Namuunga mkono Spika Ndugai, ujenzi Bandari ya Bagamoyo uendelee

Lord Diplock MR

JF-Expert Member
Mar 16, 2015
1,357
2,000
Najua topic imepita, lakini ninajua kidogo kuhusu mradi wa Bandari ya Bagamoyo na napenda kumuunga mkono Mhe Spika kwa hoja zifuatazo. Na naamini Serikali yetu itazichukulia kama ushauri wa Mbunge kwa Serikali, ambao ndio wajibu wetu wa msingi kama Wabunge.

Muhimu kujua background ya mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Kwanza, mradi huu ulibuniwa na Serikali yetu kama Bagamoyo Special Economic Zone mwaka 2004 chini ya Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Sekta Mpya ya Viwanda. Serikali ya Japan ndio ilitusaidia kwenye hili. Mradi huu uliitwa “Tanzania-Mini Tiger 2020” na ulikuwa chini ya Wizara ya Viwanda.

Mamlaka ya Bandari nayo ilibuni Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania (The Tanzania Port Development Master Plan 2009-2028) ambao ulipendekeza Bandari ya Bagamoyo ijengwe katika miaka ya 2021/2022 ili iwe tayari kujaza nafasi baada ya Bandari ya Dar es Salaam kufikia ukomo wa kuweza kuongezewa uwezo. Kwahiyo mambo mawili ya msingi hapa ni kwamba: (a) Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo tuliubuni sisi wenyewe, ulikuwa sehemu ya mipango yetu ya muda mrefu na haukujengwa kwa msukumo wa Wachina; (b) mradi wa Bandari ya Bagamoyo sio ni mradi wa Bandari, bali ni mradi wa Ukanda wa Kiuchumi ambao unaendana na mji wa viwanda.

Mwaka 2009 Mamlaka ya Bandari, kupitia kampuni ya Hamburg Port Counsulting ya Ujerumani, ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na
kuona una manufaa kutekelezwa. Mwaka 2011, Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia CowiConsult, nayo ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone (BSEZ), kwa kufungamanishwa na Mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

Mipango yote hii ilikuwa ni yetu wenyewe, na tulijiridhisha kama nchi kwamba Bandari ya Bagamoyo tunaihitaji na tukaiweka kwenye Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa kama Mradi wa Taifa wa Kielelezo.

Mwaka 2013 na 2014, Kampuni ya China Merchants Ports Limited, ikiungana na Mamlaka/Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA), waliomba kuwekeza katika Mradi wa BSEZ na Bandari ya Bagamoyo. Baadaye kidogo, Korea Kusini nao, kupitia Taasisi yao ya Science and Technology Policy Institute” (“STEPI”) ilikamilisha Upembuzi Yakinifu wa kuwekeza katika kujenga na kuendeleza “Bagamoyo High Technology Park” kwa kushirikiana na EPZA pamoja na COSTECH. Kwahiyo hoja nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba Bagamoyo sio uwekezaji wa Wachina pekee, kama inavyodhaniwa. Yapo mataifa mengine. Oman wanaweka pesa yao nyingi. Na Korea Kusini nao wanaweka pesa na maarifa yao.

Kama nilivyoeleza hapo awali, kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo (“FYDP II), Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone (BSEZ) ni Mradi wa Taifa wa Kielelezo. Mradi huo unatarajiwa kuwa utavutia uwekezaji wa Dola za Kimarekani bilioni 10; utakuwa na Viwanda 760 na hatimaye kutoa ajira 270,000 kwa awamu ya kwanza. Majadiliano ya Utatu wa Serikali ya Tanzania, China Merchants na Mfuko wa Uwekezaji wa Oman yalikuwa yanaendelea kuelekea makubaliano na hatimaye kuingia Mikataba ya Uwekezaji kabla ya kusimamishwa.

Zipo hoja kubwa tatu zinazosemwa kuhusu mradi huu: (1) utatutwika madeni kama vile Kenya na Sri Lanka ambapo Wachina walilazimika kutaifisha Bandari; (2) tutaua bandari ya Dar es Salaam; (3) haturuhusiwi kuendeleza Bandari yoyote na haturuhusiwi kutia mguu pale Bagamoyo kwa miaka 99.

Hoja hizi zote sio za kweli, na kwa kweli wawekezaji wa huu mradi wamekuwa wana-struggle namna ya kuzijibu kwasababu zinatolewa na watu wakubwa, na hao wawekezaji, hasa wa Oman, ni mamlaka za Serikali na wasingependa malumbano na Serikali yetu.

Hoja ya kwanza, kwamba tutakopa na kujitwika deni kubwa sio ya kweli: kwenye mradi huu hakuna hata senti tano ya mkopo tunachukua. Huu ni uwekezaji. Hakuna deni hapa, ni pesa ya kigeni inaingia kuwekezwa.

Hoja ya pili kwamba tutaua bandari ya Dar haina mantiki, kwasababu hata kabla Wachina hawajafika ilikuwa ni ndoto na mipango ya Mamlaka ya Bandari kujenga Bandari ya Bagamoyo. Ukisoma Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania (The Tanzania Port Development Master Plan 2009-2028), wenyewe Mamlaka ya Bandari walitaka Bandari ya Bagamoyo iwe imejengwa ifikapo mwaka 2023. Bandari za Bagamoyo na Dar sio bandari shindani. Ni bandari zitakazosaidiana kuongeza shehena ya mzigo unaopita nchi mwetu. Full stop! Pia Bandari ya Bagamoyo itajengwa kwa kuzingatia teknolojia ya uundwaji wa meli za kisasa (4th Generation Shipbuilding Technology Port). Meli hizi, ambazo zitakuwa zinaongezeka kadri miaka inavyokwenda, haziwezi kutia nanga kwenye bandari ya Dar. Na kama unaitazama nchi kwa miaka 30, 50 ijayo, Bandari ya Dar ina ukomo wa upanuzi. Lazima kama nchi kujenga Bandari mpya kubwa katika ukanda huu ili kuendelea kunufaika na faida ya kijiografia.

Hoja ya tatu kwamba Wachina wanataka tusijenge wala kuendeleza Bandari yoyote kwa miaka 99 na tuwape wao bandari hiyo bila sisi kutia mguu pale sio ya kweli. Hakuna pahala popote wawekezaji wametoa hayo madai. Ukweli ni kwamba kote duniani mwekezaji anapoweka hela yake mwenyewe kwenye mradi atataka muda wa kutengeneza faida kabla hajakukabidhi mradi. Hapa Wachina na Wa-Oman walitaka miaka 33 ya concession. Je, ni mingi au ni michache? Inategemea pesa iliyowekwa (US$10bn) na standard practice kwingine duniani. Reli ya kuunganisha UK na France, ambayo imejengwa na sekta binafsi ina concession ya miaka 50. Kwa bandari standard practice ni miaka 25-40, kutegemeana na ukubwa wa uwekezaji. Cha msingi kwa timu ya negotiators wetu ni kupata financial models za wawekezaji na kuzichambua na kuona wanaanza kupata faida baada ya muda gani. Na cha kutambua pia ni kwamba concession inahusu tu faida ya Bandari na kwamba katika kipindi hiki cha concession bado TRA itakuwa inakusanya kodi nyingine zote husika za mizito bandarini.

Suala lingine la kutazama katika kufanya maamuzi ni kuangalia dunia inaelekea wapi kwenye biashara ya kimataifa. Tutake tusitake, nchi yetu inategemea biashara ya nje kimapato na China kwasasa ndio kinara wa biashara ya import and exports duniani. Inaongoza kwa kuagiza na kuuza bidhaa nje na itaendelea kuwa kinara kwa miaka 50 inayokuja. Ukifungamana nao, utashinda. Kwa mujibu mpango wa China wa Belt-and-Road-Initiative (BRI), meli kubwa za bidhaa zitakazopita katika 21st Century Maritime Silk Road kusafirisha bidhaa kati ya China na Afrika ya Kati na Kusini, zitafikia katika moja ya Bandari za Mwambao wa Mashariki ya Afrika, kama Mlango na Kituo Kikubwa cha kupokea, kuhifadhi kwa muda na kusafirisha shehena kwa meli au usafiri wa nchi kavu. Kulingana na kudra ya kijiografia ya Tanzania ambayo inaimarishwa na uwepo wa Reli ya Kati (SGR) tunayojenga pamoja na reli ya TAZARA, Bandari ya Bagamoyo ambayo itaunganishwa na Reli ya Kati na TAZARA, itakuwa haina mshindani Nje ya Tanzania katika dhana nzima ya ushirikiano wa maendeleo ya uchumi baina ya China na Afrika, kupitia BRI kwa muktadha wa 21st Century Maritime Silk Road.

