Nchi Ilivyochezewa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,124


Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ilibariki kampuni ya bilionea wa Kimarekani ya Wengert Windrose Safaris Tanzania Limited, kupewa uwekezaji wa kimkakati, kupitia vitalu vya uwindaji inavyomiliki, kikiwamo kimoja isichokimiliki kisheria.

Agosti 20, mwaka jana, kwa kasi ya utendaji kazi isiyokuwa ya kawaida serikalini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilimwandikia mwekezaji huyo barua ya kutunukiwa Hati ya Uwekezaji wa Kimkakati; na siku hiyo hiyo aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, naye akawaandikia barua ndefu yenye kuchambua na kueleza fursa walizopewa.

Barua ya TIC na ya Nyalandu kwa mwekezaji huyo zilikuwa ni matokeo ya kikao cha Kamati ya Taifa ya Kuhamasisha Uwekezaji (NISC) kilichofanyika Agosti 17, mwaka jana, chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu. Waziri Mkuu wa wakati huo alikuwa Mizengo Pinda.

Katika kuipa uzito hoja yake na kuwatisha waliokuwa wakipingana na azma yake, Nyalandu alitoa nakala ya barua hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji, Juliet Kairuki.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East) ambacho ni mali ya kampuni ya Green Miles Safaris Limited; ndicho ramani yake imetumiwa kuwasilishwa TIC na hatimaye kufanikisha upatikanaji fursa hiyo kwa raia hao wa Marekani.

“Ramani iliyotumiwa na Wengert kumshawishi Pinda (Waziri Mkuu) ilikuwa feki kwa sababu wao si wamiliki wa kitalu hicho. Ushahidi wa hilo upo kwenye nyaraka mbalimbali za Wizara ya Maliasili na Utalii. Nyalandu alilijua hilo, lakini akaamua kumwingiza mkenge Waziri Mkuu,” kimesema chanzo chetu.

Kwa muda mrefu, kampuni ya Wingert Windrose Safaris Limited, imegoma kuachia kitalu hicho; lakini ingawa imekuwa ikisema inamiliki kitalu cha North South kilichobadilishwa jina na kuitwa North, bado inatumia ramani ya kitalu ambacho sasa ni mali ya Green Miles.

Mbinu hiyo iliifanya Serikali itoe ruhusa kwa mwekezaji huyo kujenga majengo ya kudumu kwenye vitalu ilivyopewa, kikiwamo hicho cha Lake Natron licha ya sheria kuzuia jambo hilo.

Pamoja na Wengert Windrose, kampuni nyingine zilizo chini ya Friedkin Conservation Fund na ambazo zitanufaishwa na uamuzi huo ni Tanzania Game Trackers Safaris Limited na Mwiba Holdings Limited.

Kampuni hizo zipo Lake Natron, Ranchi ya Mwiba, Makao WMA, Maswa Mbono na Maswa Kimali, Makere na Uvinza.

Pia Serikali ilimhakikishia mwekezaji huyo miaka 30 ya kuendelea kuwekeza katika vitalu ambavyo Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 inaagiza umiliki wa kitalu uwe miaka mitano tu.

Ingawa Sheria za Uhifadhi haziruhusu kampuni za uwindaji wa kitalii kuwa na askari wake wenye silaha, Nyalandu alihakikisha kwenye makubaliano hayo mpango unawekwa wazi ili askari walioajiriwa na Friedkin Conservation Fund kuwa na silaha. Hata hivyo, mpango huo utawezekana tu kwa kuzishirikisha wizara nyingine za Mambo ya Ndani ya Nchi, na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Pia, Nyalandu akitambua kuwa majina ya vitalu hivyo yalibadilishwa na Wizara ambayo yeye alikuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili, kwenye barua yake aliendelea kupuuza kuyatambua mabadiliko hayo na kuendelea kutumia majina ya zamani yaliyobadilishwa.

