Neno La Leo: Ajabu Ya Kushangilia Kushindwa...!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Haihusu mpira. Ni jambo zito sana ningependa leo niliweke hapa tulijadili.

Nchi yetu na jamii kwa ujumla imekumbwa na hali ya watu kudhani kuna njia za mkato za mafanikio. Kumezuka michezo mingi ya kamari kupitia runinga na kwengineko.

Waathirika wakubwa ni pamoja na vijana wetu, nguvu kazi ya taifa iliyo sasa kwenye ' maradhi' kwa maana ya kuwa mateja wa kamari.

Nimeliandikia hili mara kadhaa. Naandika tena kukumbusha na kupanua wigo wa mjadala kwa vile linatuhusu sote. Tuna lazima ya kupaza sauti.

Maana, hili ni tatizo tunalopaswa kuliangalia kwa uzito ule ule kama tunavyoangalia athari za matumizi ya madawa ya kulevya.

Na si vijana tu, hata watu wazima wakiwemo walimu wa vijana hawa. Tuna walimu ni mateja wa kamari. Wana kipi cha kuwafunza vijana wetu mashuleni?
Na Kamari hizi zina majina mbali mbali.

Na ajabu, zinasemwa zimekuja kubadili maisha ya Watanzania!

Watu wetu wanapoteza kwa kunyanyag'nywa kidogo walicho nacho. Ni wachache wenye akili wanaocheza na saikolojia ya watu wetu. Vijana wetu leo hawataki hata kufanya kazi. Kamari imekuwa ajira!

Wenye akili hawawezi kuwa na ujinga wa kutengeza mashine halafu wao wenyewe washindwe!

Kimsingi wenye kushinda kwenye nyingi ya kamari hizi ni kama asilimia 0.001 na wenye kushindwa ni asilimia 99.9. Walioshindwa ndio wenye kumlipa mshindi huku faida kubwa ikienda kwa waliobuni kamari hizi.

Nina mashaka, kwamba kama Dola isipoingilia kati haraka kudhibiti kamari hizi kwa kuweka taratibu zenye afya kwa jamii, yaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine ya kijamii ambayo gharama yake ni kubwa kuilipa. Na katika hili sina maana ya marufuku ya kamari, bali Serikali kusimamia taratibu na uwepo wa udhibiti ili kunusuru walio wengi.

Maggid Mjengwa.
0688 37 36 52 ( Whatsapp)
 
Back
Top Bottom