Neno La Leo: Mwanadamu Anakuwaje Anapokumbwa Na Maafa?

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,


NCHI yetu imekumbwa na msiba mkubwa, ni maafa. Ni ajali ya meli ya MV. Spice Islanders iliyotokea juma la jana kule pwani ya Nungwi, Zanzibar.


Na swali ni je; mwanadamu anakuwaje anapokumbwa na maafa?
Jibu; kwanza kabisa, maafa yana nadharia yake pindi yanapotokea. Maafa yeyote yale yana hatua mbili kubwa; mosi, mshtuko mkubwa kwa mwanadamu pindi maafa yanapomtokea, na pili, kwa mwanadamu kufanyia kazi kilichotokea.


Tumeona, kuwa Watanzania tulipatwa na mshtuko mkubwa tulipofikiwa na taarifa za maafa ya meli kuzama kule Zanzibar. Hatua ya sisi wanadamu kukumbwa na hali ya mshtuko mkubwa pindi maafa yanapotokea hutuchukua saa kadhaa hadi siku kadhaa kabla ya hali hiyo kuanza kuondoka taratibu.


Ni katika hali hii ya kwanza ya mshtuko mkubwa, mwanadamu mwenzetu aliyekumbwa na maafa huonekana kutoamini kilichotokea kwamba kimetokea. Anaweza hata kucheka ndani ya mzigo mkubwa wa huzuni ulio katika nafsi yake.


Kuna ambao hubaki kudhani ni ndoto tu. Ni wakati huu pia sisi wanadamu hupatwa na hasira, chuki na ghadhabu kwa kilichotokea. Na hata baada ya kutamka ya ghadhabu, huzuni uturejea tena kama wingu zito la mvua linalotanda kwa kasi. Ni hapa wanadamu tunapojihisi ni wenye mkosi.


Tunajiona tusio na uwezo wa kufanya lolote kurekebisha hali husika. Tunajikuta katika hali ya ombwe kuu. Tunahisi tumo katika giza nene. Tunaishiwa nguvu. Tunajiuliza maswali mengi. Hatuyapati majibu tukaridhika. Ni katika hali hii, kila mkono wa pole tunaopewa na mwanadamu mwenzetu unakuwa na maana kubwa sana.


Hata ’ missed calls’ kwenye simu unazihesabu kuwa ni ’ missed calls’ za kukutia faraja. Kwamba kuna wanadamu wenzako wenye kukujali. Ndio, maafa huwaunganisha wanadamu. Na kuna maadui wanaopatana kwenye maafa. Maana, ndipo hapo hutambua, kuwa siku zote, wanadamu tunahitajiana. Ndio maana tukaitwa wanadamu, na si wanyama.


Baada ya hatua hiyo ya kwanza ya maafa yanapotokea, huja hatua ya pili, nayo ni ya kufanyia kazi kilichotokea. Hapa wanadamu, katika hali ya kutulia, tunaanza kuirejea ile hali ya maafa iliyotumbuka na kujaribu kuielewa.


Tunatafuta tafsiri na maana ya kilichotokea. Ni hapa , ndipo wanadamu tunaanza kuelewa, kuwa kilichotokea kimetokea. Katika hatua hii tunahitaji zaidi kuzungumza kwa sauti juu ya kilichotokea. Na katika kufahamu ni kitu gani kingefanyika ili kukizuia kilichotokea.


Na yote haya ni katika hitaji letu wanadamu la kutaka kuutafuta ukweli na kujifunza. Tuutafute ukweli ili siku nyingine kisije kutokea tena kile kilichotokea. Hapa wanadamu tunaanza kurejea katika hali ya kawaida. Kwa kawaida, hatua hizi mbili hutuchukua wanadamu majuma takribani sita kuzipitia na kuzimaliza.


Kinachohitajika hapa ni kwa wanadamu wengine kuelewa hitaji la mwanadamu mwenzao kuzipitia hatua hizi. Na si baada ya juma moja tu kudhani kuwa mwanadamu aliyekumbwa na maafa na huzuni ya msiba mkubwa anaweza kurejea katika hali ya kawaida.


Kikubwa ni kuzungumza kwa uhuru juu ya kilichotokea kwa nia njema ya kutaka kujifunza na kuepuka hali hiyo isitokee tena. Maana, Watanzania tumekuwa ni watu wa kumwachia Mungu kwa hata yale tunayopaswa kuyafanya wenyewe.


Na labda nimalizie kwa kuuliza; hivi tumejiandaa vipi kama jiji kama Dar es Salaam linakumbwa na maafa ya mafuriko makubwa? Au maafa ya gesi kulipuka?
Nahitimisha Neno La Leo. ( Neno hili ni sehemu ya makala yangu iliyochapwa leo kwenye Raia Mwema)


Maggid,
Dar Es Salaam.

Septemba 14, 2011
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom