Nchi yachafuka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nchi yachafuka

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mkaguzi, Oct 23, 2008.

 1. Mkaguzi

  Mkaguzi JF-Expert Member

  #1
  Oct 23, 2008
  Joined: Sep 26, 2007
  Messages: 249
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Nchi yachafuka
  na Waandishi Wetu  MATUKIO yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini katika siku za hivi karibuni yameanza kuibua hali ya wasiwasi miongoni mwa wananchi.

  Kutokea kwa matukio hayo yanayoelezwa na baadhi ya wadadisi wa mambo kuwa ni kielelezo cha watu kukata tamaa au kuchoshwa na mwenendo wa mambo yasiyobadilika, kumezidi kuibua maswali mengi kila kukicha.

  Tayari baadhi ya wanasiasa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa kambi ya upinzani wameanza kuielezea hali hiyo ama chini kwa chini au kwa uwazi kuwa ni dalili ya kuelemewa kwa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo inakaribia kufikisha umri wa miaka mitatu madarakani miezi miwili ijayo.

  Kinachosababisha kuibuka kwa mtazamo huo ni kuibuka kwa mitikisiko mipya ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hapa nchini ambayo kila mmoja unaonekana ama kuilenga moja kwa moja serikali au viongozi wake.

  Matukio ya hivi karibuni kabisa ambayo kwa kiwango kikubwa yanaonekana kutikitisa serikali na viongozi wake ni yale ya kushika chati kwa migomo ya wafanyakazi wa sekta tofauti inayochukua sura ya kitaifa na kusababisha usumbufu mkubwa nchini.

  Katika kuonyesha namna serikali inavyoelemewa na mambo hayo, hivi karibuni, ililazimika kukimbilia mahakamani ili kuzuia kishindo cha mgomo wa walimu uliopangwa kuanza Jumatatu ya wiki hii nchi nzima.

  Uamuzi huo wa serikali ambao umetafsiriwa na wadadisi wa mambo kwa namna tofauti, kulikuja siku chache tu kabla ya wananchi wasiojulikana wa Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya kuuvurumishia mawe msafara wa Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.

  Tukio la Kikwete kurushiwa mawe ambalo hadi hivi sasa halijatolewa majibu ya kuridhisha, lilikuja siku chache tu baada ya wakazi wa eneo la Mwanjelwa, Mbeya mjini kuuzingira msafara wake wakipiga kelele za kumtaka achukue hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

  Katika kuonyesha namna mambo yalivyokuwa yakienda, sambamba, upande mwingine kabisa wa nchi, chama tawala CCM, kinachoongozwa na Kikwete mwenyewe, kilijikuta kikiangushwa katika uchaguzi mdogo wa udiwani na ubunge wa Tarime, tukio ambalo taarifa zinaonyesha lilipokewa kwa shangwe katika mitaa na ndani ya ofisi mbalimbali za umma.

  Baadhi ya makada na viongozi waandamizi wa CCM waliozungumza na Tanzania Daima baada ya matokeo ya Tarime kutangazwa na kukipa ushindi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walisema tukio hilo lilikuwa mwanzo wa safari ya kuanguka katika sanduku la kura kwa chama hicho tawala.

  Katika kuonyesha namna tukio hilo la Tarime lilivyochukua sura tofauti, walimu waliokuwa wakijiandaa kwa mgomo wao uliosimamishwa na mahakama, jijini Dar es Salaam walisikika wakihamasishana kwa ishara na nyimbo za kuisifu Chadema.

  Walimu hao ambao sasa wamekata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga kusitishwa kwa mgomo na maandamano yao ya nchi nzima, wanaidai serikali malimbikizo wanayodai yanafikia sh bilioni 16, ikiwa ni majumuisho ya fedha za likizo, nyongeza ya mishahara inayotokana na kupanda kwa madaraja na marupurupu mengine.

