Neno La Leo: Usimuige Tembo Kwa Lolote Lile!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,


Shujaa wa taifa la India Mahatma Ghandi alipata kutamka; " Bila ya ng'ombe India isingekuwepo". Mwingine angefikiri, Wahindi hawa ni watu wa ajabu sana. Iweje watoto wao wengi wafe kwa njaa kila kukicha huku wakiwaacha ng'ombe takribani milioni 200 wakizurura ovyo mitaani pasipo kuwachinja?


Katika hilo tusiwahukumu Wahindi kabla ya kujaribu kuwaelewa. Wahindi hawa wapatao milioni 800 hawawezi kuwa wendawazimu kwa kukubali kuwaacha ng'ombe wao bila kuwachinja. Kuna busara kubwa ya Wahindi kumfanya ng'ombe kuwa "mtakatifu". Sababu kubwa na ya kimsingi ni ya kiuchumi.


Karibu asilimia 70 ya Wahindi wanaishi mashambani, ni wakulima. India hukumbwa na mvua kubwa zenye kuambatana na upepo wa monsuni. Kutokana na mvua hizi, mkulima wa India anaweza kulazimika kulima shamba zima kwa siku moja na pengine kuvuna shamba zima kwa siku moja. Hali hii ya hewa hulazimisha kuwepo na uharaka katika utendaji kazi.

India haina uwezo wa kutoa matrekta ya kutosha ya kulima na kuvuna kwa idadi hii kubwa ya wakulima wa nchi yao. Hapa ng'ombe anaweza kutumiwa kufanya kazi hii ya haraka. Ng’ombe atavuta jembe la plau, atasaidia katika kuvuna, na hata kusafirisha mazao.


Ng'ombe husaidia pia katika kutoa nishati mbadala. Pamoja na ng'ombe kuzurura barabarani, ni nadra sana nchini India, kukutana na vinyesi vya ng'ombe vilivyotapakaa. Kinyesi cha ng'ombe huchukukuliwa kikiwa kibichi, hukaushwa na kufanywa kuwa nishati. Kuna majiko yenye kutumia moto wa kinyesi cha ng'ombe. Kinyesi hutumika pia kama mbolea ya shambani.


Fikiri, India ingekuwaje kama Wahindi hawa milioni 800 wangetegemea nishati ya kuni za miti?


Kimsingi kinachofanya uchumi wa India ukue kwa haraka ni mioyo ya uzalendo na utaifa wao. Kuna wakati, Rais George Bush alipotembelea India , alipokewa na kuendeshwa kwenye gari iliyotengenezwa India. Msafara wake ulikuwa ni wa magari yaliyotengezwa India. Magari kama Bajaj, Maruti, TATA na mengineyo. Yote haya ni fahari ya India.

Ndio, Wahindi wanajivunia India yao na kila kinachotengenezwa kwao. India ni taifa kubwa. wana programu za nyuklia ingawa ili linahitaji mjadala, wana viwanda vya madawa, hospitali zenye ubora, viwanda vya nguo na mengineyo mengi. Kwa miaka mingi, wenzetu hawa wamewekeza katika elimu ya watu wao na kwa lugha yao. Wameanza sasa kuvuna walichopanda.

Kwetu sisi Watanzania, hali yetu ya kiuchumi bado duni mno. Ufisadi unalitafuna taifa letu. Tuna lazima ya kukumbushana ukweli huu. Na ili kuunusuru uchumi wetu usiyumbe zaidi, tuna lazima ya kutumia fedha na rasilimali zetu kwa busara kubwa. Ilivyo sasa kuna mengine tunayoiga yenye kututia hasara zaidi. Mathalan, anasa za viongozi wetu wakiwemo wabunge , kuanzia kwenye magari hata safari zao za nje. Wananchi wakiuliza, wanajibiwa; angalieni wabunge wa Afrika Kusini!


Wahenga walinena; Usimuige tembo kwa lolote lile. Mengine afanyayo tembo yanatokana na ukumbwa wa maumbile yake. Na hilo ni Neno la Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
 
Back
Top Bottom