Kilimo cha Viazi Mviringo (Viazi Ulaya) na Masoko Yake

Makambuya

Member
Dec 6, 2011
45
3
Kilimo cha Viazi Mbatata.jpg


Kwa mwana JF yeyote mwenye ujuzi na uzoefu wa kilimo cha viazi naomba anipe detail kuhusu kilimo hicho.

Yaani kwa mfano, nikitaka kulima hekari moja natakiwa kuwa mtaji wa kiasi gani? Na vipi namna ya kupata shamba? Msimu unaanza mwezi wa ngapi? Jinsi ya kulima na tahadhari za kuchukua wakati wa kilimo hiki. Pia, ningejua masoko yake yapoje inaweza kusaidia kwangu na kwa wengi.

Please naomba msaada.

BAADHI YA WADAU WENGINE WANAOHITAJI KUJIFUNZA KUHUSU KILIMO HIKI
Habari wadau,

mimi ni mwajiriwa lakini pia mwaka jana niliamua kujaribu kulima kujaribu bahati yangu.

Nililima viazi mvilingo(ulaya) heka tatu kwa majaribio huko mpakani mwa njombe na ludewa.sasa nimepigiwa simu (mi naishi Dar) kuwa viazi vimeshakomaa na viko tayari kuvunwa, lakini tatizo ni bei iko chini kupita matarajio yangu

kwa kiroba cha debe sita za viazi ni elfu 30.sasa bei hiyo imenikatisha tamaa sana kwa sababu nilitegemea ingekuwa elfu 40 na zaidi,na mpaka sasa sijaenda huko kuvuna kwa sababu hiyo.

Naomba ushauri kama kuna mtu anajua kuhusu hii biashara ya viazi na hasa soko kwa hapa Dar na mambo mengine kwa sababu sijawahi fanya biashara hii kabla.

Natanguliza shukrani zangu za dhati.
Habari,

Nina mpango wa kulima viazi mviringo msimu ujao wa mvua, ila sina uzoefu na wala sijawahi kulima naomba kwa yoyote mwenye kujua vya zaidi kuhusu kilimo cha viazi mviringo anijuze. Nataka kulima ekari moja, labda kwa ufupi nijue ntatumia mbegu kiasi gani? Napandaje? navuna baada ya miezi mingapi?

Asanteni kwa kunisaidia.
Naombeni kujua garama za kilimo cha viazi ulaya ukilima hekari moja. Msaada juu ya:
  • Mbegu
  • Madawa
  • Kulima
Na mengine nisiyoyajua asanteni sana, location ni Lushoto.


MAJIBU YA WADAU KUHUSU KILIMO HIKI
KILIMO CHA VIAZI MVIRINGO (SEHEMU YA 1)​

MAZINGIRA
Viazi mviringo (Solanum tuberosum) hupendelea maeneo yenye baridi kuanzia 7v°C hadi 26°C kwa siku 75 hadi 135 za ukuaji wake au zaidi, Hali ya joto hupunguza kiasi cha uzalishaji. Zao hili hupendelea udongo tifutifu usiotwamisha maji na wenye rutuba na wenye maozea "Matama huruku" (Organic matter) yenye pH ya 5.0 hadi 5.5.

AINA
Nchini Tanzania kuna mbegu za aina yingi za viazi mviringo ambazo hazalishwa na taasisi mbalimbali za utafiti wa kilimo (Agriculture Research Institute). Kwa upande wa Nyanda za juu kusini mwa Tanzania, Taasisi ya utafiti wa kilimo Uyole (ARI UYOLE) iliyopo mkoani Mbeya inazalisha mbegu za viazi mviringo zifuatazo;

1. Baraka
2. Kikondo
3. Tana
4. Arika

Mbegu zote za hapo juu hufanya vizuri endapo utatunza vizuri kwa kufwata taratibu za kilimo bora.

MAANDALIZI YA MBEGU

Kabla ya kupanda viazi mviringo lazima uwe na mbegu zilizotayari kupandwa. Mbegu zilizo tayari kupandwa huwa na machipukizi au maotea. Kama utapata mbegu zenye maotea unaweza ukazipanda. Pia mbegu hizo au kiazi kimoja cha mbegu kinaweza kutoa mbegu 2 au tatu inategemea ukubwa wa hicho kiazi.