Mwisho, ni muhimu kutambua kwamba kuna siasa za ushindani na majirani zetu kwenye hili suala. Jirani zetu Kaskazini yetu wanapigana kufa na kupona mradi huu usitokee. Kwahiyo mtaona disinformation nyingi kuhusu huu mradi huku baadhi ya watu wetu wakitumika bila kujijua.

Wenzetu tayari wameanza tena kuifuata kampuni ya China Merchant kuwashawishi wahamishie ule mradi Kenya kule LAMU. Mwaka 2018 wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kiongozi wao alikwenda Shenzen kuzungumza na China Merchant kuwashawishi waende kwao. China Merchat walikataa na ndio walikutana na Waziri Mkuu Mhe Majaliwa. Na majuzi, tarehe 25 Machi 2021 wameandika barua tena China Merchant kuomba mradi upelekwe kwao (barua nimeiona).

Mwisho, nitamalizia kwa hadithi ndogo: mwaka 1970, wakati Dubai bado ni kamji kadogo jangwani, wazungu waliona potential ya location ya Dubai kibiashara na wakamwendea mfalme wa wakati huo Rashid bin Saeed Al Maktoum kupendekeza wakajenge bandari na waiendeshe kwa miaka 30. Washauri wake wakamwambia tusiwape Wazungu bandari kwenye nchi yetu. Sheikh akawauliza “sisi tuna pesa ya kujenga?”, wakajibu hapana, akawauliza “tutaipata lini”, wakasema hatujui, akawauliza “Dubai itaendelea kuwepo miaka 30 ijayo?”, wakajibu ndio, akawauliza “baada ya miaka 30 wataing’oa bandari na kuondoka nayo?”, wakajibu hapana, akasema “tuwape”. Wazungu wakajenga Port Rashid mwaka 1972. Miaka 30 ikapita haraka. Watu wa Dubai wakajenga uwezo wa kuendesha bandari na wakaanzisha Dubai Port World (DP World), moja ya makampuni makubwa duniani. Dubai sasa ni kinara wa bandari duniani. Majuzi wamechukua bandari za Senegal na Angola. Na wamejenga bandari hadi Rwanda ambapo hakuna hata bahari, wanawasaidia Rwanda kwenye biashara ya logistics.

Mpendwa wetu hayati Rais Magufuli alipenda maendeleo. Alitaka nchi yetu ipate manufaa kwenye miradi na mikataba. Namna ya kumuenzi na kufanya makubaliano yenye tija kwa taifa kwenye mradi wa Bagamoyo. Na hilo linawezekana kama timu yetu ya negotiators itakuwa makini kuzingatia maslahi ya nchi.
 

King Bill

JF-Expert Member
Feb 8, 2021
685
1,000
Asante kwa maelezo mazuri uliyotoa.

Natumaini yatasaidia sana kuwafumbua watanzania ambao hawajui undani na ukubwa wa huu mradi.

Mimi ni miongoni wa wale waliosikitika sana baada ya mradi huu kukataliwa baada ya Hayati Magufuli kupotoshwa na waganga njaa,wanaowaza kizamani.

Kutokana na uelewa wako juu ya mradi huu,ninakuomba uendelee kuwaelewesha watanzania kuhusu ukweli wa mradi huu ili tufanye uamuzi wa kuutekeleza bila kuchelewa. Ni mradi mzuri mno.

Mwisho,miss cha mfalme wa Dubai ni darasa tosha!
 

Sergeant Stonebridge

JF-Expert Member
Oct 8, 2014
233
1,000
Okay Kwa hiyo wewe ni Mbunge?
basi iwapo wewe ni mbunge
ni bahati yako tu kuwa umetumia ID feki
vinginevyo wewe ni mnafiki na usiyekuwa na akili kabisa!

Unawezaje kuandika miuzi mirefu hivi kama magazeti
Kwani ukiwa ndani ya bunge si unayo kinga
Ulishindwa nini kusema haya?

Wewe na huyo mwenzako wanafiki wakubwa mlishindwa nini kuyasema hayo John Pombe akiwa hai?
Mmepewa hela na wachina sasa unaleta ngonjera zenu hapa!
Kwa hiyo nawe ulienda China?
Mnakera sana!
Wachumia tumbo wakubwa nyie!
Mburura mkubwa wewe!
Mamaeee
 

Bugsy

Senior Member
Mar 20, 2021
148
250
Wakuu, msiangalie mtu, nani kasema, watu wanabadirika. Angalieni mawazo, huu sio mradi bali ni uwekezaji mkubwa ambao haijawahi tokea, na unabenefit nyingi kwenye uchumi na jamii. Just think it over
 

King Bill

JF-Expert Member
Feb 8, 2021
685
1,000
Mtoa mada kama si ndugu wa Mh Ndugai basi una manufaa na mradi huo. Strategically Wachina ni wabaya sana kwa nchi za Afrika. Bandari ya Sri Lanka inapata madhila ya kutosoma vizuri mikataba.
Angalia uzito wa hoja. Usikatae hoja kwa kuwa unamchukia Ndugai au wachina.

Wachina ndio wawekezaji wakubwa sasa hivi duniani. Wachina wana mapesa mengi ya kuwekeza,teknolojia na uzoefu.

Hata kwenye mradi wa bomba la mafuta uliosainiwa leo kule Uganda,wachina ni wanahisa wakubwa.

Kwa kuwa kwenye mradi huu wa Bandari ya Bagamoyo,utaratibu unaotumika ni wa kujenga na kuendesha wao hiyo bandari kwa kipindi tutakachokubaliana nao,baada ya hapo wanatukabidhi bandari yetu. Hakuna risk yoyote ya mikopo,kwamba tutashindwa kulipa.
 

exponential

Senior Member
Jul 1, 2017
134
225
Angalia uzito wa hoja. Usikatae hoja kwa kuwa unamchukia Ndugai au wachina.

Wachina ndio wawekezaji wakubwa sasa hivi duniani. Wachina wana mapesa mengi ya kuwekeza,teknolojia na uzoefu.

Hata kwenye mradi wa bomba la mafuta uliosainiwa leo kule Uganda,wachina ni wanahisa wakubwa.

Kwa kuwa kwenye mradi huu wa Bandari ya Bagamoyo,utaratibu unaotumika ni wa kujenga na kuendesha wao hiyo bandari kwa kipindi tutakachokubaliana nao,baada ya hapo wanatukabidhi bandari yetu. Hakuna risk yoyote ya mikopo,kwamba tutashindwa kulipa.
Siungi mkono hoja
 

King Bill

JF-Expert Member
Feb 8, 2021
685
1,000
Okay Kwa hiyo wewe ni Mbunge?
basi iwapo wewe ni mbunge
ni bahati yako tu kuwa umetumia ID feki
vinginevyo wewe ni mnafiki na usiyekuwa na akili kabisa!

Unawezaje kuandika miuzi mirefu hivi kama magazeti
Kwani ukiwa ndani ya bunge si unayo kinga
Ulishindwa nini kusema haya?

Wewe na huyo mwenzako wanafiki wakubwa mlishindwa nini kuyasema hayo John Pombe akiwa hai?
Mmepewa hela na wachina sasa unaleta ngonjera zenu hapa!
Kwa hiyo nawe ulienda China?
Mnakera sana!
Wachumia tumbo wakubwa nyie!
Mburura mkubwa wewe!
Mamaeee
Hoja hujibiwa kwa hoja!

Tuambie ubaya wa huu mradi kwa hoja zenye ushahidi. Kutumia hoja za uongo za Magufuli kukataa mradi siyo sahihi.

Tuelezeni kwa hoja specific siyo kutukana watu tu kwa kisingizio cha uzalendo uchwara!
 

King Bill

JF-Expert Member
Feb 8, 2021
685
1,000
Jamani msipende kudakia vitu hii haitakuwa bandari yetu itakuwa bandari ya China kwa miaka 99 hata kuingia kule ni kwa kibali acheni ujinga
Mlodanganywa mkadanganyika!

Hakuna kitu kama hicho. Magufuli alikuwa fundi wa kutengeneza uongo na propaganda ili kupata anachotaka!

Kuna bandari nyingi tu duniani zimejengwa kwa utaratibu huo
mfano Dubai. Wanachochukua wawekezaji ni port charges tu kwa miaka mtakayokubaliana. Kodi zingine zote serikali inakusanya kama kawaida.

Mbona hata Bandari ya Dar kuna TICTS? Au hamjui?
 

Bugsy

Senior Member
Mar 20, 2021
148
250
Ni ngumu Sana kwa mtu smart kuupuza huu uwekezaji, yaani ni ngumu lazima akili ichemke haswaa kwa yule anaefocus na hoja na sio watu walio toa hoja..
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom