Neno La Leo: Ujamaa Ni Imani, Mwenzangu Mfutakamba Imemshinda?

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
( Pichani juu Ndugu Mfutakamba akiwa mitaa ya Iringa na picha ya chini alipotembelea Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Ilula kuzindua mradi wa kuifadhi maji ya mvua)


Ndugu zangu,


Ujamaa ni imani. Na Wajamaa tuko wengi nchi hii.
Kuna tuliojifunza tangu utotoni, kwamba Ujamaa ni imani. Tunajitahidi kuishi kama tulivyojifunza. Kuishi kama tunavyohubiri sasa. Lakini, kama ilivyo kwa imani nyingine, ni jambo gumu, ni mitihani kila kukicha, naam, Uislamu ni mgumu, Ukristo ni mgumu. Hivyo basi, na Ujamaa pia.


Ndugu yangu Athumani Mfutakamba ( Pichani juu) ameondolewa kwenye Baraza jipya la JK. Nimesikitika, ni kwa vile, Mfutakamba niliyemfahamu tangu tukiwa nae hapa Iringa si yule niliyekuwa nikimsoma kwenye media siku za karibuni. Kwamba imeandikwa kuwa ana ugomvi na Waziri mwenzake Omar Nundu. Na ugomvi wenyewe ulikuwa na harufu ya kugombania ’ maslahi binafsi’- mambo ya rushwa na milungula.


Mfutakamba niliyemfahamu mie niliamini kuwa alikuwa ni Mjamaa mwenzangu wa Kidemokrasia( Social Democrat). Aliishi kama alivyohubiri. Hakuwa na makuu. Mjini Iringa ilikuwa nadra kumwona akiwa kwenye gari kwenye mitaa ya mji. Tulitembea nae kwa miguu. Tulisimama wote kwenye meza za magazeti, kusoma na kupiga gumzo. Ilikuwa vigumu kwa wengi kutambua kuwa Mfutakamba alikuwa na cheo cha U-DC. Mfutakamba alishuka chini kwa wananchi.


Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita niliratibu maombi ya fedha kiasi kutoka Shirika la misaada la Sweden ili zikisaidie Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Ilula kijenge matanki ya kuhifadhi maji ya mvua. Tulichoomba kama msaada ni kiasi kidogo, lakini, nguvu kazi ya kujitola ya watu wa Ilula ilitumika zaidi katika kufanikisha mradi huo.


Mradi ulipokamilika, nilifanikisha mawasiliano na Ndugu Mfutakamba, kama DC wa Kilolo, aje kutufungulia rasmi mradi huo na kusema mawili matatu. Mfutakamba aliitikia wito wetu, alifika na kuifanya kazi hiyo kwa gharama za Serikali. Hatukuombwa mchango wowote wa mafuta ya gari ya Mfutakamba kufika Ilula kutoka umbali wa kilomita zaidi ya mia moja.


Ndio, huyo ndio Ndugu Mfutakamba niliyemfahamu; hakutanguliza maslahi binafsi, bali ya wananchi. Ndiye Mfutakamba tuliyekunywa nae chai, na tulikula nae chakula cha pale kwa ’ Baba Nusa’- moja ya migahawa ya watu wa kawaida kabisa hapa Iringa. Ukweli, si mara moja, nilikaa na ndugu Mfutakamba pale kwa ’ Baba Nusa’ na kujadili mambo ya wananchi na changamoto za maendeleo yao.


Niliposikia JK amemteua Mfutakamba kuwa Naibu Waziri, nikasema, Naam, hapo JK amepata kiongozi mtumishi wa watu.


Hakika, habari kuwa Mfutakamba amekubali kupandishwa ndege na Wachina kwenda ’ kutalii’ nchi kadhaa na hatimaye kukaa chini na waliompandisha ndege kujadili masuala ya tenda za ujenzi wa gati hii na ile pale Bandarini zilianza kunitia mashaka. Si Mfutakamba yule niliyemfahamu.


Yumkini mjini kuna mengi na mambo mengi ya kuwatamanisha viongozi kutaka kujipatia fedha nyingi zaidi, na kwa haraka. Na ukawa mtihani kwa ndugu yangu Mfutakamba.


Na katika maisha kuna kuanguka. Sote tumepata kuanguka, nani ambaye hajaanguka. Kilicho muhimu kwa mwanadamu ni kujifunza kutokana na anguko. Si kusimama na kujiendea zako kana kwamba hakuna kilichotokea.


Naamini, Ndugu yangu Athumani Mfutakamba moyoni bado ni Mjamaa wa Kidemokrasi- A Social Democrat. Anaweza kujisafisha kutoka kwenye kashfa iliyomkuta, na hatimaye kurudi tena.


Naam, Ujamaa ni Imani, sidhani kama mwenzangu Athuman Mfutakamba imemshinda kabisa.
Na hilo Ni Neno La Leo.


Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
 
Mjengwa,

Tanzania na Watanzania, ni zaidi ya ujuavyo. Wanapokuwa wana nyemelea "ulaji" huwa ni kondoo, wakishapata ulaji, wanakuwa ni mbwa mwitu wa kutisha tena wenye njaa kali sana na wako tayari kufanya lolote lile ili watii njaa yao.

Ile katuni ya Masudi Kipanya ambayo ilikuwa inaonyesha panya walioshiba na matumbo makubwa, halafu juu kuna mkono unamuondoa panya mmoja, kuna kundi la mapanya wengine huko nje wanasema Bro watoe hao sisi tuje tupige mzigo ... mzigo wa kufanya ufisadi. Na hiyo ndio CCM ... Afterall, Sophia Simba was right aliposema kwamba "Ndani ya CCM hakuna aliye msafi". Yaani kuanzia Mwenyekiti wao mpaka mabalozi, labda hata wanachama wao, maana kwenye kura za maoni CCM inashika namba kwenye kuhonga, na mpiga kura yeyote anayepiga kura kwa kuhongwa naye hana usafi wowote na hana tofauti na aliyetoa rushwa. Ndio maana mtoaji na mpokeaji rushwa wote ni wachafu na huo ndo uchafu ulio CCM!
 
Back
Top Bottom