Namna ya kuandaa mbegu kutoka kwenye kiazi kimoja (Viazi vikibwa);
  • Kata kiazi hicho katika vipande kadhaa vyenye maotea kila kimoja, maotea yanaweza yakawa zaid ya moja. Yani kila kipande ulichokata lazima kiwe na maotea (buds).


  • Baada ya kuandaa vipande hivyo vianike juani, au kama jua halipo kwa kipindi cha masika vitandaze mahali pakavu ili vikauke. Lengo la kuanika ni kusaidia zile sehemu zilizokatwa zikauke na zijirudi kama kiazi cha kawaida. Ina maana kwamba ukipanda hivyo hivyo mbegu zitaoza.
Namna ya kuandaa mbegu za viazi visivyo na maotea (Chitting);
  • Chagua viazi mviringo vyenye afya
  • Andaa chumba kisafi chenye giza yani kilichofungwa madirisha na milango ili kuzuia mwanga kupenyeza ndani.
  • Weka turubai au mkeka au masalfeti juu ya sakafu (lengo ni kuzuia unyevu wa sakavu kuozesha viazi)
  • Tandaza viazi kwenye chumba hicho kwa levo au ngazi moja.
  • Funga chumba hicho kwa wiki moja au mbili mpaka utakapoona machipukizi yametoka.
  • Ukiona machipukizi yameota basi viazi vipo tayari kupandwa. (Unaweza ukavikata katika vipande na kuviandaa kama nilivyoeleza hapo juu)





Kuandaa mbegu ni jambo la msingi sana ikiwa ni pamoja na kujua kiasi gani kinahitajika kwa eneo husika (seed rate)
Kwa viazi vikubwa vyenye uzito kuanzia gamu 50 na kuendelea kiasi cha mbegu ni magunia 24 kwa hekta moja.
Kwa viazi vidogo chini ya gramu 50, kiasi cha mbegu ni magunia 8 - 10 kwa hekta moja.

KUPANDA
Viazi mviringo hupandwa kwa nafasi ya sentimita 30 kutoka mche hadi mche na sentimita 40 - 75 kutoka mstari hadi mstari. Pia unaweza kutengeneza matuta kwa kufwata nafasi hizo.
Kama utapanda viazi pasipo kutumia matuta basi hakikisha umelima shamba lako kwa kina cha kutosha cha sentimita 30, na viazi vikishaota rundika udongo maeneo ya shina (earthing) hadi kufikia kina cha sentimita 25.

MATUMIZI YA MBOLEA
Tumia mbolea za asili na mbolea za viwandani. Unaweza ukapandia samadi pamoja na mbolea za viwandani kama DAP. Alafu baada ya mimea kutoa maua, weka mbolea ya CAN halafu endelea kupulizia mbolea za maji kama VIGMAX na nyinginezo. Mbolea ya maji unaweza ukaendelea kupiga kila baada ya wiki moja. Ukifanya hivyo utaona matokeo mazuri ya uzalishaji.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
ABC's ZA KILIMO CHA VIAZI MVIRINGO
Viazi mviringo ni zao muhimu la chakula na biashara katika nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea. Viazi husitawi vizuri sehemu za miinuko, kati ya meta 1300 na 2700 juu ya usawa wa bahari. Hukomaa katika kipindi cha miezi mitatu hadi mitano. Viazi mviringo vina asilimia kubwa ya chakula chenye asili ya wanga. Pia vina kiasi cha kutosha cha protini, madini, vitamini na maji.

Mbegu bora za viazi: Zinatakiwa kuwa na sifa zifuatazo
· Zenye kutoa mazao mengi zaidi kutoka kwenye shina moja
· Ziwe zimechipua vizuri na ziwe na machipukizi mengi (zaidi ya manne)
· Zisiwe na wadudu au magonjwa
· Zitoke kwenye aina ambayo haishambuliwi na magonjwa kama vile ugonjwa wa ukungu na ugonjwa wa mnyauko bakteria
· Zenye ukubwa wa wastani (yaani zisiwe ndogo au kubwa sana) unaolingana na ukubwa wa yai la kuku wa kienyeji

Aina bora za viazi
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo uyole, mpaka sasa imetoa aina sita za mbegu bora za viazi mviringo nazo ni : Baraka, Sasamua, Tana, Subira (EAI 2329), Bulongwa [(K59a (26)], Kikondo (CIP 720050)

Muda wa kupanda viazi: August hadi Septemba na Novemba hadi Decemba

Kupanda
Tumia sentimeta 60 (futi 2) hadi 75 (futi 2.5) kutoka mstari hadi mstari, nafasi kati ya kiazi na kiazi iwe sentimeta 30

Mbolea
Ili kupata mazao mengi kutoka shambani mkulima anashauriwa kutumia mbolea, aina ya samadi, mboji, majani mabichi na za viwandani (au za chumvi chumvi).

Kwa mbolea za viwandani tumia: Kilo 300 (au mifuko 6) ya mbolea ya TSP kwa hekta moja, na kilo 300 (mifuko 6) za mbolea ya CAN au kilo 400 (mifuko 8) ya SA au kilo 175 (mifuko 3.5) za Urea.

Palizi: Palilia viazi wiki mbili au tatu baada ya kuchomoza. Inulia udongo ili kufanya tuta zuri ili pawepo na unyevu wa kutosha na kufunika viazi kutokana na mwanga wa jua.

Magonjwa na wadudu waharibifu: Ili kuzuia ugonjwa wa ukungu tumia Ridomil. Changanya gramu 100 za dawa ya Ridomil katika lita 20 za maji, na nyunyizia mara baada ya viazi kuchomoza na baadaye kila baada ya wiki mbili au tatu kutegemea na hali ya hewa. Nyunyizia dawa kama Karate kiasi cha mililita 20 mpaka 40 za dawa katika lita 20 za maji ili kuzuia wadudu kama inzi weupe na wengineo. Tumia mbinu bora za kilimo kama usafi wa shamba au kilimo mzunguko kama mbinu shirikishi katika kuzuia magonjwa na wadudu.

Kuvuna na mavuno: Viazi huwa tayari kuvunwa baada ya miezi 3 hadi 5 kutoka kupanda. Muda wa kuvuna utategemea madhumuni ya zao na aina iliyopandwa. Usiache viazi shambani bila kuvifunika (kwa nyasi au udongo) kwa muda mrefu kwa sababu zifuatazo:

· Viazi vikipigwa na jua hubadilika rangi na kuwa na rangi ya kijani ambayo inavifanya visifae kwa chakula.

· Wadudu kama vile nondo hutaga mayai juu yake, yanapoanguliwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya viazi na kuviharibu
· Iwapo vitanyeshewa na mvua vitaharibika wakati wa kuvihifadhi ghalani.

Aina bora kama Kikondo yaweza kutoa gunia 70 hadi 100 kwa ekari ikilimwa na kutunzwa vizuri.

Kuhifadhi: Viazi vya chakula vihifadhiwe kwenye ghala yenye hewa ya kutosha, pasiwe na unyevu, joto kali. Unapohifadhi viazi vya mbegu, aina mbalimbali zitengwe kwa kutumia vichanja au masanduku (maalum ya kuhifadhia) tofauti.

Shukrani za dhati kwa mtaalamu wa Kilimo mifugo na mazingira&Mratibu wa program ya CHEMA jimbo katoliki la Rulenge-Ngara padre Anthony Ndikumulimo na Mtaalam Jonas B..Kizima kutoka Chuo Kikuu cha SOKOINE SUA .

MAKADIRIO YA KILIMO KWA EKARI MOJA

Kilimo cha viazi kusini i.e Njombe, kwa eka moja
  • Kukodi 100000-150000
  • Kulima-Elfu 50
  • Mbolea elfu 50-70 (inategemeana aina ya mbolea na umenunua lini)
  • na si chini ya mifuko miwili ya kupandia
  • Mbegu gunia 7@elfu 40-50 or above
  • Mbolea ya kukuzia elfu 60 or above mara mifuko 3
  • Madawa ya ya ukungu, fanya elfu 40
  • Hela ya palizi elfu 50
  • Mengineyo 100000
Masoko yapo hasa kwa mwaka huu gunia la debe 6 lilifika 60 kwa sasa sipo sijui ni shingapi.

Changamoto kubwa ni ardhi iliyochoka na mabadiriko ya tabia ya nchi ambayo hupelekea viazi kutoota vizuri, ila ukipanda wakati mvua zimeanza kunyesha una uhakika wa kuvuna.

Mavuno inategemeana kama ulizingatia vigezo; lakini ni kati ya gunia 20-60 au zaidi za debe 6.
SHAMBA BORA NA KILIMO
Kwanza unachagua shamba zuri lisilo na bakteria, uliza historia ya shamba.

Angalia majani yalivyoshamili au mazao yaliopo yapoje.chunguza chanzo cha maji kilipo, hakikisha maji ni ya uhakika na ya siwe ya kugombania utakula hasara.

Mbegu bora ni kala na tigo na obama ipo mbegu nyingine nyeupe ipo kama tigo ni nzuri ina zaa sana na ina wahi kukomaa.heka moja unaihitaji gunia nane.

Mbolea dap npk na can, pandia dap mfuko mmoja na nusu au miwili.can mifuko 2 na mpaka 1,weka kabla ya palizi ya pili mwagilia wiki ya kwanza kisha acha vipumue siku hata tano, rudia tena mzunguko wa kumwagia na kupumua.vikichomoza, wiki ya pili anza kutifulia, vikianza kutoa watoto chini weka mbolea can na npk wiki ya 3 mpaka ya 5, mbolea weka upande wa juu usiweke mteremkoni. Kama utawahi mwezi 5 piga dawa za ukungu na mbolea za majani busta wiki ya 1 na 2.

Baadae piga npk na utamalizia vigmax wiki tatu kabla havijakomaa kutegemea aina ya viazi usiwahi vitaoza. Kama utapanda wa sita huna haja ya dawa za ukungu. Zingatia maji ukiweza weka sprinkta tatu au mbili. Kama maji mengi tumia mpira wa nchi moja hutajuta. Usitumie wasimamizi watakudanganya na utavuna mabua.

Kazi njema karibu kwa maswali zaidi.
HATUA ZA KILIMO CHA VIAZI MVIRINGO
Hatua ni nyingi ila inategemeana na mambo kadha wa kadha kama ifuatavyo;

1. Msimu unaolima, kuna viazi vya kiangazi na masika ie mwezi wa 11-12 na mwezi 3-7.Sasa unataka kulima vya mwezi wa ngapi.Tukuyu kuna maeneo wanalima hata mwaka mzima.

2. Andaa mbegu ilio bora, kuna ain a nyingi za mbe itayegemea na eneo ulipo.Arusha,Njombe, Mbeya au Iringa.Kwa kawaida heka moja haipungui mifuko 7-11

3. Andaa shamba vizuri, lisiwe na nyasi hata kidogo na lilimwe deep, kwa sababu viazi ni mizizi.

4. Andaa mbolea kulingana na eneo ulipo, uwekaji wa mbolea unatofautiana kulingana na ardhi, DAP, NPK NA CAN, kama kuna mbolea ya kuku nayo ni nzuri ila kuna utaalamu wake.Kama ardhi imechoka kila mfuko wa mbegu kiroba kimoja cha mbolea, kama haijachoka mifuko 4-5 mchanganyiko wa hapo juu.

5. Chimba mashimo sm30 kwa 75.

6. Weka kiazi kimoja kila shimo.

7. Weka mbolea iliochanganywa tafuta wazoefu wa kurusha mbolea au mwaka visoda 2 kila shimo mifuko ya mbolea isibaki hata kidogo,usipunje mbolea bora uzidishe

8. Fukia kwa kuweka vituta vidogo vidogo,usifukie sana vitaoza.

9. Andaa madawa ya muhimu ya kuchoma nyasi,ukungu,mbolea za majani na sumu ya wadudu.

10. Wiki ya 3-4 viazi vitanza kuota, hivyo vikiwa na majani kama matatu hivi piga dawa kuua nyasi na anza dawa ya ukungu na buster kwa msimu wa mvua.

11. Baada ya hapo utapiga dawa hizo 'as a routine' ratiba kwa kila siki 7-14 kulingana na msimu na hali ya hewa iliopo. Mvua nyingi dawa kwa wingi ukizembea unakula hasara hata wiki ya tano tu.

12. Piga palizi ya kwa kwanza kuanzia wiki ya sita na baade wiki 2 mbele pandishia matuta.

13. Subiri changamoto ya soko, unaweza kulima na usiuzee kabisa au ukauza kwa bei nusu iliozoeleka au unaweza piga hela ya hatari na kuuga umasikini.


KUHUSU KILIMO BORA CHA VIAZI MVIRINGO
Viazi mviringo au kwa jina jingine viazi ulaya ni jina ambalo hutumika kutofautisha zao hili na zao la viazi vitamu. Zao hili ni muhimu kati ya mazao ya mizizi katika maeneo ya miinuko ya Afrika mashariki.

Katika maeneo ya miinuko zaidi, zao hili huwa na mavuno makubwa zaidi kwa zao la mahindi na hukua kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Viazi mviringo hutumika sana kama zao kuu la chakula hapa nchini na pia husafirishwa katika maeneo ya mbali kama vile Kampala, Mombasa na Dar es salaam.

Hapa Tanzania viazi mviringo kuzalizwa katika maeneo yenye miinuko ya kaskazini kama vile Moshi, Arusha, Lushoto na meneo ya kusini yenye miinuko kama vile Njombe mkoani Iringa na wilaya za mkoa wa Mbeya. Pia maeneo ya Morogoro yenye miinuko hususani Tarafa ya Mgeta yameonekana kuweza kuzalisha zao hili kwa wingi.

II. MMEA WA KIAZI ULIVYO

Kiazi ni mzizi wa mmea unaovimba ukiwa chini ya ardhi na kuwa na vijicho vingi, ambavyo baada ya miezi 2 – 3 vijicho hivi huchipua na kuota shina, kijicho kimoja huweza kutoa zaidi ya shina 1 ambapo hutoa vitawi vingine.

Pingili zilizopo kwenye shina hutoa mizizi inayomea chni ya ardhi na miisho yake huvimba na kuwa kiazi. Viazi nyenye ngozi nyeupe huwa na maua meupe na ile yenye rangi hutoa maua ya rangi aidha pinki, bluu au zambarau.

Katika mzunguko wa ukuaji kiazi huendelea kukua hata baada ya maua kutoka; ili mradi kuwe na na unyevunyevu wa kutosha kwenye udongo na yasiwepo magonjwa.

II. HALI YA HEWA

MVUA :-


Viazi huhitaji mvua za kiasi cha sentimita 25 kwa wiki ambazo hutakiwa kuendela kwa muda wa miezi 3 .5 hii huweza kukuza viazi na kupata mavuno mazuri.

JOTO
Viazi hukua vizuri zaidi kwenye baridi kwa mwinuko wa mita 1,800 kulikoni kwenye joto. Maeneo machache ya mwinuko wa mita 1,500 huweza kukuza viazi, japo pia hukua kwenye mwinuko wa mita 2,900.

UDONGO
Viazi hutoa mavuno mazuri kwenye udongo usiokuwa mzito na unaopitisha maji kwa urahisi. Udongo wenye viini lishe vya kutosha au kuongeza samadi na mbolea za viwandani.

IV. AINA ZA VIAZI
Aina zote za viazi zimeingizwa Afrika Mashariki kutoka Ulaya ambako huzalishwa kwa wingi

i. DUTCH ROBIJN – KUTOKA HOLLAND
– Ndani ni njano
– Inavumilia kidogo ugonjwa wa ukungu
– Hushambuliwa sana na Mnyauko Bakteria
– Hupendwa na walaji wengi

ii. ROSLIN – KUTOKA SCOTLLAND
– Ngozi yake ni nyeupe
– Ndani ni nyeupe
– Huvumulia ugonjwa wa ukungu

iii. KERR’S PINK – NGOZI YAKE NI NYEUPE AU NYEKUNDU
– Ndani ni nyeupe
– Hushambuliwa sana na ukungu na Mnyauko Bakteria

iv. ATZIMBA – KUTOKA MEXICO
– Huvumilia ugonjwa wa ukungu

V. MBEGU ZAKUZALISHA VIAZI
Viazi vyenye umbile dogo hutumika kama mbegu, hutakiwa kuwa na upana wa sentimita 3 – 6. Kiasi cha robo tatu za tani huhitajika kuotesha ekari 1 sawa na tani 1.85 kwa hekta 1.

Mbegu hazitakiwi kuhifadhiwa kwenye giza nene kwani zitaanza kutoa vichipukizi virefu vyeupe.

VI. KUANDAA SHAMBA
Shamba linatakiwa kuandaliwa vituta vidogo vidogo kwa nafasi ya sentimita 75 kutoka tuta hadi tuta, hiihusaidia kuhifadhi udongo na maji na hutoa nafasi nzuri wakati wa upanukaji wa viazi.

Inashauriwa pia kama matuta hayajatumika basi ni muhimu kujaza udongo kwenye shina kwani pingili za chini kwenye shina ni lazima zifunikwe na udongo ili zitoe viazi kwa wingi na hivyo mavuno huongezeka.

