Consultant
JF-Expert Member
- Jun 15, 2008
- 11,401
- 20,661
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema watu wanaomshinikiza Rais Jakaya Kikwete kutoa uamuzi haraka kuhusu watuhumiwa wa escrow, wamepotoka kwa kuwa Bunge lilitoa mapendekezo na siyo shinikizo.
Kauli ya Nape inakuja siku chache baada ya baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa kuhoji ukimya wa Rais Kikwete kuwachukulia hatua mawaziri na viongozi waliotajwa kuchota sehemu ya Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegete Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika mapendekezo yake, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), iliviomba vyombo vya uchunguzi kufuatilia kama viongozi hao wa umma, walifuata matakwa ya sheria na hatua kali zichukuliwe kama itabainika kuwa hawakufuata, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nyadhifa zao za kuchaguliwa au kuteuliwa, kufilisiwa na kufikishwa mahakamani.
Akizungumza jana, Nnauye alisema utafiti alioufanya amebaini kuwa wananchi hawalifuatilii suala la escrow kama linavyoandikwa kwenye vyombo vya habari na kwamba hata kama Rais Kikwete hatawawajibisha wahusika CCM haitatetereka kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
"Rais hafanyi kazi kwa shinikizo la watu, anafuata sheria na Katiba ya nchi. Wanaoshinikiza wamepotoka, Bunge lilishafanya kazi yake, halikushinikiza lilipendekeza wahusika wachukuliwe hatua," alisema Nnauye.
Kiongozi huyo alisema kinachofanyika hivi sasa ni baadhi ya watu kutumia vyombo vya habari kulikuza suala hilo, wakati mfumo mbaya serikalini ndiyo uliowafikisha viongozi hao mahali walipo.
"Mara nyingi waziri amekuwa akiwajibishwa bila kuangalia mfumo uliochangia. Unakuta katibu mkuu anakuwa na nguvu sana kuliko hata waziri, lakini mambo yanapoharibika waziri ndiye anayewajibishwa," alisema.
Aliongeza: "Hata kama tungemleta malaika kutoka mbinguni, kama mfumo hautabadilishwa hataweza kufanikiwa, ndiyo maana chama kimekuwa kikishauri uwajibikaji."
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema kauli zinazotolewa na CCM zinaonyesha kuwa chama hicho kimepoteza udhibiti wa Serikali, kwa kuwa haiwezekani maoni yanayotolewa na chama tawala yakapingwa na viongozi serikalini.
"Hakuna uhalali wa kuendelea kuwa chama tawala kama hawasikilizani. Serikali kutofanya uamuzi ni udhaifu wa chama, lakini Rais anapogoma kuchukua hatua ndiyo uhusika wa Ikulu katika hili unathibitika," alisema Kafulila.
Mbunge huyo ambaye amekuwa kinara wa kulifuatilia sakata hilo, alisema ili ukweli ubainike kwa nini Serikali inasitasita kutekeleza mapendekezo ya Bunge, ipo haja ya kuwekwa hadharani Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyochunguza kuhusu uchotwaji wa fedha za escrow.
"Taarifa za akaunti ya Stabic iliyopo kwenye ripoti ya Takukuru ikiwekwa hadharani nchi itatikisika, ina majina ya wakubwa," alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Amir Manento alisema haki inatakiwa kutendeka bila kuhusisha hisia wala itikadi za uhasama wa kisiasa.
Hata hivyo, Manento alisema kuwajibishwa kwa viongozi hao kutategemea msimamo wa Rais Kikwete kutokana na muundo wa serikali ulivyo.
"Niliwahi kutoa mapendekezo yangu kwenye katiba kwamba, mawaziri wasiweze kuwa sehemu ya Bunge lakini haikuwezekana, hali hiyo inachangia viongozi wa Serikali kutowajibishana," alisema na kuongeza:
"Watuhumiwa ambao ni mawaziri wanakuwa sehemu ya Bunge, halafu wakati huo huo wanashiriki vikao vya mawaziri kwa ajili ya kutolewa uamuzi kupitia kwa mwenyekiti wake ambaye ni rais, na hao hao ndiyo wanaokaa kwenye Kamati Kuu ya CCM."
Akizungumzia suala hilo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), alisema kauli zinazotolewa na CCM ni za kujihami.
"Hao wanatafuta lugha za kujihami kwa sababu wameingia kwenye sakata hilo wanafahamu kwamba linaweza likawaadhiri," alisema Profesa Mpangala.
Aliongeza: "Ndiyo maana hata wakati sakata hilo lilipokuwa linajadiliwa bungeni Katibu Mkuu wa CCM (Abdulrahman Kinana) na mwenzake Nape Nnauye walikuwa Mtwara.
"Walikuwa wanashinikiza kwamba hao wanaohusika na sakata hilo ndiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu na za kisheria kwa sababu hilo suala ni la watu binafsi na wala si la chama."
Aliongeza kuwa, kwa kuwataka wananchi wasiwe na haraka kujua hatua zilizochukuliwa, wanaonyesha dhahiri kuwa wako katika hali ya kujihami kutokana na kwamba dhambi hiyo imetendwa na viongozi wao.
"Wanataka kuonyesha kwamba kashfa haihusiani na CCM jambo ambalo si kweli kwa sababu hiyo ndiyo serikali ya chama tawala, kwa mfumo wetu ni kwamba chama kinachoshinda ndicho kinachounda Serikali na wale wenye kashfa wote ni wana CCM kwa hiyo hawawezi kukwepa hilo. Kwa namna yoyote ile hili lazima litawaadhiri," alisema na kuongeza: "Hiyo inaonyesha dalili kwamba CCM ndiyo chimbuko la kashfa zote za ufisadi na rushwa."
Alibainisha kuwa, kashfa kama hizi zinaibuka wakati wa maandalizi ya uchaguzi kutokana na kwamba fedha zinazochotwa ni kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisisitiza kuwa jambo lolote linalozungumzwa na wabunge ni la wananchi, hivyo kama wawakilishi hao wanataka kujua hatua zitakazochukuliwa na serikali wanahoji kwa niaba ya watu waliowachagua.
"Wabunge si ndiyo wawakilishi wa wananchi na wao si ndiyo wamelivalia njuga suala hilo kwamba lazima wahusika wachukuliwe hatua, sasa hao wananchi wanaosemwa hawana haraka na hao watu kuchukuliwa hatua ni nani?
"Wananchi wenyewe ndiyo sisi, tunashangaa rais tangu arejee kutoka kwenye matibabu amekaa kimya, kwa nini hatekelezi maazimio yale nane ya Bunge?" Alihoji Profesa Mpangala.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema hayo yanayojadiliwa hivi sasa yapo kwenye mfumo uliokumbatiwa na vyama vya siasa.
"Huo mfumo siyo wa CCM tu ni wanasiasa wote… Ukishakumbatia mfumo wa ubepari uchwara mtapata matatizo tu na mtabaki mnajadili matatizo tu.
"Ndiyo maana hata Zitto Kabwe alisema hata kabla hilo yalijamalizika kuna kashfa nyingine nne na ataendelea kufichua kashfa hadi mwisho wa maisha yake ya siasa kwa sababu mfumo wenyewe unazalisha kashfa," alisema Ally.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema, "Hatuna mamlaka na mawaziri, siyo kwamba hatuwawezi ila ni wadogo sana kwetu. Sisi tuna mamlaka na rais na waziri mkuu.
"Kimsingi Bunge kusisitiza hilo ni kwa nia njema…, watafanyaje kazi na Bunge wakati limesema halina imani na wao? Kimsingi aliyetoa wazo ni mshauri tu. Sasa ni suala la uungwana ndilo lililobaki," alisema Filikunjombe.
Chanzo: Gazeti la MWANANCHI
My take: Hivi inawezekana kweli akina Werema, Muhongo na Maswi wakapeta maana Kikwete anaweza asiufuate ushauri wa Bunge? Sasa inaonekana akina NAPE wametumwa kufanya ''utafiti'' na kupima upepo; na sasa wanadiriki kusema kwamba wananchi hawalifuatilii tena suala la Escrow....Upepo umeshapita!