Neno Fupi La Usiku Huu: ' Dawa Ya Mboga!' | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Neno Fupi La Usiku Huu: ' Dawa Ya Mboga!'

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, May 3, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  May 3, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Ndugu Zangu,


  ” Awali sisi rafiki,
  Maisha yetu pamoja,
  Tuliishi kama ndugu,
  Mikutano ni ishara,


  Nashangaa sana ndugu,
  Usiwe ndumilakuwili
  Kupenda watu wawili,
  Fitina sio adili,
  Na kila jambo dalili,

  Unapotaka kusema,
  Tumia yako hekima,
  Neno liwe la heshima. ”
  - Remmy Ongala.

  Naam. Kwa mila zetu, chumvi haizungumzwi usiku kwa jina lake. Usiku chumvi ni ' Dawa ya Mboga!' Chumvi ni maisha, chumvi ni siasa.  Kwa wengine wataona ni kitu kigogo sana. Hapana, chumvi ni kitu kikubwa. Sukari na utamu wake, lakini hauzidi utamu wa chumvi.


  Kwanini?
  Maisha yaso chumvi si maisha. Ndio maana, Serikali zote Afrika huheshimu bei za chumvi. Ukimwona raia wa nchi anaanza kulalamikia bei ya chumvi, basi, hizo si ishara njema.

  Mwanadamu waweza kuwa na kila kitu nyumbani. Lakini, ukikosa chumvi nyumbani , basi, huna kitu! Na mwandani wako ni chumvi yako, au?

  Haya, umenunua nyama, vitunguu, nyanya na vingine. Jikoni unakaangiza. Kumbe! Unakumbuka, kuwa umesahau. Nyumbani hakuna chumvi.


  La haula! Giza limeshaingia, utakitafuta hata kibanda cha masikini, ukaombe chum… Shii!
  Usiku ni mwiko kutamka chumvi kwa jina lake, sema ’ dawa ya mboga’. Na unajua maana yake?


  Wazee wetu walikuwa na busara sana. Aliyesahau kuwa na chumvi nyumbani alikumbushwa kwa kupewa ’ tabu kidogo’ katika kuipata chumvi. Maana, chumvi ni muhimu sana kuwa nayo nyumbani.

  Ndio, chumvi ndio dawa ya mboga. Nyama ulokaangiza haiwezi lika bila chumvi ati! Kama kuna ’ nyama ya ulimi’, basi , chumvi ndio ’ asali ya ulimi’. Na chumvi ina kawaida yake. Ikiharibika, ndo basi tena, ni ya kutupwa hiyo. Chumvi haioshwi.

  Na mwanadamu chunga ulimi wako. Neno lako ni chumvi. Fikiri kwanza kisha ulitamke, usitamke kisha ukafikiri. Neno baya ni sawa na chumvi iliyoharibika. Haiosheki, ikasafishika, na ikabaki kuwa chumvi.


  Na mwanadamu akisemwa amekula chumvi nyingi ina maana ameishi miaka mingi. Amefaidi maisha. Binadamu aweza kupitisha siku bila kula chenye sukari. Lakini, hakuna siku ipitayo kwa mwanadamu bila mdomoni mwake kumeza kitu chenye chumvi. Na kama si chakula, basi mate, nayo yana chumvi!  Na nikisema chumvi ni tamu kuliko sukari nani abishaye?


  Mh! Dawa ya mboga! Na hilo ni Neno La Leo.


  Maggid,
  Msamvu,
  Morogoro
  0788 111 765
  http://mjengwablog.com
   
Loading...