Uchaguzi 2020 NCCR MAGEUZI: Ilani ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
1,259
2,000
1. ILANI YA CHAMA CHA NATIONAL CONVENTION FOR CONSTRUCTION AND REFORM (NCCR-Mageuzi) ITAKAYOTUMIKA KATIKA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2020

UTANGULIZI:
Mabadiliko ndiyo kitu pekee kinachodumu, na hayaepukiki. Kasi ya mabadiliko ya leo yanatokana na teknolojia. Hivyo basi, kazi kubwa ya mwanadamu ni kujijengea uwezo wa kuyapokea na kukabiliana na mabadiliko kwa njia chanya.

Teknolojia imetufungulia milango ya kupata taarifa mbalimbali kwa wepesi. Taarifa zinazoleta mabadiliko makubwa kuliko yote ni zile zinazotudhihirishia yale yaliyomo kwenye maandiko mbalimbali; kwamba sisi binadamu ni kitu kimoja na dunia ni kitu kidogo mno ndani ya uumbaji, na pia changamoto zote za kijamii zinatokana na kutolitambua hilo.

Sisi, NCCR-Mageuzi tulilitambua hili mapema na kuuhisha itikadi yetu ya Demokrasia ya Kijamii na kuwa itikadi ya UTU (hapa tunatumia herufu kubwa kwa uzito wa neno lenyewe). Katika utafiti, neno UTU hupatikana katika makabila na lugha nyingi barani Afrika. Watafiti wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema UTU ni Uafrika, ni Ubinadamu.

Hivyo basi, tumechambua misingi ya UTU kuwa ni Uhuru, Maadili, Udugu, Haki, Imani, Mabadiliko, Usawa, Wajibu, Kazi, na Endelezo (UMUHIMU WAKE). Na hii ndiyo misingi tutakayotumia katika kuendesha Serikali kwa lengo la kujenga jamii yenye Uhuru kamilifu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji, Haki za binadamu, Usawa na Ustawi wa jamii inayokubali kutegemeana kwa binadamu katika misingi ya umoja, ushirikiano na maridhiano.

Kwa kuwa tunaamini Uhuru kamilifu (kiuchumi, kisiasa na kijamii) ni ule unatokana na wanajamii kuweza kujiamulia na kujipangia mambo yao wenyewe, basi lengo letu kuu la kuwa Chama cha siasa chenye itikakadi ya UTU halitatimia bila ya kupata Katiba Mpya kwani tunaamini Katiba ni:

“Kauli ya Umma, inayotokana na Umma, Umma ujiongoze vipi”
Sasa ni miaka 28 tangu tulipoanza kudai Katiba Mpya. Madai haya yanatokana na msukumo wa mabadiliko ulimwenguni. Hatuwezi kuzuia mabadiliko. Katiba Mpya ni lazima! Katika ilani hii, tumeorodhesha sera zetu za kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa letu. Mipango hiyo ipo katika makundi manne: kimataifa, kibara, kikanda, na kitaifa. Kwa mfano mipango inayotokana na Malengo Endelevu ya Dunia (2015-2030), Ajenda ya Afrika (2013-2063), Malengo ya EAC, SADC, CEPGL, AEC na ICGLR, na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025. Hii ni mipango mingi lakini malengo yake yanaingiliana, na mingi ni endelevu ambayo lengo kuu ni kujali na kuheshimu UTU wa mwanadamu na Uhai wa dunia.

Nuru ya Utambuzi waudugu au umoja wetu wa kidunia au kitaifa, unatuangazia utambuzi wa giza linalotokana na kubaguana. Giza ambalo sisi NCCR-Mageuzi, tunalitambua kama Ujinga, Maradhi, Umaskini na Rushwa. Giza hili tuliamini, kama taifa, lilitokana na ubaguzi wa wakoloni, lakini miaka 59 ya uhuru inatusuta kwa kuendeleza fikra hiyo.

Ubaguzi unaotuumiza zaidi ni ule wa ndani, wa sisi kwa sisi ndani ya taifa, kuliko ule unofanyika kutoka nje. Ubaguzi wa ndani umeathiri sana siasa zetu na uongozi wa taifa. Ubaguzi umeleta hofu ya kuthubutu kufanana au kukubaliana katika siasa au uongozi pale inapobidi. Katika uongozi wa nchi, Rais huweza kuwa na sera tofauti na za Rais aliyetangulia. Hii haiwezi kuleta maendeleo endelevu. Sera ya serikali ya awamu moja inaweza isiendelezwe na serikali ya awamu inayofuata. Kwa mfano sera ya kupata Katiba mpya ilitekelezwa bila kukamilika kwa sababu ya kupata serikali mpya. Mwenendo huu unazidisha giza katika kujenga maendeleo.
Serikali chini ya NCCR-Mageuzi itaheshimu vipaumbele vya taifa, kwa sera zake na mikakati yake. Kwa kuwa vipaumbele vya taifa havijabadilika tangu kupata uhuru: kufuta Ujinga, Maradhi, Umaskini, na Rushwa, ilani zetu za uchaguzi tangu 1995 zimekuwa zikibadilika kidogo sana kuendana na mabadiliko ya kijamii.

I. UTEKELEZAJI WA ILANI HII NA SIFA ZA KIONGOZI
Serikali itakayoongozwa na Chama cha NCCR-Mageuzi itaweka mkazo katika kuimarisha mifumo ya kiutendaji ya serikali kuu na serikali za mitaa ili ufuatiliaji wa utekelezaji wa ilani uwe wenye tija kwa umma wa watanzania. Serikali itahakikisha usimamizi wa miradi ya serikali unafanywa kwa uwazi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, na mipango mbalimbali ya maendeleo hasa ile ya maendeleo endelevu ya dunia (2015-2030), dira ya taifa 2025 na ajenda ya Africa 2063.

Serikali hiyo itaongozwa na Watanzania wenye uwezo wa:-
1) Kusimamia zaidi maslahi ya mama Tanzania akiwa popote, ndani au nje ya nchi;
2)Kuisimamia na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulinda haki za binadamu;
3) Kuzuia upitishwaji wa sheria mbovu zinazokandamiza haki za binadamu ;
4) Kuwa wazi katika utendaji kazi wa serikali na wanaothamini katika dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya maendeleo ya umma;
5) Kuamini katika maendeleo shirikishi yenye kuinua uchumi na kuweka mazingira bora ya ajira;
6) Kuwajibika na kuwa tayari kufanya maamuzi magumu yenye tija kwa taifa letu kwa kuwawajibisha viongozi wengine wanaposhindwa kutimiza majukumu yao;
7) Kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo kwa umakini;
8) Kuwa mahiri katika kusimamia rasilimali za nchi yetu ikiwemo kupinga mikataba isiyo na tija kwa taifa;
9) Kukataa kupokea au kutoa rushwa, na kuwa tayari kuondoa mifumo ya rushwa na ubadhilifu nchini;
10) Kuthamini kwa dhati misingi ya usawa wa kijinsia kwa mapana yake; na
11) Kusimamia na kutetea maslahi ya watu wake anaowaongoza.

II. AJENDA ZETU KATIKA UCHAGUZI MKUU
NCCR-Mageuzi inaamini katika utawala wa kisheria, na uongozi shirikishi katika kujenga maendeleo endelevu katika jamii kwa kutumia itikadi ya UTU. Lengo kuu la kuanzishwa kwa chama chetu lilikuwa ni kupata Katiba Mpya, kama kiini cha uwezo wa kujipangia utaratibu wenye kuleta maendeleo kwa wote. Maendeleo yenye kulinda UTU wa kila mtanzania na uhai wa mazingira yetu.

Takwimu za kimataifa za mwaka huu kuhusiana na furaha ya mwanadamu, Tanzania tumeshika nafasi ya 153 kati ya mataifa 156. Furaha ya mwanadamu inaanzia katika kupata mahitaji msingi kulingana na mazingira aliyomo.

Hapa kwetu mahitaji hayo ni Afya njema, Uhuru wa kujiamulia, na fursa ya kujipatia kipato. Afya njema hutokana na kujipatia chakula bora na cha kutosha, maji safi na salama, malazi na makazi bora. Uhuru wa kujiamulia umejikita katika haki ya kutoa mawazo na haki ya kujumuika kwa sababu mbalimbali bila ya kuvunja sheria. Fursa ya kujipatia kipato inaanzia katika haki ya kupata elimu bora iliyo sawa kwa wote, mifumo ya uchumi iliyo rafiki kwa wafanyabiashara na isiyo na ubaguzi wa aina yoyote. kama ilivyoanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mikataba mbalimbali tuliyoridhia ya kikanda, kibara na kimataifa.
Kwa kuzingatia hayo, ajenda zetu katika uchaguzi Mkuu ni kama ifuatavyo:-
1) Muafaka wa Kitaifa
2) Katiba Mpya
3) Elimu
4) Afya na Ustawi wa Jamii
5) Mazingira na Makazi
6) Vyombo vya Habari na Asasi zisizo za Kiserikali
7) Usawa wa Jinsia na Makundi Maalum
8) Uchumi (Ardhi, Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, Mifugo, Viwanda, Biashara, Madini, Nishati, Maliasili na Utalii, Sanaa Utamaduni na Michezo, na Miundombinu ya usafiri)
9) Usalama wa Taifa
10) Vita Dhidi ya Rushwa

1. MUAFAKA WA KITAIFA
Iwapo kutakuwa na sababu isiyozulika ya kutokupata au kuchelewesha upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu ujao 2025, Serikali ya NCCR-Mageuzi itaanzisha mchakato wa kupata kwanza Muafaka wa Kitaifa. Hii ni kwa ajili ya kuleta maelewano, amani, na utawala bora. Muafaka wa kitaifa utajumuisha makubaliano katika mambo ya msingi yenye maslahi mapana kwa Taifa, licha ya watu kusimamia itikadi tofauti.

Aidha, muafaka utahusu maridhiano juu ya maadili ya kitaifa. Katika ajenda hii, Serikali ya NCCR-Mageuzi itahamasisha kuhusu muafaka juu ya misingi mikuu ya utaifa wetu. Misingi ambayo itapendekezwa na kukubalika na jamii kwa ujumla bila kujali itikadi za vyama, dini, kabila, nasaba au jinsia.

Muafaka wa kitaifa utatusaidia kupanua wigo wa fikra zetu kuhusu maadili ya viongozi na wananchi. Hivi sasa mjadala kuhusu maadili ya taifa umejali tu suala la ufisadi, lakini hoja hii ni pana kuliko ufisadi. Lazima tuzungumzie malezi ya taifa, misingi na sababu ya malezi hayo, uzalendo wetu na masuala mengineyo.

Vilevile, muafaka wa kitaifa utatuwezesha kupata Tume Huru ya Uchaguzi; na pia kuondokana na mfumo wa utawala wa chama dola Hatuna budi kuafikiana (kuwa na muafaka) kwamba licha ya tofauti zetu za kiitikadi yapo masuala ambayo chama chochote kitakachoshika madaraka lazima kiyaheshimu maana hayo ni yetu sote kama taifa.

2. KATIBA MPYA
Katiba ya nchi ndiyo sheria kuu ya nchi. Sera za serikali na sheria za nchi lazima zitokane na kufungamana na katiba ya nchi. Kama Taifa lina katiba mbaya isiyolinda haki za wananchi, basi sheria na mfumo wa utoaji wa haki utakuwa mbaya na usiotenda haki, na watendaji wa vyombo vya dola hawatatenda haki kwa kuwa haki haipo kisheria.

Kutokana na kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya uliotekelezwa kwa sehemu kubwa na muhimu, lakini ukakwama, basi ni dhahiri sasa Katiba Mpya ni takwa la watanzania wengi. Ajenda yetu kuu ya kuanzisha chama chetu, sasa inaungwa mkono na wananchi wengi.

Tutafanya nini Kuhusu Katiba?
Serikali ya NCCR-Mageuzi itarejesha na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya kupitia Bunge la Katiba lenye kujumuisha makundi yote ya kijamii.
Maboresho tutakayosimamia katika Katiba Mpya ni kama ifuatavyo:-

1) Kupata Muafaka wa kitaifa.
2) Kuipa Katiba ukuu wake wa kikatiba, ikiwa ni pamoja na kujilinda bila ya kutegemea sheria nyingine za nchi. Uvunjaji na ukiukwaji wa Katiba kuwa kosa la jinai.
3) Kuongeza wigo wa uhuru na haki za msingi za binadamu katika Katiba.
4) Kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
5) Kugatua madaraka kutoka serikali kuu kwenda mamlaka ya serikali za mitaa.
6) Kumpunguzia Rais wa nchi madaraka yake, ikiwemo kujaza baadhi ya nafasi za kazi serikalini kwa kuteua.
7) Kuwapa wananchi mamlaka ya kuwa ndio wamiliki na watawala wa taifa lao katika shughuli zote zinazohusu maslahi yao na taifa lao kwa ujumla na hivyo:-
(a) Kuweka sheria na taratibu za kuwawezesha wananchi kudhibiti na kuwajibisha dola na vyombo vyake ili viwatumikie badala ya vyombo vya dola kutumikiwa na wananchi, na
(b) Kuweka vyombo vya kutekeleza sera ya uzawa katika uchumi na uwezesho wa vijana, wanawake na wenye ulemavu.
8) Kuhifadhi kikatiba haki za binadamu ambazo hazijahifadhiwa na Katiba ya nchi kama vile haki ya mgombea binafsi, haki ya elimu, haki ya afya, haki ya kupata habari na haki nyinginezo.
9) Kuitambua sekta ya habari kikatiba ili kuimarisha demokrasia, uhuru na haki za vyombo vya habari.
10) Kulipa bunge la Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania nguvu kama chombo cha kutetea maslahi ya wananchi na kuwa na maamuzi ya mwisho katika utungaji wa sheria, kuridhia mikataba na kuwa na mamlaka ya kupitisha/kuthibitisha au kutopitisha/kutothibitisha uteuzi wa viongozi muhimu wa dola/serikali.

3. ELIMU
Udhaifu uliopo katika sekta ya elimu hususan mfumo wa utoaji elimu ndicho kirusi kilichoambukiza udhaifu kwenye sekta nyingine zote katika taifa. Tunaamini uelewa wa mwanadamu unatokana na mifumo ya elimu inayotumika katika eneo lake. Raia mwenye elimu na uelewa wa mazingira yake na haki zake atakuwa raia mwema kwa maendeleo yake binafsi na ya jamii kwa ujumla. Utafiti umeonesha upo uhusiano sababishi kati ya elimu duni na ukengeufu katika jamii na hatimaye utendaji dhaifu katika uchumi na siasa za nchi. Uhusiano huu umethibitika kitaalam.

NCCR-Mageuzi tunaamini kuwa ili nchi iweze kupiga hatua katika nyanja zote za maisha hatuna budi kuiboresha mifumo yetu ya elimu ili iweze kuwa injini na chachu kwa maendeleo ya taifa letu. Hii inajitokeza hata kwenye Dira ya Taifa ya 2025 ambapo inataja, pamoja na mambo mengine kwamba, ifikapo mwaka 2025 tuwe tumejenga taifa la watu walioelimika kwa upeo wa juu katika nyanja mbalimbali; na pia katika malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Taifa 2030, lengo la 4 ni kuhakikisha elimu bora, shirikishi na sawa kwa wote inapatikana.

Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya nini kuhakikisha elimu inakuwa bora?
Ili kufanikisha mageuzi hayo, serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya mambo yafuatayo:-

(a) Maudhui ya Elimu
1) Itaweka wazi falsafa ya elimu ifaayo kwa Tanzania ya sasa;
2) Itaboresha sera ya elimu na miongozo yake, kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu ili kuipa maudhui ya UTU;
3) Itahakikisha kwamba mtaala wa mfumo rasmi wa elimu nchini una manufaa katika maisha halisi ya mtu mmoja mmoja; na
4) Itaanzisha mpango kabambe wa elimu ya uraia na elimu ya maisha kwa jamii yenye maudhui ya UTU kupitia mifumo yote ya elimu, rasmi na isiyo rasmi.

(b) Mfumo wa Elimu
1) Itahakikisha elimu ya awali (chekechea) inatolewa nchi nzima katika maeneo ya makazi, maeneo ya kazi, na kwenye kila shule ya msingi ili kuwa na malezi makini kwa watoto na kuwapa fursa wanawake wazazi kushiriki katika shughuli zingine za kukuza familia na taifa;
2) Itaimarisha miundombinu ya shule, hasa maji safi na salama, na vyoo;
3) Itaendeleza lengo na dhamira ya kufuta ada na michango katika shule za serikali;
4) Itaweka mpango wa wasichana wote wa Elimumsingi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua;
5) Itaanzisha Tume itakayotoa ushauri juu ya ubora wa elimu yetu, na itakayohusisha wadau mbalimbali;
6) Itaboresha afya za wanafunzi kwa kupanua programu ya lishe mashuleni kwa lengo la boresha uelewa katika kujifunza na kupunguza utoro;
7) Itahakikisha kunawekwa umeme katika kila shule ili kuwezesha wanafunzi kuitumia vema teknolojia ya TEHAMA;
8) Itaanzisha mfumo mpya wa elimu ya msingi unaojumuisha elimu mpaka kidato cha nne itatolewa bure (bila malipo ya ada) kwa watoto wote wa kitanzania;
9) Itaanzisha elimu ya sekondari itakayochukua miaka miwili (sawa na kidato cha cha tano na sita) yenye lengo la kuandaa vijana kuingia vyuo vikuu. Elimu hii itatolewa pia bila malipo ya ada;
10) Itaanzisha vyuo vya ufundi na mafunzo kwa vitendo kwa wale ambao hawakuchaguliwa kwenda sekondari (kidato cha tano na sita) ili kuwaandaa kwa ajira au kujiunga na vyuo vya elimu ya juu vya ufundi na teknolojia;
11) Itapanua elimu ya vyuo vikuu kwa kuanzisha vyuo vikuu vipya ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kuupatia kila mkoa angalau chuo kikuu kimoja;
12) Itatoa elimu ya vyuo vikuu vya serikali kwa masharti nafuu, badala ya mikopo ya elimu ya juu inayowatesa wahusika;
13) Itapanua vyuo vikuu vilivyopo na kuboresha viwango vya taaluma, mazingira ya kujifunzia na mazingira ya kazi kwa wahadhiri /waendeshaji;
14) Itaboresha mishahara, marupurupu na pensheni za walimu, wakufunzi, na wahadhiri ili iwiane na viwango vya taaluma zao, na gharama halisi za maisha;
15) Itaanzisha vyuo vipya vya ualimu kulingana na mahitaji ya walimu wa fani mbalimbali za elimu, ufundi na teknolojia;
16) Itapanua vyuo vya ualimu vilivyopo na kuboresha elimu inayotolewa kulingana na mahitaji mapya ya mfumo mpya wa elimu utakaoanzishwa; na
17) Itahakikisha hakuna kaya inayokwama kumpeleka mtoto shule kwa sababu yoyote ya kijamii au kukosa mwamko.

(c) Sera ya Elimu
1) Itabadili sera ya elimu ya taifa kwa kuipa maudhui, na upeo kulingana na mahitaji ya kimaadili ya kimaendeleo ya taifa.
2) Itaweka 30% kuwa kiwango cha chini cha bajeti ya taifa kwa ajili ya elimu.
3) Itaanzisha utaratibu wa shule za bweni za wasichana ili kuzuia mimba za utotoni, kuepuka kutembea umbali mrefu na kuondokana na kufanya shughuli za nyumbani ambazo zimekuwa zikiathiri vibaya maendeleo yao ya kitaaluma.
4) Itaweka uwiano mzuri kati ya wanafunzi wa kiume na wa kike wanaojiunga na masomo vyuoni, na kuweka hoja za jinsia, uraia, haki za binadamu na utaifa katika mihutasari.
5) Itaanzisha chuo cha taifa cha kufundisha watu wazima hasa viongozi wa sekta mbalimbali ili kujenga utamaduni wa viongozi wenye kupenda kujielimisha.
6) Itaondoa kodi kwenye vifaa vya elimu na kuzipa ruzuku taasisi binafsi zinazoshiriki kutoa elimu rasmi ili kuziongezea uwezo wa kutoa huduma ya elimu kwa jamii inayofanana na ile ya taasisi za serikali.
7) Itahamasisha, itawezesha na itatoa vivutio na motisha kwa watafiti na wanasayansi ikiwa ni pamoja na kutunza na kulinda uvumbuzi wao.

4. AFYA NA USTAWI WA JAMII
Msingi mkuu wa Ustawi wa jamii yoyote ni afya na sia njema ya wanajamii. Takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba katika suala la furaha ya mtu mmoja mmoja, Tanzania tumeshika namba ya 153 kati ya mataifa 156 kwenye utafiti huo. Afya njema huendana pia na furaha ya moyoni. Itikadi yetu inatuongoza kulifanyia kazi swali hili la afya kwa nguvu zote.

Huduma za Afya hivi sasa ni kama ifuatavyo :
• Idadi ya vituo vya afya ni ndogo kulinganisha na idadi ya wakazi, kata nyingi
• Bima za afya ni mzigo kwa wananchi wengi na bado kuwafikia wananchi wote
• Uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama COVID-19, ni mdogo
• Kuna tofauti kubwa ya uwiano kati ya wagonjwa hospitalini na madaktari, hasa madaktari bingwa ; hii inadhoofisha ufanisi wa kazi kinyume na UTU
• Elimu ya kujikinga na magonjwa ni dhaifu, hasa kwa upande wa lishe kama kinga.

Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo:-
1) Itaimarisha afya ya msingi na kuanzisha programu za kudumu na kudhibiti vyanzo vyote vya magonjwa nchini, na kuzuia maambukizi. Mpango huu utajumuisha elimu ya afya kwa watu wote na uangamizaji wa mazalia ya wadudu wanaoeneza maradhi.
2) Itaimarishwa afya ya mama na mtoto kwa kusogeza huduma za afya karibu na makazi ya watu; pia itatoa chanjo pamoja na elimu kuhusu magonjwa hatarishi kwa mama na mtoto.
3) Itaimarisha program ya ukusaji wa damu salama na uhifadhi wa damu katika hospitali zetu.
4) Itarejea mara kwa mara kwa maslahi ya watoa huduma kwa kuongeza mishahara na marupurupu mengine
5) Itakamilisha lengo la taifa la kuwa na Zahanati kila kijiji, Kituo cha Afya kila Kata, na Hospitali kila Wilaya.
6) Itaendeleza sera ya ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), katika kutoa Huduma.
7) Itaimarisha tafiti za tiba za maradhi mbalimbali kwa kutumia wataalam wa ndani na nje ya nchi.
8) Itaboresha taasisi za afya ikiwemo NIMR, MSD, TFDA, NHIF na CDC ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
9) Itadahili wanafunzi 30,000 katika Vyuo vya Afya na Ustawi wa Jamii ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni jitihada za kutosheleza mahitaji ya rasilimali watu katika sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii
10) Itaimarisha mapambano dhidi ya malaria, TB, na UKIMWI.
11) Itaimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya saratani, mishipa ya fahamu, mapafu, figo, huduma za magonjwa ya moyo, na upasuaji
12) Itaifanya Tanzania kuwa na kituo cha utalii cha huduma za afya
13) Itaunganisha mifumo ya ukusanyaji na utoaji taarifa za afya kwa lengo la kuwa na mfumo mmoja mkuu wa aina hiyo nchini
14) Itaweka utaratibu utakaomwezesha kila mwananchi kumudu kuwa na Bima ya Afya yenye ubora
15) Itawahamasisha na kuwawezesha wafamasia na wawekezaji wananchi kuanzisha viwanda vya utengenezaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba.
16) Itaongeza, itakarabati na itaimarisha huduma za kibinadamu katika vituo vya kuwasitiri watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism), na pia wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu au walio katika mkinzano wa sheria
17) Itaanzisha mpango maalum wa kuwapatia wazee posho ya kujikimu kwa ajili ya mahitaji msingi
18) Itaweka utaratibu wa kutoa huduma za afya bure kwa wazee walio na umri wa miaka sabini (70) au zaidi.

5. MAZINGIRA NA MAKAZI
NCCR-Mageuzi tunatambua kuwa uhai wa binadamu unapata thamani yake endapo binadamu, mimea na viumbe vingine wanaishi katika mazingira salama. Kwa kutambua jambo hilo;moja ya madhumuni ya NCCR-Mageuzi ni kuhakikisha Tanzania ina kuwa na mazingira safi na salama.
Hali ya Mazingira yetu kwa Sasa
Katika bahari, maziwa, mito na baadhi ya vyanzo vya maji kwa uchafuzi uliokithiri; ukataji wa miti na uchomaji wa misitu kuendelea; Kilimo na Uvuvi haramu kuongezeka; utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani na majumbani bado kuthibitiwa; na Makazi holela kuongezeka
Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo:-
1) Itaiwekea mkazo sheria ya NEMC kuhusu uchafuzi wa mazingira.
1) Itatoa elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya zana za kilimo na uvuvi; na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
2) Itahamasisha wananchi kusafisha na kuweka safi makazi yao, sehemu za wazi kama fukwe za bahari na maziwa ili ziwe sehemu salama za kupumzikia.
3) Itatilia mkazo sheria dhidi ya ujenzi holela hasa kwa kutoa elimu.
4) Itaendeleza mfumo wa kutoa anuani za makazi ili wananchi waweze kufikiwa kwa urahisi na watoa huduma mbalimbali.
5) Itatizama upya maeneo yaliyotengwa ya wazi kwa ajili ya kupumzikia na kwa watoto kucheza.
6) Itajenga kuta za kudumu katika mito inayopita maeneo ya makazi au viwandani.
7) Itendeleza kampeni dhidi ya utupaji taka ovyo.
8) Itaanzisha utaratibu wa kumudu taka za aina mbalimbali (waste management)
6. VYOMBO VYA HABARI NA ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI
Sera za NCCR-Mageuzi zitatoa nafasi maalum kwa vyombo vya habari na Asasi zisizo za Kiserikali kwa kuwa zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana katika mageuzi ya kidemokrasia nchini na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Hali Ilivyo Sasa
Haki na uhuru wa vyombo vya habari kutokulindwa na Katiba ya nchi.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya nini?
Ili kuviwezesha vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali kuwa huru na kufanya kazi vizuri kwa manufaa ya wananchi, serikali itakayoongozwa na NCCR-Mageuzi itachukua hatua zifuatazo:-
1) Italinda haki na uhuru wa vyombo vya habari kama ilivyoanishwa katika mikataba tuliotia saini au kuridhia
2) Itahakikisha sekta ya habari inatambulika katika Katiba Mpya.
3) Itapunguza kodi za vitendea kazi vya vyombo vya habari vitakavyotoa huduma vijijini na kuendesha programu za elimu na maendeleo
4) Itapanua mafunzo ya uandishi wa habari na utangazaji kwa kiwango cha kimataifa.
5) Itarahisisha utaratibu wa usajili wa asasi zisizo za kiserikali.
7. USAWA WA JINSIA NA MAKUNDI MAALUM
A. Usawa wa Jinsia
Ili kujenga usawa wa jinsia na kutokomeza maonevu ya kihistoria na mila potofu zinazomdhalilisha mwanamke, serikali ya NCCR-Mageuzi itawapa wanawake nafasi na fursa maalum ili kurekebisha athari za maonevu waliyoyapata katika historia kama ifuatavyo:
1) Kuwa na idadi iliyosawa ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uwakilishi na kupanua mfumo wa uwakilishi wa uwiano(50-50).
2) Kuridhia na kutekeleza mikataba yote ya umoja wa mataifa, umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika kwa manufaa ya watanzania ili kujenga jamii yenye kutamalaki haki za binadamu na yenye kufurahia usawa kati ya wanaume na wanawake.
3) Kuwapo kwa wanawake katika ngazi mbalimbali muhimu za uongozi wa nchi kama ifuatavyo:-
a) Kuwepo kisheria kiongozi mwanamke miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya nchi yetu ambao ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuuri ya Muungano wa Tanzania.
b) Kuwa na Spika wa Bunge au Baraza la Wawakilishi mwanamke na naibu Spika atakuwa mwanaume au kinyume chake
c) Kuzingatia usawa wa jinsia katika nafasi mbalimbali za kiutawala kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, mabalozi, makatibu wakuu wa wizara, makamishna, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wenyeviti na wajumbe wa bodi za mashirika ya umma
d) Itaendelea kusisitiza vyama vya siasa, taasisi za umma na binafsi kuhakikisha wanadumisha dhana ya usawa wa jinsia
12
e) Kuwa na meya wa jiji /mji au mwenyekiti wa Halmashauri mwanamke na Naibu meya au makamu mwenyekiti mwanamke au kinyume chake
f) Kuwezesha matumizi ya vifaa vya kisasa majumbani ili iwe rahisi kwa jinsia zote kushiriki katika kazi za kuhudumia familia
g) Kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapelekwa shuleni
h) Kuungana na taasisi mbalimbali katika programu za kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni, ukeketaji na mila zisizofaa kwa kuimarisha huduma ya dawati la jinsia katika vituo vya polisi na kuwezesha vituo vya wasimamizi wa sheria katika Vijiji,Kata, Wilaya na Mikoa

B. Makundi Maalum
Serkali itakayoongozwa na NCCR-Mageuzi itatekeleza yafuatazo kuhusu makundi maalumu:-
(a) Watu wenye Ulemavu
1) Kutoa nafasi maalumu katika mabaraza ya uwakilishi kwa ajili ya wenye Ulemavu.
2) Kutunga sheria za kusimamia maslahi ya wenye Ulemavu katika huduma za umma na kuwawezesha kufanya shughuli za kujipatia kipato.
3) Kuwa na programu ya kuwatambua na kuwalinda dhidi ya vitendo vinavyoshusha na kutweza UTU wao vikiwemo ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu.
4) Kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanalindwa dhidi ya ukatili na ubaguzi wa aina yoyote.
5) Kuhakikisha vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika kupata au kutoa elimu vinapatikana kwa urahisi na kutumika.
6) Kukakikisha wanaweza kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi.
7) Kuhakikisha haki za kupata ajira na kufanya kazi zinalindwa.
8) Kupata huduma bora za afya bila ubaguzi.
9) Kuhakikisha majengo ya umma yanakuwa rafiki kwa wenye Ulemavu.

(b) Wazee
1) Kuhakikisha wazee wanawekewa utaratibu wa kisheria wa kupatiwa huduma za matibabu bila malipo.
2) Kuthamini mchango wa wazee katika kukuza na endeleza taifa letu kwa kuweka utaratibu na vigezo vitakaowezesha wazee wote nchini kulipwa pensheni
3) Kuhakikisha kuwa wazee wa taifa letu wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili vikiwemo mateso na mauaji.
4) Kuongeza nyumba za kuwatunzia wazee kwa kuboresha hadhi ya majengo wanamoishi wazee, kuongeza majengo kila mkoa na wilaya na kuhamsisha wananchi na taasisi mbalimbali kusaidia kutoa kuduma kwa wazee.

(c) Watoto
1) Kuweka maslahi ya watoto katika kutekeleza shughuli zake za kiserikali, kibunge na kimahakama.
2) Kuhamasisha wanajamii kulinda watoto dhidi ya vitendo vya kinyanyasaji na ukatili.
3) Kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa shule.
4) Kuanzisha programu ya kutenga maeneo ya kuchezea watoto karibu na mazingira yao kwa ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji.
5) Kuendeleza vita dhidi ya mila potofu za kukeketa watoto wa kike, ndoa za utotoni na kuendelea kuimarisha adhabu kwa wale wote wanaokatisha masomo kwa watoto kwa sababu mbalimbali.
6) Kuelimisha jamii juu ya athari za migogoro ya kifamilia na athari zake kwa watoto.

(d) Wanawake
1) Kuwa na idadi iliyosawa ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uwakilishi na kupanua mfumo wa uwakilishi wa uwiano (50-50), pale inapowezekana, katika ngazi zote za uongozi.
2) Wanawake wanapata haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, udhalilishaji, dhuluma, unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na mila potofu.
3) Kuhakikisha kuwa ajira za wanawake zinalindwa wakati wa ujauzito na pale wanapojifungua.
4) Kuridhia na kutekeleza mikataba yote ya umoja wa mataifa, umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika kwa manufaa ya watanzania ili kujenga jamii yenye kutamalaki haki za binadamu na yenye kufurahia usawa kati ya wanaume na wanawake.
5) Kuhakikisha kuwa elimu ya afya ya uzazi inatolewa nchi nzima kwa kuhamasisha wananchi kufuata njia bora za uzazi.
6) Kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya wanawake.

(e) Vijana
1) Vijana wanashiriki kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi ya taifa letu kutegemeana na sifa, weledi, na uadilifu, kwa kuunda na kuimarisha Baraza la Vijana la Taifa.
2) Kutoa elimu kwa vijana kwa kuwatumia wadau mbalimbali ili kuwajenga kuwa wazalendo.
3) Kuviibua, kuvitambua na kuviendeleza vipaji vya vijana katika nyanja za michezo, sanaa, elimu, ubunifu na uongozi.
4) Kuhamasisha vijana kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu.

8. UCHUMI
A. Ardhi

Serikli ya NCCR-Mageuzi itaendelea kutekeleza mipango ya kuendeleza ardhi kama ifuatavyo:-
1) Itaboresha Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System) utakaorahisisha umilikishaji wa ardhi na uhifadhi wa kumbukumbu za ardhi.
2) Itaimarisha huduma za ardhi kwa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuongeza kasi ya utoaji wa Hatimiliki za Kimila nchini.
3) Itazijengea uwezo Halmashauri za Miji na Wilaya kwa kuzipatia mafunzo, vifaa, rasilimali fedha na wataalam ili ziweze kupima viwanja na mashamba nchini.
4) Itaanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi ili uweze kufidia ardhi itakayotwaliwa kwa matumizi ya umma na uwekezaji.
5) Itafanya uhakiki wa mashamba pori yasiyoendelezwa kwa kipindi kirefu na kugawa upya kwa wananchi kwa kufuata taratibu za kisheria.
6) Itaanzisha Baraza la Taifa la Ushauri la Ardhi (National Land Advisory Council) ili kuwezesha ardhi kutumika kwa ufanisi.
7) Itatoa elimu kwa umma juu ya Sheria za Ardhi, Sheria ya Mipango miji, Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Sheria zingine zinazohusiana na utawala wa ardhi.
8) Itaimarisha huduma ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kuwa na vyombo vya maamuzi kama mahakama ambazo zitahakikisha mashauri ya migogoro ya ardhi yanawasilishwa kwa njia rahisi na kwa gharama nafuu ili kuhakikisha wananchi wanaifikia makahama kwa urahisi.
9) Itahakikisha maafisa ardhi wasio waaminifu wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za kinidhamu za kiutumishi.
10) Itawaelimisha wananchi kuzielewa sheria za mikopo ya nyumba ili wazitumie kupata mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya kujenga au kununua nyumba na kuhamasisha mabenki na asasi nyingine za fedha zitoe mikopo ya nyumba kwa muda mrefu na yenye riba nafuu

B. Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
Kwa kuwa ukulima na ufugaji ni shughuli zinazoajiri takribani asilimia 87 ya nguvu kazi ya taifa na kwa kuwa asilimia 44 ya pato la taifa linatokana na sekta hii, NCCR-Mageuzi inalenga kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuboresha maisha ya wahusika, na uchumi upate kuimarika. Hivi sasa sekta hii imebakia nyuma kiteknolojia na uwezeshwaji wa wananchi wanaoshiriki katika uzalishaji mali katika sekta hii ni mdogo mno. Wakulima walio wengi hutegemea jembe la mkono na mvua. Wafugaji huchunga mifugo yao badala ya kufuga kwa kutumia mbinu za kisasa zenye tija kubwa zaidi.

