Zurie
JF-Expert Member
- Jul 6, 2014
- 2,002
- 5,534
Naibu waziri wa Wizara ya Habari, Anastazia Wambura, ametoa siku saba kwa Menwja Rasilimaliwatu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Neema Mrindoko kujieleza ni kwanini ameandika jina lake katika kiwanja kilichopo Kisarawe mkoani Pwani.
Wambura alisema hayo jana akionesha kukasirishwa na kitendo hicho alipotembelea kiwanja hicho kilichopo eneo la Kimani ambacho mpaka sasa hakijakamilisha usajili wake na kupewa hati wakati kilinunuliwa na Shirika hilo mwaka 2012.
Kiwanja hicho kilichojaa nyasi nyingi kuonesha kilishatelekezwa, kimejengwa nyumba za watumishi ambao wangekuwa wakifanya kazi katika kituo cha Kisarawe lakini hazijakamilika.
"Natoa siku saba mtu huyu awe anipa Maelezo ya kutosha kwanini hati hiyo imesainiwa na mtu mmoja ambaye ni yeye na ameandika jina lake badala ya jina la Shirika, inamaana alikua hajui? Hii ni makusudi," alisema Wambura.
Wambura alisema mtu huyo amefanya makusudi kwa nafasi yake kushindwa kutambua kukaa miaka yote hiyo bila kupewa hati na kutelekezwa bila kuendelezwa ni ufisadi ambao hauwezi kuvumiliwa.
Awali Wambura alipokuwa akipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Mwanamvua Mrindoko, alisema kiwanja hicho chenye mita za mraba 9,567 kilipimwa na kusajiliwa kwa namba 68480 mwaka huo huo TBC iliomba kuandaliwa hati.
Mrindoko alisema utaratibu za ukamilishaji hati zilifanyika na walilipia na kujaza fomu ya maombi ya hati hata hivyo baada ya TBC kuisaini na kuirudisha Ardhi ilionekana kuwa na mapungufu ikarudishwa TBC.
Aliyataja mapungufu hayo kuwa ni hakukua na nalala halisi ya kuanzishwa shirika na pia fomu hiyo ilisainiwa na mtu mmoja badala ya wahusika wawili wa Shirika hilo na hivyo kukwamisha mchakato wa kupata hati.
Naibu Waziri huyo alipomuhoji Afisa miradi wa Wizara hiyo, Macksselin Chota ambaye alikuepo hapo, alisema Maelezo hayo ni sahihi kwamba mapungufu hayo wanayafanyia kazi.
Chota alisema viwanja vingi vya TBC havijapata hati ambapo kati ya viwanja 55 ni 19 pekee ndivyo vyenye hati na pia viwanja vingi viko katika migogoro mbalimbali kama vile uvamizi na pia uporaji.
Naibu Waziri Wambura aliagiza ndani ya siku hizo saba hati ya kiwanja hicho cha Kisarawe Iwe imepatikana, na pia TBC itoe Maelezo ni namna gani watafanya kuendelea majengo ambayo yameanza kujengwa hapo.
"Hii inatia mashaka kabisa, mnachelewesha kupata hati na baadae viwanja vinaingia kwenye migogoro, unafanya hivyo ili baadae nyie wenyewe mzunguke, tutashindwaje kuamini hivyo?" Alihoji Naibu Waziri.
Naibu Waziri huyo aliagiza TBC kuangalia namna ya kuanzia kuendeleza viwanja vya Shirika hilo kwa ubia ili kulipatia Shirika mapato na pia nyumba za watumishi wake.
Chanzo: Habari Leo