nyuma kwa kuwepo Chadema,tunawaelewa sana hao kwa propaganda za maji taka!Mtoa maoni 49818 hapo juu-Kilimanjaro mbona tuliwaaminia mnatutia aibu?lini mmeanza kukimbilia kanga,kofia na mashati ya kijani?Hao wabunge wa CCM mliochagua pigeni chini wote 2010,labda angalau abaki Anne Kilango maana ni mpiganaji kasoro anaogopa kuvaa kombati za kimapinduzi Chadema pengine babu anambania!

  na che guevara - 22.10.08 @ 10:21 | #49826

  Uchambuzi huu umetulia.... Ngawaiya ziiiiiii!!!!

  na juma, Kgr, - 22.10.08 @ 08:04 | #49843

  Mnyika rafiki, ndugu na mwanadarasa wangu; mengi msemayo na mfanyayo chadema yanaonesha ukomavu wa mawazo na moyo ( HASA AFANYAYO ZITO KABWE ). Lakini turejesheeni amani nafsini mwetu kwa kukitegua kwa vitendo kitendawili kinachodhihirika kwa macho ( achilia mbali kuhisiwa ) kuhusu UKABILA ndani ya CHADEMA.

  na mukasa - 22.10.08 @ 08:10 | #49847

  Kilimanjaro ilikuwa ya kwanza kuonyesha mapinduzi lakini hawakupata utetezi mkubwa na CCM ikawaadhibu kikweli kweli. barabara zote zikafa, kahawa imekufa na mengi ya maonevu yalijitokeza wazee (waliobaki kijijini wengi ni wazee vijana wanahangaika mijini!) wakaingizwa woga wakakubali. Kwa nguvu hii mpya yenye akina Kilango na Kimaro makamanda wa kweli ndani ya CCM tuko nyuma kuleta mapinduzi bila kujali ni chama gani. Tuwe mstari wa mbele kukusanya takwimu sahihi za ushahidi wa dhuluma na ufisadi kwa jamii ili tuweze kukabiliana na propaganda za akina ngawaiya tunapotaka kuleta mabadiliko ya uongozi. Tuwe wakweli na tusiwe na woga katika kusemea maovu kama kina Kubenea na Dr. Silaa. Naomba viongozi wote waadilifu (Safu ya Chadema, Mh. Kilango na Mhe. Kimaro) watuandikie simu zao za mikononi na email zao tuweze kuwapa habari za ufisadi kila tunapozipata. Mhe. Kikwete anahitaji msaada wa kweli

  na mzalendo, DSM, - 22.10.08 @ 08:13 | #49848

  Bravo John Mnyika,
  Wewe ni kichwa, umemuweza huyu FISADI ngawaiya, akajisafishe kwanza dhidi ya tuhuma zinazomkabili, asituletee ufisadi wa ccm hapa. Hafai hata kidogo ni wa kuogopwa kama ukoma.Nahauri CHADEMA tafuteni wenye akili vyuo vikuu wawasaidie hii vita. Kisha tumieni helicopter kuwafikia wananchi walipumbazwa kule vijijini, hamasisha kama mwenda wazimu mpaka kieleweke na MUNGU atawasaidia kuokoa taifa hili.

  na mwanaharakati no 1, UAE, - 22.10.08 @ 09:08 | #49861

  Hongera sana ndg, Mnyika usife moyo hao mafisdi wanataka kuwayumbisha, lakini ukiwa mwanamapinduzi uschoke, tuko pamoja nanyi mpaka kieleweke

  na chenji, dar, - 22.10.08 @ 09:17 | #49865

  Mnyika ni kati ya watu walio makini,ni kati ya vijana wanaotuwezesha kuona ukombozi wa nchi hii kuwa unakaribia kwa kupitia wao walio jasiri;wengine ni kama kina Kabwe, Mrema, Lucy,Mdee na wengineo.

  Hawajengi hoja kizuzu,wanakuwa na uhakika na kile wanachokieleza kwa umma.Ngawaiya ameishiwa huyu mzee,ndio kina Mtikila hawa waliokubali kula makombo yao na matapishi yao kwa ccm.

  Mukasa mbona unaturudisha nyuma kuhusu suala la ukabila chadema?ulikuwa wapi wakati ule mnyika analitolea ufafanuzi?hebu tembelea blog yake usome tena!

