Nani msaliti kwa chama chake, Zitto au Kikwete?

Greenwhich

JF-Expert Member
Nov 6, 2012
1,337
968
GAZETI moja la kila siku nchini, hivi karibuni, katika ukurasa wa mbele, lilibeba taarifa yenye kichwa cha habari: "Zitto afichua siri na JK"... "Ni iliyomfanya JK asifike jimboni Kigoma Kaskazini kumnadi mgombea wa CCM."

Ni taarifa iliyotokana na mahojiano kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na mtandao wa kijamii nchini, Jamii Forum. Yaliyoandikwa na gazeti hilo pamoja na yaliyoandikwa ndani ya mtandao huo wa kijamii, yanatuthibitishia juu ya ukweli wa uvumi uliokuwapo kwamba Rais Jakaya Kikwete na Zitto Kabwe ni maswahiba.

Nampongeza Zitto kwa moyo wake wa kizalendo, kufichulia kitendawili hiki cha muda mrefu juu ya ukaribu wake na Kikwete.

Bila shaka, Watanzania kwa ujumla wao watakuwa wameisikia kauli hiyo ya Zitto juu ya uswahiba wake na Rais Kikwete!

Kuna maswali ya muda mrefu ambayo sisi wapiga kura wa Kigoma Kaskazini tumekuwa tukijiuliza bila majibu. Pale Mwandiga nyumbani kwa Zitto, kwenye ubao wa matangazo wa CHADEMA, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010, Zitto alipenda kuandika kwenye ubao akisema: "Simba hawezi kumla mwanaye, bali ni nguruwe tu awezaye kumla mwanawe."

Sasa tafsiri ya maneno hayo tumeipata. Tumeelewa Simba ni nani, na mwanaye ni yupi. Kabla sijaendelea, tuingie kwanza kwenye tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 na 2010 ambao Zitto alishinda ubunge.

Mwaka 2005 Jakaya Kikwete wa CCM alipata kura zaidi ya asilimia 70 katika jimbo hilo. Katika Jimbo hilo hilo lenye kata 10, CCM ilishinda udiwani katika kata saba, wakati CHADEMA iliambulia viti vitatu.

Lakini pamoja na ushindi huo wa CCM, kwa mgombea urais kushinda kwa zaidi ya asilimia 70, na pia ushindi wa madiwani wa zaidi ya asilimia 70, mbunge aliyechaguliwa kutoka CHADEMA, Zitto Kabwe.

Mgombea ubunge wa CCM mwaka huo, Halimenshi Mayonga, pamoja na chama chake kupata ushindi wa kishindo katika ngazi ya urais na udiwani, alishindwa.

Sisi wapiga kura wa jimbo hili, ambao tulimuunga mkono Mayonga, tukafikiri wapiga kura walimchoka, hawakumpenda. Kumbe Zitto anajua siri ya mtungi, siri ya ushidi wake.

Mwaka 2010, mgombea urais wa CCM (Jakaya Kikwete) alipata kura zaidi ya asilimia 60. Katika uchaguzi huo, jumla ya kata zilikuwa 11. Katika matokeo ya mwisho, CCM ilizoa kata tisa na CHADEMA ikaambulia kata mbili. Lakini katika hali ya kushangaza kama ilivyokuwa mwaka 2005, mgombea ubunge wa CCM, safari hii Robinson Lembo, alishindwa.

Je, wapiga kura wa Kigoma Kaskazini kwa ujumla wao wanampenda Zitto zaidi kuliko CHADEMA? Je, wanaCCM wanampenda Zitto kuliko CCM? Zitto anapendwa kwa lipi hasa? Ametupatia majibu kupitia Jamii Forum kwamba; "kutokana na kazi nzuri anayoifanya kwa taifa hili, kwa mara mbili zote; 2005 na 2010, mgombea urais wa CCM hakuona sababu ya kwenda kumpigia debe mgombea ubunge wa CCM, hatua ambayo ingemaanisha kumpinga Zitto mgombea ubunge wa chama cha upinzani, CHADEMA, lakini ambaye ni swahiba wa Rais, na ambaye wanaheshimiana kama baba na mwanae!

