NEC imeamua kuwa chaka la mafisadi?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,099
NEC imeamua kuwa chaka la mafisadi?

Nkwazi Nkuzi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

TAARIFA kwamba Waziri Mkuu mfukuzwa, Edward Lowassa, hakuwa na hatia bali alijiuzulu kuwajibika, ila hakuhusika katika kashfa ya Richmond, ni upuuzi wa mwaka.

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) iliyokutana hivi karibuni ilitoa tamko hili la kuchusha na kukera kama lilivyokaririwa na vyombo vya habari.

Inashangaza na kukatisha tamaa kama chama kinachojidai kupigania masilahi ya Mtanzania kikiimba wimbo wa maisha bora kinaweza kuja na upuuzi kama huu! .

Kama hakuhusika na kashfa ya Richmond ni kwanini alijiuzulu? Je, ina maana taarifa nzuri ya kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe ni upuuzi?

Je, kitendo cha NEC si kulidharau na kulitukana Bunge na kulionyesha kama taasisi inayosema uongo? Je, Bunge limechukuliaje shambulio na kashfa hii? Kama Lowassa hakuhusika na Richmond, alijiuzulu kwa kosa gani au kashfa gani? Huu ni uchovu wa kisiasa usio na mfano. Huu ni mwanzo wa kifo cha CCM!

Badala ya Kamati Kuu ya CCM kufanya kazi za umma ilifanya kazi ya kusafishana. Na hii si mara ya kwanza kwa CCM kufanya hivyo. Mwanzoni akina Lowassa na wenzake walitaka kuitumia Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) .
Nayo bila tahadhari wala kuona mbali ilijaribu kuwasafisha mafisadi hawa bila mafanikio hadi Bunge lilipoamua kuunda kamati iliyoweka historia ya kuwa Bunge la kwanza katika Afrika kumtimua mkuu wa shughuli za serikali bungeni, waziri mkuu.

CCM imekuwa ikipewa kila aina ya majina mabaya kutokana na maamuzi yake mabaya yaliyojikita kwenye kulindana na kubabaisha. Hivi ni Mtanzania gani awe hata mwanachama wa CCM damu asiyejua kuwa Lowassa alifukuzwa kazi na hakujiuzulu? Ni nani hajui kuwa kilichomfukuzisha Lowassa ni ufisadi wa nyuma ya Richmond? .

Kuna siku CCM watakuja kutwambia kuwa Tanzania ni nchi iliyoendelea. Maana wanaweza kujipayukia lolote kana kwamba wanawaambia ‘mataahira’! Baya zaidi wanapodanganya wanajidanganya na wao pia!

Kama tamko la NEC halitatenguliwa, basi hakuna siri, aliyosema Mwalimu Nyerere yanatimia. Mwalimu aliwahi kuionya CCM juu ya kuvamiwa na wafanyabiashara. Wakati ule tulijua wafanyabiashara, tusijue ni mafisadi.

Je, Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete anapotuambia ana azima ya kupambana na ufisadi ilhali akikalia kiti kwenye kamati inayopitisha upuuzi na baraka kwa mafisadi, tumweleweje? .

Tunaambiwa kuwa hata waziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, hawakuwa na kosa! Mbona Msabaha aliiambia Kamati Teule ya Bunge kuwa Richmond ulikuwa mradi wa waziri mkuu wa wakati ule na Mwarabu wake? Kwa nini NEC wamesahau kuwa yaliyoandikwa huwa hayaozi (scripta manenta)?

Kama CCM itashikilia upuuzi huu ningeishauri tume teule ya Bunge na Bunge lenyewe kwenda mahakamani kupinga dharau hii na matusi kwake.

