Ndesamburo, mchumba wa Slaa wakwamisha kesi ya Chadema

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,172
Ndesamburo, mchumba wa Slaa wakwamisha kesi ya Chadema
Send to a friend
Friday, 23 September 2011 19:38


Peter Saramba, Arusha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imeahirisha kusikiliza maelezo ya awali ya kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine 18 wa chama hicho, baada ya Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo na Josephine Slaa, kutokuwapo mahakamani.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Charles Magesa,anayesikiliza shauri hilo lililotokana na maandamano ya Chadema

Januari 5, mwaka huu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, kutoa nafasi kwa washtakiwa hao waliotoa sababu mbalimbali za kutohudhuria.

Kabla ya kuahirishwa, Wakili wa Serikali, Joseph Pande, aliwaita kwa majina kila mshtakiwa kuhakikisha iwapo wote wapo mahakamani, ndipo alipogundua wawili hawapo hali iliyomlazimu Mawakili wa utetezi,Method Kimomogoro na Albert Msando, kutoa taarifa za wateja wao
kutohudhuria.

Hata hivyo, zoezi la kuwaita kwa majina nusura liingie dosari, baada mshtakiwa wa kwanza, Mbowe kunyamaza kimya bila kuitika licha ya mwendesha mashtaka kumuita zaidi ya mara tatu, kwa kile alichoeleza kukosewa kwa jina lake.

“Hakuna mshtakiwa katika kesi hii anayeitwa Aikaeli Mbowe. Mimi jina langu ni Freeman Aikaeli Mbowe,” alisema Mbowe baada ya mwendesha
mashtaka kumwonyeshea kidole akimtaka asimame baada ya kuitwa jina mara kadhaa bila kuitika.

“Kesi hii leo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kosa. Lakini nimegundua kuwa washtakiwa wawili hawapo hapa mahakamani. Licha ya kwamba hatupingi maombi ya kuahirishwa, ni rai yetu kuwa kesi hii inapaswa kusikilizwa na kumalizika ili kutenda haki
kwa washtakiwa na hata upande wa Serikali,” alisema Pande.

Wakili Kimomogoro, aliieleza mahakama kuwa Ndesamburo alishindwa kufika mahakamani kwa sababu yuko nje ya nchi kwa matibabu na anatarajiwa kurejea Oktoba 17, wakati Josephine aliyejifungua karibuni amepewa maelekezo ya kupumzika na daktari hadi Oktoba 2, mwaka huu.

Alidai hata upande wa utetezi ulikuwa umejiandaa kwa ajili ya usikilizaji wa awali na kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi Oktoba 21,kutoa nafasi kwa wateja wake wote kuhudhuria kusikiliza maelezo jinsi makosa yalivyofanyika.

Baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na pingamizi dhidi ya maombi ya utetezi, Hakimu Magesa aliahirisha kesi hiyo na kuagiza washtakiwa wote kuhudhuria mahakamani. Dhamana ya washtakiwa wote akiwamo Dk Willibrod Slaa aliyehudhuria mahakamani jana inaendelea.


 
Back
Top Bottom