Nani na nani wenye akaunti za siri nje na kwa nini?

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
rajab.jpg


Barazani kwa Ahmed Rajab

Toleo la 245
27 Jun 2012


MIONGONI mwa marafiki ambao sitoweza kuwatupa ni mwanasheria Enrico Monfrini. Huyu si mwanasheria mahiri tu lakini pia ni mwindaji. Kazi yake ni kuzisaka fedha zilizoibwa hasa na watawala wa kidikteta na zilizowekwa kwenye akaunti za siri nje ya nchi zao.

Nilianza kujuana na Monfrini mwaka 1999 alipoajiriwa na serikali ya Nigeria kuzisaka na kuzifichua fedha ambazo Jenerali Sani Abacha alikuwa amezihaulisha na kuzificha katika mabenki ya nchi za nje. Nilijulishwa naye na rafiki yangu mmoja mkubwa wa huko Nigeria ambaye ndiye aliyekutana na Monfrini usiku wa manane mjini Geneva na kumbembeleza aisaidie Nigeria kuisaka ‘ngawira' ya Abacha.

Abacha aliyefariki dunia mwezi Juni mwaka 1998 alikuwa na sifa mbili kubwa: kwanza, alikuwa mtawala wa mabavu na pili alikuwa mmoja kati ya matajiri wakubwa barani Afrika. Utajiri wake lakini aliupata kwa njia za haramu katika miaka ya 1990 alipokuwa mtawala wa kijeshi wa Nigeria. Abacha alikuwa mwepesi wa kuchota kutoka hazina ya Nigeria na kuwaibia Wanigeria wenzake.
Ingawa watu wakitambua kwamba alikuwa na utajiri huo hakuna aliyekuwa akijua kwa uhakika alikuwa na fedha kiasi gani na aliziweka wapi. Ndipo mara tu baada ya Abacha kufariki serikali ya Nigeria ikamwendea Monfrini aisaidie kuzisaka na kuzirejesha fedha hizo kwenye hazina ya serikali ya Nigeria.

Nimebahatika sana kujuana na kupanga urafiki na Monfrini ambaye sasa ana umri wa miaka 67. Yeye ni mpole, mtaratibu, mcheshi na si mtu mwenye choyo ya kumficha rafikiye kuhusu yale anayoyajua. Huo ukarimu wake ndio ulionivutia kwake na ulinisaidia laisa kiasi nilipokuwa nikiandika makala mbalimbali kuhusu wizi wa Sani Abacha na namna Monfrini alivyoweza kuzisaka dola za Kimarekani zinazokaribia bilioni mbili ambazo Abacha alizificha katika akaunti za nje. Kati ya hizo hadi sasa Monfrini amesaidia zirejeshwe dola bilioni moja na nukta tatu kwenye hazina ya Nigeria.

Monfrini amekuwa pia akizishughulikia akiba za fedha na mali nyingine za ‘Baby Doc' Duvalier, mtawala wa zamani wa Haiti ambaye ameshitakiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wakati alipokuwa akitawala katika miaka ya 1970 na 1980.
Hivi sasa Monfrini ameajiriwa na serikali mpya ya Tunisia kuusaka utajiri wa Rais aliyepinduliwa Zine el-Abidine Ben Ali pamoja na ule wa mkewe Leila Trabelsi na wa jamaa zao. Inakisiwa kwamba thamani ya fedha na mali zao nyingine haipungui mabilioni ya dola za Kimarekani. Hadi sasa Monfrini amefanikiwa kuzipata kasoro ya dola za Kimarekani milioni mia moja. Lakini yungalimo akiendelea na msako wake na anasema kuwa ana hakika ataweza kuzifichua nyingi zaidi.

Shida kubwa anayoipata Monfrini ni kukosa ushirikiano wa kidhati wa mabenki na hata wa baadhi ya serikali za nchi za Magharibi katika kuzitwaa hizo fedha ‘chafu' za mafisadi na kuzirejesha kwenye hazina za nchi zinazohusika.
Ninaijua taabu aliyokuwa akiipata Monfrini alipokuwa akiitaka serikali ya Uingereza imsaidie. Kwa muda wa takriban miaka sita alikuwa akienda London akipiga hodi kwenye ofisi za wakubwa wenye kuhusika akiwataka wamsaidie. Wakimpokea na kumsikiliza kistaarabu lakini mara nyingi akiondokea patupu. Akibahatika alikuwa akipewa taarifa zisizokuwa na faida yoyote na uchunguzi wake. Serikali ya Ufaransa kwa upande wake iliziba mdomo wake na haikumkabidhi hata waraka mmoja wa kumsaidia katika shughuli zake.

Wakati mmoja Monfrini alikwenda Luxembourg akiamini kwamba Abacha alikuwa ameficha huko fedha zipatazo dola milioni 30. Alipoanza kupiga mbizi katika uchunguzi wake aliibuka akigundua kwamba fedha alizokuwa nazo Abacha huko Luxembourg ni zaidi ya hizo dola milioni 30; alikuwa na dola milioni 650. Kati ya hizo dola milioni 400 bado zimebakia Luxembourg.
Monfrini katika uchunguzi wake amegundua kwamba Abacha alikuwa ameficha kama dola milioni 221 kwenye akaunti tatu zilizo katika mabenki ya nchi ya Liechtenstein iliyo Ulaya ya Kati. Kesi ya kutaka fedha hizo zirudishwe Nigeria iliendelea kwa muda wa miaka 12 na hata baada ya mahakama kuamrisha kwamba fedha hizo zirudishwe Nigeria zilikuwa bado ziko kwenye akaunti hizo.

Yote hayo yanaonyesha unafiki wa serikali na taasisi za kifedha za nchi za Magharibi zenye kujidai kwamba zinaupiga vita ufisadi na huku zinawasaidia mafisadi kuyaficha matunda ya ufisadi wao katika mabenki ya nchi hizohizo za Kimagharibi.
Mataifa ya Magharibi yanathubutu kuendelea kuwa pingamizi za kuuzuia ufisadi licha ya yale Mapatano ya Umoja wa Mataifa ya Kupinga Ufisadi (UNCAC) yaliyoanza kutumika mwezi Desemba mwaka 2005. Nchi zilizoyaidhinisha Mapatano hayo na kutia saini zao zinatakiwa ziwe na miundo ya kisheria itayoweza kuutambua na kuuharamisha ufisadi na pia kutoa miongozo ya ushirikiano wa kimataifa utaowezesha fedha zilizoibwa na kuwekwa katika mabenki ya nje zirejeshwe kwao.
Kwa bahati mbaya sheria hizo za kuupinga ufisadi ni dhaifu katika nchi nyingi na udhaifu huo ndio unaowakinga mafisadi waweze kuzihaulisha fedha walizoziiba kwenye mabenki ya nje. Udhaifu huo pia unawawezesha kuzifua na kuzisafisha fedha ‘chafu' kwa kuzitumia kununulia majumba au biashara katika nchi za kigeni.
Ile ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na Benki Kuu ya Switzerland (SNB) na iliyobainisha kwamba wakaazi wa Afrika ya Mashariki wana fedha zipatazo dola bilioni moja na nukta tatu katika akaunti za siri kwenye mabenki ya nchi hiyo haikuwa ya kustaajabisha.

Tulichokuwa hatukijui ni idadi ya fedha hizo na nani wenye kuzimiliki. Na hadi sasa hakuna ajuaye hao wenzetu wamezipataje fedha zote hizo na kwa nini wakaamua kuziweka kwenye akaunti, tena za siri, za mabenki ya ughaibuni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya SNB wenye akaunti hizo kutoka Kenya wamewapiku wenzao wa nchi nyingine za kanda hii. Wao wana jumla ya dola milioni 857; wakifuatiwa na wenzao wa Tanzania wakiwa na dola milioni 178; wa Uganda wana dola milioni 159; wa Rwanda wana dola milioni 29.7 na wa Burundi wana dola milioni 16.7. SNB haikusema kuwa fedha hizo zimepatikana kwa njia za kifisadi lakini hilo ndilo wengi wanalolifikiria. Swali linaloulizwa ni kwa nini watu hao waziweke fedha hizo kwenye akaunti za siri?

