Natamani Kuishi Tanzania Na si Tanganyika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Natamani Kuishi Tanzania Na si Tanganyika

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by X-PASTER, Nov 3, 2009.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Nov 3, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Natamani Kuishi Tanzania Na si Tanganyika

  Salaam ndugu zanguni wapendwa ndani ya jukwaa hili la JF, ni matumaini mpo na siha njema kabisa. Leo nami nimeonelea kuingia tena kwenye jukwaa la siyasa, maana tangia kipindi kile refa alipo amua kukwatua nami nikaamua kukaa pembeni na kuwa mtazamaji badala ya kuwa mchezaji.

  Wengi watashtuka na kichwa cha makala haya, “Natamani Kuishi Tanzania Na si Tanganyika” Naam ndugu zanguni kwani leo nimewakumbuka ndugu, marafiki, na jamaa zangu, niliokuwa naishi nao nyumbani enzi zile nchi ilipokuwa ikijulikana kwa jina la Tanganyika…!

  Kumbukumbu zangu kwenye somo la historia, nikichanganya na simulizi toka kwa Marehemu Babu na Bibi yangu walipokuwa wakinihadithia jinsi harakati za ukombozi wa Tanganyika zilivyoanza. Walinihadithia kuwa harakati zilianza pale tu mkoloni wa kwanza Mjerumani alipotia mguu wake kwenye ardhi hii tukufu ya Tanganyika.
  Mkoloni alitiwa sana adabu na mababu zetu ambao kwa namna moja ama nyingine ule ushujaa na uhodari wao hakuna aliyeweza kuurithi hata mmoja.

  Nakumbuka kuwa harakati zilishika kani zaidi Kadri muda ulivyokwenda harakati hizi ziliongezeka na kuwa maarufu haswa miaka ile ya hamsini na hasa baada ya chama cha TAA kubadili jina kuitwa TANU.

  Kipindi kile watu hawakuwa waoga kueleza kweli, vijana kwa wazee walijitolea kwa hali na mali ili kufikia malengo ya kupatikana kwa uhuru kamili katika kujitawala na kujiamulia mambo yetu wenyewe. Matunda ya harakati hizi yalipatikana mwaka 1961 ambapo Tanganyika ilipata uhuru wake… Hakika ilikuwa furaha ilioje kwa wazalendo haswa wale wanaharakati, waliojitolea kupigania uhuru wa Tanganyika.

  Ni dhahiri kuwa usiku ule wa Desemba 9, 1961 wakati ilipokuwa inashushwa bendera ya Muingereza na kupandishwa ile ya Tanganyika, wengi walitokwa na machozi ya furaha kila aliyeshuhudia alikuwa na yakini kuwa ule ulikuwa ndio mwanzo wa maendeleo ya nchi yetu Tanganyika.

  Maendeleo ambayo yangekuja kuonekana katika hali bora zaidi za kiuchumi kwa taifa na mtu mmoja mmoja, nyumba bora zaidi, kilimo cha kisasa zaidi, usafiri bora zaidi na juu ya hayo elimu bora zaidi na kwa wote.

  Ni hakika kabisa wale wote ambao leo hii tumewasahau kuwa ndio mashujaa wetu walio kufa shahidi walikufa katika harakati zile nao wamekufa wanaamini vivyo hivyo. (si ajabu wakifufuka leo hii na kukuta hali hii watakufa papo hapo kwa kihoro).

  Lahiti tungalijuwa kuwa Uhuru ule ungetuletea mashaka haya nina ukakika kabisa washujaa wetu wasingetumia mali zao na muda wao kuondoa ubaguzi wa kikoloni na hata ingekuwa tumepewa uhuru bila ya harakati basi hakuna ambaye angesheherekea kama ilivyokuwa siku ile ya uhuru.

  Lakini basi hakuna mtu yeyote aliyekuwa na mashaka siku ile ya uhuru juu ya uhusiano mkubwa uliokuwepo baina ya kuondoka kwa wakoloni, yaani kupata uhuru na kukaribisha aina mpya ya ukoloni ambao leo tunahuita kwa jina jingine la kizalendo zaidi, yaani ufisadi miongoni mwa watu wachache wakikumbatiwa na watawala wa nchi hii.

  Leo hii inakaribia miaka hamsini (50) tangia tupate uhuru wetu, wengi wa wale waliokuwepo na wale waliokuja kuzaliwa nyuma, si ajabu wakawa na wakati mgumu zaidi endapo wataulizwa kubainisha wakati ule wa mkoloni na huu tulio nao upi ni bora kwao. Si ajabu leo mtu akaulizwa uhuru na ukoloni utachagua nini? Si ajabu kwa mtu ambaye amebahatika kuona utawala wa Mjerumani na Muingereza akisema...

  “Subiri nifikirie!.... Mmmm ukoloniiii... nahisi jina ukoloni kama si jina zuri labda tuite ule utawala wa Mjerumani na Muingereza uzuri ni kuwa haukuwa wa Kifisadi...”

  Baada ya uhuru mwaka 1961 viongozi (nina maanisha watawala) wa Tanganyika walifanya mengi wakidhani kuwa wanaendeleza nchi hii. Kuna mambo mawili ambayo yalikwisha pangwa na UN (United National)… Nayo ni:

  Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na kupatika kwa Jamhuri ya Tanganyika1962.


  Haya mawili hayakuwa na shaka, lazima tungeyapata maana yalikuwa ni moja ya maazimio ya Umoja wa Mataifa.

  Baadaye Wale watawala wetu wakaamua kuunganisha nchi mbili ambazo kwa simulizi zisizo rasmi inasemekana kabla ya Gharika kuu (enzi ya Nabii Nuhu) hizi nchi zilikuwa ni nchi moja, ila baada ya ile zahma ya gharika, nchi iliyokuwa moja ikajikuta imegawanywa mapande mawili… mapande hayo ya ardhi baadae sana yaani baada ya kupita karne nyingi sana zikaja kujulikana kwa majina ya Tanganyika na Zanzibar.

  Ndipo mwaka 1964 watawala wetu shupavu (!?) kwa jeuri zote wakaamua kurejesha na kuziunganisha nchi hizo na kufanya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na nchi hizo zikajipatia jina maarufu la Tanzania.

  Watawala hawakuishi hapo, maana maazimio yao yalikuwa mengi sana… miaka mitatu baadae wakaona si vibaya kuchukuwa kwa nguvu mali, majumba, mashamba na mashirika waliyo yakuta na kuyafanya kuwa ni mali ya Umma (!?) kwa ufupi walitaifisha mali za watu binafsi na kuzifanya za taifa… (sina uhakika hapa kama kweli zilikuja kuwa mali za umma au za viongozi wachache). Mambo hayo yalijiri mwaka sitini na saba (1967) na tukaipa jina - Azimio la Arusha.

  Hawakuishia hapo fikra zao sahihi zikapelekea azimio lingine la madaraka mikoani hii ilikuwa mwaka1971… (siyasa hii ilikuja baadae kuuwa co-operatives zote zilizo anzishwa na wananchi, usiniulize tafadhali ilikuwaje kuwaje… sitaki udaku).

  Bila kuwachosha wengi wetu wanakumbuka sana kipindi ambacho wanafunzi waliomaliza darasa la saba na kuingia kwenye ualimu (U.P.E) (nahisi hapa ndipo ile graph ya elimu ilipoanza kushuka kwa kasi sana…) Bila kusahau mambo ya vijiji vya ujamaa, kama bado unakumbuka maduka ya kaya, elimu bure, kutaifisha majumba, mashamba na kila dhahma ambayo sijaiweka hapa.

  Makada nao hawakuwa nyuma maana nyimbo nyingi zilitungwa kupongeza kila hatua iliyochukuliwa. Kwa bahati nzuri miaka yote ya sitini na sabini iliwashuhudia Watanzania chini ya utamaduni wa kuheshimu na kuthamini sana viongozi wao, hivyo moyo wa uzalendo ulijitokeza wazi wazi. Kwa hakika tulizitimiza na kuzifanyia kazi Fikra sahihi za Mwenyekiti…!

  Hali hii ilijitokeza hasa pale wananchi walivyozitii hata amri ambazo ziliwaletea maafa na taabu za kimaisha maana hata serikali iliona tabu kuzitekeleza, mfano kuanzishwa vijiji vya ujamaa, kutaifisha majumba na mashamba n.k.

  Watawala hawakuishia hapo… Wakatuambia nasi tukaamini kuwa Tanzania haiwezi kuwa huru hadi Afrika yote iwe huru (Fikra nzuri eeh?). Tulitumia kila tulichoweza kufikia lengo hili. Tukawasaidi wale tulio waita ndugu zetu kusini mwa bara la Afrika vyama kama ANC, SWAPO, MPLA na FRELIMO na kule Biafra Nigeria… Hakika walifaidi sana msimamo wetu huo.

  Kwa kweli watawala hawakuchoka, maana ile siyasa ya ujamaa na kujitegemea ilikuwa imeshika kani kweli kweli… tulifunzwa mbinu nyingi ikiwemo jinsi ya kufanya propaganda za kisiyasa, na haswa kipindi kile ambacho tuliambiwa kuwa Idd Amin ni nduli tena Joka Kuu, ambalo linatumiwa na mabwana zake ili kuzorotesha harakati za ukombozi wa Afrika. Na lipo tayari kulimeza Bara lote la Afrika... loh! Wananchi tukataharuki... Maana limesha anza kuimeza Kagera yetu na kiwanda chetu cha sukari guru kimeliwa na Joka hilo... Tulilikubali hili watu walitoa mali na roho zao kuikomboa (!?) ardhi ya majirani zetu na Kagera yetu, kisha tukampa adhabu kidogo sana ndani ya mipaka ya nchi yake. Tukamweka yule tuliye mtaka…. Nina maanisha aliyetakiwa na mtawala wetu.

  Mambo yote haya yalifanyika bila mtu yeyote kuhoji kwa vile wengi walidhani kufanya vile ni katika harakati zile zile za kutuletea maendeleo.

  Leo hii ni miaka miaka 48 kasoro mwezi mmoja maana desemba hiyo yaja…., wale waliojaliwa umri na wale waliozaliwa nyuma tunalazimika kujiuliza ikiwa ndoto zetu juu ya faida za uhuru zilikuwa kweli.

  Wazalendo wale ambao enzi zile walijulikana kama Makabwela, yaani watu wa kipato cha chini, leo hii tunajulikana kwa jina la Walala Hoi, na haswa wanaoishi mikoani wanaweza zaidi kuona kile ninacho kizungumza (Kama nao wanapitia JF… subutuuu).

  Ni matarajio ya kila binadamu anayeishi kwa kupambana na maisha kumwona mwanaye akilala katika nyumba bora zaidi kuliko ile yake, akila chakula bora zaidi na kuvaa mavazi bora zaidi. Kwa kweli hali ni kinyume kabisa kwa wale tunao itwa Walala hoi.

  Si ajabu uko mikoani na haswa ukitembea siku ya gulio ukamwona dalali akiuza kitanda cha kamba... (bado kuna uwezekano wa kumpata mtu anayelalia kitanda cha kamba au telemka tukaze) karne hii.

  Mimi bado najiuliza sababu ya huu umasikini ni nini haswa. Tulikuwa tunaambia kuwa ili nchi iendelee tunaitaji mambo manne, Ardhi, watu, siyasa safi na uongozi bora… Je hivi vyote kweli hatuna hata kimoja…!?

  Kuna siku katika kupita pita zangu mitaani, nilipita kwenye kigenge cha kahawa, kulikuwa na mkusanyiko wa vijana na wazee… walikuwa wakijadili mambo ya kimaisha na pembeni yake kulikuwa na muuza magazeti, japo mengine yalikuwa yameshachakaa… nikaamua kukaa na kuagiza kahawa ili nipate mawili matatu, hakika sikuwaruhsu wafahamu kuwa nilikuwa ninawasikiliza. Mzee mmoja wa makamo aliyeonekana kama mtu wa kijiweni alikuwa amevalia kaunda suti yake ya kijivu iliyo chakaa na kuweka vilaka vya rangi mbali mbali, alitoa hoja zilizonisisimua na kunifanya niamini kuwa alikuwa ni afisa wa serikali ya ujamaa na kujitegemea aliyestaafu.


  Kimsingi haiba yake haiwezi kumtofautisha na mtu wa mtaani bali hoja zake zilimtofautisha.

  Yeye alidai kuwa uvivu wa Watanzania umeanzia kwenye vijiji vya ujamaa na utaifishaji mali za watu uliofuatia Azimio la Arusha . Anasema mtu anahamishwa kwenye eneo lake lililo karibu na shamba lake halafu anahamia mbali na shamba lake vipi tena aweze kurudi kulihudumia?

  Serikali ilipoamua kuzuia umilikaji mali binafsi na kutilia mkazo mali kuwa ya wote, au ya mtu kufanya kazi tena kwa nia ya kujipatia mali watu wengi wakaogopa kutafuta mali na kutegeana kwenye mambo ya ushirika.

  Akaongeza kuwa watu waliokuwa na majumba ya ghorofa waliponyang'anywa walio baki wakaamua kuamisha mali zao kisiri siri… Zikapelekwa Canada na Uingereza.

  Kuna mameneja na wakurugenzi ambao walikuwa wakiharibu hapa wanapelekwa pale, nayo hii iliuwa hali ya walalahoi kujituma kwenye uzalishaji mali viwandani na maofisini…!

  Kuhusu mazao ya biashara kama korosho, pamba na mengineyo ambayo serikali imeshindwa kuyapatia masoko na dhurma imeamua kulipiza kisasi kiasi ambacho hata wananchi wakaona kuwa ni kazi bure kuingia kwenye kilimo cha mazao ya biashara, kwani hayana masoko uko nje au watawala wanawaibia wakulima kwa kuwalipa kidogo sana kiasi wakashindwa hata kununua pembejeo, kazi kila msimu ni kukopa tena na tena.

  Mstaafu huyo wa serikali ya ujamaa alionyesha kuwa huenda mazao ya Biashara yamehujumiwa na wale ambao tulio wadhurumu kipindi kile cha Azimio la Arusha… Nasikia India ndio ilikuwa mnunuzi mkubwa wa korosho ya Tanzania.

  Pia alidai kuwa viwanda vingi vilivyotapakaa kuanzia Kibaha, barabara ya Nyerere, Barabara ya Kilwa, na uko mikoani vilijengwa bila kuzingatia utafiti wa kitaalamu juu ya uwezo wetu wa uzalishaji. Na vile tulivyo virithi toka mkoloni tuliwapatia watendaji wasio na uwezo wala ubunifu wa kuendeleza viwanda.

  Alihitimisha kwamba maamuzi ya kisiyasa yaliyofanywa na watawala wetu bila kuzingatia ushauri wa kitaalamu ndiyo sababu ya kukata tamaa kwa Watanzania na hivyo kuwa wavivu. Watawala walikuwa Hawa-Hambiliki

  Lakini cha ajabu leo hii kuna matajiri wakubwa kupindukia kiasi ya kwamba nafasi kati ya walio nacho na wasio nacho ni kubwa sana…!


  Nilipo angalia muda nikaona umeyoyoma, nikanyayuka na kuelekea zangu nyumbani uku nikiyatafakari maneno ya mzee yule mstaafu... Nikawa najiuliza Natamani nami nikagombee japo Ubunge, lakini nashindwa ni ahadi au matumaini gani niwape watu hao.... Utashangaa zaidi ukianza kufikiri kuwa watu hawa wamekuwa wakishiriki uchaguzi wa wabunge na Rais kama mara nane sasa tangu tupate uhuru, na hasa nashindwa kujua ikiwa wengi wao wanafahamu uhusiano uliopo baina ya thamani ya kura zao na hali yao duni ya maisha....!

  Nakumbuka kuna wakati ilisemekana kuwa baadhi ya wabunge wa kusini waliona ni heri kujitenga na kujiunga na Msumbiji. Kipindi kile tuliwaona kuwa hawa wabunge wamekosa uzalendo au wamekosa la kuongea bungeni.

  Hata mie nilidhani hivyo hivyo, lakini sasa nimeona mantiki ya tamko lile. Kwanza wenzetu wa Msumbiji wanasababu ya kuwa masikini. Uhuru wao wote, wameishi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini sisi tunajivunia amani na utulivu hali yetu shwari kabisa, "Mchawi" wetu ni nani?

  Wako watu ambao tayari walishaanza kushtuka mapema... Lakini pia wako wapiga kura walioanza kujua chanzo cha matatizo yao na kutumia kura zao vema. Wako wale ambao wanadhani hali yao ya maisha inatokana na kudura za Mungu… na hawaitaji mabadiriko maana kila kiongozi ni chaguo la mungu.

  Palipo na matatizo watu uja na njia na mbinu mbalimbali za namna ya kutatua tatizo. Kwa wale wenye mtazamo wa kisiyasa kama mimi na wewe huenda watu hawa wanahitaji msaada wa kisiyasa, katika zama hizi za uwazi na ukweli ni vyema wakazifahamu haki zao za kiraiya, wakajua kutofautisha kati ya mwananchi na raia. Na kufahamu thamani ya kura zao.

  Wakijua hili ni rahisi kujua kuwa kura yao ndiyo itakayochagua aina ya maisha watakayoishi miaka 10 ijayo. Baada ya hapo watampima muombaji kwa kile atakachowafanyia, watamtazama endapo hana uhusiano na hao waliowadumaza.

  Kwa wale walio katika madaraka njia hii huenda ikawa mbaya kwao endapo wananchi wakigundua kuwa ndiyo "wachawi" wao la sivyo ni njia nzuri ya kutofautisha wanasiyasa wa watu na wale wababaishaji.

  Ni wazi pia kuwa wako wananchi ambao hawajui kuwa wanataabu kwa vile tu hawajawaona wenzao wenye afadhali. Pia wapo wanaojua wana taabu lakini hawajui wafanye nini.

  Cha msingi ni kwamba wote tunao tegemea maisha ndani ya Tanzania yawe bora kuliko yale ya Tanganyika, hatukutegemea kuishi ndani ya "Tanganyika" hadi leo hii miaka inakaribia hamsini (50) baada ya uhuru.

  Hata Mlalahoi naye ana hadhi yake na haki zake zinazoandamana na hadhi hiyo. Tanzania bado kuna hukumu ya kifo na nina uhakika kabisa Walalahoi wote tumekwisha hukumiwa kifo tayari, japokuwa si kwenye mahakama rasmi, lakini tawala zetu zimesha tuhukumu... japokuwa si kile cha kunyongwa hadi kufa kwa kuning'inizwa kambani lakini cha moto tunakiona... Na tunakufa taratibu tukijiona na machozi yetu yenda na maji hakuna wa kuyaona.

  Walalahoi tunajiuliza "Masihi Mkombozi" wetu atazaliwa lini? Au huenda baadhi yetu tunatamaa labda ndiye huyu au yule… Maana zama hizi wapo wengi kweli kweli.

  Ninachopenda kuwaambia ni kuwa maendeleo ya watu huletwa na watu wenyewe. Tuuzeni kura zenu kwa maendeleo… Tusipapie tena pilau, vitenge na pesa za kula leo na tukabakia na njaa ya miaka kumi ijayo.

  Nyie wanasiyasa mnao jiita wapinzani “Masihi watarajiwa” wa Kumkomboa Mtanzania mmefanya juhudi zipi kutuelimisha wapiga kura wenu ili tupate kuwachagua… ? Je ni kweli mpo tayari kutuletea maendeleo tukaishi Tanzania badala ya Tanganyika au ni sawa na kubadilisha mkono, leo kushoto kesho kulia....!?
   
 2. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #2
  Nov 3, 2009
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  kabla ya wakoloni wa kijerumani, kulikuwa na wakoloni wa kiarabu mkuu. Au wewe unasemaje?
   
 3. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #3
  Nov 3, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Sikumbuki kama walitawala Tanganyika yote au walikuwa kwenye baadhi ya Maeneo fulani fulani tu, sina uhakika pia na harakati zozote za kujikwamu kutoka kwa watawala wa kiarabu zaidi ya Unguja na Pemba.
   
 4. G

  Gashle Senior Member

  #4
  Nov 3, 2009
  Joined: Mar 30, 2007
  Messages: 116
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Mkubwa X-Paster

  Bandiko lako ni kubwa na linagusa nyanja mbali mbali zinaonyesha harakati za M/Tanzania/Tanganyika katika mapambano ya kimaendeleo tangu wakati wa ukoloni mpaka hizi nyakati za ukoloni mamboleo. Nimependa uchambuzi wako japo msimamo wangu pengine ukawa tofauti kidogo na wako.

  Najiuliza, kwa watawala kuyafanya yale waliyoyafanya tangu wakati Tanganyika yetu imepatikana mpaka walipoamua kustaafu nadhani si vema ku generalize kwamba walikuwa na malicious intentions. Kama baadhi yao walivyowahi kusema hawakuwa malaika na kuna makosa waliyoyafanya kama bin adam, ni maoni yangu kuwa tusichambue katika muonekano wa 1+1=2.

  Nafikiri kunayo waliyoyafanya ya maana yakaonekana, na kuna waliyoboronga pia.

  Jambo la maana ni kuwa tutaendelea kukaa hapa tulipo mpaka lini! Angalizo lako ni nafasi ya mwananchi yeye kama yeye kuleta mabadiliko kwa kutumia kura yake. Je, huu uelewa tunashirikiana sote na kung'amua kuwa kura yangu mimi moja ndio chanzo cha mabadiliko?

  Nachelea nyimbo zilizoanza kuimbwa kwa sasa ni zile zile... hukawii kusikia mambo ya khanga, sukari, elfu kumi nk ndio wakati wake sasa.

  Kwa mtazamo wangu, likiibuka vugu vugu jipya tofauti na haya yaliyopo ndio tutaweza kulifikia lengo letu. Kwa sasa nachelea kusema kuwa zaidi ya vijana wachache waliozaliwa majuzi, wengi wetu kwenye vugu vugu tulikuwa kule kule. Kuna nyakati nafsi zetu pia zinatusuta zikijiuliza hata wewe!!!!!
   
 5. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #5
  Nov 3, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mkuu Gashle, ahsante sana kwa kusoma na kutoa maoni yako, hii inaonyesha jinsi gani unajali yale yanayo jili ndani ya taifa letu Changa (!? sina uhakika kama ni kweli)... Waandishi siku zote huwa wachokozi tu katika kuwakilisha jambo fulani, wasomaji kazi yao baada ya kusoma na kutafakari huja na mawazo yenye kujenga na kuongoza kwenye suruhisho la uhakika, aidha la muda mfupi au mrefu... Basi tuwaachie wasomi waandamizi wenye vipaji watuletee sera zitakazo weza kutekelezeka ili tupate kukwamuliwa kwenye lindi la madhira haya...!
   
 6. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #6
  Nov 3, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Tanganyika 2009

  09.jpg
  [​IMG]


   
 7. G

  Gashle Senior Member

  #7
  Nov 4, 2009
  Joined: Mar 30, 2007
  Messages: 116
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Unajua, siyo tu kujali yanayojili ndani ya Taifa, bali pia nina uchungu na yanayoendelea. Tusiende mbali, hebu angalia bandiko la picha hapo juu uliloweka, si wanasema picha moja yaweza kuongea maneno alfu moja?

  Mimi siku hizi nimefikia kwenye kutaka kuona solution za matatizo yetu, hatuhitaji mtu kuja kufanya utafiti na kutueleza kuwa tuko kwenye crisis kubwa. Swala ni nini kifanyike? Je Tanzania anayotamani X-Paster, ipo? inawezekana? kama ipo na inawezekana, how? unajua hivi vi usanii vya kupimana viatu halafu kila baada ya miaka mitano tunafuatwa kuambiwa mlikuwa mnataka viatu vya aina gani, muda wake umekwisha...
   
 8. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #8
  Nov 4, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Unayo yasema ni kweli kabisa Gashle, lakini ni wangapi ambao wana uchungu wa kweli wa kumkwamua kabwela a.k.a Mlalahoi, yule ambaye anapata mshahara wa kijungu jiko (Kima cha chini).

  Nikitoa mfano wa fikra za Mtanzania wenye kutumia mitandao kama huu JF, wengi nawaona fikra zao zimejikita kwenye kukomoana na kuwaona wenzao kuwa hawana akili, kila kukicha ni thread za matusi, fitna na majungu... mara nyingi mwandishi uwaikilisha mawazo ya jamii anayoishi... sasa kama humu JF kuna watu wenye uwezo mzuri tu wa kutoa maoni yenye kujenga, lakini kwa sababu zisizo na maana nzuri wanatumia muda na nguvu zao kurumbana kwenye mambo yasiyoweza kumkomboa Mtanzania kifikra... Unafikiri tutafika...!?

  Niritarajia JF kuwa ni kioo cha jamii, kioo ambacho kitamuonyesha Mtanzania aliye komaa kimawazo na kuweza kuelezea suluhisho la matatizo yetu bila kujali Ukabila, itikadi za kisiasa, Kiuchumi, Imani za kidini na tofauti zinginezo... Lakini hasha kila kukicha ndio kwanza makundi yenye kuchochea chuki dhidi ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe yanazidi kukua na kuongezeka...!

  Nchi za ulaya zinaungana na kuwa wamoja, sisi tunatafuta sababu za kutengena tena kwenye ngazi hizi za kijamii, mtu na mtu... Kuna safari ndefu sana mbele yetu...! Lakini macho na fikra zetu ni za panzi tunaona mwisho ncha ya pua zetu...!
   
 9. K

  K4jolly JF-Expert Member

  #9
  Nov 4, 2009
  Joined: May 21, 2009
  Messages: 366
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nimesoma mchango wako ni mrefuni mzuri na unagusa nyanja zote pia umenikumbusha historia huko nilikotoka. Nitaelezea juu juu kile ambacho kinagusa maisha yangu ya sasa.

  UPE - Hii upe aliileta Mwl Nyerere hivi nataka kujua alitaka watu wasielewe kama yeye au nini? Nafikiri kulikuwa na mbinu ndani yake ya kutupumbaza tusielewe kinachoendelea yaani tuwe wajinga wajinga, wenye kujua watatuhabalishe.

  Pia kulikuwa na hii watu wasimiliki mali huoni kuwa nayenyewe imeturudisha nyuma kwani watu walibanwa ndo sasa hivi wamezinduka kila mtu kwa pupa anajilimbikizia anavyotaka baada ya kutoka kwenye umaskini.

  Kuna wakulima na wafanyakazi - hapa TZ sitegemei kama kuna wakulima nenda huko vijijini, baba/mama/vijana hakuna hata mmoja mwenye ekali moja ya mahindi au muhogo tumekalia uvivu tena angalau enzi hizo sijui kulikuwa na kilimo cha kulazimisha kama haulimi ******* pingu, angalia KILIMO KWANZA inavyokuja na umwagiliaji na pembejeo mimi bado sielewi mpaka sasa hivi yule mkulima maskini kama ataweza. Bila kulazimishana hapa kuna mtu atalima?


  Wafanyakazi maofisini sijui kama kuna wafanyakazi wa kusimamia sheria zenyewe za kazi, sasa hivi mfanyakazi anaingia leo kazini anawaza kujenga nyumba, gari, pesa yaani ni rushwa tupu, ndo hiyo serikali inaongoza.

  Viongozi wetu hawawajiki, na wenyewe ndo hivyo wanawaza mali ukichanganya na siasa basi pesa yote ya kodi inaishia kwenye mambo yanayolenga uchaguzi. Hivi serikali inaweza kushindwa hata madawati hiyo hata sielewi. Na ukifanya uchunguzi watu maskini ndo wale wanaopiga kura kuchagua chama kinachowapa umaskini.
   
 10. G

  Gashle Senior Member

  #10
  Nov 4, 2009
  Joined: Mar 30, 2007
  Messages: 116
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  k4J,

  Nakubaliana na baadhi ya usemayo, japo kuna baadhi yananitatiza. Unajua, hii tabia ya kumlaumu Nyerere kwa kila kitu nayo ni sehemu ya tatizo kubwa tulilo nalo. Mzee yule aliongoza kama miaka 24 hivi baada ya uhuru, haya tu assume kuwa alikuwa hivyo watu wanavyopenda aonekane, inawezekanaje miaka karibu 20 baada ya yeye kuondoka ndio hali yetu inazidi kuwa mbaya kuliko?

  Nyerere ndie aliewafundisha mafisadi ufisadi wao? hata kile kizazi kilichozaliwa baada ya Nyerere kinalishwa kasumba, Nyerere alitulostisha, ya kweli haya?

  Maoni yangu, kwamba nani alitupelekea huku tuliko inaweza isiwe sababu kubwa sana, hapa cha kuangalia kifanyike nini. Kama ingekuwa ni habari ya kutafuta mchawi, hivi sasa Rwanda ingekuwa inaongoza kwa ufisadi duniani, si walikuwa na mauaji ya kimbari bwana? na wakusingiziwa si yupo?

  Wito wangu, shime wananchi, tumevamiwa, tuamke. wakati wa kulala usingizi watosha.
   
 11. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #11
  Nov 6, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Ahh wapi! Ndio kwanza wanakoroma kwa usingizi mzito na ndoto zisizo kwisha.
   
 12. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #12
  May 16, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  [​IMG]
   
 13. jmushi1

  jmushi1 JF-Expert Member

  #13
  May 16, 2010
  Joined: Nov 2, 2007
  Messages: 17,582
  Likes Received: 1,942
  Trophy Points: 280
  Kuna mameneja na wakurugenzi ambao walikuwa wakiharibu hapa wanapelekwa pale, nayo hii iliuwa hali ya walalahoi kujituma kwenye uzalishaji mali viwandani na maofisini…! Hayo ni yale yale ya ma Mr Yes,matokea tunayajua,ndio waliotulet down kwa unafiki wa kujidai wanakubalina na fikra zote "Sahihi"
  Nakumbuka kuna wakati ilisemekana kuwa baadhi ya wabunge wa kusini waliona ni heri kujitenga na kujiunga na Msumbiji. Kipindi kile tuliwaona kuwa hawa wabunge wamekosa uzalendo au wamekosa la kuongea bungeni
  Tarizo ni lile lile la "Kutoambilika/kushahuriwa na kuulizwa maswali magumu!Sera na itikadi nzuri mbona zipo tu?anya knyume na hayo basi wewe ni unpatritoc na unaweza kuwa detained indefinetly ama kutengwa na kunyiwa nafasi ya uongozi naogopa viongozi wasipenda kuulizwa maswali magumu,tatizo tunalo!
   
 14. k

  kasimba123 JF-Expert Member

  #14
  Apr 20, 2011
  Joined: Apr 18, 2010
  Messages: 1,318
  Likes Received: 188
  Trophy Points: 160
  U.P.E(uwalimu Pasipo Elimu)
  nakumbuka salamu ya darasa la nne
  Ili tuendeleee tunahitaji vitu vinne Watu, Ardhi, Siasa safi, na Uongozi bora shikamoo mwalimu hehe
   
Loading...