"Ndugu yako yuko wapi? Damu yake inanililia udongoni"

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,337
51,855
"NDUGU YAKO YUKO WAPI? DAMU YAKE INANILILIA UDONGONI"

Kwa Mkono wa, Robert Heriel.

Leo katika pita pita zangu kwenye kitabu cha Biblia, nilianza kusoma kitabu cha mwanzo sura ya 1, 2, 3 nilipofika sura ya 4 nikashangaa akili yangu ikipata fikra mbalimbali. Nikashangaa nikimkumbuka Ben Saanane, Azory Gwanda, na wengineo waliopotea wasijulikane walipo, hata hivyo sura hiyo inaelezea tukio baya la kikatili la mauaji yaliyofanywa na KAINI ambapo alimuua ndugu yake Abel. Umaarufu wa tukio hili umejijenga kutokana na kuwa ndilo tukia la kwanza la mauaji lililofanywa na binadamu ambapo Kaini anakuwa mtu wa kwanza kufanya uuaji na kumsababishia ndugu yake kuwa mtu wa kwanza kuonja uchungu wa Mauti.

Akili yangu inanambia kuwa, Kaini kabla hajamuua Abel ndugu yake, alimfanya Mateka, alimteka kijanja bila ya Abel kujua. Unajua utekaji upo wa aina nyingi, moja wapo ni utekaji rahisi wa kirafiki ambapo mtekaji hujifanya rafiki kwa mateka wake kisha akishampeleka kwenye mazingira mazuri humgeuka na kumuangamiza. Hiki ndicho alichokifanya Kaini, Mtekaji na muuaji wa kwanza katika historia ya dunia kwa mujibu wa Biblia.

Utawala uliokuwa madarakani kipindi hicho ulikuwa utawala wa Mungu mwenyewe ambapo yeye ndiye alikuwa mfalme mwenye kutoa sheria na kutoa oda zote. Mungu kama mtawala, aliona atekeleze wajibu wake wa kuhakikisha viumbe wake wapo wote salama lakini kwa bahati nzuri au mbaya Hamuoni mtu mmoja, ndiye Abel, hapo akaamua kumuuliza Kaini; Ndugu yako Abel yupo wapi. Kaini akajibu, mimi sijui, kisha akamuuliza Mungu, je mimi ni mlinzi wa Ndugu yangu? Mungu akijua alichofanya Kaini akamuambia; Damu ya ndugu yako inanililia udongoni.

Kwa wapenzi wa kusoma, Mwanzo 4:
8. Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua.
9. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10. Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni.
11. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua.

Kisa hiki ukiendelea kusoma kinaonyesha jinsi Mungu alivyoumizwa na Mauaji yaliyofanywa na Kaini dhidi ya ndugu yake. Mungu kwa hasira alimpa laana Kaini na kulaana ardhi, na kumfanya awe mtu wa kuweweseka mwenye kutanga tanga.

Kisa hiki kinatupa somo kubwa mno katika nyakati zetu. Wapo ndugu zetu, rafiki, na jamaa ambao waliuawa au kupotea ambao mpaka leo kiza ni kinene haijulikani nini kilitokea, na hiyo haijulikani kwetu tuu lakini kwa Mungu anajua watu hao wako wapi, na kama waliuawa waliuawa na kina nani.

Swali hili nila kila mtu, Mungu anatuuliza ndugu zetu wako wapi?
Ikiwa wewe ndiye uliyeua au kufanya maasi,, Mungu anakuuliza, ndugu yako yupo wapi?

Mwisho kabisa Mungu anakuambia kuwa "Damu ya ndugu yako" uliyemuua inamlilia na bila shaka atakujibu kwa wakati wako.

Wewe kiongozi wa jeshi la polisi, Mungu anakuuliza ndugu zako wako wapi? Kwani damu zao zinamlilia Mungu.
Wewe Waziri mwenye dhamana na masuala ya ulinzi, Mungu anakuuliza, Ndugu zako wako wapi? Kwani damu zao zinamlilia Mungu.
Mhe. Rais uliyeingia utawalani, swali hili pia linakuhusu. Lazima uchunguzi ufanyike kama kweli mnayodhamiri ya kweli ya kumjibu Mungu swali hilo, kisha mtende haki na hukumu kwa waliotenda.

Lakini kama mtanyamaza na kupiga kimya ni sawa na majibu ya Kaini alivyo jibu kuwa yeye sio mlinzi wa ndugu yake.

Tupendane, tutende haki.

Ulikuwa nami, mwana wa Tibeli, nyota yenye mbawa mbili irukayo.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Njombe
 
Hawatakujibu, lakini wakumbuke siku ya hukumu kila mtu atatoa hesabu yake mwenyewe. Na kama hilo ni mbali, hukumu ya mtu ni hapa hapa duniani, directly or indirectly.
 
Back
Top Bottom