Kama Lowassa na wenzake hawakuwa na hatia wala kushiriki kwenye uchafu wa Richmond, basi NEC ituambie nani wako nyuma ya Richmond. Au ni yale yale kuwa Richmond inafutikwa chini ya busati kuepuka kumtaja mhusika wa kweli aliyeiidhinisha? Je, Watanzania nao kwa upande wao watakubali kugeuzwa mabwege kiasi hiki ilhali kila kitu kiliwekwa wazi mbele yao na kamati teule ya Bunge? Enyi Watanzania ‘wapumbavu’, nani aliwaroga hadi mkaaminishwa kuwa Lowassa na wenzake hawakuwa na hatia bali waliwajibika? Mbona Lowassa na wenzake waliwekwa ‘uchi’ mbele zenu mkajionea na kusikia kila kitu! Namna hii inatisha na si vibaya kusema: Sasa, rasmi CCM imeikabidhi nchi kwa mafisadi .

Tuliwahi kuonya kuwa CCM, kwa sasa ina ombwe la uongozi wenye akili timamu. Tulionya kuwa uchafu wa wakuu wa CCM utaiangamiza nchi. Kweli kama Lowassa hahusiki na Richmond, ni kwa nini ametupwa nje? Je, hii inaweza kuwa janja ya kumsafisha ili arudishwe kwa mlango wa nyuma? Je, uswahiba wake na Kikwete umeshinda hata haki? Je, akirudishwa, Watanzania watamkubali na kumpokea? Maana, kupitia wapambe na ‘waganga’ wake aliwahi kukaririwa bila hata chembe ya aibu akijilinganisha na mzee Ali Hassan Mwinyi aliporejea kwenye siasa na kuwa rais baada ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani wakati ule kukumbwa na kashfa ya mauaji ya kina Nzegenuka .

Hivi karibuni Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati, alikaririwa akipindisha maneno ya tume teule ya Bunge kuwa waziri mkuu wa zamani Lowassa, apime na kuamua la kufanya. Baada ya Lowassa kupima aliamua kujiuzulu. Je, huyu kama aliamua mwenyewe kujiuzulu kama tunavyoaminishwa, hii si ishara ya kukiri kuwa alifanya makosa? Kinachonichefua zaidi ni ile hatua ya NEC kuwamwagia sifa mafisadi shutumiwa waliojiuzulu kuwa walikiletea heshima chama hicho! Je, maana yake hii ni nini? Au ni yale kuwa Lowassa aliamua kuachia ngazi ili serikali yote isianguke? Kama Lowassa aliubeba msalaba wa serikali chafu inayonuka, basi iwe ni kwa faida ya walioko nyuma ya kashfa hizi na si kuwahadaa Watanzania kuwa Lowassa na wenzake hawakuwa na makosa .

Kama CCM ingekuwa ni ile ya Nyerere, Lowassa na wenzake walipaswa kufukuzwa kwenye chama hapo hapo na kuchukuliwa hatua za kisheria, badala ya kumwangiwa sifa za uongo na NEC. Kama kuna kitu kimefanywa na NEC kwa kuwatetea na kuwapongeza kina Lowassa, si kingine bali kuonyesha sura halisi ya Kikwete, wenzake na CCM.

Kinachoonekana hapa ni kwamba CCM sasa ni chama cha mafisadi. Kinachojibainisha hapa ni kwamba pesa iliyoibwa na hawa watu na washirika wao si chochote, isipokuwa ushindi kwa CCM! Je, CCM imewapongeza hawa mashujaa wake kutokana na kazi yao njema ya kulihujumu taifa ili CCM ishinde kupitia takrima? .

Kama si hivyo, sasa ni nini kilichoishawishi kamati kuu kufanya upuuzi wa mwaka? Je, wajumbe nao walihongwa kiasi cha kuja na usanii huu usioingia akilini?

CCM sasa inafikia ukingoni. Katika kikao hiki cha NEC, tunaarifiwa kuwa kulikuwa na mgawanyiko. Wana CCM safi walitaka mafisadi wasulubiwe huku wakubwa wao wakiwapinga. Je, wadogo walilazimishwa na wakubwa kuridhia upuuzi huu? Je, NEC imeamua kutoa taarifa yake na si ya wajumbe? Maana hatujaambiwa jinsi walivyofikia kutoa tamko hili hatari kwa nchi na hata kwa chama chenyewe

Je, wale wana CCM safi watakubali kuburuzwa na kuonekana wasaliti kwa taifa lao kwa kuogopa wakubwa wao? Je, tutegemee nini? Wapo watakaojitenga na CCM kuhakikisha haki inatendeka au nao watageuka wanafiki na wachumia tumbo kiasi cha kukubaliana na jinai hii? Hata kama CCM itazika tofauti zake kwa ujanja au nguvu, ukweli ni kwamba ina nyufa nyingi kiasi cha kushindikana kuzibwa. Na hili likiongezewa na kuwa na uongozi mgando usio na visheni wala udhu, siku za CCM zinaanza kuhesabika .

