Ndege ya Lowassa inayopaa, na abiria walioachwa wameduwaa!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,115
M. M. Mwanakijiji

MWALIMU Nyerere katika mojawapo ya maandishi yake ambayo kama leo yangesomwa tena yangewazibua masikio na kuwafumbua macho watawala wetu, alisema hivi kuhusu asili na kiini cha dhana nzima ya maendeleo:

“Ukweli ni kwamba, maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Barabara, majengo, kuongeza uzalishaji wa mazao, na vitu vingine kama hivi siyo maendeleo; hivi vyote ni vyombo tu vya maendeleo… Ongezeko la madarasa katika shule fulani ni maendeleo pale tu majengo hayo yanaweza, na yanatumika kuendeleza uelewa na maarifa ya watu.

“Kuongeza uzalishaji wa ngano, mahindi, au maharage vinakuwa ni maendeleo pale tu vyakula hivi vinawapatia watu chakula bora.

“Vivyo hivyo kuongeza uzalishaji wa pamba, kahawa, au mkonge vitakuwa ni maendeleo pale tu mazao hayo yanapoweza kuuzwa na fedha zinazopatikana kutumika kujipatia vitu vingine ambavyo vitainua maisha ya watu katika afya, maisha mazuri, na kuelewa.

“Maendeleo ambayo si maendeleo ya watu, yanaweza kuwa ni somo kwa wanahistoria wa mwaka 3000.”

Katika maneno hayo ya Mwalimu, kumejaa somo ambalo baadhi ya wanasiasa na viongozi wetu wa leo naona wamelikwepa au limekuwa somo gumu kwao kulifuzu. Miongoni mwa viongozi hao si mwingine bali ni yule kiongozi hodari, shujaa na mahiri, aliyetamba bungeni.

Kwa mara nyingine tena akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake katika kikao cha bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliwatangazia wabunge kwa kutamba, tena na kwa kujidai akionyesha kuwa alikuwa na uhakika wa kile alichokisema.

Akitupilia mbali madai mbalimbali ya vyama vya upinzani kuhusu utekelezaji wa sera za CCM, kiongozi huyo alitamba akitumia mfano wa Rais Mkapa kuielezea Tanzania.

Namnukuu: “Ndege ile (isomeke Tanzania ile) ya Mkapa ilikuwa ni ndege kwenye runway, (hii ya) sasa tumeanza kupaa.

“We are on track, we are on time. Tuko timamu, na tuko na wakati… Ndege imeanza kupaa!”

Maneno yake hayo yalisindikizwa na mrindimo wa makofi kutoka kwa wabunge wa chama chake ambao alitumia muda huo kuwaasa kuisimamia ilani ya uchaguzi ya CCM.

Ni hili suala la kuifananisha Tanzania na ndege, tena ndege iliyoanza kupaa ndio jambo ambalo limenigusa na kunifanya nijiulize hivi Lowassa na viongozi wenzake wa CCM wanaishi katika ulimwengu upi au Tanzania ipi?

Na hii ndege ambayo wenzetu wanaishangilia kuwa imeanza kupaa, inaruka uwanja gani? Imenichukua karibu wiki mbili tangu Waziri Mkuu ayatamke maneno hayo bungeni kwa mbwembwe zote za mwanasiasa huku kidole chake kikipepewa angani kama onyo kwa mimi kuweza kupata jibu.

Nimegundua kuwa ndege ya Lowassa ambayo mwenzetu ameanza kuiona imeanza kupaa, ni ndege ya nchi ya kufikirika, ambako abiria wake ni yeye anawajua, kwani kwa hakika ndege ya Watanzania wengi, hata kutoka kwenye hanga haijatoka!

Niwape wazo kidogo kuhusu ndege kupaa. Miaka ya mwanzoni mwa themanini nikiishi karibu na Kipawa (maeneo ya Karakata), jijini Dar es Salaam, kabla ya ile bomoabomoa, mimi na wenzangu wachache tulikuwa tunapenda kwenda pale uwanja wa ndege siku za Jumamosi kuona ndege zinavyotua na kupaa.

Kitu kimoja ambacho kilikuwa kwenye mawazo yangu wakati wote huo, ilikuwa ni hisia ya kutobahatika kupanda “pipa” hilo kwenda kokote lilikokwenda.

Nilipokuwa nikiona ndege za Sabena zikitua au KLM na British Airways, wazo la kutamani kuwemo kwenye mojawapo ya misafara hiyo lilikuwa likinijia kila kukicha.

Ilipofika wakati wangu wa kupanda ndege kwa mara ya kwanza, hisia ya hofu na hamasa ilikuwa imechanganyika.

Kitendo cha kuwa angani, nikiwa nimejifunga mkanda kwenye kiti changu, kilikuwa ni kitendo cha kijasiri.

Tulivyokuwa tukipasua anga na uharaka wa safari yenyewe, ilinihakikishia kuwa hakuna usafiri salama na wa haraka kama wa ndege.

Nina uhakika bado kuna watu wetu wengi tu ambao hawajapata nafasi ya kusafiri kwa ndege na hivyo wao kama mimi miaka ile, wamebakia kuangalia angani kila ndege ipitapo na kubakia wakiitamania siku ile na wao wataruka na “mchuma” huo.

Hivyo, Waziri Mkuu anapoiona Tanzania kuwa ni ndege iliyoanza kupaa bila ya shaka ana kila sababu na ushahidi wa kuiona hivyo.

Kwa maoni yangu, hata hivyo Tanzania inayopaa ambayo Waziri Mkuu na wabunge wa CCM walikuwa wanaishangilia ni Tanzania ya watu wachache ambao wamebahatika kupanda ndege hiyo na wanafurahia viti vyao vya daraja la kwanza ambako hakuna bughdha zozote.

Watu hawa ni kina nani hasa ambao wanafurahia ndege iliyopaa huku lile daraja la tatu likiwa tupu na abiria wote wakiwa bado wameachwa Kipawa wakiwa wameduwaa?

Ni kina nani hawa wanaotaka tuamini kuwa nchi yetu si tu imeanza kutambaa na kujiandaa kukimbia, kuwa ati leo hii imeanza kupaa?

Sasa sitaki kueleweka kuwa napinga hakuna mafanikio yoyote ambayo nchi yetu imeyapata mpaka hivi sasa, najua ni mengi na watetezi wake wapo na mifano ipo.

Hata hivyo nimekereka kabisa na mfano wa Waziri Mkuu kuwa Tanzania yetu imeanza kupaa! Mwalimu alisema wazi kuwa “itabidi tukimbie wakati wenzetu wanatembea”.

Ninachosema ni kuwa Tanzania ya Lowassa ina watu wachache ambao kwa hakika hawajui adha ya maisha ya kawaida ya Watanzania, kwani Tanzania yao imezunguka maeneo ya miji yetu mikubwa, lakini hawana wazo hata chembe la maisha ya watu wa vijijini kwetu (zaidi ya kutuonyesha kuwa hata huko kuna simu za mkononi!)

Lakini hawa wanaonufaika na Tanzania hii na ambao wanafurahia kuona Tanzania imeanza kupaa (licha ya ushahidi wote kuwa hata kwenye runway hatujafika) ni kina nani?

Viongozi wa juu wa CCM. Hawa ni watu ambao kwao Tanzania imeanza kupaa.

Viongozi hawa bila ya shaka ndio wa kwanza kuifurahia nchi inayopaa kwani hawana matatizo yoyote na mambo mengine.

Hawako tayari kuona mabadiliko ya kweli ya kisheria yanafanyika ili kupigana na rushwa na ufisadi, wako na haraka ya kwenda kuzoa wanachama wa vyama vingine ili kuwakaribisha airport, hata kama hawatapata nafasi ya kuingia kwenye ndege hiyo, na kila kukicha wanawaza ni jinsi gani wataitumia serikali wanayoiongoza kukinufaisha chama.

