Nauli isipopatikana, mjomba atakuja mwenyewe kijijini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nauli isipopatikana, mjomba atakuja mwenyewe kijijini

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Bikra, Jun 1, 2009.

 1. Bikra

  Bikra Senior Member

  #1
  Jun 1, 2009
  Joined: May 13, 2009
  Messages: 103
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  BILA ya kusubiri kuombwa wala kupata mwaliko, tayari tumekwisha anza harakati za kuitafuta nauli. La mgambo likilia…… si mara zote unapaswa kusubiri kupata mwaliko, wakati mwingine harufu nzuri tu inakufanya ujumuike ‘shughulini’. Hatusemi kuwa ndio muanze kuvamia misosi ya harusi za majirani zenu.

  La mgambo limekwishalia siku nyingi, tunaweza kusema kwa siku za karibuni, kila mmoja asiyekuwa na subira ya kungojea mwaliko wake binafsi ulioandikwa ‘njoo na ubavu wako’ amejitahidi kutia mchango wake katika kupuliza mbiu. Kuanzia migomo ya walimu, wanafunzi, wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, baadhi ya wanasiasa hasa wa kambi ya upinzani na wachache wa kutoka ndani ya CCM.

  Baadhi ya waandishi wa habari na wachambuzi wa mambo, wanataaluma wa ngazi mbalimbali nao wamekwishapuliza filimbi kwa namna mbalimbali na katika nyakati tofauti. Hiyo yote ni kuashiria kuwa liko jambo, tunahitajika wewe, yule na mimi, kuonyesha mshikamano.

  Wewe vipi, bado unafikiria, unaangalia wapi pa kujishikisha au unataka kuwa popo. Tunao popo wengi sana tafadhali, usiwe mmoja wao. ‘Upopo’ (hali ya kutaka kuwa huku na kule kutegemea na hali ya kutokuwa na upande) ni ukengeufu unaodhihirisha uoga na kutokujiamini na zaidi ya yote kutokujua wajibu na mchango wako katika harakati za kufanikisha kupatikana mchuzi wa maana kwa ajili ya akina pangu pakavu.

  Badala ya maji ya chumvi tunayoyapata sasa hivi mchuzi wa kioo. Kila ukipeleka tonge unaona taswira yako ndani ya bakuli.

  Hata katika kundi la wanamuziki wapo wanaoweza kutajwa kwa mchango wao katika kuitikia na kupuliza mbiu ya ‘La Mgambo’. Akina Joseph Haule na nyimbo zake za Ndiyo Mzee, Siyo Mzee, Nang’atuka na mwenzake Nakaaya na wimbo wake wa Mr. Politician. Orodha ni ndefu, huwezi kuimaliza bila kutaja jina la Mrisho Mpoto.

  Mpoto anatafuta nauli ya kwenda mjini kumuona mjomba aliyeamua kulowea na kusahau kuwa ‘huku kwetu kuna shida.’ Harakati za kusaka nauli zinapaswa kuwa moja ya kauli mbiu hivyo usisite kujiunga katika msako wa kutafuta nauli hiyo.

  Ingawa yeye kasema anatafuta nauli kivyake ili atuwakilishe akina pangu pakavu tutakaobaki ‘kijijini’ wengine tumeamua kazi isiwe yake peke yake.

  Tukimwachia peke yake, ‘mawili’ inaweza kumchukua muda mrefu ama naye akaja kutugeuka. Pia huwezi kujua huko ‘mjini’ mjomba kajipanga namna gani kumkabili mtu mmoja pekee. Akienda Mpoto peke yake mjomba anaweza kumwingiza ‘kingi’ akapewa lamba lamba akasahau masahibu yetu.

  ‘Natania tu’. Lakini imewahi kutokea ,wako baadhi yao mjini huko walitoka huku tuliko walipofika mjini na kupata mapochopocho, wakasahau walichopaswa kumwambia mjomba. Wanampatia habari njema tu, kutuhusu sisi kuwa maisha yetu shwari ili waendelee kukuza matumbo yao, bila shaka.

  Tutoe wito hapa. Katika safu hii ya wasaka mchuzi kwamba tumuunge mkono Mjomba Mpoto katika kusaka nauli ya kwenda kumuona Mjomba ‘wetu’ huko mjini.

  Kila mmoja sasa kwa nguvu zote aanze kusakanya huku na huko kadri awezavyo kupata fungu la kumtosha kwenda mjini kumweleza mjomba masahibu yetu huku ‘kijijini’. Hapa ndipo vibubu vinapopaswa kufanya kazi yake haswa.

  Hali inatulazimu kumuibukia Mjomba huko huko mjini maana njia za barua hazifai tena. Yuko ‘busy’ hawezi kujibu au wasaidizi wake hawamfikishii barua zitakazomkumbusha yale aliyopata kutuahidi siye wapwa wake. Wako tayari kumfikishia barua za mialiko ya kutumbua nje ya nchi. Namba za simu tulizokuwa tukizitumia kuwasiliana nae mapema kabla mji haujammeza siku hizi hazipatikani.

  Wakati ule tulikuwa tunaweza kumwambia, fulani, aliyemteua kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wa njiani ni mroho, mlafi, mchoyo, mwenye inda. Hawezi kutusaidia sie wapwa wake. Tulimpigia simu tukamwambia hata orodha ya wauza bangi, wanaoharibu binamu zetu kwa kuwafanya mazezeta wengine huwaita mateja.

  Siku ukibahatisha iko hewani, anapokea ‘anti yetu’ anasema “namba unayopiga kwa sasa haipatikani, jaribu baadaye.” Hiyo baadaye haina ukomo maana ukipiga tena utaambiwa vivyo hivyo. Hatuwezi tena kumwambia kuwa ile barabara aliyoaahidi kuwa itajengwa kufumba na kufumbua ili kurahisisha usafiri na uchukuzi, imeshakuwa njia ya mapitio ya ng’ombe na wachungaji.

  Haifai kwa matumizi ya binadamu, yale makorongo ambayo yangetumia fedha kichele kuyafanyia matengenezo yameshakuwa mahandaki ambayo yangemfaa, Laurent Kunda kujifichia. Asikamatwe kinafiki na Wanyarwanda.

  Hatua kadhaa ambazo zimekwishakufanyika katika maandalizi hayo ya kwenda mjini, zimezaa matunda kwa kiasi fulani. Zimetuonesha kwamba mjomba anatambua nguvu tuliyo nayo. Tukiifanikisha hiyo safari, mjini patakuwa hapatoshi. Walimu wamelipwa madai yao (ingawa bado kuna matatizo). Wanafunzi wamepinga sera ya kibaguzi wamefukuzwa. Wahalifu wa madawa ya kulevya, bado wanatamba mitaani, pamoja na mamlaka kukiri kuwa majina yao yapo.

  Wengine ndiyo hivyo tena wanaachiwa kimya kimya, wanafanyiana umafia na ujasusi wa kunyweshana sumu. Kisa! Ubabe wa binamu Kagoda Agriculture Ltd, ambaye mjomba anaonekana amekosa ujasiri wa kumkanya na kumkaripia.

  Lakini pia Mpoto na sisi sote hatuna haja ya kufa moyo hata kama nauli atakosa au tutakosa wote. Mjomba atakuja mwenyewe tena kama namwona akija. Anarudi kijijini. Kwa nini? Taharuki ya uchaguzi.”

  Mwisho wa siku lazima ajilete mwenyewe kwenye kikaango, dalili za kuwa karibu ataanza safari tumwekwisha kuziona.

  Akifika ndipo tutamwuliza kuhusu malalo yetu yaliyogawiwa bure au sawa na hivyo. Yako mengi kuanzia ya Buzwagi, Geita, Bulyanhulu, Mererani, Mgolola, IPTL. Tutamuuliza pia kuhusu binamu zetu wale wakorofi akina Kagoda, Kiwira, Richmond, kwa nini anawaachia watambe watakavyo kiasi ambacho tunahisi kabisa wamemzidi kete mjomba.

  Au kwa sababu walimpiga ‘tafu’ wakati akipita kijijini kutuomba ridhaa ya kwenda mjini kwa niaba yetu.

  Mwakilishi au kiongozi yeyote wa wananchi aliyepewa dhamana ya kuongoza kwa niaba yao, hawezi kuendelea kukaa ofisini (Ikulu, bungeni au kokote kule) bila ruksa yetu. Wapiga kura ndiyo wenye nguvu ya kuamua nani awe ‘in’ au ‘out’. ‘Uhuru’ wao wa kuongoza, Kweli, kila mmoja atakapoisaka nauli na kuipata, huko mjini kutakuwa hakutoshi.. Kinyume chake ni kwamba tutamsubiri mjomba huku huku kijijini.

  “Tafadhali” mjomba usisite kuja, wapwao tutakuwepo. Ingawa wengi wetu wamekwisha kutangulia mbele ya haki, kwa kukosa huduma za hospitali, kukosa hewa kwenye majengo ya disko, n.k. tutakaokuwepo tutakusubiri kwa hamu.
   
 2. M

  MathewMssw Member

  #2
  Jun 3, 2009
  Joined: Mar 27, 2009
  Messages: 92
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mwenye masikio na asikie ya huyu muungwana la akishupaza shingo mwisho wake ni kuvunjika! Very straight and strong massage.
   
 3. H

  Hondo Member

  #3
  Jun 3, 2009
  Joined: May 6, 2009
  Messages: 49
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Uncle ni kiziwi anatakiwa kufungiwa safari.
   
 4. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #4
  Jun 3, 2009
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 720
  Trophy Points: 280
  hii imenikuna sana.

  mjomba haangalii nini anafanya ameziba masikio
  we ngoja tu, tukija wote huko mjini udugu utakufa
  sikufichi mjomba!
   
 5. Crashwise

  Crashwise JF-Expert Member

  #5
  Jun 3, 2009
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 22,172
  Likes Received: 862
  Trophy Points: 280
  Nilikutana na huu ujumbe huko moro....
   

  Attached Files:

 6. M

  Mwanawani JF-Expert Member

  #6
  Jun 5, 2009
  Joined: Jan 17, 2008
  Messages: 206
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Anko anko, ... chonde anko, upepaayii!!! Tusijeshuhudia yaliyotokea kwa Bob kule Ziim Bobwe. Kumbuka kuwa kama wewe unefikiri kuwa ni mbuyu, wale wanaonyanyasika ni kama mashoka ambayo yako tayari kuukata mbuyu hata chini kabisa.
   
Loading...