Ndiyo maana nasema wanauza utu wao pamoja na miili yao, bora hata dada poa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ndiyo maana nasema wanauza utu wao pamoja na miili yao, bora hata dada poa

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by August, Oct 27, 2010.

 1. A

  August JF-Expert Member

  #1
  Oct 27, 2010
  Joined: Jun 18, 2007
  Messages: 4,509
  Likes Received: 723
  Trophy Points: 280

  Ndiyo maana nasema wanauza utu wao pamoja na miili yao, bora hata dada poa

  [​IMG]
  Hidaya ​
  Oktoba 20, 2010[​IMG]
  Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
  Uzitoni Street,
  Bongo.​
  Mpenzi Frank,
  WE kijana mwenzangu, mzima wewe? Ni matumaini yangu kuwa ni mzima bila wazimu ya vijana wenzetu.
  Yaani, unaonaje jinsi vijana wanavyotumiwa kwa wakati huu? Eti wanadanganywa washike mapanga kulinda wanaokaa kwenye maofisi yenye viyoyozi! Kwa vijisenti vichache wanauza utu wao hadi wako tayari kuumiza watu wengine ambao wala hawawafahamu. Kisha watarudishwa katika lindi lao la umasikini huku wale wanayoyoma na viyoyozi vyao.
  Ndipo hapo najiuliza tangu lini chama kiwe na walinzi wake wenyewe wakati Polisi wapo? Kama kweli chama chochote kinaheshimu demokrasia, iweje walipe watu wao kufanya fujo? Pamoja na kukasirika sana, naogopa mpenzi, hasa upande wako wewe usiye na dogo. Angalia wasikukatekate bila sababu tumaini la maisha yangu.
  Sitanii mpenzi. Juzi nilikuwa naenda sokoni kumbe jamaa wa chama fulani alikuwa na mkutano wake huko. Alivyojisifusifu kwamba yeye ni kiboko cha viboko, watu wakaanza kumzomea. Ghafla wakajitokeza watu waliovaa rangi ya chama na kuanza kuwafukuza watu na mapanga. Yaani! Wengine walijeruhiwa, wengine walikanyagana, ili mradi fujo tupu. Na wale vijana walikuwa wanacheka tu, kana kwamba wanafurahi kuwaumiza watu. Ndiyo maana nasema wanauza utu wao pamoja na miili yao, bora hata dada poa.
  Hata mimi ilibidi nikimbie mpenzi maana walikuwa wanatisha na hata kumpiga yeyote waliyemkuta mbele yao. Angalao nilifanikiwa kujificha pembeni mwa ghorofa fulani na bahati nzuri hawakuniona wakipita huku mapanga yao yakimeremeta na mengine yakiwa na alama nyekundu tayari.
  Kwa kweli nilikumbuka yote tuliyoangalia huko Kenya wakati wa uchaguzi wao. Ilitisha na nakumbuka bosi alivyokuwa anatamba kwamba hayo hayawezi kutokea kwetu kumbe sasa naangalia yakitokea laivu. Nani anataka hayo hapa petu?
  Baadaye niliwaona wakirudi huku wakichekacheka na kusema leo watapata donge nono kweli. Nilipoona wahalifu wote wamepita nami nikajitokeza ili niweze kurudi kwa Mama Bosi.
  Kumbe alibaki ‘mlinzi’ mmoja ambaye sijui alikuwa amepotezana vipi na wenzie. Nilitaka kukimbia tena, lakini nilishtuka vibaya sana. Kumbe kijana mwenyewe tulisoma naye darasa la saba akachaguliwa kwenda sekondari lakini ilibidi aache shule maana wazazi wake walishindwa karo. Hata wewe lazima unamkumbuka mpenzi, maana tulimpa jina la Karo Kero kutokana na alivyokuwa analalamikia maisha.
  ‘Jamani mbona nimejitahidi hivyo! Mbona nilikuwa wa kwanza darasani lakini hawa wengine sasa wataendelea kwa sababu wazazi wao walijidai masikini na kupewa msaada wakati walikuwa na uwezo. Ufisadi kila ngazi, kwa hiyo mimi mtoto wa masikini basi tena. Ah! Karo ni kero! Karo yatukosesha maisha bora. Nchi hii kweli ni ya wenye uwezo. Wenye akili hatutakiwi kabisa’
  Basi tulisikia alikuja Dar es Salaam kutafuta maisha. Kumbe maisha ndiyo hayo. Ikabidi nimwite.
  ‘Karo Kero, kweli ni wewe?’
  Akashika panga lake kwa nguvu tena hadi niliogopa lakini hatimaye alinitambua.
  ‘We Hidaya, unafanya nini hapa?’
  ‘Si nimekuja sokoni kununua vitu jamani!’
  ‘Mbona unapitapita karibu na mikutano ya kampeni! Hujui ni hatari!’
  ‘Hatari gani mwenzangu. Hii ni nchi ya amani na demokrasia.’
  Basi KK akacheka kwelikweli.
  ‘Nani kakudanganya Hidaya? Nchi hii ina amani ili mradi wenyewe wanaendelea kutawala. Sasa wameona kutawala kwao kuko hatarini hivyo wanatutumia sisi. Ajira nzuri hii.’
  ‘KK!! Ajira nzuri? Kama nisingejificha si ajabu ungenikatakata kweli na panga lako.’
  ‘Hapo sasa. Ndiyo maana nakuambia ukae mbali na mikutano hii. Huwezi kujua litakalotokea.’
