Nchi ya Ahadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nchi ya Ahadi

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Njaare, Oct 1, 2010.

 1. N

  Njaare JF-Expert Member

  #1
  Oct 1, 2010
  Joined: Sep 26, 2010
  Messages: 1,075
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Tafakuri Jadidi


  [​IMG]Tumeiona nchi ya ahadi kwa mbali, tusonge mbele!

  [​IMG]
  Johnson Mbwambo​
  Septemba 29, 2010[​IMG]
  MIMI ni mtu mwenye mhemuko, na hata marafiki na ndugu zangu wanaujua udhaifu wangu huo (kama unakubali kuwa ni udhaifu). Hisia zangu ni kali kiasi kwamba hata hotuba tu yenye maneno ya simanzi inaweza kunitoa machozi nikiisikiliza au kuisoma!
  Moja ya hotuba ambazo hunitoa machozi kila mara ninapoisikiliza au kuisoma, ni ile iliyotolewa Aprili 3, 1968 na mtetea haki za watu weusi wa zamani wa Marekani, Dk. Martin Luther King Jr.
  Hotuba hiyo, maarufu kama Mountaintop Speech, ina maneno na kauli zenye hisia kali zinazonitoa machozi. Lakini nahisi kinachosababisha zaidi nitokwe na machozi, ni ukweli kwamba mpambanaji huyo wa haki za binadamu aliuawa kwa kupigwa risasi siku moja tu baada ya kutoa hotuba hiyo.
  Katika hotuba hiyo, Dk. Martin Luther King Jr. anawahimiza Wamarekani weusi (Waafrika-Wamarekani) kutokata tamaa na kuendelea kupigania haki zao kwa njia ya amani; maana tayari wameshafikia mahali pazuri ambapo itakuwa ni ujinga kukata tamaa na kurudi nyuma.
  Dk. Martin Luther King alisema hivi: “God has allowed me to go up to the mountain. And I have looked over. And I have seen a promised land. I may not get there with you. But I want you to know tonight that we, as a people, will get to the promised land.”
  Yaani (kwa tafsiri isiyo rasmi): “Mungu amenifikisha kileleni mwa mlima. Na nimeangalia pande zote nikiwa kileleni na kuiona nchi ya ahadi. Yawezekana sitakuwa hai kufika katika nchi ya ahadi nikiwa nanyi. Lakini nataka mjue, usiku huu, kwamba sisi kama Wamarekani weusi, siku moja, tutaifikia nchi ya ahadi.”
  Nirudie kueleza tena kwamba Dk. Martin Luther King Jr. aliuawa kikatili kwa kupigwa risasi siku moja baada ya kutoa hotuba hiyo yenye hisia kali. Ni kama vile alikuwa akitabiri kifo chake alipokuwa akisema usiku ule: “I may not get there with you…”
  Leo hii ukiisoma historia ya mapambano ya kale ya Wamarekani weusi (wenyewe hupenda kuitwa Waafrika-Wamarekani) na kuyafahamu mateso waliyoyapata chini ya tawala za ubaguzi wa rangi za Marekani, na ukizingatia kwamba udhalimu huo sasa umetokomezwa kiasi kwamba Marekani imeweza hata kuwa na rais mweusi (Barack Obama); hutasita kukubali kwamba “wameifikia nchi ya ahadi” kama alivyotabiri Dk. King miaka 42 iliyopita.
  Ndugu zangu, Oktoba 31, tutakuwa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Napenda kuyaazima maneno ya Dk. Martin Luther King katika hotuba yake ya Mountaintop kuwahimiza Watanzania wenzangu kutokubali kurudi nyuma; maana tumeshafika kileleni mwa mlima na kuiona nchi ya ahadi kwa mbali!
  Ninaposema tumeshafika kileleni na kuiona nchi ya ahadi kwa mbali; naamanisha manufaa ambayo tumeyaona katika bunge lililopita kwa kuwa na wabunge wachache wa upinzani waliokubali ‘kufa kidogo’ na kutetea maslahi ya taifa letu kwa nguvu zao zote bila kukatishwa tamaa na kejeli za wabunge wenzao wa CCM au watawala.
  Naamanisha watu kama Dk. Wilbroad Slaa, Zitto Kabwe, Hamad Rashid na wengine kadhaa. Nina hakika kama si wabunge hawa, umma wa Tanzania usingejua lolote kuhusu ufisadi mkubwa wa pesa zao unaofanywa na watawala kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa Ki-Mafia kama ule wa EPA, Richmond, Meremeta, Tangold, Rada, Twin Towers nk.
  Nimepata kusema huko nyuma, na narudia kusisitiza tena kwamba; kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa bungeni na kina Slaa, Kabwe, na Hamad , kwa kushirikiana na vyombo vya habari na NGOs kadhaa, siasa za Tanzania kamwe hazitakuwa tena kama zilivyokuwa; hata kama Kikwete atashinda tena urais Oktoba 31.
  Na hiyo ndiyo maana yangu ninaposema kuwa tumefika sote kwenye kilele cha mlima na tumeiona sote nchi ya ahadi, na hivyo tusikubali kukatishwa tamaa na kurejeshwa nyuma kwa ghiliba na hotuba za kisanii za baadhi ya wagombea wa CCM akiwemo Kikwete mwenyewe.
  Nimekuwa nikirudia kueleza, tena na tena, kwenye safu hii, kwamba, kama taifa, tumepotea nyikani na tunatangatanga. Tumepotea kwa sababu viongozi wa CCM wameiacha njia waliyoonyeshwa na Mwalimu Nyerere ya kutufikisha nchi ya ahadi, na baada ya kuiacha wametupoteza nyikani.
  Ni dhahiri watawala wa CCM hii ya sasa hawawezi kututoa nyikani na kutuweka katika njia sahihi itakayotufikisha nchi ya ahadi. Watakuja kina Mkapa na kina Kikwete watapiga usanii wao wa miaka kumi kumi. Watakuja wengine tena kutoka chama hicho hicho na kuendelea na usanii ule ule kwa miaka mingine kumi kumi, na bado hatutaiona njia ya kuelekea nchi ya ahadi.
  Tunamhitaji Nyerere mwingine wa kutuonyesha tena njia. Tunamhitaji Mussa wetu wa kutuongoza kuifikia nchi hiyo ya ahadi. Yeyote nchini mwenye kufikiri sawasawa atakubaliana nami kwamba ‘Nyerere mwingine’ au ‘Mussa wetu’ wa kutukomboa, hawezi kutoka katika chama hiki cha CCM katika mazingira yake ya sasa ambapo kimejenga uswahiba mkubwa na mafisadi wakubwa wa sampuli ya ki-Mafia!
  Ndiyo maana chama hiki CCM hakitaki wananchi waamshwe kuhusu ufisadi mkubwa unaoendelea nchini; kikidai eti Watanzania wamechoka kuusikiliza ‘wimbo wa ufisadi’. Lakini ndani ya mioyo ya viongozi wake wanajua kwamba kuzungumzia maendeleo mahali ambapo ufisadi umetamalaki, ni kucheza usanii! Mahali ambako uadilifu kwa viongozi na watawala umetupwa kapuni, kamwe hapawezi kuwa na maendeleo makubwa.
  Chukulia mfano wa tambo za uboreshaji miundombinu zinazotolewa hivi sasa na Rais Kikwete kwenye kampeni zake. Ni kweli kwamba barabara zimejengwa na kukarabatiwa hapa na pale nchini. Lakini ni ukweli zaidi kwamba kama uadilifu ungekuwepo kwa viongozi, barabara nyingi zaidi zingejengwa katika maeneo mengi nchini kuliko hizi wanazozizungumzia.
  Chukulia, kwa mfano, ufisadi unaoendelea kwa muda mrefu katika TANROADS inayoongozwa na Ephraim Mrema. Mabilioni kwa mabilioni ya pesa za walipa kodi yanapotea chini ya mikataba ya kifisadi ya ujenzi wa barabara; baadhi ikihusisha kampuni za Kikorea, Kichina na za wafanyabiashara wa Kihindi ambao CCM inawakumbatia kama wafadhili wake!
  Jambo la kusikitisha ni kwamba japo ufisadi huo umeanikwa hadharani na gazeti hili kwa muda mrefu, na hata kuzungumzwa ndani ya bunge, bado Rais Kikwete ameendelea ‘kumkumbatia’ huyo Mrema hadi dakika za mwisho; licha ya watendaji wake wa chini wizarani kupendekeza muda mrefu kwamba ang’olewe.
  Swali la kujiuliza ni kwamba mabilioni kwa mabilioni haya yaliyoyeyushwa TANROADS kwa mikataba ya kifisadi, yangesaidia kujenga na kukarabati barabara ngapi nchini kama yangeokolewa?
  Ninachojaribu kufafanua hapa ni kwamba kama Serikali ya CCM inajivuna, hivi sasa, kuwa imeimarisha au imejenga (mathalan) barabara 15, ukweli ni kwamba kama kusingekuwa na ufisadi mkubwa ndani ya TANROADS, na kama viongozi wangekuwa waadilifu, tusingezungumzia kujengwa barabara 15; bali tungezungumzia kujengwa hata barabara 30!
  Kwa hiyo, masuala ya ufisadi na uadilifu hayakwepiki katika kampeni au katika kujadili mustakabali wa nchi yetu; maana, kama alivyopata kusema Kikwete mwenyewe, mafisadi wanatafuna fedha za walipa kodi kama mchwa.
  Niende mbali kwa kusema kwamba kama CCM haitaki kusikia ‘wimbo wa ufisadi’, basi, Watanzania wana kila sababu ya kukipigia kura chama mbadala kitakachoufanyia kazi ‘wimbo’ huo; maana kwa mtazamo wa mtu yeyote mwerevu; hilo ndilo tatizo kuu la nchi yetu linalotufanya tuendelee kutangatanga nyikani bila kuiona njia ya kutufikisha nchi ya ahadi.
  Tukilitatua tatizo hili la ufisadi, ukosefu wa uadilifu na umomonyokaji wa maadili, safari yetu ya kuelekea nchi ya ahadi itakuwa fupi na rahisi; maana hakutakuwa na vikwazo vya aina ya skandali za Richmond, EPA, Meremeta, Rada nk.
  Aidha, hakutakuwa na tofauti kubwa ya kimapato kati ya walichonacho na wasichonacho, na wala hakutakuwa na kuoneana, kupendeleana katika ajira na vyeo au kuziachia maliasili zetu zinufaishe wageni; ilhali sisi wenyewe ni kilio na kusaga meno kwa dhiki!
  Ndugu zangu, Dk. Martin Luther King Jr. alisema kuwa amefika kileleni mwa mlima na kuiona nchi ya ahadi kwa mbali, na akasema yeye binafsi yawezekana akafa na asifike na watu wake katika nchi hiyo, lakini akatabiri kwamba, dhahiri, Wamarekani weusi wataifikia nchi hiyo siku moja.
  Nami nasema kina Slaa na kina Zitto na wabunge wengine kadhaa wa upinzani (wakiwemo wachache wa CCM) wametufikisha kileleni mwa mlima na kutuwezesha kuiona nchi ya ahadi kwa mbali.
  Kwa hiyo, ni wajibu wetu kutokubali kurejeshwa chini. Tusonge mbele sote kuitafuta njia ya kutufikisha nchi ya ahadi, na namna ya kusonga mbele ni kuchagua wagombea wengi zaidi wa upinzani (CHADEMA wengi zaidi na CUF wengi zaidi) kuingia bungeni ili sauti zao ndani ya bunge ziongezeke kiasi cha kuwaamsha watawala wetu serikalini waitafute kwa juhudi njia ya kufikia nchi ya ahadi.
  Kama alivyosema Dk. King; yawezekana wote hatutaishi kuweza kuifikia nchi hiyo, lakini hakika, kama Watanzania, ipo siku tutaifikia nchi hiyo.
  Tuombe tu Mungu kwamba watoto wetu au wajukuu wetu wakakapoifikia nchi hiyo, bado tanzanite, dhahabu na almasi zetu zitakuwa hazijamalizwa na wageni kwenye ardhi yetu!
  Tafakari.

  Source Raia Mwema
   
 2. Henge

  Henge JF-Expert Member

  #2
  Oct 1, 2010
  Joined: May 14, 2009
  Messages: 6,762
  Likes Received: 78
  Trophy Points: 145
  Nadhani ufisadi utangazwe kuwa janga la kitaifa na chama chochote ambacho kinatetea ufisadi hakifai kabisaaa
   
Loading...