Ndiyo, tuwazomee mpaka wakose raha

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Ndiyo, tuwazomee mpaka wakose raha

Johnson Mbwambo Mei 7, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

WIKI iliyopita kuna kitu kilichotokea mjini Dar es Salaam ambacho kilinifariji mno; nacho ni kuzomewa na wananchi kwa waziri mmoja wa zamani ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wakubwa wa ufisadi.

Habari zinasema kwamba waziri huyo, ambaye alijiuzulu uwaziri kwa sababu ya kuhusishwa na tuhuma hizo za ufisadi, alikuwa akiingia katika tawi moja la benki jijini, lakini kabla hajafanya hivyo wananchi wakamtambua na kuanza kumzomea.

Kelele za “fisadi huyo… fisadi huyoo” zilipozidi, waziri huyo wa zamani alilazimika kugeuka haraka na kwenda kuingia katika gari lake na kuondoka katika eneo hilo. Habari nyingine zinasema mtoto wa waziri mwingine anayetuhumiwa kwa ufisadi; naye alilazimika kufanya hivyo hivyo alipozomewa wakati akitaka kuingia katika supamaketi moja jijini.

Kwa hakika, taarifa katika mtandao pia zinaeleza habari za mtoto mmoja wa waziri wa zamani anayetuhumiwa kwa ufisadi anayesoma Marekani ambaye naye amenyong’onyea mno baada ya baba yake kukumbwa na kashfa hiyo, na hatimaye kulazimika kujiuzulu uwaziri.

Inadaiwa kwamba kabla ya hapo mtoto huyo, anayesoma katika chuo kikuu ghali, alikuwa akiwakoga, kwa matanuzi, wanafunzi wenzake wanaosoma katika vyuo vingine vya Marekani. Mara kwa mara alikuwa akisafiri kati ya Marekani na Uingereza kwa first class; huku nguo zake zote akizinunua katika maduka ya bei mbaya.

Lakini tangu baba yake akumbwe na kashfa hiyo, wanafunzi wenzake wamekuwa wakimtumia sms na ujumbe wa intaneti wa kumkejeli; huku wakimkumbusha kwamba kumbe matanuzi yake yote yalitokana na pesa ambazo baba yake alikuwa akiwaibia wakulima na wafanyakazi masikini wa Tanzania!

Yawezekana mtoto huyo hakuwa anajua hivyo (kwamba pesa zilikwibwa), na ndiyo sababu hivi sasa amenyong’onyea kupita kiasi. Ni dhahiri kwamba, pamoja na kuwa ameshayaacha matanuzi na majigambo hayo; bado nafsi yake itaendelea kumsuta (haunted) kwa kosa (la kuwaibia masikini) ambalo kimsingi lilifanywa na baba yake.

Nafahamu kwamba wapo wachache watakaonituhumu kuwa mimi ni sadist, lakini nataka nisisitize kwamba matukio hayo ya kuzomewa yamenifariji kwa sababu moja kubwa tu; nayo ni kwamba yanatuma ujumbe kwa mafisadi wote na wengine wote wenye nia ya kuichagua njia hiyo ya maisha, kwamba mwisho wao si mwema.

Watakaonituhumu u-sadist sijui fikra zao ni zipi inapotokea mkulima masikini wa kijiji cha wilaya kama ya Same ‘anawindwa’ na mgambo kwa sababu tu hajatoa mchango wa kujenga sekondari! Je, mapesa yanayochotwa na mafisadi wa aina ya waziri huyo, kama yale ya EPA, si yangetosha kujenga sekondari hizo bila kulazimika kumchangisha mkulima huyo masikini?

Watakaonituhumu hivyo sijui fikra zao ni zipi wanapoambiwa kuwa mtoto wa waziri fulani anasafiri kila mara, kati ya New York na London, kwa tiketi za first class, lakini chanzo cha ukwasi huo ni mapesa ambayo baba yake anayapata kifisadi serikalini katika nchi masikini kama yetu ambayo bado raia wanasafiria malori!

Kwa hiyo, kwa mtazamo wangu, kuzomewa au kusakamwa ni bei ndogo tu wanayolipa kwa ulafi wao wa pesa wa kupindukia; ulafi ambao Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Kenya, Sir Edward Clay aliuelezea kwa kauli ile maarufu ya “wanakula kwa ulafi na kisha wanatapikia miguu ya wafadhili”. Pengine tofauti tu ni kwamba hawa wa kwetu Tanzania wakishavimbiwa hutapikia si tu miguu ya wahisani; bali pia ya walalahoi (kauli za visenti).