Kwa hawa, Tanzania inayopaa haitengani hata chembe na manufaa kwa CCM.

Kwa kadiri ndege ya Tanzania inavyopaa ndivyo chama nacho kinavyozidi kupaa katika anga za siasa za Tanzania.

Watendaji wa serikali wakubwa. Hawa bila ya shaka wanafaidika na CCM inayofurahia kupaa kwa Tanzania.

Watendaji hawa hawana wasiwasi wa kuboronga kwani kwa kadiri ya kwamba wanawanufaisha wakubwa wa chama, basi Tanzania yao nayo inapaa.

Hivi karibuni kuna tuhuma kubwa za ufisadi huko Benki Kuu (BoT), watendaji wetu badala ya kutafuta ukweli na undani wa tuhuma hizo na hasa kwa vile zinamhusisha mtendaji mkuu wa benki hiyo, wanaanza kutafuta ni nani alizitoa tuhuma hizo.

Kwa hawa watendaji, tuhuma zinapotolewa kuwa serikali imewatelekeza wanafunzi Ukraine, badala ya kutafuta ukweli wanawauliza wanaotuhumiwa ukweli wa tuhuma dhidi yao!

Kwa vile serikali ya Lowassa haina nia na mazoea ya kushughulikia ufisadi mkubwa, basi watendaji wa serikali wanajua wameshakata tiketi katika ndege hii ya Lowassa.

Kwa hakika kwa watu hawa ndege yao imepaa, wakati abiria wengi wamepigwa na butwaa!

Wafadhili na wafanyabiashara wakubwa wenye ushabiki wa CCM. Hakuna watu ambao kwa hakika Tanzania yao inapaa kama wale wafanyabiashara ambao biashara zao zimepewa baraka zote za kichama na hivyo hawakumbani na matatizo ya kila siku ya kiutendaji.

Wale Watanzania wachache ambao hawakutaka kukata tiketi za ndege hii ya Lowassa, wamejikuta wakinyanyasika kila kukicha na mambo yao yakiwaendea kombo hadi pale waliporudi “kundini”.

Mfano mzuri ni mfanyabiashara mmoja wa Nyanda za Juu Kusini ambaye alikuwa upinzani na alikuwa amejenga karibu na kituo cha FFU.

Bwana huyu alianza kupatiwa barua za kutakiwa kuhamisha makazi yake kwani eneo alilojenga lilikuwa ni mali ya serikali (Polisi).

Jamaa alipoelewa kuwa ilikuwa ni usumbufu wa kisiasa, aliamua kurudi chamani na kelele zote hizo zikayeyuka kama ukungu alfajiri.

Wapo watu wengi ambao wamegundua kuwa kufanikiwa kweli kibiashara ni lazima uabudu katika altare ya CCM, huku ukiimba mapambio ya nyimbo za sifa za chama huku kasida za kushangilia sera na ilani za CCM zikisika. Vinginevyo ndege yako wewe itaendelea kukaa kama jumba la maonyesho!

Ndege imepaa kwa wawekezaji wa nje. Hawa kwa namna fulani wamegundua kuwa katika Tanzania ya sasa wanaweza kwa haraka kutengeneza mamilioni ya dola kwa haraka labda kuliko sehemu nyingi kweli duniani.

Kwa hawa wamegundua kuwa ndege ya Tanzania inapaa kama helikopta haihitaji kukimbia kwenye runway! Walianza Loliondo, ikaja IPTL, DAWASA, ATC, KIA, TANESCO, Richmond, rada, ndege ya rais, na mikataba ya madini.

Kwa wawekezaji hawa, Lowassa anaposema Tanzania “imeanza kupaa”, ni lazima washangilie kwani wao wako kwenye daraja la kwanza!

Ninaweza kuendelea kuorodhesha ni makundi gani ya watu ambao wanaiona Tanzania imeanza kupaa, hata hivyo kila mtu anajua kabisa kuwa Tanzania inayopaa si ya Watanzania wote.

Ni Tanzania ya watu wachache ambao wamefungamana na chama tawala au na serikali ambao kwa hakika hawana wasiwasi wa wapi watakula au biashara zao zitakwenda vipi.

Ni Tanzania ya watu hawa ambao hawana wasiwasi kama watoto wa wakesha hoi wanalala nje ya ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine au wanaishi kwa kushindia mikate na maji!

Ni Tanzania ya watu hawa ambao wanasifia ujenzi wa vyuo vikuu halafu kesho yake wanashangaa mbona vyuo vinachukua watu wachache!

Ni Tanzania ya watu hawa wachache inayopaa kwa kutoa mikopo ya mamilioni ya fedha kwa viongozi walio madarakani na wanaposhituliwa wanasema “hata watu wasio viongozi wanastahili mikopo hiyo!” Tanzania hiyo bila ya shaka inapaa kwao.

Hata hivyo, kwa mamilioni ya wana wa nchi yetu, Tanzania inayopaa ni ya njozini, ni ile ambayo wote tunaitamani.

Kwa hawa ambao hadi leo bado wanajenga kwa kutumia udongo na nyasi, na kuchota maji mtoni huku wakipeleka watoto wao hospitali kwenye matenga ya maembe, kwa hawa Tanzania haipai! Kwa mamilioni ya watoto wetu ambao licha ya madai kuwa kuna chakula cha kutosha, bado tuna tatizo la utapiamlo katika nchi yetu, yaani tumeshindwa hata kuwalisha watoto wetu chakula bora!

Kwa Watanzania hao, kupaa anakozungumzia Lowassa ni msemo tu wa kisiasa usio na ukweli wa mantiki, ni hadaa ya viongozi ili wapigiwe makofi!

Katika Tanzania ya leo, bado tuna watu wanaohangaika kwenda shule ya msingi na kama habari zilizoripotiwa kwenye gazeti moja zina ukweli, basi kwenye nchi hii inayopaa shule ambayo ina mwalimu mmoja na kaka mkuu ni kaimu, basi Tanzania hiyo haijapaa na haipai!

Tunatamani Tanzania inayopaa, Tanzania ambao watoto wake wote licha ya maeneo wanayotoka, uwezo wao wa kimaisha au vyama wanavyotoka wana nafasi sawa ya kufanikiwa endapo watapewa nafasi. Hiyo itakuwa ni Tanzania inayopaa.

Pale ambapo tutaweza kuhakikisha kuwa vijana wetu hawakatishiwi masomo kwenye vyuo vyetu vikuu kwa uzembe wa Bodi ya Mikopo, Tanzania hiyo itakuwa imeanza kupaa.

Pale ambapo tutachunguza ukweli wa tuhuma dhidi ya mtu yeyote na kuchukua hatua za kisheria inapobidi badala ya kutafuta nani alitoa tuhuma hizo, basi Tanzania itaanza kupaa.

Ni pale ambapo badala ya kuendelea na katiba ambayo imepitwa na wakati na tukaamua kama watu wamoja kufanya mazungumzo ya kikatiba ili tujitengenezee katiba mpya yenye kubeba matarajio na matamanio yetu, basi Tanzania itaanza kupaa.

Tanzania inaweza kupaa, lakini hivi sasa haijaanza kupaa! Tusidanganywe na tusidanganyane.

Tanzania yenye neema inawezekana, maisha ya furaha na mafanikio yanawezekana, mabadiliko ya kweli ya maisha ya watu wetu yenye unafuu na ahueni ya kimaisha yanawezekana.

Hata hivyo, hayo yote yanawezekana pale tutakapokuwa wa kweli kwa nafsi zetu na kwa wale tunaowaongoza.