VII. KUOTESHA VIAZI
Viazi hutakiwa kuoteshwa mara karibu kabisa na mvua zinapotaka kuanza kuchelewa kuotesha kutapunguza kipindi cha ukuaji wa ile mizizi ili iwe viazi na hivyo kukabiliwa na kipindi cha ukavu.

Uoteshaji hufanyika kwa mikono na mbegu ziwekwe chini udongo kwa kina cha sentimita 10. Kama mbegu zitaoteshwa bila matuta basi zioteshwe kwa kina cha sentimita 15 na kufunikwa na udongo mchache na wakati wa palizi udongo utaongezwa ili kuongeza utoaji wa viazi kwa wingi. Nafasi ya kuotesha ni sentimita 75 toka mstari hadi mstari na sentimita 23 – 30kwa mche hadi mche.

VIII. MBOLEA
Viazi hustawi vizuri zidi kwenye udongo ulioongezwa samadi na ni muhimu chimbiwe katika kina kirefu. Mbolea za viwandani zinazotakiwa ni zile zenye Nitrogeni kwa kiasi cha kilo 22 – 45 kwa ekari; zenye Chokaa P2O5 kwakilo 45 – 65 kwa ekari.

Ni vyema kuongeza mbolea na samadi wakati kuna mategemeo mazuri ya mavuno kwa kuzingatia kuwa mbegu zilizooteshwa hazina magonjwa ya aina yoyote.

IX. PALIZI
Zao la viazi likioteshwa kwa nafasi zilizoshauriwa basi huweza kufunika ardhi yote na hivyo kugandamiza magugu, hii husaidia kwa kipindi cha wiki 6 za mwanzo. Katika mpando wa matuta, basi huwa ni kuondoa magugu na kujaza udongo kwenye mashina.

X. KUVUNA
Uvunaji wa viazi hufanyika kwa kutumia jembe la mkono, viazi vikishang’olewa kutoka chini ya udongo visiachwe kwa muda mrefu kwani vitabadilika rangi na kuwa kijani.

Ili kuifanya ngozi ya viazi kuwa ngumu na isiharibike kirahisi basi mashina yote yanyofolewe wiki 2 – 3 kabla ya kuvuta viazi juu ya udongo. Baada ya viazi kuvunwa haviwezi kuhifadhiwa kwa muda mrefu kwani huanza kuchipua.

Viazi huweza kuhifadhiwa kwenye ardhi, lakini si zaidi ya wiki 6 kwani vitakabiliwa na magonjwa na kushambuliwa na minyoo fundo.

XI. MAVUNO
Mavuno huwa mengi kama utunzaji wa kitaalamu umezingatiwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti magonjwa, kutumia aina zinazostahimili magonjwa. Kiasi cha tani 6 – 8 kwa ekari huvunwa,sawa na tani 15 – 20 kwa hekta.

KUHIFADHI :-
Uhifadhi wa zao hili ni mgumu, hivyo inashauriwa kuwa sehemu iliyotengwa kwa biashara iuzwe mapema, sehemu ya kutumia nyumbani ihifadhiwe katika banda au ghala safi lenye sakafu, lisilo na unyevu, mwanga wala joto- liwe na hewa safi na ya kutosha.

Vinginevyo husababisha viazi kuota haraka. Viazi vilivyowekwa ghalani visilundikwe kwa kina kirefu, visambazwe ili visipate joto.

XII. WADUDU
Vidukari:-

Ni wadudu wadogo wanaoshambulia majani na mashina kwa:
– kufyonza utomvu na kusababisha kunyauka kwa mmea.
– Majani kujikunja kuelekea juu.
– Majani kuwa magumu
– Mimea kudumaa
– Pia hubeba vimelea aina ya virusi ambao huathiri mimea.
– Pia hueneza ugonjwa wa virus.

TIBA:- Wakati wa utunzaji wa mbegu za viazi ni muhimu kupiga dawa ya wadudu ili kuepuka kupuliza shambani kwani dawa nyingi itapotea.

NONDO WA VIAZI :-
Wadudu huathiri viazi vilivyooteshwa wakati ambao sio wa msimu wa viazi. Viwavi wanaoanguliwa huingia ndani ya viazi na kusababisha kuoza. Pia huingia ndani ya viazi wakati vikiwa stoo.

KUZUIA :-
– Otesha viazi katika kina kinachoshauriwa au zaidi ya sentimita 3 kwani kiwavi aingiae ndani ya hawezi kuchimba kina kirefu na inulia matuta wakati viazi vinakuwa, hii husaidia kuzuia nondo kutaga mayai.
– Viazi vyote vilivyochimbwa ni muhimu viwekwe kwenye mifuko na mapema kabla ya alasiri ili kuepuka nondo kutaga mayai.
– Vikihifadhiwa stoo majani ya aina ya LANTANA CAMARA yaweza kutumika.

TIBA :-
Wakati viazi vikiwa stoo, dawa ya unga ya Aldrin hutumika kwenye viazi vya mbegu.

Nyunyizia majani ya viazi wakati mmea ukiwa na mwezi 1 dawa aina ya Dipterex, Diazon, Thiodan, Permethrin, ACtellic au Sumithion.

KAMA NI VIAZI VYA KULA BASI TUMIA PYRETHRUM.

MINYOOFUNDOO :-
Hushambulia viazi vilivyoachwa kwa muda mrefu ardhini na kwenye ardhi iliyoathirika na mmomonyoko.

KUZUIA :-
– Usioteshe mbegu ambazo zimeshambuliwa na wadudu.
– Andaa shamba mapema ili masalia yote ya mazao yaweze kuoza ili kutoruhusu makazi ya minyoo fundo.

MBAWAKAVU :-
Ni wadudu wadogo ambao hutafuna majani na kuacha matundu matundu.

KUZUIA :
Tumia dawa aina ya Malathion, Thiodan

MUHIMU: Pamoja madhara ya wadudu pia hueneza magonjwa mbali mbali ya mimea, hivyo kutunza shamba kuwa safi hasa kupalilia; kuchimba na kutupa mbali maotea pamoja na masalia yote na kubadilisha viazi na vipando kama maharage, mahindi, hupunguza madhara.

Credits: farmersmarket.co.tz
 
I have forgotten much but still remember mbatata za urojo Forodhani. Viazi mviringo hadi Uyole, Mbeya. Wondering if there are GMO varieties suitable for coastal regions.
 
Habari wadau,

Mimi ni mwajiriwa lakini pia mwaka jana niliamua kujaribu kulima kujaribu bahati yangu.

Nililima viazi mviringo (Ulaya) heka tatu kwa majaribio huko mpakani mwa njombe na ludewa.sasa nimepigiwa simu (mi naishi Dar) kuwa viazi vimeshakomaa na viko tayari kuvunwa, lakini tatizo ni bei iko chini kupita matarajio yangu.

kwa kiroba cha debe sita za viazi ni elfu 30.sasa bei hiyo imenikatisha tamaa sana kwa sababu nilitegemea ingekuwa elfu 40 na zaidi,na mpaka sasa sijaenda huko kuvuna kwa sababu hiyo.

Naomba ushauri kama kuna mtu anajua kuhusu hii biashara ya viazi na hasa soko kwa hapa Dar na mambo mengine kwa sababu sijawahi fanya biashara hii kabla.

Natanguliza shukrani zangu za dhati.
 
Ni vema ukaenda shambani kuvuna chagua viazi vizuri visiwe vidogo sana wala makuuuubwa pakia zako kwenye gunia sijui kama mitaa hiyo wanaruhusu lumbesa,shona vizuri tafuta gari lete sokoni MABIBO pale aka mahakama ya ndizi tafuta dalali utauza bei nzuri sijajua juzi na jana leo bei yake ila J3 bei ya gunia ilikuwa kati ya 80000 to 110000.
 
Ni vema ukaenda shambani kuvuna chagua viazi vizuri visiwe vidogo sana wala makuuuubwa pakia zako kwenye gunia sijui kama mitaa hiyo wanaruhusu lumbesa,shona vizuri tafuta gari lete sokoni MABIBO pale aka mahakama ya ndizi tafuta dalali utauza bei nzuri cjajua juzi na jana leo bei yake ila J3 bei ya gunia ilikuwa kati ya 80000 to 110000

Asante kwa ushauri mkuu.
 
Mkuu angalia, kama kiazi chako kimeshatoka, vuna peleka sokono fasta. Kuanzia february mwishoni kiazi toka Makete,Mby na pande za Kipengere kitafurika sokoni, hali hiyo itadumu mpaka May mwishoni, vinginevyo unaweza tunza ikawa mbegu.