Kwa ufupi, ninachojaribu kueleza ni kwamba ni jukumu letu sote, raia wema, kukataa kuukubali ufisadi kuwa ni sehemu ya utamaduni wa maisha yetu; maana tukiukubali, basi, tutakuwa tumekaribisha umwagaji damu nchini mwetu; kwavile penye ufisadi wa kupindukia hakuna haki na pasipo na haki, damu (hatimaye) humwagika.

Yapo mambo mengi tunayoweza kuyafanya kuuzuia ufisadi usiwe sehemu ya maisha yetu, na moja ya hayo ni kumchukia fisadi kama vile tunavyomchukia shetani. Katika hali hiyo, kumzomea fisadi ni kuonyesha hisia zetu za jinsi tunavyouchukia uovu huo.

Mwisho wa yote, hakuna familia itakayoona fahari kuwa na fisadi miongoni mwao, hata kama fisadi huyo atakuwa na mapesa kiasi gani, kwa sababu ufisadi ni ushetani.

Kama kweli tunalitakia taifa letu mema, basi, hizo ndizo fikra tunazopaswa kuzipandikiza katika bongo za wanetu kungali mapema. Tukichelewa, utamaduni huu wa kuuenzi ufisadi utakita katika bongo za wanetu, na hilo litakuwa jambo la hatari mno kwa Tanzania ya kesho.

Majuzi hapa nilishuhudia vijana kadhaa wakiuenzi ufisadi kwa namna ambayo wao wenyewe hawakuwa wakifahamu uzito wa ubaya wa tendo lao. Vijana hao walikuwa wamekusanyika katika tawi la Azikiwe la Benki ya CRDB, mjini Dar es Salaam, wakiwa na fomu za maombi ya kusomeshwa za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Kimsingi, mikopo hiyo hutolewa kwa wanafunzi waliopo katika mazingira fulani fulani ikiwa ni pamoja na wale ambao ni yatima, na katika fomu hizo kuna sehemu wanapaswa kuthibitisha kwamba kweli wao ni yatima.

Katika mazungumzo yao, vijana hao walikuwa wakibadilishana mawazo ya jinsi walivyodanganya kuthibitisha kwamba wao ni yatima. Baadhi yao wakawa wanajisifu jinsi walivyowahonga viongozi wa serikali za mitaa ili wathibitishe katika fomu hizo u-yatima wao. Ni dhahiri waliufanya ufisadi huu kwa kushirikiana na wazazi wao!

Hebu fikiria, mpenzi msomaji, wazazi ‘wanajiua’ na wanawashirikisha vijana wao katika ufisadi huo ili tu wapate mkopo wa kusomeshwa chuo kikuu!

Hebu fikiria, kijana ‘anayeua’ wazazi na kujiita yatima wakati si yatima - kijana anayeshirikiana na baba yake kumhonga kiongozi wa serikali ya mtaa ili athibitishe u-yatima huo, akimaliza chuo kikuu na kuajiriwa atakuwa mwadilifu kiasi gani?

Nauliza hivyo; maana huyu tayari alishafundishwa ufisadi tangu akiwa kijana mdogo kabisa. Waingereza wanasema old habits die hard.

Kwa wale waliopata kusoma kitabu cha Rais Museveni kinachoitwa Sowing the Mustard Seed, wataelewa ninachokizungumza au ninachojaribu kutahadharisha katika mfano wangu huo wa vijana wanaojiandaa kuingia chuo kikuu.

Katika kitabu hicho ambacho Rais Museveni anaelezea harakati zake za ukombozi, kuna mahali ameandika katika hali ya kujisifu namna alivyokuwa akiwahonga polisi wa mjini Kisumu pesa na ndizi za Uganda (bogoya) ili wamruhusu yeye na makamanda wake kupitisha silaha kuziingiza Uganda.

Hata kama Museveni alilazimika kufanya hivyo katika mazingira yale ya mwaka 1981-83 ya harakati za ukombozi, bado alilolifanya ni tendo ovu (la kifisadi) ambalo hakustahili hata kulirekodi katika kitabu chake hicho; achilia mbali ukweli kwamba alilielezea tukio hilo kwa namna ya kujisifu; kana kwamba kuwahonga polisi wa nchi nyingine ni jambo jema kwa rais mtarajiwa.

Ndiyo maana sikushangaa, mwaka juzi, iliporipotiwa, mjini Kampala, kwamba Rais Museveni aliwaita wabunge wote katika hoteli ya kitalii ya Sheraton na kuwapa bahasha za kaki zenye mapesa kibao ili wapitishe muswada bungeni wa yeye kuendelea tena kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula mwingine!

Kwa mfano huo wa Museveni, ni dhahiri tabia za kale hazifi haraka, na ndiyo maana nasisitiza kwamba ni jukumu la raia wema wote kufanya lolote lile wanaloweza kuwaepusha wanetu na utamaduni huu mwovu wa kuuenzi ufisadi.

Na moja ya njia za kufanya hivyo, ni sisi kuendelea kuwatenga na kuwazomea mafisadi popote pale walipo; ili wanetu waone na waishi wakijua vichwani mwao kwamba ufisadi ni ushetani.

Tafakari.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
Haya jamani, RPC anasema hakuna aliyemzomea Mkapa, Kulikoni na THISDAY wanakuja na hii.....

www.thisday.co.tz/news/3942.html

Polisi wasaka vijana
waliomzomea Mkapa

• Watano mbaroni kwa kumwita fisadi
• RPC akana, asema ni msako wa kawaida

MWANDISHI WETU
Dar es Salaam

WATU watano wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kmzomea na kumtukana kwa kumwita fisadi Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Habari za uhakika kutoka polisi zinaeleza kwamba watu hao walikamatwa eneo la Masaki na kufikishwa kituo cha polisi cha Oysterbay Dar es Salaam na kudhaminiwa juzi.

Kwa mujibu wa habari hizo, waliokamatwa wote kwa pamoja walidaiwa, "kutumia lugha ya matusi, kumkashifu kiongozi mstaafu, kwa kumzomea na kumwita fisadi na matusi mengine."

Pamoja na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, kukanusha kufahamu kuhusu kukamatwa kwa watu waliomzomea Mkapa, habari zimethibitisha kukamatwa watu hao.

Waliokamatwa wametajwa kwa majina ya Ayubu Masoud, Kagungi Shukuru, Hassan Ramadhani, Juma Rashid na Peter Steven, wote wakiwa wakazi wa Masaki na Msasani wilayani Kinondoni.

Uchunguzi wetu umebaini kwamba watuhumiwa hao walikamatwa na kuwekwa mahabusu na kuingizwa katika Daftari la polisi namba OB/RB/8201/2008 ikieleza bayana kwamba wanatuhumiwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya kiongozi mstaafu.

Maelezo ya kukamatwa kwao yamekwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba katika kutenda kosa hilo, "walimzomea na kumwita fisadi" kiongozi huyo mstaafu akiwa katika msafara wake.

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, Kamanda Rwambow alipinga maelezo hayo na kudai kwamba hakuna kesi kama hiyo wala taarifa zinazofanana na hizo.

"Katika taarifa zangu sina kesi yoyote ambayo watu wanashikiliwa kwa kosa la kumzomea kiongozi yeyote wala kukashifu…na kama taarifa hizo unazo wewe naomba niletee nitazifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu zetu," alisema Kamanda Rwambow.

Alisema polisi Kinondoni wamekuwa wakiendelea na misako ya kawaida ya kuwatafuta na kuwafikisha mahakamani vijana ambao wamekuwa wakizurura na kushinda vijiweni huku wakijihusisha na uvutaji bangi na kuwafikisha Mahakamani.

"Hivi karibuni tuliwakamata vijana kadhaa eneo la Masaki Mwisho ambao walikutwa wamekaa kijiweni na wengine kujihusisha na uvutaji wa bangi, walifikishwa mahakamani na waliopatikana na hatia walichukuliwa hatua na wengine ambao hawakuwa na hatia waliachiwa," alisema.

Vijana waliokamatwa Jumatatu jioni walikutwa maeneo ya Masaki Mwisho karibu na kituo cha daladala cha Masaki ambapo vijana hao huwa na kawaida ya kukaa nyakati za jioni.

Hata hivyo, polisi walifanikiwa kuwakamata vijana watano tu kati yao na wengine walifanikiwa kukimbia walipoona polisi.

Mkapa aliyeingia madarakani mwaka 1995 kwa jina la ‘Mr. Clean' akipigiwa debe na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, amebainika kubadilika na kuanza kuwa ‘mjasiriamali' katika kipindi cha pili cha uongozi wake 2000-2005. Katika kipindi hicho Mwalimu Nyerere alikuwa amekwishaaga dunia.

Tuhuma dhidi ya Mkapa zimekwenda mbali kiasi cha kubainika kwamba yeye na familia yake walianzisha kampuni iitwayo ANBEM kwa kutumia anuani ya majengo ya Ikulu, mtaa wa Luthuli, namba 15, na baadaye kutumia kampuni hiyo kujipatia fedha kutoka Benki ya NBC Limited na CRDB Limited.

Baada ya kuanzisha kampuni yao, Mkapa na familia yake akishirikiana na familia ya aliyekuwa Waziri wake wa muda mrefu, Daniel Yona, walinunua mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira kutoka serikalini na kujitwalia mradi mwingine wa Kabulo kabla ya kuingia mkataba wa kuzalisha umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Hivi karibuni, tuhuma za Mkapa zimeingia Bungeni baada ya Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, kutaka uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya rais huyo mstaafu na waziri wake kuhusiana na mradi wa Kiwira walioununua kwa milioni 70/- pamoja na makubaliano ya milioni 700/- ambazo nazo zinaeleza kuwa ndogo kulingana na thamani halisi ya mradi.


Source: KULIKONI Namba 325, Alhamisi Mei 8, 2008
 
Ndiyo, tuwazomee mpaka wakose raha

Johnson Mbwambo Mei 7, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

....

Inadaiwa kwamba kabla ya hapo mtoto huyo, anayesoma katika chuo kikuu ghali, alikuwa akiwakoga, kwa matanuzi, wanafunzi wenzake wanaosoma katika vyuo vingine vya Marekani. Mara kwa mara alikuwa akisafiri kati ya Marekani na Uingereza kwa first class; huku nguo zake zote akizinunua katika maduka ya bei mbaya.

Lakini tangu baba yake akumbwe na kashfa hiyo, wanafunzi wenzake wamekuwa wakimtumia sms na ujumbe wa intaneti wa kumkejeli; huku wakimkumbusha kwamba kumbe matanuzi yake yote yalitokana na pesa ambazo baba yake alikuwa akiwaibia wakulima na wafanyakazi masikini wa Tanzania!

Yawezekana mtoto huyo hakuwa anajua hivyo (kwamba pesa zilikwibwa), na ndiyo sababu hivi sasa amenyong’onyea kupita kiasi. Ni dhahiri kwamba, pamoja na kuwa ameshayaacha matanuzi na majigambo hayo; bado nafsi yake itaendelea kumsuta (haunted) kwa kosa (la kuwaibia masikini) ambalo kimsingi lilifanywa na baba yake.

.....


Tafakari.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com

Na bado,

wewe mtoto wa fisadi ujiandae kwa shaming the devil party inayoandaliwa karibuni karibu kabisa na unakoishi ili ukome kulinga na pesa za ufisadi.

Niliapa kuwa nitafuatilia mafisadi na familia zao ili wakose usingizi na sasa yameanza kutimia.
 
Hii ndiyo hatari inayotukabili hapo mbeleni kwani nchi inakuwa na matabaka (Tabaka la wananchi na lingine la mafisadi). Wananchi wameanza kwa kuwazomea wanaowaona kwamba wanahusika kwa ufisadi, huu ni mwanzo. Inaweza ikifikia hatua ya kuwarushia mawe au kuwadhuru kwa namna yeyote.

HOJA ni vipi wananchi wataweza kumtambua fisadi na asiye fisadi?

Rai yangu, ni vema Mhe. Rais akachukua jitihada za makusudi na zilizowazi za kuuchukia na kuushughulikia ufisadi kabla hatujafikia hali mbaya zaidi. Kwasasa mimi sijaona kama Rais anachukia ufisadi, ila anaona kuwa ni sehemu ya maisha yetu, which is totally wrong.
 
Mwafrika wa kike,Kuwazomea hakutoshi,kuna cha zaidi cha kufanya ili kuwamaliza kabisa..nenda kasome thread yangu nani kawaloga Watanzania??Dawa ni hii hapa.nimeelezea nini kifanyike ili tupate ushindi wa 'kishindo'
 
Mwafrika wa kike,Kuwazomea hakutoshi,kuna cha zaidi cha kufanya ili kuwamaliza kabisa..nenda kasome thread yangu nani kawaloga Watanzania??Dawa ni hii hapa.nimeelezea nini kifanyike ili tupate ushindi wa 'kishindo'

Nimekusoma mkuu na bado natunza kumbukumbu maana umetoa shule ya nguvu pale.

Kwa sasa huyu mtoto wa fisadi lazima aandamwe na kuzomewa kama baba yake kwa ufisadi ambao amekuwa anaufurahia miaka yote hii.

hii "shaming the devil party" ni lazima ifanyike ili kuanza kazi kama wanigeria walivyowafanya watoto wa Abacha. Ndugu na watoto wa Abacha walikuwa wakizomewa na kutengwa na Wanageria kila mara walipojitokeza kwenye function huru zao hadi wakakoma ubishi!
 
Hivi ni mjamaa gani wa njozi yule aliyesema tukiwazomea Mabepari watabadilika? Mabepari wakauchuna tu na kuendelea kunyonya.

Tunaweza kujifurahisha kuwazomea Mafisadi ila sidhani kama itawafanya wabadilike.

Wanachohitaji ni kwenda Keko kwa muda mrefu. Kifungo tu ndio kitawatisha watu mpaka kuacha ufisadi.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom