NEC huru ndiyo ‘mwarobaini’ wa vurugu katika chaguzi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

NEC huru ndiyo ‘mwarobaini’ wa vurugu katika chaguzi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Oct 4, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Oct 4, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  [h=2][/h]Alhamisi, Octoba 04, 2012 05:21 Na Alexander Joseph
  [​IMG][​IMG][​IMG]

  HIVI karibuni, maofisa kadhaa wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), walizuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) jijini Dar es Salaam ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayisaidia MEC kuufanya Uchaguzi Mkuu wa Nchi hiyo wa mwaka 2014 kuwa bora zaidi.

  Kamishna wa MEC, Gloria Chingota aliyeongoza msafara uliokuja Tanzania anasema, yapo mambo ya kujifunza kutoka katika Tume yake yatakayozifanya chaguzi mbalimbali nchini Tanzania kuwa huru na haki zaidi.

  Miongoni mwa mambo aliyosema kuwa NEC (Tanzania) inaweza kujifunza toka MEC (Malawi) kuwa ni pamoja na namna ya kupata viongozi wa Tume na hasa makamishna tofauti na hali ya sasa nchini ambapo makamishna (wajumbe wa tume) wanateuliwa na Rais.

  “Kule kwetu vyama vya siasa hupendekeza majina ya makamishna kisha rais huyapitisha. Ni mwenyekiti tu, ndiye huteuliwa na Rais, lakini wengine hupendekezwa na vyama na siyo lazima wawe wanasheria, wapo hata viongozi wa dini,” anasema Chingota.

  Alikwenda mbali na kujigamba kuwa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), iko huru kiasi cha kutosha kuendesha chaguzi zilizo huru na za haki na akaongeza kuwa, kuna makamishna 10 walioteuliwa Mei 12, mwaka huu, hivyo wameamua kuja Tanzania kujifunza baadhi ya mambo katika NEC.

  Akasema, “Tume hii ina uhuru wa kutosha. Katika mazingira ya mfumo wa vyama vingi vya siasa… Baada ya mabadiliko ya Katiba 1993, MEC imesimamia chaguzi nne ambazo zilifanyika mwaka 1994, 1999, 2004 na 2009…,” anasema Chingota.

  Mambo mengine ambayo MEC ilikusudia kujifunza Tanzania ni uhusiano kati ya Tume na wadau kama vile vyama vya siasa na wagombea wake na vyama vya kiraia na elimu ya mpiga kura.

  Mengine ni utunzaji wa rasilimali za Tume na upigaji kura ambapo wanajifunza namna nzuri zaidi ya kuajiri wafanyakazi, kuwapa rasilimali, mafunzo, masilahi, usafiri na ulinzi na kwa upande mwingine, kuangalia muda wa kutoa matokeo.

  Itakumbukwa kuwa, kwa muda mrefu Tanzania kumekuwa na malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wengine wa siasa juu ya uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokana na muundo wake katika kusimamia chaguzi nchini.

  Nchini Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaundwa na makamishna saba wakiongozwa na Mwenyekiti, Mwakamu Mwenyekiti na Mkurugenzi. Watu hawa wote huteuliwa na Rais.

  Historia ya Tanzania inaonyesha kuwa, rais huyo ndiye wakati huo huwa Mwenyekiti wa Chama Tawala (CCM) ambaye wakati mwingine miongoni mwa wagombea wanaoshindana na wagombea wa vyama vingine.

  Hapa, ndipo kuna kiini cha malalamiko dhidi ya NEC yanayotokana na mamlaka inayowateua watendaji hao wakuu wa Tume.

  Kimsingi, Watanzania wengi wanaamini hivyo na hii ndiyo hali halisi inayoifanya Tume hiyo kukosa uhuru hasa kwa kuwa wateule hao wa Rais hulazimika kufuata amri za “Mwenye mpira ambaye naye ni mchezaji anayeweza kuchukua mpira wake na kuuweka kwapani kama kuna jambo lisilomfurahisha hata kama ni la kweli na haki.”

  Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamishna wa Tume hiyo inayoundwa chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977, hufanyakazi kwa kipindi cha miaka mitano.

  Tume ndiyo chombo chenye mamlaka ya mwisho katika masuala ya uchaguzi nchini ambayo haiingiliwi na mtu, chama au Serikali katika kufanya shughuli zake na nchini Tanzania, baada ya Tume kutangaza matokeo ya Urais, hakuna mwenye haki ya kuhoji au kupinga hataka kama “giza limeonekana.”

  Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa NEC Jaji Damian Lubuva amekiri kuwepo kwa changamoto nyingi katika Tume hiyo ingawa amesisitiza kuwa, bado NEC iko huru na inatenda haki sawa kwa washiriki wote katika chaguzi.

  Kadhalika, amekiri kuwapo malalamiko hasa kwa kuwa viongozi wa Tume hiyo huteuliwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Tawala ambacho ni CCM.

  “Yapo malalamiko mengi ya kutokuridhishwa na muundo huu kutoka kwa vyama vya siasa na wanaharakati wa kiraia kuwa tume hii siyo huru. Huo ni utaratibu wa kikatiba. Utaratibu huo utaendelea hadi hapo Katiba itakapobadilishwa katika mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea.”

  “Hatukatai mabadiliko, kama wananchi hawaridhishwi, watoe maoni kwenye mchakato wa Katiba ili ibadilishwe. Kama nilivyosema awali kwamba, uhuru wa Tume katika utendaji kazi wake unalindwa na ibara ya 74(7) na 11 ya Katiba. Hadi sasa Tume haijapata maelekezo au maagizo kutoka Serikalini au kwa mtu yoyote mwenye mamlaka. Inafanya kazi kwa uhuru,” anasema Jaji Lubuva.

  Ametaja changamoto nyingine zinazoikabili Tume hiyo kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, usimamizi wa uchaguzi, usajili wa wapiga kura, elimu ya wapifa kura, upitiaji upya wa daftari la kudumu la wapiga kura, miundombinu, mawasiliano na teknolojia hafifu na watu wachache kujitokeza katika uchaguzi.

  Baada ya utangulizi huo mrefu kwa kadiri hiyo, sasa tukumbuke kuwa katika chaguzi ndogo za miezi ya hivi karibuni katika majimbo ya Igunga na Arumeru Mashariki, pamoja na matukio mengine ya harakati za kisiasa katika mikoa kadhaa nchini ikiwamo ya Morogoro na Iringa, shughuli hizo ziligubikwa na vurugu zilizoishia katika umwagaji damu na vifo.

  Kama ilivyotokea hivi majuzi katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Bububu Visiwani Zanzibar, vurugu, majeruhi, umwagaji damu na harakati za hofu, ni mapato ya ugonjwa sugu miongoni mwa Watanzania wa kutoaminiana baina ya vyama vya CCM na vingine vya upinzani, na imani haba dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vya dola.

  Muundo wa Tume ya Uchaguzi unastawisha ukosefu wa imani juu ya Tume hiyo.

  Uchaguzi Mdogo wa Bububu kumtafuta Mwakilishi wa Jimbo hilo licha ya kumalizika na kumpa ushindi Hussein Ibrahim Makungu wa CCM kwa kura 3,371 dhidi ya kura 3,204 alizopata Issa Khamis Issa wa CUF, ulikumbwa na vurugu zilizosababisha kukamtwa baadhi ya watu na Jeshi la Polisi akiwamo Mbunge wa Jimbo la Mtoni, Faki Haji Makame..

  Uchaguzi huo ulivishirikisha vyama vingine vya NCCR-Mageuzi, NRA, SAU, Jahazi Asilia, Tadea, AFC na ADC vilivyonyang’anyana kura 71 zilizosalia kati ya kura 6,646 zilizopigwa.

  Vurugu hizo zilitokea kabla Tume ya Uchaguzi Visiwani humo (ZEC) haijatangaza matokeo baada ya watu waliodhaniwa kuwa wafuasi wa CUF, kutamka na kudai kwamba CCM kilikuwa kimeingiza mamluki jimboni humo ili wakipigie kura.

  Kutoaminiana kiasi cha vyama vya siasa vyenyewe kutiliana shaka, kunakwenda mbali na kufikia vyama kutoamini utendaji wa Tume (NEC) kiasi kwamba, mara nyingi utendaji wake unatiliwa shaka na baadhi ya vyama, huu ni ugonjwa “unaopaswa kutibiwa” mapema.

  Pamoja na mambo mengi, matibabu hayo yanaweza kupatikana kwa kubadili muundo na mfumo wa utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Katiba mpya ijayo.

  Kwa msingi huo, ili kutibu na kukomesha manung’uniko mintarafu umma kukosa imani kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni vyema Watanzania wote wenye sifa, kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwa dhati katika kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana Katiba mpya itakayobadili mfumo wa upatikanaji wa makamisha na watendaji wengine wa Tume ili kila mmoja aiamini kiasi kwamba, chama au mtu anayeshiriki uchaguzi, anaposhindwa, asisingizie udhaifu wa Tume maana siku zote mbaazi akikosa maua, husingizia jua.

  Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, ndiyo mwarobaini wa vurugu zitokanazo na chaguzi nchini Tanzania.

  MUNGU IBARIKI TANZANIA.

   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Oct 4, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145

  Kwanini VIONGOZI WA TUME YA UCHAGUZI ni Wale WASTAAFU kina DAMIEN LUBUVA...
  CHAGUENI VIJANA ambao bado Damu ni Changamfu na bado Wanataka AJIRA ZAO; LUBUVA kaisha SHIBA
  WATOTO WAMESOMESHWA na Serikali ya CCM Nje ya NCHI; Kajenga Mahekalu kwa Msaada wa Serikali ya CCM Lini atakuwa FAIR and SQUARE? MPE KIJANA ndio ajira yake ya kwanza sio Mchezo hapo...
   
Loading...