  Hizo acussations za ukabila ndio hizo znazoitwa propaganda chafu.Kwan mnyika wa wap?si msukuma huyo?Baregu yuko naye baraza kuu la chadema?wa wapi huyo?bob makan je?kina wangwe wenyewe wametoka wapi?chambueni mambo kwa facts!
  Mapambano kwa ukombozi wa nchi hii kupitia chadema wakati wake ndio sasa!

  na Ng'wanahollo, Nairobi,Kenya, - 22.10.08 @ 09:27 | #49869

  BIG UP Mnyika, endelea kutoa somo ili pepo la ujinga lilowakalia Watanzania kwa miaka mingi liweze kutoka na CCM waadhirike, nafikiri habari hizi zikiwafikia Watz wote CCM watakuwa UCHI kama mwanga aliyefumaniwa Usiku.
  CHADEMA HOYEEEE!!!!!!!!!!!!!

  na Michael Laiser, Dar, - 22.10.08 @ 10:00 | #49886

  HUYU NGAWAIYA NI MTU AMBAYE YUPO CCM KIUNAFIKI ILI KULINDA BIASHARA ZAKE NA WALA SIYO KWAAJILI YA MAENDELEO YA WALIO WENGI NA WANYONGE;

  ALIKUWA MBUNGE WA JIMBO LETU LA MOSHI VIJIJINI KWA MUDA MREFU NA HAKUNA CHOCHOTE ALICHO TUSAIDIA ZAIDI YA KUSHUHUDIA HATA ZAO LETU LA KAHAWA LIKIISHIA BILA YA KUTOA MALALAMIKO YA WANANCHI TULIOMPIGIA KURA ZA KUINGIA BUNGENI KATIKA VIKAO VYA BUNGE;

  CHAMA CHA USHIRIKA KNCU KIME KUFA NA WATU WACHACHE WAKA GAWANA MALI ZOTE ZA CHAMA BILA KUWA KUMBUKA WAKULIMA WA KAHAWA WALIO KIANZISHA KWA KUKATWA FEDHA KILA WALIPO PELEKA KAHAWA SOKONI, JE HUYU NDUMILA KUWILI HAKUWEPO KIPINDI HICHO?
  NI HATUA GANI ALIZOCHUKUA AKIWA KAMA MBUNGE?
  NI BARABARA IPI ILIJENGWA HATA KWA KIWANGO CHA CHANGARAWE KIPINDI CHA UONGOZI WAKE(UBUNGE WAKE)?
  NIBORA HATA ANGEONGEA MREMA KIDOGO TUNA MENGI MAZURI ALIYO TUFANYIA NA TUNA MPONGEZA KWAHILO ILA NAMSIHI AUNGANISHE NGUVU NA CHADEMA ILI TURUDISHE HADHI YA MKOA WETU KAMA ILIVYO KUWA ZAMANI.

  KUWA NA VIONGOZI VIGEUGEU KAMA NGAWAIYA MKOA WETU UTAZIDI KUDORORA KIUCHUMI HIVYO NIBORA TUMKWEPEE MBALI.

  Wenu: MWANA MAWELLA(URU) CASTRO NATHO.


  na CASTRO MUSHI (NATO), Dar es Salaam, - 22.10.08 @ 11:07 | #49904

  Heko Jahn Mnyika.Mtu aliyeua Demokrasia nchini na kubagua watu wanaochagua upinzani ni Benjamini Willium Mkapa.Wananchi wote Tanzania msife moyo sasa ndio umefika wakati wa kukizika chama cha Mapinduzi kwani kina kiongozi Bubu na Kiziwi.Mpatieni kura mtu anayejua kukemea maovu na kuwachukulia hatua wezi na mafisadi.JK kwa vile amekuwa Bubu na Kiziwi hata ukimchagua kesho mimi nadhani utakuwa umechelewa.Chagua mtu mwenye uwezo wa kukemea maovu.CCM kwako utakuwa umechagua chama cha kukupotosha.Habari ya Ngawaiya achana naye kwani ni mmoja wa Mafisadi wanaotajwa sana katika Mkoa wa Kilimanjaro.Wacha avute pumzi wakati wanamapinduzi wanakaribia kuchukua nchi.Atasema mali alizo nazo amepata wapi wakati tunajua alikochuma.

  na OLE LETIPIPI, TANZANIA, - 22.10.08 @ 11:42 | #49917

  Castro na Mzalendo nimewapata.Nasikitika sana kuona hata mbunge Chami badala ya kuwaletea maendeleo kwa nafasi aliyo nayo kama naibu waziri amekuwa mstari wa mbele kugawa pombe(mbege) na nyama vijijini,mbege kila siku ipo mbona hafikirii barabara zilizokuwepo zinavyozidi kuharibika bila ukarabati!!angalia barabara za Uru mashariki iliyowekwa lami tangu enzi za mwl Nyerere imekuwa mahandaki!!nenda Kibosho kirima mapipa ya lami yalivyorundikwa miaka mingi!!nenda old moshi n.k wanavijiji wamechoka mbaya ndio maana anatumia njaa zao kuwadangangya na kurubuni madiwani wapinzani kurudi CCM,Ndio kazi aliyoifuata bungeni?CHADEMA tunaomba mtuandalie mtu makini tumpige chini.

  na MU-URU JASIRI - 22.10.08 @ 14:37 | #49980
   
 2. M

  Mundu JF-Expert Member

  #2
  Oct 23, 2008
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,719
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  Nina uhakika masuala nyeti ambayo Sisiem inayaongea kimzaha mzaha yakipatiwa majibu yakinifu kama haya, umma utaelewa nini pumba na nini mchele.

  Wasiwasi wangu asilimia kubwa ya watanzania ni maskini na hawana uwezo wa kupata habari hizi kwenye magazeti au labda TV. Ushauri wangu kama mnaweza kumudu kutumia helcopta endeleeni nayo ili mfikie wananchi wengi wa vijijini. Huko ndiko Sisiem hubeba kura za kutosha kwa sababu ya uongo na vitisho wanavyowapa wananchi juu ya demokrasia ya vyama vingi.

  Ikishindikana kutumia helcopta, basi endeleeni na mkakati kama ule mnaofanya sasa wa operesheni sangara ili itakapofika wakati wa uchaguzi ujao muwe mmewafikia wananchi wengi wa vijijini.

  Nasisi tulio mijini ole wetu. Sisiem ilituibia kura katika ule uchaguzi wa kwanza 1995, hasa hapa DSM. walipoamua kufuta na kurudia uchaguzi wananchi wakavunjika moyo. Ila kwajinsi nchi inavyoendeshwa sasa, sisi wakazi wa mijini katu haturubuniwi na sukari na fulana. uchaguzi wa maka 2010 utakuwa ni fundisho kwa Sisiem.

  Haiwezekani idadi ya watu unaokutana nao mijini wote wako kinyume na Sisiem lakini ikifika wakati wa uchaguzi Sisiem iinashinda viti vyote Dar... Kisa, wananchi makini, waelewa, wasomi walisusa kupiga kura. Tuamke sasa!!
   
  Last edited: Oct 23, 2008
 3. M

  Mama JF-Expert Member

  #3
  Oct 23, 2008
  Joined: Mar 24, 2008
  Messages: 2,858
  Likes Received: 20
  Trophy Points: 0
  inawezekana ant-sisiemu wengi si wapiga kura... either wako nje ya nchi au wanaona uvivu kwenda kupanga foleni kujiandikisha kupiga kura na kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi. Mfano mdogo tu, ukiangalia wakati wa campaigns wale wanaohudhuria ile mikutano majority sio ant-sisiemu....muda huo ant-sisiemu huwa busy maofisini, au inawezekana kuomba ruhusa kazini kwenda kuhudhuria hii mikutano?
   
 4. M

  Magabe Kibiti JF-Expert Member

  #4
  Oct 23, 2008
  Joined: Jan 20, 2008
  Messages: 292
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Huyu Ngawaiya hakujua kinachoendelea Tarime, hakuwajua wananchi wa Tarime na kwa sasa inaonekana hatakuja kuelewa kinachoendelea Tanzania. Alivyotoa uchambuzi wake hapa kuhusu Tarime kabla ya uchaguzi, niliandika hapa na kwenye media outlets zingine kumsahihisha na kumtafadhalisha kuhusu makosa mengi aliyoweka kwenye uchambuzi wake.

  Kosa kubwa la Ngawaiya ni kudhani kuwa watanzania wote ni kama yeye na kuwa wakipewa vipesa kidogo basi wataacha misimamo yao na imani zao. Watu wa Tarime wametoa somo kubwa sana kwa watu kama Ngawaiya na Makamba. Kuna kikomo kwenye uovu na udanganyifu bila kujali wingi wa pesa (bilioni 2 za Tarime?) zinazotumika.
   
 5. AbdulKensington

  AbdulKensington Member

  #5
  Oct 23, 2008
  Joined: Oct 21, 2008
  Messages: 72
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nina Swali la Kuuliza:
  Chama gani linaonekana kuwa na 'potential' zaidi....CCM au CHADEMA?
   
 6. K

  Kithuku JF-Expert Member

  #6
  Oct 23, 2008
  Joined: Nov 19, 2006
  Messages: 1,395
  Likes Received: 96
  Trophy Points: 145
  Ngawaiya ni mufilisi kabisa kisiasa tangu zamani hizo akiwa na kina Mrema. Ni mbabaikaji opportunist. Nitashangaa sana kama bado kuna watu wanaosoma au kusikiliza hoja zake.
   
Loading...