Neno La Leo: Siasa Hizi Za Ki-Hodorono!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Sisi wa Kizazi Cha Azimio na wanyuma yetu bado tuna kumbukumbu ya ' Senema za Omo'.
Mara moja kwa mwezi ' tabaka la Wafanyakazi' wengi wakiishi Ilala lilikuwa likionyeshwa filamu. Hawa ni wazazi wetu wakati huo. Ilala ni karibu na eneo la viwandani kule Pugu Road.

Pale viwanja vya Shule ya Msingi ilikuwa ni moja ya sehemu za wananchi kukusanyika kuangalia senema ya bure.
Hakukuwa na televisheni enzi hizo na filamu ya picha zinazotembea kwenye kitaambaa kikubwa cheupe ilikuwa jambo la kuvutia sana. Na kwenye ' Senema za Omo' ndipo tulipokuwa tukionyeshwa matangazo ya biashara pia.

Nilikuwa mdogo sana, lakini, moja ya matangazo ninayoyakumbuka sana ni tangazo la Hodorono. Haya ni manukato ya kujipulizia makwapani ama maarufu kwa jina la perfume.

Tulionyeshwa abiria anayeingia kwenye basi, na mara abiria mmoja huku akiwa ameshika pua akaanza kutamka kwa sauti; " Hodorono! Hodorono!". Na wengine wakaitikia " Hodorono! Hodorono! Hodorono! Huku wakitokea madirishani. Mwisho kwenye basi akabaki abiria yule aliyeingia. Akaonekana aliyeshangaa asijue kilichowafukuza wenzake. Ujumbe ukawa umefika kwake na jamii, kuwa tutumie Hodorono!

Miaka mingi imepita tangu nilione tangazo lile. Katika fikra zangu hizi za ukubwani, tangazo lile si kingine bali ni tangazo la kibaguzi na ambalo halikufaa kuonyeshwa katika jamii.

Na siasa zetu za siku hizi nazo zimekuwa za staili ya Hodorono. Ni siasa za kibaguzi unausukumwa na ubinafsi.
Tunaona vijana wa leo wameanza kuukataa kwa vitendo ubaguzi huu wa kisiasa. Ni jambo jema. Huko nyuma TANU na baadae CCM viliamini kuwa asiyefikiri kama wao basi si mwenzao. Ni mpinzani, ni adui wa maendeleo. Ni adui wa umma. Ni msaliti. Si mwenzao na alibaguliwa. Alitengwa na pengine kuishia kifungo cha ndani au cha nje kwa kurudishwa kijijini alikozaliwa au asikozaliwa.

Huko Mtanzania huyo aliyebaguliwa kisiasa alifikia kuambiwa kuwa kila siku awe anaripoti kwa Balozi wa Nyumba Kumi. Na kutoka kijijini kwake kwenda kijiji kingine ni sharti aombe ruhusa ya uongozi wa kijiji! Na kutoka nje ya wilaya ni sharti apate kibali cha DC! Hii nayo ni historia yetu. Ili tuelewe tulipo na tunakokwenda tuna lazima ya kuipitia historia yetu.

Ubaguzi wa kisiasa ni jambo baya sana. Kwamba kuna wanaojiona wao wana haki zaidi kuliko wenzao katika nchi hiyo hiyo ambayo wenzao pia wanaiiita nchi waliyozaliwa. Kwamba wana uwezo wa kuwafanya Watanzania wenzao waishi maisha magumu kwa vile tu wanatofautiana au wanapingana kifikra na walio kwenye mamlaka ya dola au Chama kilicho madarakani.

Ubaguzi wa kisiasa huzaa chuki ya kisiasa. Na mara zote, uvumilivu wa wanaobaguliwa na kukandamizwa hufikia kikomo. Na yanapolipuka, basi, huwa kama nusu ya kiyama. Moto huwaka. Hakukaliki.

Kule Misri vijana wengi wanajua sasa ni kwanini wazazi wao walihangaika sana kutafuta ajira lakini hawakupata na kuishia kuishi maisha magumu. Wanajua sasa ni kwanini baadhi yao ( Vijana) hawakupata scholarship au ajira baada ya kufuzu masomo yao.

Wanajua sasa, kuwa Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Hosni Mubarak, familia yake na jamaa zake wa karibu walikuwa na faili maalumu yenye orodha ya majina ya WaMisri, vijana kwa watu wazima, ambao walionekana kuwa ni wenye fikra za kipinzani. Kuna waliochunguzwa tangu wakiwa kwenye mijadala ya vyuo vikuu. Na ambaye jina lake limeingizwa kwenye faili hilo, basi, ataandika kurasa kwa maelfu za barua za maombi ya kazi, na atasaga lami sana hadi soli za viatu ziishe akitafuta ajira bila mafanikio. Serikali ya Hosni Mubarak ilikuwa na mikono mirefu, na miguu pia. Tatizo lilikuwa kwenye 'kichwa cha Serikali'. Kilikuwa kidogo sana, maana hatma ya yaliyomfika Hosni Mubarak ingepaswa kuepukwa na mtu mwenye kichwa kinachofikiri. Kwa vile kilichotokea kingetokea, ilikuwa ni suala la wakati tu.

Ndio, Usalama wa Taifa ( Zaidi Usalama wa Hosni Mubarak na Chama chake) ulihakikisha Mmisri ambaye jina lake limo kwenye kitabu chao hapati kazi yeyote ile labda iwe ya kubeba zege ili hali ana digrii ya chuo Kikuu.

Nimefurahi sana hii leo kuwasilimulia juu ya tangazo la Hodorono kwenye enzi za utoto wangu. Hakika, ni tangazo la kibaguzi.

Na siasa zetu siku hizi zimekuwa za Ki-Hodorono. Ni siasa za kibaguzi. Tunajenga nyumba moja, lakini tunagombania fito. Ni hulka za ubinafsi. Kama nchi , siasa za hodorono zitatupelekea si tu kuvuja jasho na makwapa kunuka, bali kuvuja damu kwa kukatana mapanga. Kwa viongozi tuliowapa dhamana kutotanguliza busara na hekima.

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam.
0788 111 765
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
 
nzuri
ila ningekushauri ufunguke laivu kwa majina au any other indicator ambayo ingekuwa rahisi kwa wale tusiofuatilia siasa kwa sana kuwaelewa kiyabisia/kuihalisia ni akina nani unaowalenga
 
Hivi Mkuu Maggad

Mbona huwa huchangii mada za wenzako? This is bullshit kutokuwa na ushirikiano na wenzako sijangii tena hapa
 
Kwa wapenda mabadiliko
wameelewa, kama hujui
kutafakuri ni tatizo lako
hilo!.
 
Back
Top Bottom