Nani Kairoga Tanzania!? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nani Kairoga Tanzania!?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Nov 15, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 15, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,601
  Likes Received: 82,165
  Trophy Points: 280
  Na Mbasha Asenga
  MwanaHALISI

  ZIPO kauli za mawaziri wengine ukizisikia utaishia tu kusema, hawajui wasemalo. Wiki iliyopita Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, alikuwa akijibu maelezo binafsi bungeni ya Mbunge wa Ngorongoro, Kaika ole Telele, juu wananchi waliochomewa maboma yao huku Loliondo.

  Alisema ni eneo dogo tu ambalo wananchi wameondoshwa kwa nguvu ni ambalo limekodishiwa kwa uwindaji wa kitalii kwa kampuni ya Ortelo.
  Kwamba katika eneo lote la pori tengefu lililoko Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000, ni eneo la takribani kilomita za mraba 1,500 ndiko wananchi waliondoshwa kwa kuwa shughuli za uwindaji wa kitalii zimekabidhiwa kwa kampuni hiyo ya Kiarabu.

  Ukweli wa aliyosema Mwangunga kuhusu madhila waliokumbana nayo wananchi hao, wabunge wengi walionyesha kutoyakukubali, ndiyo maana hoja iliyotolewa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, kwamba ufanywe uchunguzi iliungwa mkono na Bunge.

  Sasa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira itachunguza tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni ya kuhamisha wakazi hao.

  Nia yangu ni kujiuliza na kutafakari kwa mapana juu ya uelewa wa viongozi wetu kuhusu rasilimali tulizojaliwa na muumba. Rasilimali hizi ni kama ardhi, mbuga za wanyama, mapori ya akiba ya wanyama, madini, maji, mito, bahari, misitu na kila kinachoweza kutumika vizuri kubadili maisha yetu kutoka watu dhalili kabisa katika ulimwengu huu uliojaa ushindani wa kiuchumi hadi taifa lililopiga hatua kimaendeleo.

  Mwangunga akitoa majibu ya Telele, pamoja na kutumia muda mrefu kuzunguka huko na huko, alishangaza kwa kiwango kikubwa aliposema kwamba mgogoro unaozungumziwa upo kwenye sehemu ya pori la akiba la Loliondo lenye ukubwa wa km za mraba 4,000.

  Katika eneo hilo , waziri alisema ni km za mraba 1,500 tu ndiyo alipewa kampuni ya uwindaji ya Ortelo. Kwa maelezo yake eneo hilo likilinganishwa na pori lote tengefu la Loliondo, km za mraba 1,500 ni kidogo! Kabla ya kuhoji maswali magumu juu ya kauli ya km za mraba 1,500 ni eneo dogo ni vema kumjulisha waziri Mwangunga yafuatayo; Visiwa vya Zanzibar vina ukubwa wa km za mraba 1,660. Kwa maneno mengine eneo ambalo imepewa kampuni ya Ortelo kufanya kinachoitwa uwindaji wa kitalii ni karibu sawa na ukubwa wa visiwa vya Zanzibar ikiwa na wakazi takribani 900,000. Utalii unaingizia Zanzibar zaidi ya asilimia sita ya pato la taifa.

  Ukiacha Zanzibar kuna visiwa vya Trinadad & Tobago vikiwa na ukubwa wa km za mraba 5,128 yaani inazidi pori tengefu la Loliondo kwa km za mraba 1,128 tu, visiwa hivi vina idadi ya wakazi 1,362,000 lakini uchumi wake ukiwa juu mno. Inakisiwa kwamba pato la mwananchi wa visiwa hivi ni Dola za Marekani 21,700 kwa mwaka. Utalii katika visiwa hivi unafuatia sekta ya mafuta katika uchumi wake.

  Nimetaja visiwa hivyo viwili kwa sababu kinacho zungumzwa zaidi hapo ni utalii, kwamba Ortelo imepewa km za mraba 1,500 za pori kuendesha uwindaji; lakini kwa ukakika ni wanyama wangapi wanawindwa kwa mwaka, na ni kiasi gani wanaingizia taifa, hakuna majibu ya haraka kuhalalisha wananchi wetu kuburuzwa ndani ya nchi yao.

  Hilo la kwanza, lakini la pili ni hili la kudhani kwa kuwa nchi hii ni kubwa ikiwa na takribani km za mraba milioni moja, basi inawezekana kabisa kugawa ardhi ovyo ovyo tu kwa mikataba ya uwindaji na mingineyo kama huu wa Loliondo.

  Waziri alithibitisha kwamba Ortelo kama zilivyo kampuni nyingine za uwindaji wa kitalii, ina kiwanja kidogo cha kutua ndege, lakini hasemi kuna udhibiti gani kwa ndege zinazotua kwenye mbuga hizi?

  Serikali si tu kwamba inaona ni halali kwa Watanzania kuwa raia wa daraja la pili ndani ya nchi yao, bali pia inaonyesha kuhalilisha kosa moja kwa vile kuna wengine wana makosa kama hayo. Nilifikiri kwamba tangu harakati za kukomboa rasilimali za nchi hii zianze hasa kwenye sekta ya madini, basi viongozi wangekuwa wameamka na kuchukua hatua za kukabiliana na mambo kama haya ya Loliondo.

  Tujiulize, hivi Ortelo wanaingizia nchi hii kiasi gani hasa kwa mwaka? Kwa miaka yote hii ambayo wamejichimbia Loliondo wamefanya nini? Je, tunaweza kuelezwa kwamba mchango wao unafanana kwa vyovyote na thamani ya rasilimali wanayobeba kila mwaka chini kivuli cha uwindaji wa kitalii? Mbona Kenya hawana uwindaji wa kitalii na wanapata fedha nyingi kupitia utalii kuliko sisi?

  Kuna tatizo Loliondo na wala si la jana wala juzi, ni la miaka mingi sasa tangu utawala wa awamu ya pili, lakini zote hizi ni tawala chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hiki ni chama ambacho hakiwezi kukwepa lawama za kuasisi ufisadi ndani ya nchi hii.

  Kutokana na viongozi wake kupofushwa na ufisadi hawaoni tena, wanatoa majibu yenye ukakasi kwa umma juu ya mambo yanayohusu maisha na ustawi wa jamii, fikiria kuchomwa kwa maboma ya wananchi, halafu waziri anaeleza kwamba ni halali, nani asiyejua kwamba tangu zama za kale Wamasai wanaishi na wanyama pori?
  Yupi kavamia eneo la mwingine, kampuni ya Ortelo iliyokuja nchini miaka ya 90 au Wamasai ambao vizazi vyao vyote wanaishi pamoja na wanyamapori?

  Kenya wana eneo na wanyamapori dogo zaidi, lakini wananufaika zaidi na wanyama hao kuliko sisi. Tanzania ina ardhi yenye kila aina ya rasilimali, lakini ni kwa jinsi gani kama taifa tumejipanga ili kujineemesha kwa rasilimali hizo. Jibu liko wazi kwamba hakuna!

  Iko shida kubwa katika taifa hili, na shida nyingi zinajitokeza kila kwenye rasilimali za maana; tangu mwaka jana tunalia na Richmond, tumelia na suala la Buzwagi, tumelia na North Mara na tunaendelea kulia nayo; tulilia na ada za vitalu vya uwindaji, bado tupo pale pale; sasa hivi tupo kwenye sakata la umeme, mgawo na nani apewe kazi ya kuwasha mitambo ya kuzalisha nishati ya dharura, IPTL imeibuka tena kwa gharama zetu.

  Mwaka baada ya mwaka, utawala baada ya utawala chini ya chama hicho hicho, kazi ni moja, kashfa juu ya kashfa katika kutumia rasilimali zetu. Ulevi wa fedha au ulevi wa madaraka?

  Julai mwishoni mwaka huu, serikali ilithubutu tena kusoma ripoti ya kuchefua kabisa ya Richmond, safari hii Mwangunga ametuacha na kichefu chefu kingine cha Ortelo. Swali moja, hivi yu wapi waziri mmoja wa serikali hii mwenye upeo wa kutosha kutoa majibu yanayoonyesha walau alifikiri kabla ya kutamka?
   
 2. M

  Magezi JF-Expert Member

  #2
  Nov 15, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  Huwezi kusikia wizara yenye maana kama ya nishati na madini au mali asili anapewa waziri mahiri kama magufuli. Utasikia miwaziri uchwara ndio inapewa wizara zenye maana na zenye raslimali kwa sababu wanantekeleza matakwa ya mafisadi.
   
 3. W

  Wazalendo halis Member

  #3
  Nov 15, 2009
  Joined: Oct 30, 2009
  Messages: 13
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  nimefurahishwa sana na kichwa cha habari ,hii nani kailoga Tanzania,Tanzania haijalogwa ila watu wake wamejiloga wenyewe,Duniani kote 'UMMA' yaani wananchi ni tajiri wa kwanza ,unaweza ukawa billionea lakini kama huna watuutajiri wako ni bure,maana yake ni kuwa wananchi wa Tanzania wanapaswa sasa kuamua wapo kwa kuipeleka nchi.tuna uchaguzi majimboni huko tujue tunamchagua nani kutuwakilisha na kusaidia matatizo yetu yakasikika na kutatuliwa .sio tunamchagua mtu ambaye anakuja kutumia nafasi kulipiza visasi kwa masilahi yake binafsi.tuache kulalamika tumeshafanya makosa tusiyarudie ,tuanze kuelimisha wananchi kuwa kura yake ni muhimu sana kwani ndio inayotuonyesha mustakabali wa nchi hii .hivyo muda wa kuamua ni sasa ,tumeona mengi na tumeshuhudia mengi sasa si muda wa kulalamika tena ni wa kufanya maamuzi
   
 4. P

  PauliMasao JF-Expert Member

  #4
  Nov 15, 2009
  Joined: Nov 26, 2007
  Messages: 286
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Makanisa yalishaanza!
   
 5. m

  mwanamasala JF-Expert Member

  #5
  Nov 15, 2009
  Joined: Jun 20, 2009
  Messages: 248
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Sio kurogwa!Nchi imekuwa inaendesha kiswahili swahili.
  U know what i mean!
   
 6. Mshiiri

  Mshiiri JF-Expert Member

  #6
  Nov 15, 2009
  Joined: Jun 16, 2008
  Messages: 1,893
  Likes Received: 66
  Trophy Points: 145
  Mchonga meno
   
 7. Pape

  Pape JF-Expert Member

  #7
  Nov 15, 2009
  Joined: Dec 11, 2008
  Messages: 5,513
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 0
  hatuja rogwa ila ni 'ujinga na uzembe' wa watu wachache fulani fulani'
   
 8. Chimunguru

  Chimunguru JF-Expert Member

  #8
  Nov 15, 2009
  Joined: May 3, 2009
  Messages: 9,843
  Likes Received: 270
  Trophy Points: 180
  kingunge ngombale mwiru katuloga wadanganyika
   
Loading...