Kama imeweza kutekwa na kushindwa na kundi la wahalifu wachache, kweli kitaweza kupambana na changamoto za kuendesha taifa kubwa kwenye karne hii ya sayansi na teknolojia, ambapo kashfa za wateule wake zinavujishwa kwenye mitandao kila uchao? Je, huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM? Nani anajua? Tuhitimishe: Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM ni matusi na kejeli kwa Watanzania. Inapingana na anayotuaminisha kila uchao Rais Jayaka Kikwete na mwenyekiti wa CCM. Hakika chama hicho kimegeuka chaka la ufisadi .

Je, kwa CCM hii ya mafisadi tutaweza kuushinda ufisadi na kuwaletea Watanzania maisha bora? Kama CCM inataka kurejea kwenye uchaguzi ujao, basi badala ya kuwasafisha mafisadi, ije na hoja ya kuwabana warejeshe pesa yetu na kushitakiwa kwa ufisadi.

Isiharibu ushahidi utokanao na kuwajibika kwao. Na kama kuna ndoto ya kumrudisha kwenye ulingo wa siasa yeyote kati ya wale tuliokwisha kuwatimua, ijulikane ni ndoto ya mchana.

mpayukaji@yahoo.com
 
nchi hii tunahitaji RAIS Dikteta ili kuweka mambo sawa la sivyo CCM inatupeleka kuzimu. tujipange kuwang'oa 2010 siyo mbali tunaomba vyama vya Upinzani vijiimarishe kipindi hiki ili kujenga imani zaidi kwa wale wanchi wa vijijini wakati wa uchaguzi. hata kama kama watatuhonga na hizo fedha zao za kifisadi tuzile lakini tusiwachague.
 
Wabongo hatuaminiki,wakati wa kampeni tutashabikia upinzani ukija siku ya kura unashangaa mwenyewe, nitatoa mfano hai, ilikuwaje wakulima wa Mpanda Kati wakachagua Chadema, halafu Dsm yote tunakoishi wajanja/wasomi/watalaam/waelewa na vyo vyote utakavyo ita tukaipigia CCM au tukahongwa kirahisi ktk uchaguzi wa 2005 !!

Tusikate tamaa,tutashinda tuu.
 
Wabongo hatuaminiki,wakati wa kampeni tutashabikia upinzani ukija siku ya kura unashangaa mwenyewe, nitatoa mfano hai, ilikuwaje wakulima wa Mpanda Kati wakachagua Chadema, halafu Dsm yote tunakoishi wajanja/wasomi/watalaam/waelewa na vyo vyote utakavyo ita tukaipigia CCM au tukahongwa kirahisi ktk uchaguzi wa 2005 !!

Tusikate tamaa,tutashinda tuu.

Kweli Malila hapo umenipata kwelikweli. Si wasomi wa DSM tu, bali wasomi wote popote tulipo tujiulize ni wapi tunakolipeleka taifa hili? Hivi mjukuu wako akijauliza huko mbele kwamba "babu ulikuwa wapi wakati nchi inafanywa hivyo?" Utajibu nini?
Wasomi wa TZ tumekuwa wanafiki ati tunatetea kamhogo ketu. Hivi Nyerere angejifanya hivyo tungepata uhuru?
Tuamke, wakatii ni huu.
 
Wananchi wanahitaji elimu tu, na vile vile kwa kutegemea upinzani ni kupiga makelel ili KATIBA ya nchi ibadilishwe ,nafikiri kila mmoja wetu anawaona Vigogo vya CCM jinsi vinavobadilika sura ukivitajia suala la kubadilisha KATIBA ,ni jambo ambalo hawalipendi sio kulitekeleza bali hata kulisikia lile neno KATIBA ,kwao wao inakuwa kama unawagusa sehemu yenye donda ,ndio hapo Upinzani unahitaji kupagusa na kudidimiza kila siku bila ya kusita la si hivyo watabaki kuibua hoja na CCM kuekana kikao na kutuliza na kuondoka wakiwa wote salama baada ya kusafishana kama wanavyosema siku hizi, Upinzani ni lazima ujiweke upande wa wananchi likiwemo shinikizo la kususia vikao vya Bunge ,kama wanavyosema watakwamisha bajeti basi ionekane kweli wanaikwamisha bajeti.
CUF Zanzibar imeongeza nfuvu kwa kuwa wanapoamua kususia vikao vya Baraza la Soga au Uwakilishi basi hufanya kweli harudi mtu nyuma na anaerudi basi hugeuka jiwe na hivyo ndivyo inayotakikana katika Bunge la Muungano kwa wabunge wa Upinzani na sio maneno matupu na kurusha mate kama mvua za masika maana anaposema Mbunge wa upinzani basi aliekaribu hujikinga kwa kutumia makabrasha kwa jinsi mdomo unavyotoa cheche za mate.
Upinzani haujaonyesha madai ya kweli juu ya kuanzishwa KATIBA mpya katika mfumo wa vyama vingi ,na kama wamewahi kutamka basi hawajaiendelza hoja hiyo maana jambo hilo halimhusu mtu mmoja tu ambae husema bado haijafikia kuwa na muhimu wa KATIBA mpya.
Vyama vya upinzani vinatakiwa vione hii hali inayokwenda sasa ya ufisadi na jinsi inavyochezewa na viongozi wa CCM kana kwamba nchi hii ni yao na wanafanya na kuamua pale wanapopenda wao.
Polisi hana nguvu ya kuwakama ,takururu hawana ubavu wa kuwahoji,mahakama haina nguvu ya kuwahukumu imekuwa wao CCM wapo juu ya sheria za nchi hii,si mkubwa si mdogo ,tumesikia mahakama zikisema kesi zao hazina mkubwa au mdogo lakini sio kweli kesi zinaonekana na watu wanaona na kusikia na hukumu zinaonekana kama wewe ni CCM maarufu basi utapeta tu.
Yote adhabu hii anayopata Mtanzania wa hali ya chini au asiekuwa katika mstari wa top CCM basi matatiz ya KATIBA ambayo inahitaji kufanyiwa ukarabati wa nguvu. Haya shime vyama vya upinzani kuwashawishi wananchi waingie katika mkakati wa kuunda KATIBA mpya ,niliwahi kusikia wakitangaza sijui kama ni wao au ni mtu mmoja ambae atatangaza na kufikisha Bungeni MGOGORO wa KATIBA ,sijui ameishia wapi.
WaKENYA walidai na kutangaza mgogoro wa KATIBA kwa kiasi fulani wamefanikiwa na uungwaji mkono umeonekana na wanaci wameupokea na leo Kenya utaona KATIBA yao inafanya kazi na wengi wa walioko katika vyombo vya serikali wanaiogopa na mtu huwa anasema kweli tu japo ukweli haufuatwi lakini anaepuka kuja kubanwa na KATIBA .
 
Elimu itolewe kwa uhakika, siyo elimu ya chuki kama sasa hivi, manake watu hawan principles wanakomelea tu mtu yeyote ambaye wanamchukia.
Mfano wakati Dr slaa anawakilisha hoja ya wizi bot, epa ilikuwa agenda mojawapo tu, lakini kwakuwa zimepata moto, basi hao ndio kafara,
lakini laiti pesa yote iliyopotea ingetafutwa, (YOTE) bila kujali kampuni hii ni yangu au yako au ya Rostam aziz, tungefika mbali tena bila kurudi nyuma, sasa tunashambulia watu,
tuache tuanze kushambulia maovu,
wako wengi tu ambao sijui wanawalipa waandishi wa habari au kwa kuwa wamejirekebisha, basi hawasemwi ovyo.
tushambulie maovu yote kwa juhudi zote, tusioneane aibu, najua wengi watakumbwa ila tunaweza kuweka margin kuwa kuanzia sh fulani adhabu ni hii na chini ya hapo ni warning na constant monitorship.
au kukatiwa leseni
bila kujali nani atakumbwa na fagio.
sasa hivi wanasema wanaonewa kwani wanajua wenzao ambao yao hayaandikwi kila siku.
 
Chenge azidi kuwa lulu CCM

2008-11-11 10:24:03
Na Midraji Ibrahim, Dodoma

Licha ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kujiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada huku akichunguzwa na makachero wa Ofisi ya makosa makubwa ya jinai (SFO) ya Uingereza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kumwamini na kumpa majukumu mazito.

Hivi karibuni CCM ilimteua Chenge pamoja na makada wengine wawili CCM, Dk Abdallah Kigoda na Pindi Chana kusaidia kuboresha mkataba wa jengo jipya la Umoja wa Vijana, hatua iliyopigiwa kelele na wananchi.

Pamoja na kelele hizo, juzi Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliunda tume ya kupitia mapendekezo ya jinsi ya kupata uwakilishi wa wanawake asilimia 50 ya wabunge na Chenge ni miongoni mwa wajumbe wa kamati ya watu tisa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, alisema kamati hiyo itaangalia jinsi ya kutekeleza mapendekezo hayo na kuwasilisha taarifa yake baada ya mwezi mmoja.

Kamati hiyo inaundwa na Waziri Kiongozi mstaafu, Dk Gharib Bilal, Makamu Mwenyekiti ni Naibu Spika, Anne Makinda, Dk Maua Daftari, William Lukuvi, Machano Othman, Mtumwa Kassim Iddi, Dk Makongoro Mahanga, Jenister Mhagama na Chenge a.k.a mzee wa vijisenti.

Chiligati alisema pendekezo la kwanza ni kuundwa kwa majimbo mapya ambayo yatakuwa wilaya. Hivi sasa kuna wilaya 117 na Zanzibar ina wilaya 10; kila itatoa wabunge wawili.

Pendekezo lingine ni jinsi ya kuunganisha majimbo yaliyopo na kila jimbo liwe na mwanamke na mwanaume, ili idadi ya wabunge wasizidi 360 kwa sababu, serikali haitajenga ukumbi mwingine wa Bunge.

Pia, kamati hiyo inatakiwa kuangalia utekelezaji wa mfumo wa uwiano na kwamba, hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya CCM na azimio la Umoja wa Afrika la kuhakikisha wanawake wanakuwa idadi sawa na wanaume bungeni.

Katika hatua nyingine, CCM kimeitaka serikali kuharakisha marekebisho ya sheria ya maadili ya viongozi kutokana na kukiri kwamba uchaguzi wa chama hicho umejaa faulo nyingi.

Pia, imeitaka serikali kutunga sheria ya matumizi ya fedha katika kampeni ili kuweka ukomo wa kiasi ambacho mgombea atatumia katika mchakato wa uchaguzi.

Chiligati pia alisema NEC imeagiza wagombea wa nafasi mbalimbali wa chama hicho kujaza fomu za upekuzi.

�Kwenye chaguzi zetu faulo zimekuwa nyingi, hivyo tumetaka kamati za maadili ziwe macho, hatua zichukuliwe bila huruma.

Huruma imeharibu chama chetu,`` alisema Chiligati na kuongeza: ``Kamati za uchujaji ziwe makini bila upendeleo au kukomoana. Haki tu itendeke wagombea watajaza fomu maalum za upekuzi.``

Alisema NEC imetoa onyo kwa wagombea watakaotumia rushwa, ukabila, hila, lugha chafu na kupakana matope kwamba watachukuliwa hatua za nidhamu au kuondolewa kwenye kinyang`anyiro.

SOURCE: Nipashe
 
Back
Top Bottom