Natoa Rai: Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi Wanawajibika Kwa Hizi Ajali | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Natoa Rai: Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi Wanawajibika Kwa Hizi Ajali

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by mambomengi, Aug 11, 2012.

 1. m

  mambomengi JF-Expert Member

  #1
  Aug 11, 2012
  Joined: May 16, 2009
  Messages: 829
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 35
  Wizara na Viongozi Wao Wanawajibika Moja kwa Moja

  Barabara za Tanzania zimegeuka machinjio ya watumiaji wake, wasafiri wanaotumia barabara wanaendelea kuwa roho juu wanapokuwa safarini wakati serikali ya JMT haijafanya chochote kuondoa machinjio safarini. Hivi Wizara husika zinasubiri msaada wa nchi za kigeni kutokomeza hizi ajali? Katiba ya nchi inatoa fursa na haki sawa kwa kila raia wake kuishi na kuipa serikali jukumu la kulinda uhai wa raia na wakaazi wa nchi yake. Kutokufanya lolote la maana kuondoa hizi ajali barabarani ni sawa na kuvunja moja ya vipengele vya katiba.

  Nimekaa na kutafakari kwa kina kuhusu ongezeko la ajali za barabarani kila siku. Nikajiuliza je ni mimi pekee yangu mwenye uchungu? Je Serikali na watendaji wake wakuu hawajaona hili tatizo? Ni kajiuliza mara je kuna vitengo maalumu kukabiliana na hizi ajali za barabarani? Nikatafuta takwimu (kwingineko) kuelewa ukubwa na undani wa tatizo la ajali barabarani. Nikafahamu (kupita Benki ya Dunia & Shirika la Afya Duniani) kuwa mwaka 2007-2009 ajali za barabarani zilishika namba mbili, nyuma ya Malaria kuangamiza wananchi wasio na hatia yoyote nchini Tanzania. Nikatambua (kwa kutumia uwezekano na uwiano mrefusho) kuwa kati ya 2010 -2012, ajali za barabarani zitakuwa chanzo kikuu cha kuua wananchi Tanzania. Nikajiuliza zaidi je Serikali inatambua hilo? Katika pitia yangu kwenye habari zilizochapwa na Benki ya Dunia na Shirika la Afya duniani, nikaona kuwa Tanzania inawakilishwa vizuri kwenye makongamano ya kumaliza ama kupunguza ajali za barabarani duniani. Nikahitimisha kuwa watendaji wetu wanaelewa hili tatizo na juhudi za kimataifa zifanyazwo kumaliza hili tatizo. Zaidi ya hapo wawakilishi wamesaini makubaliano yaliyofikiwa kwenye makongamano husika. Nilipopitia kwa undani zaidi habari zilizochapwa na Wizara ya Uchukuzi na ile Wizara mama ya Ujenzi, sikuona sera wala dira ya usalama barabarani. Nikatamuba kuwa nchi kubwa yenye wakaazi zaidi ya milioni arobaini haina mkakati madhubuti wa kutokomeza ajali za barabarani. Kwa haraka nikahitimisha kuwa hizi wizara (na serikali kwa ujumla) haziwajali wasafiri barabarani.

  Napenda kutahadharisha kuwa hizi ajali zina madhara makubwa zaidi ya msongamano wa magari katikati ya jiji la Dar es Salaam. Napenda kuwakumbushia kuwa mbali ya kupoteza maisha, Taifa linaendelea kupoteza nguvu kazi, walemavu wanaongezeka, wategemezi (yatima, wajane, nk) wanaongezeka, uchumi wa nchi unadumaa, hofu inaongezeka, n.k. Fikiria ndugu yako yoyote aliepoteza maisha (ama kulemaa) barabarani, na ujiulize familia yake inavyojuta kumpoteza.

  Mara nyingi Taifa limeshikwa na simanzi pale ajali mbaya za vyombo vingine (visivyo magari) zinapochukua watu wengi kwa mpigo na limesahau kuwa kwa mwezi mmoja zaidi ya watu MIA MOJA (100) huwa wanapoteza maisha barabarani na maelfu wanabaki walemavu wa viungo vyao. Nachotaka kusema hapa ni kuwa ajali za barabarani zilizotokea mwaka huu zimechukua maisha ya watu wengi pengine kuzidi zile mbili zilizotokea bahari ya Hindi hivi karibuni. Nazidi kujiuliza kwanini wizara husika hazitoi takwimu za watu wangapi wamepoteza maisha barabarani kila mwezi au walau hata kila mwaka. Hizi takwimu zikiwekwa wazi na zikachapwa kwenye vyombo vya habari zitasaidia kuelimisha wananchi ukubwa wa tatizo. Binafsi nimechoshwa na ninasikitishwa na utendaji serikalini.

  Namaliza kwa kutoa rai kwa Mawaziri wetu kama wameshindwa kazi basi wakae pembeni. Nawaomba mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi wajiuzulu kwani wanawajibika moja kwa moja kwa hili tatizo sugu linalozidi kuchukua maisha ya raia na wakazi wa Tanzania. Nimesikitishwa na Wizara kukosa vipaumbele kwenye utendaji kiasi cha kutokufahamu au kupuuzia umuhimu wa mipango na mikakati madhubuti ya kulinda watumiaji wote wa barabara (abiria, madereva, wabaiskeli, na wapita njiani). Mfano, majuzi Waziri anasimama mbele ya Bunge anaongelea kujisetiri na kujisaidia (kuchimba dawa) safarini anaacha kuongelea vipaumbele vitakavyochukuliwa ili kuzuia maisha yanayopotea barabarani.

  NDUGU ZANGU, TAIFA HALIWEZI KUENDELEA KUWA MSIBANI KILA SIKU KWA SABABU YA UZEMBE AU UKUTOKUJUA AU SINTOFAHAMU KWENYE SUALA NYETI LA AJALI BARABARANI.
   
Loading...