  Wiki hiyo hiyo pia wakati walimu wakiwa bado kwenye mgomo baridi, umma ulishuhudia mgomo mwingine wa wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

  Wanafunzi wa chuo hicho, walikuwa wakitaka kuongezewa muda wa kulipa fedha wanazodaiwa mpaka muhula wa masomo ujao wakati wahadhari wao walikuwa wakidai stahiki zao.

  Kabla ya mgomo wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kulikuwa na mgomo mwingine wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na Muhimbili na kusababisha ARU kufungwa, huku Chuo cha Ustawi wa Jamii, nacho kikiwa kwenye mgogoro mkubwa unaotokana na sababu hizo hizo.

  Wiki hiyo hiyo, wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), waliendelea kuweka kambi mbele ya ofisi ya Wizara ya Fedha na Uchumi, wakidai mafao yao na wakafikia hatua ya kupiga mawe gari la serikali, wakilalamikia kushindwa kutekelezwa kwa ahadi aliyoitoa rais bungeni mwishoni mwa Agosti kwamba wangelipwa mafao yao.

  Ugonjwa huo wa kisasa wa migomo katika vyuo, juzi ulihamia nchini Uganda ambako wanafunzi zaidi ya 200 wa Tanzania wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Kikuu cha Biashara (MUBC) na Mbarara, waliandamana hadi kwenye ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo, kuwasilisha malalamiko yao.

  Miongoni mwa malalamiko yao ni malipo ya dola za Marekani 1,000 kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na dola 800 za kuanzia kwa mwaka wa kwanza.

  Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini, George Nyatega, alisema jana kuwa, baadhi ya wanafunzi walioko katika mgomo nchini Uganda hawahusiki nao kwa madai kuwa walijipeleka wenyewe, sababu ambazo zinafanana na zile zilizotolewa na serikali mwaka jana wakati wanafunzi wa Tanzania walipogoma nchini Ukraine.

  Akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza, (BBC), jana mkurugenzi huyo alisema, idadi ya wanafunzi waliolipiwa na bodi hiyo nchini Uganda ni 121 ambapo hadi sasa wamekwisha kulipa jumla ya sh milioni. 209.3.

  Wakizungumzia mateso yanayowasibu, Adam Nyombi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere alidai kuwa hadi sasa ni miezi miwili walikuwa hawajalipwa fedha, hali iliyosababisha washindwe kumudu mahitaji yao ya kitaaluma.

  Malalamiko ya wanafunzi hao wa Uganda yanakuja katika kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini Urusi kuandamana hadi katika Ubalozi wa Tanzania nchini humo wakilalamikia kutolipwa stahili zao, hatua ambayo ilisababisha wajikute wakiandamwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

  Vurugu hizo za Urusi zilikumbusha kile kilichotokea mwaka jana, wakati wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini Ukraine nao walipoingia katika mvutano na serikali kwa madai ya namna hiyo hiyo.

  Hali hiyo ya wanafunzi kugoma na kuitisha maandamano imekuwa ikishamiri kwa kiwango kikubwa hata katika vyuo vikuu vingine nchini, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho ndicho kikongwe kuliko vyote hapa nchini.

  Wakati hayo yakitokea, wananchi bado wana kumbukumbu za mgomo wa nchi nzima wa wafanyakazi wa Benki ya National Microfinance (NMB).

  Mgomo huo wa wafanyakazi wa NMB ambayo ndiyo benki kubwa kimtaji na kimtandao kuliko nyingine yoyote, uligusa matawi yote 121 yaliyosambaa nchini.

  Hali hiyo ya mambo ilisababisha Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ben Christianaanse, kuitisha mkutano wa dharura na waandishi wa habari na kueleza namna hatua hiyo ya wafanyakazi ilivyosababisha na itakavyosababisha madhara makubwa. Hadi leo hakuna takwimu rasmi za hasara iliyopatikana.