Juhudi zake za kutaka rafiki zake Wamarekani walitwae eneo hilo, zilifikia kilele baada ya kutumia ushahidi wa mkanda wa video uliowaonesha wageni wa Green Miles wakiwinda, kuifutia leseni hiyo. Licha ya Green Miles kukata rufani kwa kigezo kuwa wenye kustahili kuadhibiwa walikuwa ni Mwindaji Bingwa (PH) na Askari Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii waliohusika, Nyalandu alihakikisha anamaliza muda wake bila kushughulikia rufani hiyo.

Aliendelea hivyo licha ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Mei 6, mwaka jana kumwandikia barua na kumshauri: “Muda uliokwisha kupita tangu rufaa husika ilipowasilishwa kwako unatosha kuwa umeshashughulikia sababu yoyote ya msingi ambayo ingeweza kuwa ndiyo sababu ya kutotolewa mapema kwa uamuzi wa rufaa husika ya Green Miles Safaris Limited.

“Naomba kushauri ufanye uamuzi kuhusiana na rufaa hiyo mapema ili kila upande katika rufaa ujue hatima yake.”

Kimya cha Nyalandu, na barua ya AG Masaju vilimpa nguvu Waziri mpya wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Mei 9, mwaka huu afute adhabu aliyopewa Green Miles Safaris Limited.

Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 Kifungu 66(3) inaelekeza kuwa uamuzi uliofanywa na Mkurugenzi wa Wanyamapori kwa kutumia mamlaka yake katika Kifungu cha 66(1) na (2) cha Sheria hiyo unaweza kukatiwa rufaa dhidi yake kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya maliasili na utalii, ndani ya siku 30 tangu mwathiriwa wa uamuzi husika alipopokea uamuzi uliomwathiri.

Kwa kuzingatia kifungu hicho, AG Masaju alimshauri Nyalandu: “Japokuwa sheria hiyo iko kimya kuhusu muda ambao ndani yake rufaa kwa Waziri inatakiwa iwe imetolewa uamuzi na Waziri, matakwa ya Haki na Utawala wa Sheria yanataka uamuzi wa Serikali katika suala kama hili kutochelewa, isipokuwa kama kuna sababu ya msingi kwa ajili hiyo.”

Chanzo cha mgogoro

Ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii uliofanywa kwa msimu wa mwaka 2013-2018, kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited ilipata kitalu cha daraja la II cha Lake Natron Game Controlled Area (North South). Kampuni hiyo ilitaarifiwa uamuzi huo kwa barua ya Mkurugenzi wa Wanyamapori ya Septemba 6, 2011.

Kampuni ya Green Miles Safaris Limited ilipata kitalu cha daraja la I cha Lake Natron Game Controlled Area (North) na kupewa taarifa ya uamuzi huo Septemba 6, mwaka huo huo.

Baadaye, kampuni zote zilipewa taarifa ya mabadiliko ya majina ya vitalu. Kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (North-South) kikaitwa Lake Natron Game Controlled Area (North); na kile cha Lake Natron Game Controlled Area (North) kikajulikana kwa jina la Lake Natron Game Controlled Area (East).

Hadi Mei, 2013, kampuni ya Wingert Windrose iliendelea kuwa ndani ya kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East) ambacho kinamilikiwa kihalali na Green Miles Safaris Limited. Kampuni hiyo imeendelea kukalia kitalu hicho licha ya Green Miles Safaris Limited kulipa ada za kila mwaka zilizowekwa kisheria.

Lake Natron Game Controlled Area yenye vitalu vinne sasa baada ya kugawanywa kwa msimu wa uwindaji wa mwaka 2013-2018, awali ilikuwa na vitalu vitatu.

Marekebisho hayo yalimega sehemu ya kitalu kilichokuwa kinamilikiwa na Wengert Windrose na kutoa vitalu viwili. Kwa mabadiliko hayo, vitalu vinne na wamiliki wake wakawa ni:

1: Lake Natron GCA (North South) chenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,885-kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited

2: Lake Natron GCA (North) chenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,304-kampuni ya Green Miles Safaris Limited.

3: Lake Natron GCA (South-West) chenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,767-kilicho chini ya kampuni ya Michel Mantheakis Safaris Limited; na

4: Lake Natron GCA (South) chenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,768 kilichokabidhiwa kwa kampuni ya Kilombero North Safaris.

Mabadiliko hayo ya majina yalihusisha vitalu vitatu tu vya Lake Natron GCA pekee. Vitalu hivyo ni Lake Natron Game Controlled Area (North-South) kuwa Lake Natron Game Controlled (North)-kijiografia kitalu hiki kipo kaskazini mwa vitalu vingine.

Kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (North) kuwa Lake Natron Game Controlled Area (East). Kitalu hiki kipo upande wa mashariki mwa vitalu vingine; na kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (South-West) kuwa Lake Natron Game Controlled Area (West) ambacho kipo magharibi mwa vitalu vingine.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mara kadhaa Wengert Windrose wamekuwa wakitaka wachukue eneo lote la “North” na “East”, lakini mpango wao umegonga mwamba kutokana na kampuni ya Green Miles kugoma, lakini pia kwa kuzingatia matakwa ya kisheria yanayotaka kampuni ya kigeni isiwe na vitalu zaidi ya vitano.

Uamuzi wa Waziri Maghembe

Uamuzi wa Waziri Maghembe wa kuirejeshea leseni kampuni ya Green Miles unaelezwa kuwa umetokana na kujiridhisha kuwa kampuni hiyo ilifungiwa leseni kwa makosa, kwa vile waliostahili kuwajibiwa si mmiliki wa kampuni ambaye hahusiki kwa namna yoyote na wageni wanapokuwa wakiwinda, bali PH na askari wanyamapori.

“Dereva wa basi anapopita kwenye taa nyekundu anayeadhibiwa ni dereva! Huwezi kumwadhibu mmiliki wa basi kwa kumfutia leseni. Hili tukio kama busara ingetumiwa na Nyalandu, wa kufungiwa ni wale walioambatana na wageni kama kweli kulikuwa na makosa.

“Unafunga leseni lakini PH ameachwa, askari wanyamapori ambaye ni wa wizara anayepaswa kusimamia uwindaji, wanaachwa wote. Huwezi kufungia kampuni ambayo imewekeza mamilioni ya dola kwa makosa ya PH na askari wanyamapori.

“Alichofanya Waziri Maghembe ni haki kabisa, lakini nani hajui kuwa Nyalandu alifurahia kuifungia kampuni ya Green Miles ili rafiki zake Wamarekani wapate kitalu wanachokitaka kwa udi na uvumba?

“Unahitaji akili gani kubwa kujua hata haya waliyowapa kwenye Hati ya Uwekezaji wa Mkakati yanalenga urafiki zaidi kuliko miongozo ya kikanuni na kisheria?” kimehoji chanzo chetu cha habari.

Wiki iliyopita, Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara kupitia kwa Jaji Jacob Mwambegele, alitupilia mbali shauri lililofunguliwa na kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwenye shauri hilo lenye Na. 89/2016, Wengert walikuwa wakiomba Mahakama izue utekelezwaji wa agizo la Waziri Maghembe, la kuiondoa kampuni hiyo katika kitalu kinachomilikiwa na Green Miles.

Jaji Mwambegele alisema asingeweza kutoa uamuzi kwa shauri hilo kwa kuwa tayari lipo katika Mahakama ya Rufaa. Hiyo ilikuwa mara ya nne kwa Mahakama kutupa mashauri mbalimbali yanayofunguliwa yakizihusisha kampuni hizo mbili.

JAMHURI imewasiliana na Msemaji wa kampuni za Friedkin, Pratik Patel, kumtaka ufafanuzi juu ya mvutano huu, ila yeye akasema yupo safirini, na akaomba aelezwe ujumbe anaotafutiwa ndipo ajibu.

Baada ya kumweleza kuwa waliwasilisha ramani ya Kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East) kinachodaiwa kumilikiwa na Green Miles Safari na kuelezwa kuwa zipo barua kutoka wizarani zikiwataka kuachia kitalu hicho, alijibu kwa ufupi tu, akisema: “Ok.”

SOURCE: Gazeti la Jamhuri
 
Back
Top Bottom