Ndege mwenye Makinda Mia?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,370
39,186
1. Fumbo ninawafumbia, wajuaji mfumbue,
Ni siri nawaambia, werevu na wategue,
Ni swali nawarushia, Malenga jitutumue,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

2. Apendeza kama nini, hilo ninawatajia,
Na arukapo angani, sifa tunamwagia,
Rangi zake mabawani, mwilini kajipambia,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

3. Ashangaza duniani, jinsi alivyotulia,
Na hao ndege jirani, alipo wakimbilia,
Sasa yuko hatarini, adui wamepania,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

4. Nimezipata habari, makinda yake ni mia,
Yameurithi uzuri, watu wameniambia,
Yamelelewa vizuri, wengi wameshuhudia,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

5. Adui kadhamiria, Makinda yaje pigana,
Kisa akawazulia, Ili ndugu kugombana,
Kisirani kuingia, damu moja warundana,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

6. Adui kajitahidi, kuwagawa kwa makundi,
Akafanya makusudi, yeye ndege hawapendi,
Wivu wake umezidi, kushawishi moja kundi,
Ndege huyu ndege gani, na makinda yake mia?

7. Kundi moja likasema, sisi tunabaguliwa,
8. Tunaye mmoja mama, mbona sisi twaonewa,
Na kitakuwa kiama, haki tusipopatiwa,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

9. Na lile kundi jingine, la wale makinda mia,
Likasema na tuone, vita mnatutakia,
Ubaguzi tusione, mama mnamzulia,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

10. Hasira ikajazana, makundi kutoonana,
Adui walipoona, furaha ikajazana,
Wakasema sasa ona, hawa ndege kupigana,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

11. Adui mbinu katunga, ili ndege wapigane,
Mama ndege akapinga, wanae wasivaane,
Hoja mama akajenga, ndugu washirikiane,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

12. Ndipo mama kasimama, kasema wamoja nyie,
Mtakileta kiama, kiota mtuvunjie,
Majirani wanasema, mabaya yatushukie,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

13. Mama akawatazama, makinda kundi la kwanza,
Ukweli mmeusema, mama akawaliwaza,
Makosa ya huko nyuma, sahihisha tutaanza,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?

14. Acheni vitisho vyenu, damu isije mwagika,
Kwani hawa ndugu zenu, kumoja ninyi mwatoka,
Aibu ikawa yenu, nduguyo akidondoka,
Ndege huyu ndege gani, na makinda yake mia?

15. Kiota nimekijenga, ni chenu wanangu wote,
Wala mimi sikulenga, kupendelea yeyote,
Ukweli huu ni nanga, nawapenda ninyi nyote,
Ndege huyu ndege gani, na makinda yake mia?

16. Ndipo mama ageuke, kwa lile kundi jingine,
Macho yenu yafumbuke, ndugu zenu muwaone,
Hofu yenu iwatoke, ili msikilizane,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia.

17. Pamoja mshikamane, matatizo kutatua,
Na maadui waone, aibu ikawatua,
Nami mama nijivune, wanangu wameshakua,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia.

18. Furaha ikajazana, kicheko kwenye kiota,
Nami nilipowaona, nikadhani ninaota,
Ndege wameshikamana, Majuto kutowakuta,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia.

19. Nao ndege majirani, nao wakashangilia,
Wakasema sivioni, vita tulivyodhania,
Darasa hilo yakini, toka ndege hawa mia,
Ndege huyu ndege gani, na makinda yake mia.

20. Chini kalamu naweka, nami sasa naondoka,
Mia na moja waruka, pamoja wanasikika,
Nyimbo zao zasifika, hadi mbali zinafika,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia.
 
.

3.Ashangaza duniani, jinsi alivyotulia,
Na hao ndege jirani, alipo wakimbilia,
Sasa yuko hatarini, adui wamepania,
Ndege huyu ndege gani, Na makinda yake mia?
.......

Nimezipata salamu, mzee wa kijijini
Ukatumia kalamu, kutuletea mjini
Swali lako ndiyo gumu, tunajigonga vichwani
Ndege mwenye rangi rangi, nahisi namjulia

Umeeleza makinda, ambayo ni mia mia
Siyo timu ya kandanda, ni bunge lilotimia
Wawakilisha kwa kanda, bila pande kujalia
Ndege mwenye rangi rangi, nahisi namjulia

Rangi hizo ni bendera, ambayo inapepea
Ikipepea yang'ara, na raha hutuletea
Kwa amani na busara, ingawa tunahofia
Ndege mwenye rangi rangi, nahisi namjulia

Ni mambo ya kawaida, wana ndugu hugombana
Hata kaka na madada, wazee pia vijana
Watagombea vigoda, na hata watalogana
Ndege mwenye rangi rangi, nahisi namjulia

Nasema ni Tanzania, ambayo twaililia
Walakini umejaa, muungano nasemea
Yabindi kujadilia, na vita tutakwepea
Ndege huyu nchi yetu, ni bara na visiwani!
 
Safi sana, nimependa hii.
 
Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom