Nchimbi , Nahodha Bado Wanaweza kuwania urais

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797


Na Elias Msuya na Fidelis Butahe,Mwananchi

Posted Jumatano,Decemba25 2013 saa 9:30 AM

KWA UFUPI

Mtazamo wa Mallya unaungwa mkono na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala ambaye anasema kimsingi matatizo yaliyotokea yanasababishwa si na watu binafsi, bali mfumo mbovu.

Baadhi ya wasomi nchini wamesema kwamba licha ya hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne, kugusa mustakabali wa kuwania urais wa miongoni mwa wanasiasa hao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wanaweza kuwania nafasi hiyo kwa kuwa waliwajibika kisiasa.

Mawaziri walioenguliwa kutokana na athari za Operesheni Tokomeza Ujangili ni wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.

Wakati Nchimbi akitajwa kuwa mmoja wa wanasiasa tishio katika mbio za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, Nahodha anatajwa kuwa mmoja wa wale watakoingia katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo upande wa Zanzibar lakini baada ya Dk Shein kumaliza muda wake wa vipindi viwili.

Katika msingi huo, gazeti hili liliarifiwa kuwa baada ya tangazo la kutenguliwa kwa uwaziri wao, baadhi ya kambi zinazojiwinda kwa ajili ya kuwania nafasi za juu za uongozi wa nchi 2015, zilishangilia na kuandaa tafrija za kupongezana.

Kumekuwa na mawazo kwamba ikiwa Nchimbi na Nahodha wanataka kuendelea na mipango yao, basi inabidi wafanye kazi kubwa kwani kuondolewa kwao katika nafasi za uwaziri ni kete itakayotumiwa na wapinzani wao kisiasa.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema kung’oka kwa mawaziri hao kunaweza kusiyumbishe ndoto zao kisiasa siku za usoni.

“Inategemea wanazipangaje karata zao na tukumbuke kwamba bado Rais anaweza kuwateua kwenye nafasi nyingine ijapokuwa ni kweli kwamba kuenguliwa huku kutawayumbisha katika matamanio yao ya baadaye kisiasa,” alisema Mallya na kuongeza:

“Dk Nchimbi na Nahodha siyo kwamba walikuwa tishio kubwa kati ya wanaotajwa kuwania urais, ingawaje ni watu wenye mikakati mingi na wako kwenye makundi mazuri yanayowaunga mkono. Itategemea jinsi wanavyojipanga upya.”

Mtazamo wa Mallya unaungwa mkono na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala ambaye anasema kimsingi matatizo yaliyotokea yanasababishwa si na watu binafsi, bali mfumo mbovu. Profesa Mpangala alisema hakuna waziri anayeweza kufanikiwa kiutendaji katika mfumo mbovu uliopo na unaoendelea kutumika.

Alisema haoni kama mawaziri hao wameathirika kisiasa kwani wameathiriwa na mazingira wanayofanyia kazi. “Yaliyotokea kwenye operesheni ya ujangili ni kielelezo cha mfumo wa ubabe uliokithiri muda mrefu,” alisema Profesa Mpangala.

Nchimbi ni nani?

Nchimbi, ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini ni kati ya wanasiasa waliokuwa wanatajwa kuwania nafasi ya urais kutokana na historia na rekodi yake ndani ya Serikali na CCM huku nafasi nyeti alizoshika katika miaka ya karibuni zikimwongezea sifa.


Dk Nchimbi ameondoka akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ambayo ni kati ya wizara nyeti za Serikali kutokana na jukumu lake la kusimamia vyombo vya usalama.

Pia aliwahi kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na kabla ya hapo aliwahi pia kushika wadhifa wa Naibu Waziri katika Wizara za Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Kazi na Ajira; Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Uzoefu unaonyesha wale walioshika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano waliwahi kuongoza wizara nyeti.

Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Benjamin Mkapa, ambaye alimfuatia aliwahi kuongozi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kama ilivyo kwa Rais Kikwete.

Nguvu na uzoefu wake unatokana na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM tangu mwaka 1998 na sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Udhamini la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa miaka 10 katika kipindi ambacho jumuiya hiyo ilikuwa na nguvu na ushawishi mkubwa, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na baadaye kuchaguliwa kuwa mbunge, nafasi ambayo ilimpa fursa ya kuwa waziri.

Nahodha ni nani

Nahodha ni kati ya wanasiasa vigogo wa CCM akipewa nafasi kubwa kuongoza Zanzibar na wengine wamekuwa wakimtaja kama mtu anayeweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anahesabiwa kuwa miongoni mwa vinara kutokana nyadhifa nzito alizowahi kushika.

Anashikilia rekodi ya kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwani alishika wadhifa huo kwa miaka 10, kati ya 2000 na 2010. Nahodha aliwania urais wa Zanzibar kupitia CCM, lakini hakufanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa 2010.

Aliamua kugombea nafasi ya uwakilishi katika Jimbo la Mwanakerekwe na kushinda na wakati huohuo, aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge, hivyo kupata fursa ya kuteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ulinzi na JKT ambako aliondolewa.

Kagasheki na Mathayo

Balozi Kagasheki kwa upande wake, hajasikika kama ana ndoto za urais lakini ni kati ya vigogo linapokuja suala la siasa za Mkoa wa Kagera akiwa Mbunge wa Bukoba Mjini.

Hivi karibuni, aliingia katika mgogoro na Meya wa Bukoba, Dk Anatory Aman akimtuhumu meya huyo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kwa ufisadi na hadi suala hilo kufikishwa kwenye vikao vya juu vya CCM.
Hata hivyo, mgogoro huo unahusishwa na kampeni za ubunge za 2015 huku Meya Amani akitajwa kupania kupambana na Kagasheki kugombea ubunge kupitia CCM.

Kwa upande wake, Dk Mathayo ambaye pia ni Mbunge wa Same Magharibi ni kati ya wanasiasa wachanga wa CCM ingawa inaelezwa atajikita zaidi katika kutetea jimbo lake linalonyemelewa na Chadema ambao wameanzisha kile wanachokiita `Operesheni Mathayo Out’.

Katika mazingira hayo, ni dhahiri ana kibarua kigumu cha kuwashawishi wapigakura wake kumwelewa kwani kung’oka kwake katika nafasi ya uwaziri ni dhahiri itatumiwa na wapinzani wake si nje ya CCM pekee, bali hata ndani ya chama hicho.


 
Unaona ilivyo SAFI na RAHISI kuwasafisha WANA-CCM waliofanya MADHAMBI kwa JUMUIA??
Kweli na wataweza kuwa MARAIS wetu...

Sasa ije wale walioghushi VYETI vyao VYA SHULE... ? hilo linaonekana kama ni style ya CCM
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom