Nani anamlinda saidi mwema na chagonja by lula wa ndali mwananzela | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nani anamlinda saidi mwema na chagonja by lula wa ndali mwananzela

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mukizahp2, Sep 2, 2012.

 1. mukizahp2

  mukizahp2 JF-Expert Member

  #1
  Sep 2, 2012
  Joined: Jul 28, 2012
  Messages: 635
  Likes Received: 94
  Trophy Points: 45
  Nani anawalinda Mwema, Chagonja na kwa nini?

  Lula wa Ndali Mwananzela

  Toleo la 256
  29 Aug 2012
  • Je, ni Kikwete shemeji wa IGP Mwema?
  INGEKUWA kwenye nchi ambayo ina utawala wa sheria na haki za kiraia na zile za kibinadamu hushikiliwa kama tunu, basi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema na Kamanda wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja wangekuwa wameshaondolewa kwenye nyadhifa zao, kutiwa pingu na tayari wanatumikia vifungo virefu jela. Bahati mbaya katika nchi kama ya kwetu utawala wa sheria unawafuata watawala walio juu ya sheria. Ndugu zangu, matukio ya mauaji ya mara kwa mara hasa katika mazingira ya kisasa yanavyozidi kutokea najikuta nafikia hitimisho la kuudhi kuwa uongozi wa Jeshi la Polisi ambao umeshindwa, unalindwa na wanaoulinda wananufaika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za raia na haki za binadamu.
  Kwa mara nyingine taifa letu limeanza wiki hii na habari ya kushtua ya kifo cha kijana mmoja mjini Morogoro ambaye taarifa za awali zimedai kuwa, alikuwa ni muuza magazeti ambaye hakuwa sehemu ya maandamano lakini alijikuta anapatwa na mauti baada ya kupigwa na silaha (haijulikani kama ni risasi au bomu la machozi). Lakini hili limetokea tena katika mazingira ya kisiasa zaidi na kuwa ni sehemu ya mlolongo wa matukio ya aina hii ambayo taifa limeyashuhudia kwa miezi kadhaa sasa kama si miaka. Nitawakumbusha wasahaulifu.
  Mwezi Juni, mwaka jana huko Mara Jeshi la Polisi lilituhumiwa kumuua mwananchi aliyekuwa nyumbani kwake na mkewe kwa kumdhania kuwa ni jambazi. Askari wa Kituo cha Mugumu (Serengeti) walifika nyumbani kwa Nyitamboka Mwita (28), usiku wa manane na kumuamuru atoke ndani. Kilichofuatia baada ya hapo hakijulikani sana lakini moja linalojulikana ni kuwa dakika chache baadaye Mwita alikuwa ameuawa kwa kupigwa risasi ya mgongoni. Hilo lilikuwa tukio la nne la mauaji ya wananchi kufanywa na polisi wa kituo hicho katika kipindi cha muda mfupi tu.
  Mwezi Januari, mwaka 2011 huko Mbarali Mbeya Jeshi la Polisi hilo hilo lilihusika na mauaji ya raia wawili ambao walikuwa ni miongoni mwa wananchi waliokuwa wamesimama kupinga kupita kwa lori lenye uzito mkubwa kwenye eneo lililokatazwa malori mazito kupita.
  Nani atasahau tukio la Februari mwaka huu huko Songea, Jeshi la Polisi lilijikuta kwenye kashfa nyingine ya mauaji ya raia wanne ambao kosa lao lilikuwa kuandamana dhidi ya Mkuu wa Mkoa na dhidi ya uongozi wa polisi wa mkoa. Tukio hili likawafunua viongozi uchwara ambao kwa haraka wakadai ati watafanya uchunguzi na kuahidi kuwa tukio kama “hilo lisitokee tena”. Hata mwaka haujaisha limetokea na siwezi kushangaa linaweza kutokea tena huko Iringa!
  Na hapa hatujagusia kabisa yale mauaji ambapo yamedaiwa kuwa “polisi yaua majambazi” kiasi kwamba tuhuma tu kuwa mtu ni jambazi zinatosha kabisa kupitisha hukumu ya kifo. Na hapa hatujagusa maeneo mengine ambapo watu wamefia mikononi mwa polisi tena wengine wakiwa chini ya ulinzi! Hatujagusa wengine ambao wanapigwa tu wanapokuwa mikononi mwa polisi na kuja kufa baadaye kutokana na majeraha yao.
  Na hapa sijagusa mauaji yale yaliyotokea Arusha au yale ya Mbeya! Tukio hili la Morogoro haliwezi kuwa la mwisho na halitakuwa la mwisho kwa kadiri ya kwamba Said Mwema, Charles Chagonja na uongozi wa juu wa jeshi la polisi bado unabakia ule ule, wenye fikra zile zile za kibabe na ambalo linaamini liko kwa ajili ya kuwalinda watawala wasichukiwe!
