Namna ya kuendesha vikundi vya ujasiriamali na biashara

Kasomi

JF-Expert Member
Sep 3, 2014
11,036
20,337
Maana ya neno kikudi,

Kikundi ni mkusanyiko wa watu kadhaa wenye rika tofauti au linalofanana, jinsia moja au tofauti ambao walioamua kufanya shughuli za kujiingizia kipato kwa mujibu wa sheria, pamoja na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo yao .Leo nitaomba tujadili kuhusu vikundi vya vijana wenye umri kati ya miaka 15-35, hili ni rika ambalo linachangamoto nyingi sana za kimaisha katika jamii yetu

NAMNA YA KUUNDA VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI KWA VIJANA

Hatua ya kwanza
ni lazima mtafute vijana kwanza ambao mnalengo la kuunda kikundi chenu yaani vijana mnaofahamiana kitabia, wenye nidhamu na heshima katika kazi, wenye tabia njema kwa jamii inyowazunguka, vijana msio na tabia ya wizi, ubakaji, ulevi na utumiaji madawa ya kulevya, vijana wenye uthubutu na bidii katika kazi.

Kwa kukosa sifa zinazoendane hapo ndipo vijana wengi huwa tunashindwa na kujikuta baada ya miezi miwili kikundi kimekufa. Ni vizuri tukaanza kwa kutambuana kwanza, sisi wenyewe kuwa ni vijana wa aina gani,tunataka kujiunga kwa sababu gani,je sababu tu ni kelele za viongozi kuwa tujiunge kwenye vikundi?.Eneo hili linahitaji fikra na busara sana, mkishindwa hapa huko mbele hakuna litakalofanyika.

Hatua ya pili
Ni muhimu kikundi kikawa na malengo ya muda mafupi na malengo ya muda mrefu ambayo yamepangwa pamoja na wanakikundi wenyewe siyo mtu mmoja apange kwa niaba ya watu wengine, malengo hayo yaweza kuwa ya miezi mitatu, miezi sita, mwaka na hata miaka mitano kulingana na aina ya shughuli mtakazokuwa mnafanya.

Malengo yakipangwa na wanakikundi wote inakua raisi kutekelezeka kwani kila mtu anaona yeye ni familia ya kikundi kile, lakini mkishindwa kuwa na ushirikiano basi ni vigumu kuyafikia malengo yenu.

Hatua ya tatu
Ni muhimu kutafuta uongozi wa muda kwani hapa ndiyo mahali ambapo uongozi wa muda unatafutwa ili uweze kuratibu na kusimamia shughuli za kuimarisha kikundi, najuwa mpaka kufikia hatua hii kikundi bado kinakuwa kinapitia changamoto nyingi sana wapo watakaoona wanapoteza muda, wapo watakaokua wanajaribu tu kama mtaweza fika mbali n.k

Hatua ya nne
Kuandaa mchakato wa utengenezaji wa katiba ya kikundi, hapa ndipo jina la kikundi hupatikana, malengo na shughuli zitakazofanywa na kikundi hujadiliwa na kwa kina, majukumu ya viongozi watakaochaguliwa yatakua ni yapi, adhabu na mafao ya mwanakikundi, kwa kifupi katiba ndiyo mhimili wa kikundi, ikikosewa hapa ndio dira na muelekeo wa kikundi utakuwa unaenda kombo. Katiba ni lazima ijadiliwe na wanakikundi wote.

Hatua ya tano
Ni kusajili katiba ya kikundi, ni muhimu katiba ikasajiliwe katika halmashauri husika ili kuweza kufanya shughuli kihalali.

NAMNA YA KUENDESHA VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI
i) Kutengeneza katiba iliyobora.Kikundi ni lazima kitengeneze katiba ambayo itatoa muongozo wa namna ya kujiendesha, majukumu ya viongozi na wajumbe wengine wa kikundi. Katiba ya kikundi ni lazima ipendekezwe na wajumbe wengine ili kila kitu kilichomo kwenye katiba kieleweke na kila mjumbe. Sio vizuri na ni mbaya kunakili katiba ya watu wengine na kuifanya iwe yenu kwani vikundi hutofautiana kwa aina ya watu waliopo na shughuli wanazofanya.

ii) Kuwa na uongozi imara.Kikundi ni lazima kiwe na uongozi imara katika kusimamia shughuli mbalimbali za uzalishaji na utawala.Ni muhimu kuchagua viongozi wenye nia na lengo la kufanikisha kikundi kinasonga mbele,usimchague mtu sababu/kiongozi sababu ni ndugu au rafiki yako au mnafahamiana.

iii) Wanakikundi lazima waheshimiane wao wenyewe bila ubaguzi wa aina yoyote ile wa rangi,jinsia,kitikadi,kiuchumi,kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa na mali zingine za kikundi.

iv) Ni lazima maamuzi yanayofanywa ndani ya kikundi yafuate sera,sheria na kanuni zilizowekwa na kupitishwa na wanakikundi wenyewe.Maamuzi yasifanyike kwa kumkandamiza mtu au kikundi cha watu Fulani ndani ya kikundi.

v) Kikundi pia lazima kiwe na mikakati ya kubuni miradi ya uzalishaji mali ambayo ina tija kwa wanachama wake,miradi hiyo yaweza kubuniwa na wanachama wenyewe au kuomba msaada toka kwa wadau wengine wa serikali na mashirika binafsi.Vile vile kikundi lazima kijenge utamaduni wa kuaminiana baina ya viongozi na wanachama wenyewe,kwani hii huongeza mahusiano mazuri baina ya wanachama na kupelekea kikundi kufanikiwa.

vi) Viongozi wa kikundi lazima muwe na utaratibu wa kutafuta taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo ya kikundi,ni muhimu kutafuta taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo ya vijana na stadi mbalimbali za maisha ili muweze kujiendesha kiuchumi na kijamii pia.Kila mwanakikundi awe kiongozi na asiwe kiongozi ni lazima ayaweke maslai ya kikundi mbele kuliko maslai binafsi,ni vibaya kutumia pesa na mali za kikundi kwa kujinufaisha mwenyewe.

vii) Viongozi wa kikundi wanajukumu la kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo mzuri wa majukumu kwa wanakikundi na wafanyakazi walioajiriwa ili shughuli zote za kikundi ziweze kwenda kama zilivyopangwa.

viii) Vilevile wanakikundi wanatakiwa kuwa na mtazamo wa mbali na kuweka mawazo yao katika mpangilio mzuri wa kutekelezeka.

ix) Ni muhimu pia kuwa na vikao vya ndani vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria na katiba ya kikundi. Kutofanya vikao kunaweza kuibua maneno baina ya wanakikundi na kukigawa kikundi.

Tafadhali; Kabla ya kumaliza nitakua mchoyo wa fadhila kama sitozungumza ili,vikundi vingi vya vijana vinavyojishughulisha na ujasiriamali huwa ni vikundi vya mazoea, huundwa kulingana na undugu wa watu Fulani, urafiki Fulani na hivyo kupelekea mambo mengi kufanyika kwa mazoea.

Lakini pia vikundi vingi vya vijana vya ujasiriamali vinaanzishwa kwa lengo kuu la kupata pesa au kuwezeshwa na mtu Fulani, na pale msaada unaposhindikana basi hufa mara moja. Hivyo basi ni vyema vijana tunapoamua kuwa pamoja, tunapoamua kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ni vyema tukaepuka mambo haya, ni bora mkawa wachache wenye lengo la kujikwamua kiuchumi kuliko kuwa wengi ambao hamna faida yoyote.
 
Back
Top Bottom