Nataka Pesa Zangu Zote wakati wa kustaafu

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
Nini kingetokea iwapo kingesikilizwa kilio cha "Nataka Pesa Zangu Zote wakati wa kustaafu"?

Karibu tukokotoe.

Tukubaliane *dhana* za awali:

*Fungu A.*
Mshahara kwa mwezi wakati wa kustaafu: 1,000,000 TZS
Mshahara kwa mwezi muda wote wa utumishi: 1,000,000 TZS
Muda wa utumishi: Miaka 20 (miezi 240).
Mtumishi atastaafu kwa lazima.
Mtumishi hataishi kupokea pensheni ya kila mwezi hata ya mwezi mmoja.

*ZINGATIA*; katika hali halisi wengi huanza na mishahara midogo na hupata mishahara iliyoongezeka mwishoni kuliko mwanzoni.

Zingatia pia watumishi wengi hawafariki siku ya kustaafu.

Makato: (i) Asilimia tano kwa mwezi (5%)
(ii) Asilimia kumi kwa mwezi (10%).


*Fungu B.*
Mshahara kwa mwezi wakati wa kustaafu: 1,000,000 TZS
Mshahara kwa mwezi muda wote wa utumishi:

Miaka mitano ya kwanza: 400,000 TZS
Miaka mitano ya pili: 600,000 TZS
Miaka mitano ya tatu: 780,000 TZS
Miaka mitano ya mwisho: 1,000,000 TZS

Muda wa utumishi: Miaka 20 (miezi 240).

Makato: (i) Asilimia tano kwa mwezi (5%)
(ii) Asilimia kumi kwa mwezi (10%).

Mtumishi atastaafu kwa lazima.
Mtumishi hataishi kupokea pensheni ya kila mwezi hata ya mwezi mmoja.

*MATOKEO:*

*FUNGU A*
Jumla ya Akiba (Michango yako makato 5%) 12,000,000.00 TZS

Jumla ya Akiba (Michango yako makato 10%) 24,000,000.00 TZS

Hizo ndio pesa *ZAKO* ulizoziweka kwenye mfuko wa pensheni. Bila kujumuisha michango ya *MWAJIRI*.

Pensheni ya Jumla: 62,068,965.52 TZS

Kiinua Mgongo siku ya kustaafu: 15,517,241.38 TZS

Pensheni ya kila mwezi: 310,344.83 TZS

Pensheni ya Kila Mwezi kwa miaka mitatu: 11,172,413.88 TZS

Jumla ya Malipo toka kwa Mfuko: 26,689,655.26 TZS

Kiinua Mgongo + PensheniYaMiaka3 – Michango Yako (5%) = 14,689,655.26 TZS

Kiinua Mgongo + PensheniYaMiaka3 – Michango Yako (10%) = 2,689,655.26 TZS



*TAFSIRI RAHISI*

Kwa utaratibu ulioko sasa,

Wenye makato 5%, kwa Mshahara wa 1,000,000 toka kuajiriwa kwa miaka ishirini;

Unalipwa kiinua mgongo 3,517,241.38 TZS *ZAIDI* ya michango uliyotoa.

Ukiongezea na pensheni ya miaka 3 watakayolipwa warithi: atakuwa amepokea 14,689,655.26 TZS *ZAIDI* ya michango yake aliyotoa.



*FUNGU B*
Jumla ya Akiba (Michango yako makato 5%) 8,340,000.00 TZS

Jumla ya Akiba (Michango yako makato 10%) 16,680,000.00 TZS


Hizo ndio pesa *ZAKO* ulizoziweka kwenye mfuko wa pensheni. Bila kujumuisha michango ya *MWAJIRI*.

Pensheni ya Jumla: 62,068,965.52 TZS

Kiinua Mgongo siku ya kustaafu: 15,517,241.38 TZS

Pensheni ya kila mwezi: 310,344.83 TZS

Pensheni ya Kila Mwezi kwa miaka mitatu: 11,172,413.88 TZS

Jumla ya Malipo toka kwa Mfuko: 26,689,655.26 TZS

Kiinua Mgongo + PensheniYaMiaka3 – Michango Yako (5%) = 18,349,655.26 TZS

Kiinua Mgongo + PensheniYaMiaka3 – Michango Yako (10%) = 10,009,655.26 TZS


*SOMO*
Endapo kilio cha "nilipwe *HELA ZANGU NILIZOCHANGIA!1!*" kitasikilizwa, Mtumishi atapokea kiinua mgongo kidogo kuliko anachopokea sasa hivi.

*"Be very careful what you wish for, because you might very well get it"*. ~ Msemo wa Bazungu.


*HINT:* Pakiwa na makosa ya ukokotoaji popote hapo, nijuze.
 
Mkuu Mlenge

Kuna mengi yamejitokeza tangu mabandiko yako. Kadri siku zinavyosonga watu wa mifuko wanakuja na hoja mpya. Nadhani hilo linazidi kuwachanganya wananchi na kuhisi jambo

Mkuu naomba urejee tuongee kidogo, ninaamini katika mifuko ya jamii, lakini hii ya Tz kuna walakini
 
Mkuu Mlenge

Kuna mengi yamejitokeza tangu mabandiko yako. Kadri siku zinavyosonga watu wa mifuko wanakuja na hoja mpya. Nadhani hilo linazidi kuwachanganya wananchi na kuhisi jambo

Mkuu naomba urejee tuongee kidogo, ninaamini katika mifuko ya jamii, lakini hii ya Tz kuna walakini

Mkuu Nguruvi3 ,

Kipindi hiki ilibidi kutulia kwanza. Michango mingi ilijaa ghadhab kusikia wenzetu waliostaafu miezi michache tu iliyopita, kama walipata mafao ya kiinua mgongo cha TShs 80m, basi sisi wa sasa tutapata 20m. Kwa nini tupate 25% ya kile wenzetu walipata? Kwa nini siyo zote 100%? Kwa nini tulipwe kwa miaka 12 tu baada ya kustaafu? Itakuwa wanataka kujengea Stigla Joji au kununulia Bombadia nyingine kwa kutumia hela ZETU. Hiyo ni dhulma na wizi wa waziwazi. Vyama vya wafanyakazi vipo wapi kukemea udhulmat huu? Watu wakanukuu maandiko yanayowalaani watunga sheria kandamizi.

Tatizo, ghadhabu hizo hazikutokana na hali halisi. Na kila mara akijitokeza mtu wa kutoa ukweli wa taarifa, ili mjadala uanzie pahala penye usahihi wa taarifa, mtu huyo alishambuliwa vikali -- yeye -- na siyo hoja au ukweli anaoubainisha.

Kwa kifupi:

1. 25% ni kanuni isiyotungwa na Bunge.
2. Ilitungwa toka mwaka 2014, na kuanza kutumika wakati huohuo wa Awamu ya Nne.
3. Kama mtu alistaafu miezi michache kabla ya sheria hii mpya alipata 80m, atakayestaafu baada ya sheria mpya atapata 80m hiyohiyo kwa vile kanuni ni ya toka 2014.
4. Hiyo 25% ni ya kwenye Total Pension na siyo 25% ya kiinua mgongo kama inavyodhaniwa na wengi. Pensheni ya mwezi haina mwisho wa kulipwa.

Je, hii ni kusema 25% ni nzuri au ni mbaya? Hapana. Hii ni kusema mijadala izingatie hali halisi.

Zamani (kabla ya 2014) wapo waliokuwa wakilipwa 50% pesa ya mkupuo. 50% pensheni kila mwezi. Kwa mfano wetu hapo juu, Akichukua 80m, na anachukua 400,000 kwa mwezi pensheni (mfano tu), kwa 25% atachukua 40m kiinua mgongo na 800,000 pensheni ya mwezi mpaka mwisho.

Lakini inavyoonekana walio wengi wanapenda kiinua mgongo kiwe kikubwa, hata kama pensheni ya mwezi itapungua.

Kukumbushia tu: fursa ya kutoa maoni ilipita humu JF kama haipo, mpaka pale matokeo yanapotokea ndio tunalalamika wakati treni lishaondoka:

Maoni Kuhusu Muswada Mpya PSSSF Hifadhi ya Jamii - JamiiForums

Ukweli Kuhusu Mafao ya PSSSF Sheria Mpya ya Kustaafu - JamiiForums

Nini Kifanyike?

Pana mapendekezo haya hapa chini, yaliyotolewa na Tanzania Higher Learning Institutions Trade Union (THTU), chama cha wafanyakazi wa taasisi za elimu ya juu, niliyoyakopi kama yalivyo kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo hapa: THTU YATAKA SULUHISHO KUHUSU TAHARUKI YA KIKOKOTOO CHA MAFAO YA KUSTAAFU - Full Shangwe Blog

THTU YATAKA SULUHISHO KUHUSU TAHARUKI YA KIKOKOTOO CHA MAFAO YA KUSTAAFU

Utangulizi

Hivi karibuni, umeibuka mjadala mkali juu ya mafao ya watumishi wanaostaafu ajira baada ya mfuko mpya wa PSSSF kuanza kufanya kazi. Mjadala huo unajikita kwenye kikokotoo cha mafao ambacho kinapunguza mafao yanayolipwa kwa mtumishi aliyestaafu. Mjadala huu ambao umetawaliwa na hisia kali umepelekea kurushiana lawama kwa taasisi na wadau wote wanaohusika na sekta ya hifadhi ya jamii. Ni wazi kabisa kwamba Vyama vya wafanyakazi vimelaumiwa, Bunge limelaumiwa, Serikali imelaumiwa na Mamlaka ya hifadhi ya jamii (SSRA) imelaumiwa. THTU tunaamini kwamba kuacha hili jambo liishe bila muafaka ni kutojitendea haki sisi kama Taifa lenye watu wakomavu na waliostaarabika. Kimsingi, mjadala wa mafao ya kustaafu limekuwa likijirudia mara kwa mara bila muafaka wa pande zote na hivyo kuendelea kuacha hisia za kurushiana lawama.


THTU tunaamini kwamba jambo hili liko ndani ya uwezo wetu kama Taifa kulipatia muafaka na ufumbuzi wa kudumu. Kwa msingi huo, tunapenda kuungana na wafanyakazi wote nchini na umma wa Tanzania kutoa maoni yetu machache kama kichocheo cha kuhamisha mjadala kutoka kulaumiana kwenda kwenye suluhisho ili hatimae hali ya utulivu irejee.


  1. Awali ya yote, tunakiri kwamba tulishiriki kikamilifu kutoa maoni yetu wakati wa kuandikwa sheria iliyounda mfuko wa PSSSF. Tunaishukuru na kuipongeza Serikali pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Huduma za Jamii kwa kutumia zaidi ya masaa matatu kusikiliza maoni yetu (wakati huo). Maoni mengi tuliyotoa kama chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu yalizingatiwa kwenye sheria husika. Tunathubutu kusema kwamba tunaikubali sheria iliyounganisha mifuko. Ni bahati mbaya sana kwamba uundaji wa kanuni ambazo ndizo zenye vikokotoo haukuwa shirikishi kwa upande wetu sisi THTU. Hata hivyo, tunaamini bado muda upo wa sisi kutoa maoni yetu kwa lengo la kuboresha
  2. Mjadala mkubwa ulioibuka baada ya mfuko wa PSSSF kuanza kazi umejikita katika vikokotoo vinavyoshusha mafao ya mkupuo kwa wastaafu hasa kwenye kipengele cha asilimia sihirini na tano (25%).
  3. Ieleweke kwamba ni kweli Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imejitahidi sana kuboresha mafao hasa kwa Mifuko ya PPF na NSSF ambayo ndiyo ilikuwa inalipa mafao kidogo sana kuliko mifuko mingine kabla ya kuunganishwa
  4. Mfano mzuri ni kikokotoo cha PPF ambacho awali kilikuwa 1/960; baada ya majadiliano na SSRA na mfuko husika ikawa 1/600 na mwaka 2014 SSRA ilisawazisha kikokotoo kwa mifuko yote ikawa 1/580 isipokuwa kwa watumishi wa mifuko ya LAPF na PSPF kabla ya Julai 2014 ambao walibaki na 1/540. Ndio maana wakati huo Profesa aliyefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 akichangia mfuko wa PPF alilipwa fao la mkupuo la milioni isiyozidi ishirini na tano (25,000,000) wakati mtumishi aliyestaafu akiwa PSPF/LAPF alipokea milioni sitini mpaka mia moja. Mfano huu pekee utupe faraja kwamba majadiliano ya pamoja huleta suluhisho lenye manufaa kwa pande zote
  5. Baada ya vikokotoo kusawazishwa mwaka 2014, wale watumishi waliokuwa wakichangia mifuko ya PSPF na LAPF kabla ya Julai 2014 waliruhusiwa kubaki na kikokotoo chao kilichokuwepo ambacho ni 1/540, miaka 15.5 na 50% ya fao la mkupuo. Kikokotoo kilichosawazishwa ni 1/580, miaka 12.5 na 25% ya fao la mkupuo. Hii ina maana ilitengenezwa makundi mawili katika ulipaji wa mafao ya kustaafu.
  6. Baada ya mfuko wa PSSSF kuanzishwa, kikokotoo kilichosawazishwa na ambacho kilianza kutumika mwaka 2014 kimeondoa yale makundi mawili yaliyokuwepo hasa kwenye vipengele vya asilimia na miaka. Hii ina maana kwamba wastaafu wote wanaanza kutumia kikokotoo cha 1/580, miaka 12.5; 25% ya fao la mkupuo na 75% ya pensheni ya kila mwezi. Kwa msingi huu, walioathiriwa zaidi na kikokotoo kipya ni wale waliokuwepo kwenye mifuko ya PSPF na LAPF kabla ya Julai 2014. Kundi hili lililoathiriwa limesaidia kutoa picha halisi ya mafao ya hifadhi ya jamii baada ya mtumishi kustaafu
  7. Sisi THTU tunaamini ukweli huu uliodhihirika au uliojidhihiri wenyewe unapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na kurekebishwa kwa mjadala wa pamoja. Wizara husika kupitia SSRA inaweza kuratibu zoezi la kupokea maoni ya wadau wote kwa lengo la kurekebisha kikokotoo kilicholeta taharuki na hivyo kutuliza wafanyakazi. SSRA imeshafanya mikutano mingi na wadau hasa wafanyakazi kupitia vyama vyao tangu ilipoanzishwa. Majadiliano ya pamoja itapelekea uwepo wa muafaka wa pamoja na kuacha kulaumiana.
  8. Sisi THTU tunatoa pendekezo la kuanzia kuelekea mjadala wa pamoja kwamba kikokotoo KIBORESHWE ili kuondoa makundi yaliyopo sasa. Pendekezo letu la kuboresha kikokotoo ni 1/540, miaka 15.5 na 50% ya fao la mkupuo na 50% inayobaki iwe pensheni ya kila mwezi. Bahati nzuri SSRA imetoa ufafanuzi mzuri kabisa kwamba kwa kikokotoo cha sasahivi, mstaafu atalipwa pesa zake zote kwa utaratibu wa 25% mkupuo na 75% kila mwezi. Kumbe mwisho wa siku mstaafu atalipwa pesa zake zote. Mjadala wa pamoja ujikite kwenye swali hili; Je! Tunaweza kuboresha kikokotoo kikawa 50% ya mkupuo na 50% iliyobaki ikaingia kwenye pensheni ya kila mwezi? Maeneo mengine yanayolalamikiwa yatajadiliwa kwenye mjadala wa pamoja.


Hitimisho

Ni pendekezo letu THTU kwamba sasa tatizo limeshafahamika. Tuhamishe mjadala kutoka kulaumiana kwenda kwenye suluhisho. Sasa tuunganishe nguvu na akili zetu kutafuta suluhisho. Mwalimu Nyerere anatuasa kwamba tujisahihishe. Tusiogope kujisahihisha. Sisi tumeanza na pendekezo. Tunawaalika wadau wote kuelekea kwenye mjadala wa pamoja kupata muafaka wa pamoja. Hakuna linaloshindikana, tutimize wajibu wetu.


Muhimu:

THTU itakutanisha wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii ili kuandaa mapendekezo ya kina na kuwasilisha SSRA na Wizara husika kwa ajili ya mjadala na ufumbuzi. Tunaamini mapendekezo yetu yanaendana na malengo ya kulinda afya za muda mrefu ya mifuko na pia kutimiza malengo ya hifadhi ya jamii.

DKT Paul Loisulie

MWENYEKITI THTU Taifa
 

Attachments

  • Taharuki ya Pensheni.pdf
    75.1 KB · Views: 13
Back
Top Bottom