Porojo za kisiasa ni nzuri wakati wa kampeni, lakini wakati wa kufanya kazi ni lazima tuwe wa kweli.

Hivyo hoja ya Waziri Mkuu kuwa Tanzania imeanza kupaa na kwenda ‘ayeya’, haina msingi, haina ukweli, na imetokana na hisia za kisiasa zaidi kuliko ukweli ardhini!
Ndege hiyo wamepanda vigogo. Sisi abiria wengine ambao ndio wengi zaidi na ambao tumeilipia ndege hiyo, tumebakia Kipawa wakati wenzetu wanapaa, sisi tumebakia tunashangaa huku tumepigwa na butwaa, mbona wametuhadaa?

Siku moja tutatafuta marubani wengine.
 
Kama mko tayari kwa nini sasa msifungue mashitaka? Au katiba hairuhusu mtu/ watu binafsi kumshitaki kiongozi wa ngazi ya taifa?
 
Kama mko tayari kwa nini sasa msifungue mashitaka? Au katiba hairuhusu mtu/ watu binafsi kumshitaki kiongozi wa ngazi ya taifa?

I will have to see what is in our constitution; however, it is possible according to the rule of law.

“…every official, from the Prime Minister down to a constable or a collector of taxes, is under the same responsibility for every act done without legal justification as any other citizen. The Reports abound with cases in which officials have been brought before the courts, and made, in their personal capacity, liable to punishment, or to the payment of damages, for acts done in their official character but in excess of their lawful authority. [Appointed government officials and politicians, alike] ... and all subordinates, though carrying out the commands of their official superiors, are as responsible for any act which the law does not authorize as is any private and unofficial person.”
 
MKJJ

Bado uko mjini?

Kuna ndege za kisasa zinaitwa VTOL (Vertical Take Off and Landing); nadhani hazijawa maarufu sana lakini zimeanza kutengenezwa kwa jeshi la marekani (Marines) kwa ajili ya kutumiwa kutoka kwenye meli zao za kijeshi-aircraft carriers.

Chini ya utaratibu wa ndege za Lowassa, wawekezaji wa kutoka nchi za nje hapa Tanzania wao wanatumia VTOL, hawahitaji hata ule uwanja wa Kipawa kuruka.
 
Si umesema ushahidi upo wa kutosha...

Kama ushahidi wa kutosha upo haina maana watu waende mahakamani. Suala ni kwenda mahakamani na kushinda kesi, it takes more than ushahidi wa kutosha. Angalia The People v. O.J. Simpson utajua ninaongea nini?
 
Hhhmmm...you say so!
So far it is Rev. Mtikila alone who has walked the talk! All others are full of hot air until I see action. If/when that happens, then I will recant my words.
 
Ndege Imeruka?.... duh mbona abiria wengi tumeachwa!..
Schedule yake ilikuwa wapi Ikulu, ama!...
Na ndege hiyo jamani umetengenezwa kwa kutumia nguvu ya ya jua ama maanake hata baiskeli tumeshindwa kutengeneza itakuwa ndege!..

Mwanakijiji, Ndugu yangu yawezekana kweli Tanzania ni ndege inayopaa ktk ndoto za Matrix, wenzetu wameisha kunywa ile Pill.
 
Admn.. unaweza kuacha hii breaking kikatuni news up to the end of the day.. halafu unganisha na ile ya "majibu ya waziri mkuu" Ndugu zangu kikatuni hiki kilienda sambamba na makala ya "ndege ya lowassa inayopaa, na abiria walioachwa wameduwaa". Siku ile Jumatano Bungeni ilikuwa ni kicheko ndani ya kicheko.. na ndipo kiongozi wetu mahiri, hodari, shujaa aliyetamba Bungeni alipoagiza wajibu mapigo!!

ndegeyalowassa.jpg
 
Interesting: it says all.

Je mchoraji wa katuni hii naye "amekimbia" nchi?
 
Back
Top Bottom