  “Tumepata hasara kubwa kifedha, lakini hasara kubwa zaidi ni ya kupoteza imani kwa wateja wetu. Maelfu ya Watanzania leo wanahangaika kupata huduma zetu kwa sababu ya mgomo huo. Hiyo ni hasara kubwa zaidi,” alisema mkurugenzi huyo wakati huo.

  Katika kipindi hicho hicho, wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), walikuwa wanaingia kwenye mgomo kabla ya serikali kuingilia kati dakika za mwisho kwa kuamua kulipia mishahara mipya ya wafanyakazi kwa kipindi cha miezi mitatu.

  Ni kipindi hicho hicho, wafanyakazi wa Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), nao waliingia kwenye mgomo, wakipinga hujuma zinazofanywa dhidi ya shirika lao, madai ambayo juzi yalithibitishwa kuwa kweli na Kamati ya Bunge ya Miundombinu.

  Wakati kumbukumbu ya matukio hayo ikiwa haijatoweka, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), kama kilivyokuwa kwa vyama vingine kabla, kimetangaza azima ya kuitisha mgomo wa wafanyakazi nchi nzima, kikisema kinalenga kuikumbusha serikali iliwalipe mafao yao kwa kufanya mgomo kama ya wenzao.

  Naibu Katibu Mkuu wa TALGWU, Freddie Bhalijuye, alisema jana kuwa, serikali inapaswa kuwalipa madai yao kabla hawajatangaza rasmi kugoma kama walivyogoma walimu, wafanyakazi wa NMB, TRL na wengine.

  Aliyataja madai yao kuwa ni pamoja na malimbikizo ya likizo, uhamisho, matibabu, mafunzo, nyongeza ya saa za kazi na kukaimu madaraka.

  Bhalijuye alisema wafanyakazi hao wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 3.5 na kwamba fedha hizo wamekuwa wakizidai na kuahidiwa kulipwa kwa miaka 13 tangu mwaka 1995 bila mafanikio.

  “Sisi tulikaa kimya kwa muda mrefu tukisubiri uamuzi wa serikali kuhusu madai yetu lakini sasa naona wametusahau, hivyo hatuna budi kuwakumbusha kistaarabu, endapo itashindwa kutulipa, basi tutafuata taratibu kama zilizofanywa na wenzetu kwani ni haki yetu kufanya hivyo,” alisema.

  Alisema awali serikali iliahidi kuyashughulikia madai hayo, lakini kadiri siku zinavyokwenda, imekuwa ikiyapuuzia.

  Kiongozi huyo alisema kwa kuanzia, wamepanga kuonana na Waziri wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa, kueleza tatizo hilo ili kujua serikali inafikiria nini juu ya hatima ya madai yao.

  Mbali ya TALGWU, wastaafu wa EAC, jana waliamua kutoa kauli nzito na kutishia kufanya pigo moja kwa serikali wakisema kile watakachofanya kitalitikisa taifa na ulimwengu.

  Tishio hilo walilitoa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wao wa kujadili mikakati ya kuibana serikali iwalipe fedha zao.

  Mwenyekiti wa wastaafu hao, Nathaniel Mlaki, alisema wanataka kila mtu alipwe kiasi kisichopungua sh milioni 31 kutokana na kuitumikia jumuiya hiyo na pesa zao kukaa serikalini kwa muda usiopungua miaka 31.

  Alisema baada ya serikali kutoa orodha ndogo ya watu wanaostahili kulipwa ambayo hawakukubaliani nayo, wanajipanga kutoa pigo hilo ambalo litaushtua ulimwengu mzima.

  Hata hivyo waastaafu hao hawakuwa tayari kulitaja pigo hilo kwa madai kuwa serikali imekuwa ikituma wapelelezi wake katika mikutano hiyo.

  Alisema wapelelezi hao kamwe hawawezi kuambulia kitu safari hii, kwani pigo hilo linaandaliwa kwa tahadhari kubwa na kwa kuwatumia watu makini wasioweza kuhadaika kirahisi.

  Alisema mara ya kwanza walipanga kwenda Marekani lakini jambo hilo liligunduliwa na watu waliotumwa na serikali katika mikutano yao.

  “Tunajiandaa kufanya pigo moja takatifu ambalo litaushangaza ulimwengu na taifa kwa ujumla iwapo hatutapewa fedha zetu na hatutaki kulitaja pigo hilo,” alisema Mlaki.

  Alisema tabia ya serikali kuwapandikiza watu wake katika umoja wao ili kuwagawa kamwe haitafanikiwa, kwani wazee hao wamechoka dhuluma inayofanywa na serikali.

  Alisema wastaafu hao wana umoja imara, wenye lengo la kudai haki na nguvu zao walizolitumikia katika taifa hili ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa mwaka 1967 na kuvunjwa mwaka 1977.

  Alisema jitihada za serikali ni vema zikaelekezwa katika kutatua kero za wastaafu hao kwa kuwaandalia malipo lakini si kwa ajili ya kutaka kuvunja umoja wao.

  “Jitihada za serikali kuvunja umoja wetu kamwe hazitafanikiwa, wasipoteze muda kwa hilo, ni vema wakajikita katika kutulipa malipo yetu,” alisema Mlaki.

  Mlaki, alisema serikali imekubali kufanya mazungumzo nao kuhusu malipo yao na wanapanga siku ya kukutana baada ya jana kushindwa kufanya hivyo.

  Alisema misingi ya mazungumzo hayo wanataka isimame kwa kila mstaafu kulipwa si chini ya sh milioni 31, lakini si chini ya hapo.

  Aidha, alisema kauli ya serikali kuwa fedha wanazowalipa wastaafu hao ni mali ya walipa kodi, si za kweli, kwani Uingereza ilishatoa fedha hizo kupitia wakala wake wa Grown Agencies.

  Alisema fedha za walipa kodi ni zile zinazodaiwa na walimu na madaktari wanaogoma kila kukicha na serikali imekuwa ikihaha kuwatuliza lakini fedha za wastaafu zilikuwapo miaka mingi bila kulipwa wahusika.

  “Fedha zetu sisi si za walipa kodi ni za Malikia Elizabeth na zilishatololewa siku nyingi, hizo za walipa kodi ni zile za walimu na madaktari wanaogoma kila siku,” alisema Mlaki.

  Naye Makamu Mwenyekiti wa wastaafu hao, Sarah Kapella, alisema serikali itapata laana kwa kuwadharau wazee na kutowaogopa na kuwadhulumu haki zao waliozitolea jasho siku nyingi.

  Alisema hata vitabu vya dini vinaeleza kuwa wazee ni watu wa kuheshimiwa lakini serikali badala ya kuwaheshimu inawanyanyasa.

  “Serikali hii ina laana, yaani inatunyanyasa na kudai kuwa fedha zetu ni za kodi za wananchi wakati ukweli unajulikana wazi kuwa fedha hizo si za walipa kodi,” alisema Kapella.

  Alisema Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yusuf Mzee, akae kimya kuhusu jambo hilo kuliko kuanza kutoa kauli asizozijua kwamba wastaafu hao walishalipwa fedha na wengine wanaodai hawastahili kwani walikuwa vibarua.

  “Hebu angalieni serikali inavyojichanganya, hivi ni kibarua gani ambaye anaweza kufanya kazi kwa miaka 10 au kupewa likizo?” alihoji.

  Pamoja na wastaafu hao kuuungana, kuna dalili za serikali kutaka kuwagawa kwa makundi, baada ya baadhi ya viongozi kujiengua na kudai kuwa wao ndio wanaostahili kuwatetea wenzao.

  Jana kundi moja liliingia Wizara ya Fedha na Uchumi kudai kuwa mkutano uliokuwa ufanyike katika viwanja vya Mnazi Mmoja, umeahirishwa na vyombo vya habari vikapewa nakala ya barua iliyotoka kwa msemaji wa wizara hiyo.  Mod, ka imeshapostiwa waweza iondoa.
   
Loading...