Naona lugha gongana katika ujenzi wa mnara wa Babeli

Aman Ng'oma

JF-Expert Member
Nov 8, 2011
961
533
Nakumbuka siku za nyuma Chama cha Mapinduzi CCM kilielemewa sana na upinzani wakati wa katibu mkuu mzee wetu Yusuph Makamba na baadae Bwana Wilson Mkama. Upinzani ulishika hatamu, kila kona walitawala wao kuanzia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, mitaani, kwenye vijiwe vya kahawa na hadi maofisini. Kila siku hoja nzito zilikuwa zikiibuliwa na upinzani, hoja za kukidhoofisha Chama na Serikali yake hasa kwenye mambo ya ufisadi.

Mabadiliko ya Sekretarieti kutoka ya Yusuph Makamba hadi ya Mheshimiwa Abdurahamani Kinana, kama katibu mkuu wa chama, Philip Mangula, kama makamu mwenyekiti huku Mheshimiwa Nape Nnauye, akiwa kama katibu Mwenezi wa Chama kulileta fikra na mawazo mapya ya kuendesha chama. Nadhani kila mtu anakumbuka kazi iliyofanywa na Sekretarieti hiyo katika kurudisha uhai wa chama. Mheshimiwa Kinana yeye kwa upande wake alizunguka nchi nzima kufufua chama na kuleta matumaini mapya kwa wanachi huku Bwana Nape Nnauye yeye kwa upande wake alikuwa shupavu na shapu kujipu hoja yoyote inayotolewa na upinzani na kuitolea ufafanuzi wa kina. Kwahakika wapinzani walimgwaya ile mbaya bwana Nape Nnauye na mara nyingi walipokuwa wakishindwa kujibu hoja zake waliishia tu kumwita mlopokaji lakini kimsingi kama katibu mwenezi aliweza kusimama katika nafasi yake vizuri na kukiweka chama katika uimara ambao umesaidia hata kukivusha vyema chama hicho katika kipindi cha uchaguzi uliyopita, uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania tangu kuasisiwa kwake mwaka 1992. Katika uchaguzi huo kama kusingelikuwa na Sekretarieti imara naamini leo hii tungelisema mambo mengine juu ya uhai wa Chama cha Mapinduzi.

Lakini leo hii asubuhi nimesikia Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri na katika mabadiliko hayo Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na sheria wakati Dkt. Harrison Mwakyembe amechukua nafasi ya Mheshimiwa Nape Nnauye katika nafasi ya Uwaziri wa Habari, Michezo na Utamaduni. Ni kweli ni uamuzi wa Rais kufanya mabadiliko kadili ya matakwa yake na hakuna wa kumpangia. Na mamlaka haya amepewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Lakini ni muhimu kutambua mchango wa mtu katika chama na nchi. Nape Nnauye ni kijana anayehitaji kufunzwa pale anapokosea kama kijana. Kumwajibisha kama ilivyotokea sioni kama kutasaidia kuimarisha chama na kuleta mustakabari bora wa nchi. Nilidhani kama kuna kutofautiana kidogo ni muhimu zaidi kutumia vikao kumaliza tofauti hizo. Wahenga walisema Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni. Nape Nnauye ni kijana chapakazi haswa asiyekubali kunyamaza pale anapoona kwenye mamlaka yake kuna jambo limetokea. Ni mwepesi kupaza sauti ili kutolea ufafanuzi hasa yale masuala yenye kuzua taharuki.

Kitu ninachokiona kwa sasa katika chama cha Mapinduzi chama kongwe nchini na bara la Afrika kwa ujumla wake ni kama kuna lugha gongana katika ujenzi wa mnara wa Baberi. Na nadhani matokeo ya lugha gongana katika ujenzi wa mnara ule wote tunajua kama ulivyoanishwa katika vitabu vitakatifu. Ni muhimu kama chama kinachoongoza dola kuwa makini katika maamuzi yanayochukuliwa vinginevyo tutakuja kujilaumu wenyewe kwa makosa madogo ya kimkakati tunayoyafanya. Kama mtu atajaribu kutatazama mgongoro huu kwa jicho la tatu, anaweza kubaini dhahiri kuwa kama kuna ugomvi wa kugombea fito katika ujenzi wa nyumba kitu ambacho kama haitachukuliwa hatua za haraka kutatua tatizo, huwenda ikaleta madhara makubwa kwa ustawi wa chama na nchi kwa ujumla wake. Ni muhimu kukumbuka kuwa siku zote majuto ni mjukuu. Na vita vya panzi huwa ni furaha kwa kunguru. Siku zote vyama vikongwa barani afrika hung'oka madarakani kutokana na magomvi ya wao kwa wao kama ambavyo tumeanza kushuhudia yanayotokea katika Chama cha Mapinduzi CCM.

Hivi ndivyo nianavyo mimi.

Aman Ng'oma
Dodoma
0767989713
 
Back
Top Bottom