  ‘Lakini wewe KK, ulivyokuwa unalalamika kuhusu kulaliwa na wazito hadi unageuka chapati. Sasa unawatetea na panga?’
  ‘Nifanyeje Hidaya? Kwa njia hii, naweza hata kupata pesa za kurudia masomo.’
  ‘Kwa kuwaumiza wengine? Si bora utafute mgombea ambaye ataleta hali ya unafuu kwa wote!’
  KK hakujibu. Alicheka kicheko kimoja tu cha kebehi kisha akakimbia kukatakata bendera ya chama kingine. Kwa kweli nilisononeka sana mpenzi. Basi niliamua kufuata nyayo za KK kidogo nikamkuta yeye na wenzie wamemzunguka mgombea wakidai posho yao ya kuwakatakata watu mapanga. Na wengine walikuwa wanadai pia kwa kazi ya kumshangilia na kumfagilia.
  Hivi kweli KK hana njia nyingine ya kuweza kuendelea na masomo? Yaani sisi vijana kutokana na maisha yetu kuwa magumu hivi, tunaona bora kuuza utu wetu kuwapiga wengine wasio na hatia zaidi ya kutokubaliana na matakwa ya mgombea huyu au yule. Kwa kweli inasikitisha.
  Lakini upande wa pili mambo ni mabaya zaidi. Yaani mpenzi nimechoka kabisa kusikia eti watu wote wanapata UKIMWI kutokana na viherehere vyao. Labda hao wakubwa wanaopenda kutuambia hivyo. Wao si wana uhuru wa kuamua wamwage radhi kwa vibinti au la.
  Lakini wasichana wangapi wanabakwa hivihivi, tena na zaidi ya mwanamume mmoja, tena kwa sababu alimkataa mmojawao. Kiherehere? Hata hapa nyumbani alikuja kijana wa shirika fulani la kiraia ambalo linafanya kazi katika jimbo la bosi.
  Wakati wa kumngoja bosi, alikuwa anamsimulia Binti Bosi mambo yanavyokwenda huko. Kwa mfano, wazazi wanahamia shamba na kumwacha binti atunze familia bila hata pesa za matunzo. Mwisho analazimika kununua mboga, na pesa hana, afanye nini?
  Ilisikitisha mpenzi. Wakati sisi wasichana tunalaaniwa kwa tamaa, yule alikuwa anaeleza msichana akipata shilingi mia tano, mia tano tu, ananunua maji kwa ajili ya familia.
  Tamaa? Kiherehere? Na huko shuleni usiseme. Walimu wengine wanatongoza utadhani hawajawahi kumwona msichana. Na ukimkataa, ni adhabu ya kiboko, na kunyimwa mtihani hadi ukubali. Nani mwenye tamaa na viherehere hapa?
  Basi yule kijana akazidi kumwaga mifano ya jinsi wasichana wanavyolazimika kuingia kwenye ngono kwenye umri mdogo sana. Msichana mwingine aliambiwa waziwazi na wazazi wake kwamba shea yake ya kula haipo kama haleti pesa. Na unajua huyu msichana alikuwa na miaka mingapi? Kumi na miwili tu! Atapata wapi pesa? Na mwingine wa darasa la saba ambaye anamtafuta mwanamume kila siku kwa sababu ni mtoto yatima na ndugu wa wazazi wakachukua kila kitu wakamwacha na wadogo zake ili awatunze. Kiherere? Tamaa ya nani?
  Mara nyingine mpenzi naona hawa wakubwa wanaishi dunia tofauti na sisi, ndiyo maana wanaweza kuamka na kulaani bila kuelewa kitu. Waje na wao kujaribu maisha tunayoishi, viherehere vyao vya kutusema bila sababu vingekoma.
  Kwa hiyo mambo ndiyo hayo. Wengine wanaishi maisha ya kuwazidi hata watu wa Ulaya wakati sisi vijana tunalazimika kuuza miili yetu, wengine mikono yao ya kuwakatakata watu, wengine sehemu nyeti, huku wale ambao mbwa wao wanakula vizuri mara dufu kuliko sisi wanatucheka na wanatukebehi.
  Hata bosi juzi alikuwa anabwatabwata vilevile kidogo nimwagie chai kichwani. Inakera mpenzi.
  Akupendaye kijana mwenzangu mwenye dhamiri si viherehere
  Hidaya.
   
 2. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #2
  Oct 27, 2010
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Hii kali sana .... Kikwete atakoma ubishi mwaka huu na kampeni zake za kifisadi
   
 3. A

  August JF-Expert Member

  #3
  Oct 27, 2010
  Joined: Jun 18, 2007
  Messages: 4,509
  Likes Received: 723
  Trophy Points: 280
  hii makala nimeitoa kwenye gazeti la raiamwema
   
 4. Mtende

  Mtende JF-Expert Member

  #4
  Oct 27, 2010
  Joined: Sep 27, 2010
  Messages: 4,072
  Likes Received: 338
  Trophy Points: 180
  hehehe chadema tunasonga mbele,rais wetu ni mtu safi ndio maana anwataja mafisadi hadharani
   
 5. A

  August JF-Expert Member

  #5
  Oct 28, 2010
  Joined: Jun 18, 2007
  Messages: 4,509
  Likes Received: 723
  Trophy Points: 280
  naona mwandishi wa makala alikuwa anawalenga wale watongozaji feki wa ladio klaudz, na wale wa magazeti ya mafisudi, na wasanii wanao hongwa hovyo hovyo
   
Loading...