Nimekupata kiongozi wacha nifanye fasta. Thanks
 
Ni vema ukaenda shambani kuvuna chagua viazi vizuri visiwe vidogo sana wala makuuuubwa pakia zako kwenye gunia sijui kama mitaa hiyo wanaruhusu lumbesa,shona vizuri tafuta gari lete sokoni MABIBO pale aka mahakama ya ndizi tafuta dalali utauza bei nzuri cjajua juzi na jana leo bei yake ila J3 bei ya gunia ilikuwa kati ya 80000 to 110000

Kaka nimepita MABIBO SOKONI bei imeshuka sana ukilinganisha na bei uliyotaja hapo juu.bei ni shs 60000 mpaka 65000, labda kama utakuwa na Dalali unamfahamu pale sokoni itakuwa poa ukanipa namba yake.
 
kaka nimepita MABIBO SOKONI bei imeshuka sana ukilinganisha na bei uliyotaja hapo juu.bei ni shs 60000 mpaka 65000, labda kama utakuwa na Dalali unamfahamu pale sokoni itakuwa poa ukanipa namba yake.
Hahaha kaka hiyo ndo kawaida ya bei za masoko nadhani itakuwa soko limetapika (mzigo mwingi) coz week ile niliyokuwepo gari zilikuwa kama 15 hv so kulikuwa kweupe kabisa ndo mana ikawa juu, mengineyo nimeku-PM.
 
Kavune uuze hivyo hivyo urudishe pesa yako mimi nililima Makete vimekomaa bei zipo chini sana ni sh 20,000 kwa gunia ninaenda next week nivune halafu nipande ngano itanipa faida zaid. Ukisubir zaid utakuja kuuza elfu 18 gunia better save now!
 
kavune uuze hivyo hivyo urudishe pesa yako mimi nililima makete vimekomaa bei zipo chini sana ni sh 20,000 kwa gunia ninaenda next week nivune halafu nipande ngano itanipa faida zaid. Ukisubir zaid utakuja kuuza elfu 18 gunia better save now!

Makete upande upi mkuu, wa Ikuwo au kule Magoma/Bulongwa/Matamba?

Kuna mchezo unachezwa vizuri sana kule Uwanji, kuna jamaa wa Itaka Mby, huwa wananunua viazi vya Ikuwo Uwanji wanavifanya mbegu ktk kipindi hiki. Sijui hawa jamaa waligundua nini ktk viazi vya kutoka kanda ile kwa kipindi hiki. Bado nafanya utafiti. Walisema hata vya Njombe huwa wanavigeuza mbegu ya kiazi cha kutoa June.

Bado mkulima wa malimbichi anaishi kwa mashaka sana.
 
Habari,

Nina mpango wa kulima viazi mviringo msimu ujao wa mvua, ila sina uzoefu na wala sijawahi kulima naomba kwa yoyote mwenye kujua vya zaidi kuhusu kilimo cha viazi mviringo anijuze. Nataka kulima ekari moja, labda kwa ufupi nijue ntatumia mbegu kiasi gani? Napandaje? navuna baada ya miezi mingapi?

Asanteni kwa kunisaidia.
 
Vizuri sana bila kusahau siku hizi ukitaka kuwa na Mafanikio wekeza katika mahitaji ya kila siku kwa binaadam especialy Chakula.
 
Habari,

Nina mpango wa kulima viazi mviringo msimu ujao wa mvua, ila sina uzoefu na wala sijawahi kulima naomba kwa yoyote mwenye kujua vya zaidi kuhusu kilimo cha viazi mviringo anijuze. Nataka kulima ekari moja, labda kwa ufupi nijue ntatumia mbegu kiasi gani? Napandaje? navuna baada ya miezi mingapi?

Asanteni kwa kunisaidia.
Panda vile vya kwenye mifuko ndo vinatoka vingi kuliko vya shambani.

Vizuri ukaenda Mbeya ukatembelee wakulima wakupe semina hapa naona mabwanashamba huwa hawapiti.
 
Habari,

Nina mpango wa kulima viazi mviringo msimu ujao wa mvua, ila sina uzoefu na wala sijawahi kulima naomba kwa yoyote mwenye kujua vya zaidi kuhusu kilimo cha viazi mviringo anijuze. Nataka kulima ekari moja, labda kwa ufupi nijue ntatumia mbegu kiasi gani? Napandaje? navuna baada ya miezi mingapi?
Asanteni kwa kunisaidia.

Wapi shamba lilipo? Aina ya udongo, n.k
 
Back
Top Bottom