Tunajua kwa mujibu wa habari tunazozipata kwamba Watanzania wenye akaunti hizo za siri ni wanasiasa na wafanya biashara. Wanasiasa wanaosemakana kuwa na akaunti hizo ni vigogo katika siasa za Tanzania. Inavyosemekana ni kwamba hao wenye akaunti hizo si walioziweka fedha hizo benki. Na kama si wao basi waliekewa na nani na kwa sababu gani?
Kwa mujibu wa Muungano wa Afrika (AU) kila mwaka nchi za Kiafrika zinapoteza zaidi ya dola bilioni 150, kama asilimia 25 ya Jumla ya Pato lao Taifa, kwa sababu ya rushwa na ufisadi. Kima hicho ni kikubwa mno na athari yake ni kuzifanya bidhaa zinazouzwa barani Afrika zipande bei kwa takriban asilimia 20.
Isitoshe ufisadi huo unawavunja moyo wenye kutaka kuwekeza barani Afrika na hivyo unarejesha nyuma maendeleo na kuwafanya wengi barani humu waselelee na umasikini wao.

Nyingi ya fedha hizo zinazozinyima nchi za Kiafrika fursa ya kuukwepa umasikini zimejikalia katika mabenki ya Switzerland, nchi ambayo kanuni na sheria zake kuhusu shughuli za benki zinawakinga mafisadi na fedha walizozipata kwa njia za haramu.

Kwa ufahamu wangu wanasiasa wengi Wakiafrika wenye kujulikana kwamba wana au walikuwa na akaunti za siri katika mabenki ya Switzerland ni wale watokao nchi zenye kuchimba na kuuza mafuta au maadini.

Ndiyo maana orodha yao ina majina ya Marais José Eduardo Dos Santos wa Angola, Dennis Sassou-Nguesso wa Congo-Brazzaville na Obiang Nguema wa Equatorial Guinea.
Wakuu wa kampuni ya mafuta ya Elf Aquitaine wamekiri kwamba kila mwaka walikuwa wakimuingizia Rais wa zamani wa Gabon Omar Bongo dola milioni 50 kwenye moja ya akaunti zake za siri za benki huko Switzerland. Malipo hayo yalikuwa ni hongo kwa Bongo kwa kuipa kampuni hiyo haki ya kuchimba mafuta nchini Gabon.

Serikali ya Switzerland haikusema lolote kuhusu hayo na inavyoelekea ni kwamba Gabon haitofanikiwa kuzipata fedha hizo ambazo zitaweza kuisaidia nchi kupambana na changamoto za kuleta maendeleo. Huenda ikawa taabu pia kwa serikali ya Gabon kumkashifu Omar Bongo kwa vile serikali hiyo sasa inaendeshwa na Rais Ali Bongo ambaye ni mwanawe.
Inakisiwa kwamba mabenki ya Switzerland yana asilimia 35 ya fedha zote zinazowekwa akiba katika mabenki ya dunia. Hizo ni fedha nyingi sana. Miongoni mwa wenye akaunti hizo ni marais, mawaziri wakuu, wafanya biashara wa halali, majambazi na wauzaji mihadarati. Sheria na kanuni zinazoyaruhusu mabenki ya nchi hiyo yaendeshe shughuli zao kwa kisirisiri zinayatatiza hata mataifa makubwa kama Marekani na Uingereza yenye kujaribu kuzuia fedha zinazopatikana kwa njia zisizo halali au zinazotumiwa kwa mambo yasiyo halali kama vile ugaidi zisingizwe katika mfumo wa mabenki.Wenye kuathirika zaidi kutokana na shughuli hizo za kibenki za Switzerland ni nchi kama zetu zenye kukosa maji safi, shule za kutosha, vifaa vinavyohitajika katika hospitali zetu, barabara zinazopitika, umeme na mbinu za kukuza kilimo. Fedha ambazo pengine zingeweza kusaidia kuzitoa nchi zetu kutoka kwenye majanga hayo zimeibwa na kuhaulishwa kwenye mabenki ya Switzerland.

Serikali ya Tanzania inawajibika kuchukua hatua za kisheria, tena kwa haraka, ili tuweze kujua ni akina nani waliowekewa fedha katika akaunti za siri na kwa sababu gani. Lazima tuwatambuwe watu hao kuwa ni maadui wa nchi na kama upo ushahidi wa hayo basi wachukuliwe hatua kali za kisheria.
 
Yoote yalioandikwa na mwandishi ni sahihi. Ila hapo alipomalizia ndo naona kapotea kabisa. Serikali ya Tanzania chini ya viongozi wabovu(wenye kansa... maneno ya mwalimu) hawawezi kututajia majina ya hao watu. Labda uandike makala ingine ujadili namna gani tunaweza kupata majina ya hao hayawani.
 
Back
Top Bottom