Tutafakari; mwaka 2005 Zitto hakuwa mbunge, huo mchango wake kwa taifa hili aliupata kupitia jukwaa gani ambalo wazazi na ndugu zake wa Kigoma hatukuwa tumebaini isipokuwa Kikwete?

Mwaka 2010, Zitto alipambana na mgombea wa CCM, Robinson Lembo, ambaye alikuwa mtumishi serikalini kwa zaidi ya miaka 30, na kati ya miaka yote hiyo, miaka 25 alikuwa katika ngazi ya juu kabisa ya utumishi wa umma kwa nafasi ya mkurugenzi. Kati ya Zitto na mgombea huyo wa CCM, ni nani alikuwa ameifanyia nchi hii kazi nzuri ya kumpendeza Rais?

Mbali ya Lembo mwaka huo wa 2010, alikuwapo mgombea ubunge kwa tiketi ya CUF, ninayemkumbuka kwa jina moja la Dunia. Huyu anamiliki shule binafsi kadhaa za sekondari nchini zinazotoa mchango mkubwa kielimu kwa vijana. Lakini pia anamiliki Chuo cha Ualimu Mkigo, mkoani Kigoma. Kwa nini huyu mchango wake kwa taifa hili hauonekani, bali wa Zitto tu?

Katika muktadha huu, nasema Zitto asiudanganye umma. Aeleze msingi wa mapenzi yake kwa Kikwete. Zitto asiwafanye wanaCHADEMA, wanaCCM na Watanzania kwa ujumla wao kuwa wajinga.

Wachambuzi makini watajiuliza, je, ni uhusiano gani unaokuwapo kati ya mgombea na chama chake kilichomteua? Je, kiongozi wa chama cha siasa kuwa na uhusiano wa karibu na mgombea wa chama kingine, kunajenga au kubomoa demokrasia? Je, tunapokwenda kwenye uchaguzi, wapigakura waangalie sera za chama au haiba ya mgombea? Je, katika kuendesha kampeni za uchaguzi wagombea wa makundi tofauti, yaani madiwani, wabunge na rais wafanye kampeni ya pamoja kama chama au kila mtu afanye vyake bila kumpigia kampeni mwenzake wa chama chake?

Binafsi naamini ushindi wa mgombea ni ushindi wa chama. Ndiyo maana mgombea urais, udiwani na mwenyekiti wa kitongoji anapitishwa na chama chake.

Kwa hiyo, hakuna namna mtu anaweza kutenganisha uhusiano wa mgombea na chama chake.

Na kwa mtazamo wa CCM, inapofika wakati wa kampeni za uchaguzi, ni chama kwanza mtu baadaye. Kwa hiyo, ni wajibu wa kila mwanaCCM kukipigania chama kwanza na mgombea wa chama chake. Inapotokea tofauti, hakuna lugha sahihi juu ya hilo zaidi ya usaliti kwa chama, na adhabu ya mwanachama huyo imo ndani ya kanuni za uchaguzi.

Kuhusu uhusiano kati ya kiongozi wa chama na mgombea mwingine wa chama pinzani, uhusiano huo hauwezi kuwapo pasipo kukidhuru chama husika. Kiongozi wa CCM kuweka mazingira ya mgombea wa chama pinzani kushinda, maana yake ni kukikosesha chama chake ushindi, na kwa msingi huo anapunguza nguvu ya chama chake bungeni. Huo ni usaliti wa hali ya juu!

Inapotokea kiongozi wa chama tawala kumsaidia ushindi mgombea ubunge wa kambi ya upinzani, basi anamsaidia si kama mbunge wa upinzani, bali kibaraka wa upinzani. Je, tukubali sasa kwamba Zitto ni kibaraka wa CCM na viongozi wa CCM upande wa upinzani? Msingi hapa ni kwamba katika siasa, hakuna msaada wa bure. Kwa msingi huo, siri za chama cha mbunge husika wa upinzani, haziwezi kuwa siri kwa chama tawala.

Kwa mfumo wa siasa tulionao, mgombea wa nafasi yoyote kisiasa lazima atokane na chama cha siasa. Kwa maana nyingine, kinachogombea pale ni chama, na si mtu, maana mtu lazima apate baraka za chama kwanza, na ndiyo maana mgombea hunadi sera za chama chake.

Inapotokea mgombea akanadi haiba, uswahiba, urafiki na mengine yanayofanana na hayo badala ya sera alizotumwa na chama chake wakati kinampa baraka za kugombea, basi hapo malengo na matarajio ya wanachama na wapigakura kwa ujumla yanawekwa rehani.

Katika mantiki ya kawaida, ikitokea kweli urafiki huo upo, lililo jema na afya kwa ustawi wa chama, ni kwa kiongozi huyo kumshawishi swahiba wake huyo ahamie chama chake ili kukipa nguvu. Mifano ya hili iko mingi, Dk. Aman Walid Kaborou alipoanza uswahiba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Makamba alimshawishi Kaborou kutoka CHADEMA na kujiunga CCM.

Hata kwa upande wa vyama vya upinzani, mifano ipo. Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa aliweza kumshawishi mzazi mwenzie, Rose Kamili kuachana na CCM na kujiunga na CHADEMA. Huu ndio uswahiba na urafiki unaoleta afya ndani ya chama.

Kinyume cha hapo ni usaliti tu kama usaliti mwingine bila kujali nafasi ya kiongozi, na kwa maana hiyo, kama kweli maneno ya Zitto ni sahihi, Kikwete ni msaliti namba moja kwa chama chake anachokiongoza, na kwa hili hatutashangaa chama hiki kikimfia mikononi.

Kwa wote waliofuatilia kampeni za uchaguzi wa 2010, wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM zilizofanyika kata ya Mwamgongo, ambako ndiko nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kigoma Vijijini, na ambaye pia alikuwa anagombea udiwani wa kata hiyo ya Mwamgomgo, watakumbuka kwamba nyumbani kwa mgombea huyo na kiongozi wa CCM, kulikuwa kumebandikwa mabango yanayompigia kampeni Zitto Kabwe wa CHADEMA na mgombea wa CUF Omar Nkwarulo maarufu kama Dunia, badala ya mabango ya mgombea ubunge wa CCM na chama chake.

Kama kweli haya aliyoyasema Zitto ndiyo yaliyotokea mwaka 2005 na 2010, ni wazi hata Zitto hakujihangaisha kuwaombea kura wagombea wake wa urais, bali alimpigia debe mgombea wa CCM kutokana na uswahiba wao huo. Mwaka 2005 inawezekana, Zitto hakumuombea kura za urais Freeman Mbowe, na hata 2010 hakufanya hivyo kwa Dk. Slaa, bali kwa swahiba wake, mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Huyo ndiye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, na mgombea urais mtarajiwa wa CHADEMA. Ni muhimu kwa CHADEMA sasa kuzinduka na kuona kwamba jeuri inayomsukuma Zitto kutaka kugombea urais mwaka 2015, inawezekana haitokani na utashi wake, bali makubaliano na uhusiano wa swahiba wake. Swahiba wake huyo, alishaona dalili za kuzama kwa CCM na hivyo, anaona ni heri aondoke akiiacha nchi mikononi mwa swahiba wake kuliko mikononi mwa Dk. Slaa au Mbowe. Bila CCM imara, nchi itayumba! Je, nchi yetu haijayumba bado?


Source: RAIA MWEMA
 
Na wewe ni GT na umepania kabisa hii thread kuiweka hapa?? kwa hiyo wewe unataka kila kitu anachofanya zzk lazima akueleze?? ok, labda tuseme zzk hakuwa ametoa mchango wowote kwa taifa by then, ndio tuseme hakustahili kugombea huo ubunge?? kumbuka kila mja ana nyota / bahati hapa duniani. labda nisaidie, je kuna dhambi ambayo wewe unajua zzk kalifanyia taifa hili?? ni ipi?? kwani mgombea wa CDM kuungwa mkono na wa CCM ni dhambi?? mbona hata CDM waliwahi kumsifia dk Mwakyembe?? binfsi, naona una lako jambo dhidi ya zzk, ila unayo kazi kubwa mbele yako ya kumchafua, maana unaweza ukaambulia frustrations tu na ukamwacha msafi. pole sana. pipooooooooooooz pawaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!
 
wewe ni mpinzani.na ndio mana kwenye makala yako huonyeshi kuwa objective hata kidogo.Huyo unayemsifia lembo katumikia uma miaka 30 na zito miaka 5 mitano tu ameweza kuipaisha kigoma mpaka ww kama ni mtu wa kgm unatembea kifua mbele kwa kusema unatoka kwa zitto.

mnyonge mnyongen hak yake mpeni.kwa ngazi ya mkoa zitto kawafaa sana mselete upinzani wa bei ndogo kama huu.msaidieni pale anapojikwaa asianguke
 
Zitto ni msaliti kibaraka wa kikwete. Hili kundi lote la vijana linalotoa chokochoko liko chini yake. Jamaa amempatia kwelikweli.
 
.... Na chuki zake kwa Dr Slaa hajazianza leo. Kuna kipindi hapa jamvini alikuwa anajiita selemani na alikuwa anaandika mambo mabaya sana juu ya Dr Slaa. Siku moja nikambamba na ki-laptop chake anaandika coments mbaya za Dr Slaa na alishtuka kweli. Alifikiria sijagundua na tangu siku hiyo akaacha kutumia ile ID.
 
.... Na chuki zake kwa Dr Slaa hajazianza leo. Kuna kipindi hapa jamvini alikuwa anajiita selemani na alikuwa anaandika mambo mabaya sana juu ya Dr Slaa. Siku moja nikambamba na ki-laptop chake anaandika coments mbaya za Dr Slaa na alishtuka kweli. Alifikiria sijagundua na tangu siku hiyo akaacha kutumia ile ID.

mh kazi kweli kweli kama ni kweli
 
Zitto ni msaliti kibaraka wa kikwete. Hili kundi lote la vijana linalotoa chokochoko liko chini yake. Jamaa amempatia kwelikweli.

Ukitaka uthibitishe maneno haya, tafuta vijana wanaodowea visenti vyake!.. Kazi yao ni moja kueneza udini, ukanda na kumchafua Slaa!.. Mtafute Eddo Makata mwamalala, Habibu Mchange, na Mtera Mwampamba!. Hakika wakimchafua mtu lazima nao watachafuka tu!.. Hivi ukitaka ugombee urais ni lazima usake vijana wenye njaa wanchafue kiongozi mwenzako?... Leo amejibu kwenye thread ya maandamano ya Bavija page no 6, kuwa asihusishwe na mambo haya, lakini ukweli utabaki pale pale kuwa anatakiwa akemee ujinga huu maramoja.
 
tenende unataka zitto awakeemee vijana wake? utakuwa na matizo ya ubongo wako kwanza elewa kitu kimoja hawawezi kumsema vibaya kiongozi yoyote ya cdm kama mambo hayo hawayazungumzii kwenye vikao vyao..
 
Hata kama ingekua kweli..! Zitto katoa mchango mkubwa sana katika bunge letu..! To me he is still a hero,.

Pia hata baba Mwanaisha akiamua kuwa na Urafiki na Zitto anakua tu because they have alot to share in common..

Hii nchi ni yetu sote.. Uwakilishi wa mbunge jimboni haumanishi kwamba nibweteke kwakuwa kuna mbunge ananiwakilisha tayari.. Huo ni utaratibu tu, KILA RAIA anawajibu wa kuchangia katika hali na mali ili kulikomboa taifa hili.

Mbali na hilo nataka nikwambie mtoa mada kuwa Zitto ni mwanaume wa haja na huwezi jilinganisha nae hata siku moja. Kama huamini maneno yangu 2015 fanya michakato ugombee ubunge hata kupitia tiketi ya CCM then utajua ni kwanini nakwambia Zitto huwezi fanana nae hata iwaje.

Mwisho, tuungane kuhakikisha tunapiga hatua kutoka hapa tulipo bila kujali itikadi zetu.

Africa is for Africans, Our Motherland..
 
Back
Top Bottom