Neno La Leo: IGP Siro Na Changamoto Ya Rufiji..

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Kwenye picha inayomwonyesha Rais wa Jamhuri akimtunuku cheo cha U-IGP, kamanda Simon Siro anaonekana kimawazo, akiwa mbali sana na Ikulu . Bila shaka ni katika wakati huo, anazidi kuuelewa uzito wa mzigo anaotwishwa.

U-IGP bila shaka yeyote ni moja ya vibarua vigumu katika wakati tulio nao kutemegea na approach au msogeleo wa IGP mwenyewe na timu yake. Ni kwenye mbinu za kukabiliana na changamoto za kiusalama za wakati huu.

Kwetu wachambuzi, mara nyingi tunahangaika sana kutafuta kauli ya kwanza kwa aliyekabidhiwa madaraka. Kiuchambuzi, huo ndio huwa mguu wa kuanzia safari, ambao pia utusaidia kuona mwelekeo wa safari.

Afrika safari unaweza kuianza kwa mguu mzuri au mbaya. Nimeisikia kauli ya kwanza ya IGP Siro.
Ameweka wazi, kuwa kazi ya kupambana na uhalifu haiwezi kufanywa na polisi tu. Ushirikiano na raia ni muhimu.

Katika hilo, IGP Siro ameanza safari yake na mguu mzuri. Kuanza na kunyosha mikono ya kushirikiana na RAIA. Akichanganya mambo mbele ya safari itakuwa ni bahati mbaya kwake na nchi pia.

Imekuwa hivyo na zaidi sasa, kuwa masuala ya Ulinzi na Usalama wa nchi yanahitaji uzalendo na approach ya ' People Centred Security'.

Jana nimemsoma Profesa Eginald Mihanjo ambaye amepata kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Chuo cha masuala ya Ulinzi na Usalama ( National Defence College).

Naye anazungumzia umuhimu wa kushirikisha raia. Profesa Mihanjo anasema raia huungana na kuyaona mapambano ni yao na kuwa tayari kuyapigana pale wanapoelewa kuwa yanahusu maslahi yao. Anasema Profesa Mihanjo.

Bila kuingia kwa undani juu ya changamoto ya Rufiji. Binafsi naiona nafasi ya changamoto ya Rufiji kumalizwa haraka kwa kutumia nadharia za kiulinzi zenye kumweka raia kama sehemu ya mapambano badala ya kuwa adui.

Naona umuhimu pia wa kuikabili changamoto ya Rufiji kwa kuangalia historia. Nimeandika mara nyingi, kuwa Historia ni Mwalimu Mzuri.

Kwa kushindwa kuingalia historia, kuna makosa yalifanyika tunakapata hali ile ya vuguvugu la ' Gesi Haitoki'. Wengi wa vijana wetu wale walioshiriki vuguvugu lile hawakuwa na uelewa wa kwanini ' Gesi itoke'. Inahusu mahusiano kati ya viongozi na raia. Inahusu mawasiliano.

Tuna ya kujifunza pia kutokana na vuguvugu la Majimaji na wananchi kung'oa mazao ya biashara. Ni enzi za mkoloni, naye mkoloni alifanya makosa.

Mwingine anayetupa somo katika changamoto hizi ni Marehemu Profesa Sethy Chachage.

Nimemsoma sana Mwalimu wangu Profesa Chachage. Wakati wa uhai wake nimemsikiliza pia kwenye mijadala ya hadhara, kwenye runinga na redioni.

Laiti Profesa Chachage angekuwa hai leo, ningelipenda kunywa nae chai na kuchambua kinachotokea leo na kulinganisha na kilichotokea zamani.

Wote tumeviona kupitia simulizi na maandiko ya kitafiti. Na duniani hapa tafiti hutusaidia pia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili.

Naamini , kama taifa, Changamoto ya Rufiji bado imo ndani ya uwezo wetu. Muhimu kabisa, ni kushirikisha raia. Tuna raia wema wengi wakati raia waovu wachache. Tutafanya makosa tukiongeza kila kukicha, idadi ya raia waovu.

Kwa kuwanyoshea mikono ya ushirikiano raia, IGP Simon Siro ameanza na mguu mzuri.

Kila La Heri IGP Simon Siro.

Maggid Mjengwa.

Iringa.
 

Attachments

  • 2.jpg
    2.jpg
    21.1 KB · Views: 80
Back
Top Bottom