  Swali linalonisumbua (naweza kuhisi jibu lake hata hivyo) ni kuwa ni kina nani wanawalinda viongozi hawa wa polisi kiasi kwamba wanaweza kuacha ubovu uendelee kutokea na wao kuendelea kupiga saluti bila kujali matokeo. Imekuwaje – naendelea kujiuliza- jeshi ambalo linajitapa kuwa ni la ‘usalama’ wa raia kugeuzwa kuwa ni jeshi la ‘uhasama na raia”. Hivi ni kweli kina Chagonja na Mwema hawajui kuwa haki ya kuandamana kuipinga serikali au hata kupinga jambo fulani katika hali ya amani ni haki ya msingi kama vile kupiga kura? Ni lini watatambua kuwa wananchi kuandamana katika mkutano wa kisiasa ni jambo zuri na la kawaida? Hivi ni kweli katika upeo wao wa fikra wao na watendaji wao wa chini hawana uwezo wa kutoa ulinzi tu kidogo kuhakikisha kuwa maandamano yanakuwa katika njia zilizokubaliwa na yanakuwa salama? Mbona inaonekana jeshi lina polisi wengi wa kuvunja maandamano kuliko wanaohitajika kulinda maandamano?
  Lazima kuna watu wanawalinda hawa. Upande mmoja naamini ni wakubwa serikalini ambao wanawatumia hawa kama mabosi wa kikoloni walivyotumia jeshi la mkoloni. Matokeo yake maofisa hawa wa polisi hawajioni kuwa wanatumikia wananchi na wanawajibika kwa wananchi bali wanajitahidi kujitafutia ujiko mbele ya wakubwa zao ambao ni wanasiasa. Ni ulinzi huu unazama zaidi hasa tunapokuja kugundua kuwa kumekuwapo na ujamaa au udugu kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi na Rais Kikwete (wanaitana mashemeji). Je, inawezekana ni huu ushemeji ambao unafanya hata kumuuliza Mwema kwa nini inatokea, haiwezekani? Je, inawezekana ni huu ugumu kiasi kwamba hata wabunge wameshindwa kutaka awajibishwe au kuwajibika kwani wanajua watamchongea vipi shemeji ya Rais?
  Lakini pia wengine ambao wanalinda uongozi huu mbovu wa Jeshi la Polisi ni viongozi wenyewe wa upinzani. Hawa kina Mbowe na wengine wamekuwa watumishi wa kwenda kuzika mashabiki na wanachama wao huku wakiahidi “haki ya Mungu” nyingi! Ni lini watatambua kuwa tatizo ni uongozi wa Jeshi la Polisi? Uongozi ambao umejikita katika kukandamiza haki za kiraia ili kuwafurahisha watawala walioshindwa? Ni lini kina Mbowe na wale ambao wanajiona ni viongozi wa upinzani watafunga safari kwenda kwa Said Mwema na Chagonja na kumpa ujumbe usio na utata kuwa hawatovumilia tena Jeshi la Polisi kuua wananchi katika mikutano yao na kuwa ikitokea tena basi hapatakalika? Je, inawezekana ni upole huu wa vitendo ndiyo umewapa nguvu kina Chagonja na walio chini yao? Nani atawafokea?
  Ndugu zangu sisi wenyewe wananchi ndiyo tunawalinda pia kwa sababu licha ya kuwa tunaona wanavyofanya dhidi ya ndugu zetu tunafikiri kuwa haiwezi kututokea sisi wenyewe au jamaa zetu hivyo tunaamua kuwa washirika wa ukimya. Hatutaki kusema.
  Binafsi nasema – na Mungu awe shahidi yangu – Said Mwema na Chagonja wanatakiwa watu wa kwanza kutiwa pingu kwa matumizi mabaya ya madaraka na wanastahili kushtakiwa kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kivita kule The Hague, Uholanzi. Kwani chini yao wananchi wetu wengi wameuawa huku wao wakiendelea kula na kunywa vitamu vya jeshi. Wakitabasamu mbele ya saluti na kucheua mbele ya vimulimuli!
  Ni matumaini yangu kuwa kuna mtu atawaambia hawa kuwa vitendo vyao vinahesabiwa na siku moja watasimama kujibu na kulipa. Kama Gaddafi alianguka na kulipa na Saddam na wauaji wake wote waliondolewa na kulipa hata hawa –na wale wanaowalinda- watakuja kuondoka tu. Na hawatoondoka bila kwanza kulipa gharama ya ubovu wao wa kiuongozi. Tuwaapie mbele ya haki ya Mungu kuwa siku moja watalipa tu vitendo viovu vinavyotokea chini yao na wao wakivitetea.
  Watalipa kwani damu za ndugu zetu zinalia ardhini zikidai haki “mnidaie mnidaie” kama vile damu ya Habili aliyeuawa na yule muuaji wa kwanza Kaini na hazitonyamaza hata kama ni kizazi kingine. Watalipa tu, walahi watalipa. Hata katika mikono ya wajukuu wetu watalipa. Mungu atupe nguvu siku moja tuwalipishe
   
Loading...