Ili kukabiliana na hali hii isiyoridhisha, serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo:
1) Itawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuboresha mifumo ya utoaji wa ruzuku na pembejeo pamoja na kuwaunganisha wakulima na taasisi za fedha ili kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara chenye tija na ambacho mazao yake yatakuwa yameongezewa thamani kwa uzalishaji wa bidhaa za kilimo na chakula kwa ajili ya soko la ndani na nje.
2) Itawezesha wananchi kiujasiriamali katika sekta ya kilimo ili waanzishe miradi mbalimbali ya kuzalisha bidhaa za kilimo na mifugo pamoja na viwanda vya kusindika bidhaa zilizo tayari kwa matumizi ya binadamu kwa ajili ya soko la ndani na nje.
3) Itatoa elimu kwa wakulima juu ya kanuni bora za kilimo, miradi ya umwagiliaji, matumizi ya majosho na kuongeza idadi ya maafisa ugani na washauri wa kilimo.
4) Itatengeneza mpango imara na endelevu wa huduma za ughani katika huduma za kilimo na mifugo.
5) Itaimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua kwa kuongeza eneo la umwagiliaji.
6) Kutathmini aina za mbegu bora za mazao mbalimbali zenye sifa ya kutoa mavuno mengi, zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi na zenye viinilishe vingi.
7) Itaboresha mfumo wa utafiti wa kilimo nchini ili matokeo ya tafiti hizo yawafikie wakulima kwa kupanua vyuo vya kilimo na utafiti kuhusu mbinu za kilimo, ardhi, mbegu bora na udhibiti wa maradhi ya mifugo na mimea.
8) Itahamasisha sekta binafsi na vyama vya ushirika wa mazao kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo hususan kwenye maeneo ya uzalishaji wa mazao hayo.
9) Itaanzisha masoko yenye hadhi na mvuto wa kimataifa katika miji ya mipakani ili kuimarisha biashara na nchi jirani.
10) Itafuta kodi kwa wakulima na wafugaji kufidia gharama za pembejeo, madawa na pia itafuta kodi ya mazao ya kilimo na mifugo.
11) Itatunga upya sheria ya ushirika ili kutoa uhuru kamili kwa vyama vya ushirika kuendesha shughuli zake na kuwezesha vyama hivyo kiujasiriamali katika mifuko ya hifadhi ya jamii ya wakulima na wafugaji.
12) Itaanzisha taasisi za bima na usalama wa kipato cha mkulima na mfugaji
13) Itapitia upya mgawanyo wa matumizi ya ardhi nchi nzima kwa kuainisha na kupima maeneo ya ardhi ya kilimo ili kuwawezesha wakulima kujiajiri katika sekta ya kilimo
14) Itaandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kilimo kwa kuendelea kupima mashamba ya wakulima na kutoa hati miliki za kimila kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuondoa migogoro ya ardhi na kutumia hati hizo kama dhamana ya kupata mikopo.
15) Itawezesha upatikanaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo kwa kushirikisha sekta binafsi kujenga miundombinu ya masoko na maghala bora ya kuhifadhia mazao mbalimbali.

C. Mifugo
Serikali ya NCCR-Mageuzi itajizatiti kuhakikisha kuwa sekta ya mifugo inaleta tija ili kuweza kuinua hali ya maisha na ya wahusika. Serikali itahakikisha yafuatayo yanatekelezeka:-
1) Kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji nchini ili kuongeza maeneo ya ufugaji yaliyopimwa.
2) Kujenga miundombinu ya mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo.
3) Kuongeza uzalishaji wa mitamba kwenye mashamba inakozalishwa na kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta Binafsi kuendelea kuzalisha mitamba ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa.
4) Kujenga mabwawa katika mikoa yenye mifugo mingi.
5) Kutoa elimu kwa wafugaji wanaomiliki na watakaomilikishwa ardhi ili kutumia hati zao kama dhamana ya kupata mikopo kutoka asasi za fedha.
6) Kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia ya uhamilishaji katika kuboresha koosafu za mifugo nchini kwa kutoa huduma za uhamilishaji kwa wafugaji kwa gharama nafuu kupitia ruzuku itakayowekwa katika mbegu za uhamilishaji.
7) Kukuza na kuendeleza masoko ya mifugo na mazao yake yanayozalishwa na wafugaji na kujenga viwanda vya ngozi.
8) Kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vya nyama na mazao mengine yatokanayo na mifugo.
9) Kuishughulikia kwa wakati na kuitafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya wakulima na wafugaji.

D. Uvuvi na Ufugaji Samaki
Sekta ya uvuvi haijawekewa msisitizo wa kutosha hapa nchini, japo ni sekta muhimu katika ukuzaji uchumi na kipato cha raia mmoja mmoja.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha yafuatayo yanatekelezwa katika kukuza na kuendeleza uvuvi na ufugaji wa samaki:-
1) Kuhamasisha na kuhakikisha wananchi wanachukua fursa ya ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa kwa kushirikiana na vyuo vya uvuvi na ufugaji samaki vya Mbegani na Nyegezi.
2) Kupunguza au kufuta kodi ya uagizaji wa chakula cha samaki kutoka nje ya nchi.
3) Kupunguza masharti ya ufugaji wa samaki wa vizimba kwa kurahisisha wananchi kupata vibali kwa wakati na katika kituo kimoja cha kutolea huduma.
4) Kuhamasisha wananchi kutumia fursa ya kulima mazao ya bahari kama majongoo bahari na mwani na kuongeza thamani ya mazao hayo.
5) Kuhalalisha mialo iliyopo na kuongeza idadi ya mialo katika pwani ya bahari ya Hindi na maziwa. Kuongeza na kuimarisha maeneo ya uuzaji ya samaki kwa kuimarisha miundombinu ya masoko hayo.
17
6) Kununua meli za uvuvi angalau saba zenye uwezo wa kuvua samaki bahari kuu.
7) Kujenga bandari ya uvuvi katika ukanda wa Pwani ambayo itawezesha meli zinazovua Bahari Kuu kutia nanga.
8) Kurejesha mazalia na makulia ya samaki yaliyoharibika kutokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira kwa kuweka matumbawe bandia na kupanda mikoko katika bahari.
9) Kushirikiana na Mashirika ya Umma yenye dhamana ya uvuvi nchini, kuwavutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, vyombo na zana za uvuvi.
10) Kuboresha maeneo ya uvuvi kwa kutumia teknolojia rafiki ya mazingira kwa kuweka vifaa vya kuvutia samaki baharini ili kuwawezesha wavuvi wadogo kuyafikia maeneo yenye samaki wengi na hivyo kuongeza upatikanaji wa samaki.
11) Kuendeleza utafiti wa kurudishia samaki na kupandikiza ili kuongeza wingi wao katika maziwa, mito na mabwawa.
12) Kuanzisha na kuimarisha vikundi na vyama vya ushirika vya wafugaji wa samaki kwa lengo la kukuza ufugaji wa samaki nchini.
13) Kushirikiana na wadau wa ufugaji samaki ili kuongeza uzalishaji wa samaki kwa kujenga mabwawa ya kufugia samaki na kuongeza uzalishaji ili kupanua wigo wa ajira kwa vijana.

E. Viwanda
Serikali itakayoongozwa na NCCR-Mageuzi itafanya mambo yafuatayo katika sekta ya viwanda:-
1) Itawahamasisha wananchi na kuwawezesha kiujasiriamali katika sekta hii kwa kubuni na kujenga viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
2) Itahakikisha kuwa mali ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
3) Itaanzisha viwanda vya msingi vinavyotumia malighafi ya chuma katika maeneo ya Liganga na Mchuchuma.
4) Itaendeleza kasi ya ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati hasa vinavyosindika mazao. NCCR-Mageuzi itahakikisha kunawekwa ushuruti wa kutaka mazao ya Katani, kahawa, tumbaku na chai kusindikwa nchi, kuzuia uuzaji nje ya nchi ngozi ambayo haijasindikwa na kutoruhusu uuzaji nje ya nchi wa korosho isiyobanguliwa na kuhakikisha kuwa korosho yote inayolimwa Tanzania inabanguliwa hapa Tanzania.
5) Itahakikisha kuwa kunakuwa na uwiano bora kati ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, na kuwa ujenzi wa viwanda unazingatia msingi wa kuhifadhi na kulinda mazingira.
6) Itahakikisha kuwa viwanda vinavyojengwa ni vya kisasa kiteknolojia ili bidhaa zetu ziwe na ushindani kwa ubora na bei nafuu kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki, Jumuiya ya Uchumi ya SADC, Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla.
7) Itaimarisha vyama huru vya wenye viwanda na wafanyabiashara ili kuvipa uwezo wa kutoa huduma za ushauri kwa wanachama wao kuweza kupata ubia na soko la bidhaa nje ya nchi.
8) Itaanzisha bandari huru, bandari kavu, kuboresha bandari ya Tanga kwa ajili ya soko la Afrika mashariki, kuboresha Bandari ya Mtwara kwa ajili ya soko la Kusini mwa Afrika na Bandari za Dar es Salaam na Zanzibar kwa ajili ya soko la Dunia; kwa kuziongezea ufanisi.
9) Itatenga maeneo maalumu katika mipaka ya nchi yetu kwa ajili ya kujenga masoko ya kimataifa ili kuchochea biashara baina ya nchi yetu na nchi za jirani.
10) Itaimarisha sera ya ubia baina ya serikali na sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara

F. Biashara na Uchumi Imara
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha yafuatayo yanatekelezwa:-
1) Kudhibiti mfumko wa bei ili uendelee kubaki kwenye tarakimu moja;
2) Kudhibiti nakisi ya bajeti ili iendelee kushuka hadi kuwa chini ya asilimia 3 ya Pato la Taifa;
3) Kusimamia Deni la Taifa kuwa himilivu;
4) Kuhakikisha thamani ya Shilingi yetu inatengamaa ili kujenga imani ya uchumi wetu kwa lengo la kuongeza shughuli za uwekezaji, uzalishaji na biashara;
5) Kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi, kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni na kuepuka kuagiza bidhaa zisizo za lazima kutoka nje ya nchi;
6) Kuendelea kuwa na mikakati itakayowezesha kuwa na akiba ya fedha za kigeni zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje kwa urahisi;
7) Kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kupanua wigo wa walipa kodi;
8) Kuweka mazingira yatakayowezesha kushuka kwa riba ya mikopo katika Taasisi za Fedha.

G. Madini
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha yafuatayo yanatekelezwa katika sekta hii:
1) Kuzipitia upya sheria za madini.
2) Kuweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi kunufaika kutokana na madini na maliasili zinginezo zilizopo katika maeneo yao.
3) Kuweka na kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini na kufuatilia maduhuli yatokanayo na madini.
4) Kuimarisha ukaguzi wa migodi katika masuala ya usalama, utunzaji wa mazingira na afya migodini.
5) Kuweka na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuvutia mitaji ya uwekezaji katika Sekta ya Madini, hususan kwenye madini adimu.
6) Kuweka utaratibu maalum wa kusaidia na kukuza uwezo wa wachimbaji wadogo wadogo.
7) Kuimarisha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
8) Kubuni mikakati mahsusi itakayowezesha kukomesha na biashara haramu ya madini.

H. Nishati, Gesi na Mafuta
Serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia yafuatayo katika sekta hii:-
1) Kubadili miundombinu ya uzalishaji wa nishati kutoka vyanzo mbalimbali ili kuwa na nishati nafuu kwa matumizi ya nyumbani na kwenye shughuli za uzalishaji mali hasa viwandani, mashambani, usafirishaji na migodini, vyanzo hivyo ni pamoja na nguvu ya jua, maji, upepo, gesi asilia, makaa ya mawe na nishati jadidifu.
2) Kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme mijini na vijijini.
3) Kutekeleza Sera na Sheria za kusimamia mapato yanayotokana na gesi asilia na mafuta ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa manufaa ya Wananchi wa kizazi cha sasa na kijacho.
4) Kupunguza kodi ya uzalishaji wa mafuta, gesi na umeme
5) Kuhakisha kwamba utafutaji, uchimbaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia ni shirikishi.
6) Kuwasaidia wanaobuni njia za kisasa za usambazaji wa gesi.

I. Maliasili
Serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia yafuatayo katika sekta hii:-
1) Kupiga vita ujangili na kuimarisha utunzaji wa hifadhi za taifa na mazingira kwa kuboresha miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba dhidi ya ujangili na kuongeza vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya doria na upelelezi nje na ndani ya maeneo ya hifadhi.
2) Kuimarisha doria za ulinzi wa wananchi dhidi ya wanyamapori kwa kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za wanyamapori waharibifu.
3) Kuchochea ujenzi na kukarabati miundombinu ya hifadhi na maeneo ya zama za kale ili kuongeza unadhifu wa vituo vya utailii.
4) Kusimamia kwa uvunaji na matumizi ya rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
5) Kuendelea kujenga mahusiano mema baina ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hizo kwa namna ambayo wananchi hao watanufaika na uwepo wa hifadhi hizo.
6) Kuzingatia utawala wa Sheria katika kusimamia rasilimali za maliasili

J. Utalii
Serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia yafuatayo katika sekta hii:-
1) Kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia milioni sita kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuwezesha Sekta Binafsi kuwekeza katika huduma za miundombinu ya utalii.
2) Kuongeza msukumo katika utalii wa kihistoria kwa kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya malikale na kuyatangaza maeneo hayo.
3) Kuongeza bajeti ya Sekta ya Utalii ili kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi.
4) Kuimarisha mafunzo ya Hoteli na Utalii hususan katika ngazi ya shahada.
5) Kuhamasisha wananchi kufanya utalii wa ndani na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani kwenye utalii.
6) Kuendelea kujenga mazingira rafiki kwa vijana kujiajiri kwenye maeneo mbalimbali ya utalii
7) Kuhifadhi malikale kwa kuishirikisha jamii kutumia Malikale kama chanzo cha kujipatia kipato kwa kutoa elimu ya ujasiriamali, kutenga maeneo ya biashara, kuishirikisha sekta binafsi na kutoa elimu ya uhifadhi kwa umma

K. Sanaa, Utamaduni na Michezo
Serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia yafuatayo katika sekta hii:-
1) Kulinda na kutunza utamaduni wa taifa kwa kuwahimiza wananchi kudumisha maadili ya kitaifa.
2) Kuwezesha na kuimarisha miradi ya raia ya kuendeleza fani zinazoelezea utamaduni kama vile muziki, michezo, ngoma, filamu, uchoraji, ufinyanzi, uchongaji na sanaa nyinginezo. Hii ni pamoja na kuwawezesha kimtaji wasanii na kulinda haki ya kazi zao (haki miliki).
3) Kuimarisha vyuo vya kuendeleza utamaduni wa taifa na fani zinazoelezea utamaduni wa taifa.
4) Kuanzisha, kuendeleza na kuwezesha programu maalumu ya kuwezesha vijana wenye vipaji katika kila fani zinazoelezea utamaduni wa taifa, ili kukuza ajira kwa vijana, uzalishaji wa bidhaa za kitamaduni.
5) Kujenga miundombinu ya kisasa na ya kutosha ya michezo ili kuwezesha sekta hii kuajiri vijana wanamichezo ndani na nje ya nchi.
6) Kuanzisha na kuendesha olimpiki ya kitaifa ambapo michezo yote ya kisasa na ya kienyeji itashiriki, kila baada ya kipindi kitakachopangwa.

L. Miundombinu: Reli, Barabara, Usafiri wa Anga na Usafiri wa Majini
Serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia yafuatayo katika sekta hii:-
1) Kuongeza kasi ya ujenzi wa mfumo mpya wa reli wa kisasa (SGR) nchini kwa ubia na sekta binafsi
2) Kujenga mfumo mpya wa usafiri wa barabara na reli katika miji mikubwa
3) Kujenga barabara kwa kiwango cha lami ili kuhakikisha kuwa kila makao ya Halmashauri yanafikika kwa barabara za lami.
4) Kuhakikisha barabara za vijijini zinapitika kwa urahisi kwa vipindi vyote vya mwaka.
5) Kuimarisha uwezo wa kifedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Barabara (TANROAD) na ule wa TARURA.
6) Kuimarisha usafiri wa anga kwa kushirikiana na sekta binafsi.
7) Kuboresha na kupanua miundombinu ya bandari nchini kwa kuweka mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa mizigo na uchukuzi wa abiria kwa ubia na sekta binafsi.

9. USALAMA WA TAIFA
A. Ulinzi na Usalama
Serikali ya NCCR-Mageuzi itatekeleza yafuatayo:-
1) Itahakikisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinapatiwa zana za kisasa kabisa ili viweze kumudu kudhibiti uhalifu.
2) Itaweka utaratibu wa kudumu na kuwapatia askari wetu mafunzo kazini ya mbinu bora zaidi, na kuhakikisha kuwa wamejengeka na kuwa waadilifu wa hali ya juu.
3) Itaboresha maslahi ya watendaji katika vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo: makazi, utoaji wa mikopo nafuu kuongeza posho ya chakula na kuboresha mazingira ya vituo vya kufanyia kazi.
4) Itashirikiana na Mataifa mengine na Asasi za Kimataifa katika kupambana na makosa yanayovuka mipaka hasa ugaidi, uharamia, utakatishaji wa fedha haramu, biashara haramu ya madawa ya kulevya na usafirishaji wa binadamu.
5) Itaweka vituo vya ulinzi karibu sana na wananchi, lengo likiwa ni kuhakikishia wananchi ulinzi na usalama wao.
6) Itaweka mazingira yatakayowezesha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuimarisha mafunzo kwa vijana wanaojiunga kwa hiari na wale wanaojiunga kwa mujibu wa Sheria,ili kuwafanya vijana wa kitanzania kuwa wakakamavu, wasikivu na wenye nidhamu.
7) Itaimarisha na kujenda mfumo endelevu wa uhusiano na ushirikiano baina ya raia na vyombo vya ulinzi na usalama.
B. Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Serikali ya NCCR-Mageuzi itatekeleza yafuatayo:-
1) Itaimarisha mahusiano mema ya kimataifa kwa maslahi ya taifa katika nyanja mbalimbali za kijamii, uchumi, na utawala bora.
2) Itajenga uwezo na ujuzi wa kuingia mikataba yenye tija ya uwekezaji wa kimataifa.
3) Itaweka mazingira salama na ya uhakika ya kuridhia mikataba ya kimataifa inayotetea na kulinda haki za binadamu.
4) Itahakikisha Tanzania inaweka mazingira rafiki kwa wananchi na taasisi zingine kuzifikia vyombo vya utoaji haki vya kikanda.
5) Itajitahidi kushughulikia migogoro, mikwaruzano na malumbano na nchi zingine kwa njia za kidiplomasia.

10. VITA DHIDI YA RUSHWA
Serikali NCCR-Mageuzi itaendeleza vita dhidi ya ufisadi na rushwa kwa kutekeleza mkakati ufuatao:-
1) Kutengeneza vyombo vyenye nguvu kubwa na mtandao ulioenea hadi kona zote za nchi, vyombo vyenye meno makali ya kutokomeza ulaji rushwa.
2) Kuunda dola kwa kuzingatia weledi, uwezo kitaaluma na maadili ya uongozi kwa watendaji na viongozi wa umma.
3) Kuvipa uhuru mkubwa wa vyombo vya habari ili viandike bila hofu ufisadi vitakaoubaini katika taasisi yoyote nchini. Vyombo hivi na waandishi wake watapewa ulinzi wa kisheria.
4) Kulinda haki ya kila raia kupata na kutoa habari ili kwa kufanya hivyo uwezekano wa kuficha siri za kifisadi uondolewe, na kuhakikisha kwamba serikali inatoa taarifa za uendeshaji wa shughuli za umma kwa vyombo vya habari na asasi za kijamii zinazolinda na kutetea haki.
5) Kuelimisha, kulea na kufunda watumishi na viongozi katika misingi ya uadilifu na uongozi bora. Hili litaendana na kujenga taifa adilifu kwa njia ya elimu kwa watanzania tangia wakiwa na umri mdogo na kuwakuza katika maadili hayo.
6) Kurahisisha mfumo wa ulipaji kodi na kupunguza kiwango cha kodi ili kuwahamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari, ili waondokane na kishawishi cha kutoa rushwa badala ya kodi.
7) Kuimarisha Ofisi ya kudhibiti na kupambana na rushwa TAKUKURU kuwa inakuwa chombo huru kinachofuata taratibu za sheria na kanuni za nchi katika utekelezaji wa shughuli zake.
8) Kuhakikisha kuwa ajira au teuzi mbalimbali za serikali zinakuwa za kushindaniwa kwa usawa.

MWITO KWA WANANCHI
Sisi, NCCR-Mageuzi tunasimamia Itikadi ya UTU, ambayo moja ya msingi wake ni Uwajibikaji. Kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumejipangia kufanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano. Hii ina maana kila mwenye sifa za kupiga kura, ana muda wa miaka mitano wa kutathmini ubora wa utumishi wa viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita.

Kazi hii haiepukiki, kwani ni wajibu. Sisi wananchi ndio waajiri wa viongozi hao, kwani wanalipwa kwa “thumuni” zetu za kodi katika kila kipande cha sabuni tunachonunua au chumvi tunayonunua.

Tutafakari!
Mwajiri anamwezesha Mwajiriwa kuishi maisha ambayo mwenyewe hawezi kuyamudu. Huu ni upendo wa ajabu. Kweli huu ni UTU.
Tafakari hii lazima itatuumiza wengi wetu ambao ni Waajiri. Hivyo basi ni muhimu tuheshimu hizi hisia za maumivu. Hisia hizi zinatuweka kwenye mwanga mkali wa

kuweza kuwachambua wagombea wetu, na kuona ni nani KWELI anayestahili kupokea “thumuni” yangu kwa kuniwakilisha katika vyombo vya maamuzi.
Lakini kwa kuwa sisi binadamu ni kitu kimoja, lazima kujiulize kama huyu mpokea “thumuni “anajitambua na ana uwezo wa kuwajibika kurudisha upendo kwa kunitumikia ipasavyo chini ya sheria tulizojiwekea.

Kwa kuwa kufanya uchaguzi ni wajibu wa kikatiba basi hatuna uwezo wa kuzuia hiyo “thumuni” isitumike, lazima itakwenda kwa mmoja wa wagombea hao.
“Thumuni” yako umeitokea jasho, una wajibu wa kutumia UTU wako kumpatia mgombea atakayejali UTU wako kwa miaka mitano, na sio kukusahau kwa miaka mitano.
USIKUBALI “thumuni” YAKO ITUMIWE NA MTU MWINGINE KUFANYA UAJIRI.

Sote Twendeni Tukapige Kura,

Kuwajibika ni UTU,

Pamoja Tutashinda.
 

Attachments

  • ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2020 -2 (1) NCCR Mageuzi.pdf
    232.9 KB · Views: 29

CAPO DELGADO

JF-Expert Member
Aug 31, 2020
1,161
2,000
Wamekopy chadema nini.

Inafanana na Ilani bora kabisa ya CHADEMA.

Hongereni sana NCCR
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom