Neno La Leo: Nchi Ni Kama Shamba...

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Jumapili ya leo inatumiwa na wengi duniani kutafakari juu ya Nelson Mandela na yale aliyoishi akayesema na kuyatenda.

Na hakika, Nelson Mandela ni ishara ya upendo na uvumilivu. Na Mandela anatukumbusha pia umuhimu wa mwanadamu kuishi na kutenda kwa kuzingatia kanuni. Ndio, kuwa na misingi ya kiitikadi na kanuni za kuzifuata.

Ndugu zangu,

Nahofia kuwa Mandela amekufa huku pia tukishuhudia kufa kwa itikadi. Viongozi wetu wa leo wengi hawaongozwi na wala hawaongozi kwa kufuata misingi ya kiitikadi.

Mathalan, kwa kiongozi anayefuata misingi ya kiitikadi ya kijamaa kamwe hawezi akawa kiongozi kwenye chama kinachojinasibu kuwa kinafuata misingi ya itikadi za kihafidhina. Huo ni mkanganyiko.

Mazungumzo ya Julius Nyerere na Nelson Mandela pale nyumbani kwa Mwalimu Msasani mwaka 1962 yalijikita kwenye misingi ya kiitikadi. Unaweza kuyaona haya ukisoma kitabu cha Mandela;( Nelson Mandela, Long Walk to Freedom).

Kwenye mazungumzo yale Nyerere alimwelewa Mandela na kubadili mtazamo wake juu ya PAC ni kwa vile wawili hao ' Walikutana kiitikadi' na kisha wakauona mkakati sahihi wa kwenda mbele.

Ndugu zangu,

Mara nyingi tunazungumzia juu ya nchi kusonga mbele kimaendeleo, lakini, ni mahali gani tunapobaini kuwa nchi inarudi nyuma kimaendeleo?
Ninaposoma maandiko mbali mbali, nami nikikumbuka pia utoto wangu miaka ya 70, hufika mahali naona kama vile tunarudi nyuma kimaendeleo.

Kwamba vingi tunavyovitafuta sasa tulikuwa navyo, lakini, tumevipoteza wenyewe. Maana, nchi ni kama shamba. Na kwa vile maendeleo ya nchi yanatokana zaidi na akili ( elimu) ya watu wake,hivyo, nchi ambayo raia wake wengi wako duni kielimu isitegemee mafanikio makubwa kimaendeleo.

Ndio, Nchi ni sawa na shamba. Unapoliacha bila kupalilia linaota magumu. Ili tuendelee tunahitaji kufanya juhudi za dhati, kama taifa, kupalilia shamba letu kwa kuwekeza ' kama wendawazimu' kwenye elimu ya watu wetu.

Itachukua miaka 10 hata 20 hadi hapo tutakapoanza kuvuna mazao kwenye shamba letu. Kwamba tutakuwa na raia wengi wenye kumiliki ' K' tatu muhimu kwenye vichwa vyao; kwa maana ya raia wenye Kujitambua, Kujiamini na Kuthubutu.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa.
Iringa.
0754 678 252
MjengwaBlog :: Habari, Picha, Matangazo na Matukio
 
Back
Top Bottom