Ndugu zangu,
Na leo tena nina neno. Asubuhi ya leo niliongozana na watoto wangu wawili kwenda sokoni kupata mahitaji ya nyumbani. Ni pale Soko Kuu la Miyomboni. Sokoni pale nilisimama ili ninunue bamia, nyanya chungu na njegere. Aliyejitokeza kuniuzia alikuwa msichana mdogo wa chini ya miaka 13. Alifanya biashara ile akiwa amekaa chini juani.
Niliingiwa na simanzi kubwa, maana msichana yule alikuwa na umri uliokaribiana na watoto wangu. Nao niliwaona wakimwangalia mtoto mwenzao ambaye ameacha kuwa mtoto na kuchukua majukumu ya watu wazima. Nilimwuliza jina lake, anaitwa Rehema. Anafanya biashara ili arudi nyumbani na senti za mahitaji mengine ya nyumbani, ametumwa na wazazi wake. Ndivyo alivyonieleza, nilimwamini, nimesikia simulizi kama hizo kabla.
Nilimpa noti ya shilingi elfu mbili. Nilivyoona kuwa alivyonifungia vimejaa mfuko nikamwuliza kama kuna hela nyingine napaswa kuongeza. Alinijibu; Wewe ndio unanidai shilingi mia tatu, ngoja nikatafute chenji. Nikamwambia asiende kutafuta chenji. Mia tatu ile abaki nayo.
Ilinitia simanzi zaidi. Hakika, msichana Rehema hana kosa. Tatizo ni la kimfumo zaidi. Ndio, tunazidi kuukumbutia ubepari, mfumo unaozidi kuongeza idadi ya masikini, idadi ya wanaoshindia mlo mmoja kwa siku, idadi ya wanaopitisha siku kama walivyoipokea. Idadi ya wasio na ajira na wasio na hakika ya kupata huduma bora za msingi za kijamii; shule na afya.
Wanaofuturisha yatima walipaswa kulipa kodi zitakazosaidia kugharamia elimu na afya za wanyonge walio wengi. Ndio, katika mfumo huu wa soko huria tulipaswa tujenge nidhamu ya kukusanya kodi ili zisaidie kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. Iliwezekana huko nyuma, inawezekana sasa.
Maana, hii ni nchi yetu.Hatima yetu kama watu binafsi, kama vikundi vya watu na kama taifa inatutegemea sisi wenyewe. Umasikini wa watu wetu ni umasikini wetu. Kiitikadi mimi ni Social Democrat na bado naamini mfumo wa enzi za Mwalimu wa Ujamaa na Kujitegemea bado una nafasi katika jamii yetu. Mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea uliofanyiwa mabadiliko ya kimsingi unaweza kutuhakikishia ulinzi wa maslahi ya nchi yetu. Ni kwa sera zenye kuhakikisha usawa wa watu. Sera zitakazohakikisha kodi inakusanywa na kutumika katika yaliyo muhimu na yenye kumsaidia pia mwananchi wa chini katika nchi yetu. Aweze kupata elimu bora na huduma bora za afya kati ya mengineyo ya msingi.
Tuazimie kuwajibika kwa pamoja kwa maslahi ya nchi yetu. Na tukifanya ajizi, tutaigeuza nchi yetu kuwa nyumba ya njaa. Na hilo ni Neno La Leo.
mjengwa