Namna Hii Kuna Haja Ya Serikali Kubanwa Zaidi Kueleza Aliko Balali,...tujue Zaidi

Augustoons

JF-Expert Member
Oct 31, 2007
409
29
Wakuu nimesoma habari hii ambayo inanifanya nishindwe kuelewa lipi ndio lipi na hasa inafaa kukaa wapi katika forum hii.Lakini hata hivyo nadhani serikali yetu inapaswa kubanwa zaidi kutueleza huyu jamaa aliko,tumrudishe nchini tupate kuondoa utata uliomo.Maanake kutorudi kwake ni kufunika ukweli mwanharamu apite.Na ninachoelewa mimi yamekatwa matawi wakati mizizi na shina bado inachipua sijui ndio tusemaje hapo
Na Francis Godwin, Mufindi

NDUGU wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Daudi Balali, wameeleza kushangazwa na tuhuma anazoelekezewa ndugu yao huyo.

Akizungumza na gazeti hili kijijini alikozaliwa Gavana huyo cha Luganga, Mufindi, mkoani Iringa, mdogo wake, Bw. Paschal Balali (48), alisema wameshangazwa, kwani wanaamini hakuna mtu mwadilifu kama alivyo kaka yao.

Bw. Paschal alisema ni vyema Watanzania wakaamini kuwa kuondoka kwa Dkt. Balali kwenda Marekani kutibiwa, si kwamba alikimbia tuhuma hizo.

Alisema kabla tuhuma hizo hazijaanza kumkabili, Dkt. Balali alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kupooza mkono.

Aliongeza kuwa kutokana na wanavyomfahamu ndugu yao huyo, ni mtu mwadilifu asiyependa kujilimbikizia mali kama walivyo viongozi wengine.

"Pamoja na kuwa katika nafasi nzuri, ndugu yetu hawajaweza kunufaika na nafasi hiyo kutokana na jinsi alivyokuwa na uadilifu wa kulitumikia Taifa," alisema.

Bw. Paschal alisema yeye ni mtoto wa nane katika familia ya marehemu Mzee Balali ila hadi leo tangu ndugu yao huyo apate ugavana hajaitumia nafasi hiyo kunufaisha ndugu zake kutokana na "alivyokuwa mwoga wa kuchukua hata shilingi moja kwa ajili ya kuwapa ndugu zake".

Hata hivyo, alisema mbali na ndugu kwa sasa kuwa katika mawazo mazito kutokana na vyombo vya habari vinavyoendelea kutoa taarifa dhidi ya kaka yao, ndivyo wao wanavyoendelea kujaribu kuwasiliana naye kwa njia ya simu lakini bila mafanikio.

Bw. Paschal alisema awali waliwasiliana na Dkt. Balali, ila kwa sasa mawasiliano yamekatika na hawajui hali yake inaendeleaje.

Pia alisema kutokana na nyumba ambayo alizaliwa Gavana huyo kuwekwa alama ya X kutokana na kuwa jirani na barabara, hivi sasa ndugu zake wako katika jitihada za kutafuta fedha za kuendeleza ukarabati wa nyumba hiyo ambayo ipo katika hali mbaya.

Hivyo alisema kutokana na maisha wanayoishi ndugu, ni vigumu kwa Mtanzania kuamini kuwa hapo ni nyumbani kwa Gavana na kuwa hata hao wanaomtuhumu kwa ubadhirifu ni vyema wakafika kuangalia maisha wanayoishi ncugu hao.


Wakati huo huo, baadhi ya wazee wa kijiji cha Luganga wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa jitihada zake za kushughulikia watu wanaotuhumiwa katika Serikali yake na kumwomba achunguze kwa kina juu ya Dkt. Balali.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalumu kijijini hapo mwishoni mwa wiki iliyopita, wazee hao Bw. Joseph Kadege (49), Bw. Atilio Katefu (55) na aliyekuwa Mwenyetiki wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Bw. Tasili Mdoga (75), walisema pamoja na kwamba lengo la Serikali ni kuwa na viongozi waadilifu wamesikitishwa sana na hatua ya kumhusisha Dkt. Balali na ufisadi.

Walisema kwa upande wao wamemfahamu Dkt. Balali tangu akiwa mdogo na mwenendo wake wanaujua tofauti na watu wanavyozungumzia kuwa ni fisadi, alisema Bw. Katefu.

“Balali ni kijana wetu safi na ni vigumu kumtofautisha na mwanakijiji wa kawaida ... tangu utoto wake alikuwa hapendi magendo ... na hata ukiangalia nyumbani kwake alikozaliwa, huwezi kuamini kuwa alikuwa mtu mkubwa katika Benki Kuu, hivyo ninachotaka kusema Kikwete bado ana kazi nzito ya kuwapata waliochukua fedha hizo ila kwa Dkt. Balali wanamwonea ... ila tunaomba sana Rais Kikwete kama anatusikia afanye uchunguzi wa kina," alisema Bw. Katefu.

Naye Bw. Kadege alisema maisha ya Dkt. Balali ni vigumu kuamini kuwa ni mtu mkubwa katika Serikali ya Tanzania na duniani kwa ujumla, kwani kati ya viongozi wasiopenda kujilimbikizia mali, basi yeye ni mmojawapo.

Bw. Kadege alisema pamoja na kuwa yeye ni mkulima, maisha ambayo anaishi kijijini hapo hayawezi kulinganishwa na ambayo ndugu wa Dkt. Balali wanaishi kijijini hapo.

“Katika wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa, ukisikia mtu anafanya kazi ya kuchuma chai, ni kazi ambayo inakwepwa na wakazi wengi kutokana na kutokuwa na heshima ... ila pamoja na Dkt. Balali kuwa katika nafasi nzuri bado hajaweza kuwa msaada kwa ndugu zake, kwani wadogo zake hadi sasa wanafanya kazi katika mashamba ya chai... tena kazi ya kuchuma chai,” alisema Bw. Kadege.

Alisema pamoja na kuwa ni vigumu kwao kupinga kama Dkt. Balali anahusika au hahusiki wanachoweza kusema kuwa kati ya viongozi walioonesha kupenda utaifa ni pamoja na Dkt. Balali.

Hata hivyo wazee hao walisema iwapo wataitwa watu wa kutoa ushahidi jinsi wanavyomfahamu Dkt. Balali na tuhuma zinazoelekezwa kwake wao watakuwa tayari kufanya hivyo.

Pia walisema wanaamini kuwa Dkt. Balali amebambikizwa tuhuma hizo ila iwapo atajitokeza hadharani huenda wahusika kamili wa fedha hizo watapatikana na kutahadharisha kuwa si vyema kwa viongozi wa juu serikalini kuendelea kumsakama Dkt. Balali, kwani wengi wao wanahusika kwa namna moja au nyingine kuchukua fedha katika benki hiyo.

Bw. Mdoga kwa upande wake, mbali ya kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali iliyopo madarakani katika kupambana na ufisadi, alimpongeza Rais Kikwete kwa kufuata mwenendo wa Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere katika kupambana na dhuluma na kutetea utaifa.

Alisema juhudi za Rais Kikwete zinaonekana, ila watendaji wake wamekuwa wakionesha kumkwamisha kwa kushindwa kuwajibika pale wanapotuhumiwa kwa ufisadi.

Hivyo aliwataka viongozi wanaotuhumiwa, kuiga mfano wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Peter Siyovelwa, ambao waliwahi kujiuzulu baada ya ofisi zao kutuhumiwa kati ya mwaka 1972 na 1973 baada ya sungusungu kutuhumiwa kuua wazee wenye macho mekundu Shinyanga na wao kutuma viongozi wa usalama ambao pia walionesha kutumia nguvu zaidi.

Bw. Mdoga alisema hana uhakika kuwa Dkt. Balali ndiye anayehusika na upotevu huo wa fedha za BoT peke yake, ila alisema ni vyema Dkt. Balali akajitokeza kama hali yake inaendelea vizuri ili aweze kuanika ukweli badala ya hivi sasa ambapo yeye pekee ndiye anaonekana mbaya.

Akielezea jinsi anavyo anamfahamu Dkt. Balali, alisema anavyosikia juu yake ni tofauti na yeye anavyomjua na kuwa bado hamtetei kuwa hahusiki ila anatambua kuwa kati ya watu ambao wamekuwa katika hali ya uaminifu Dkt. Balali pia yumo.

Alisema kwa nafasi aliyokuwa nayo na maisha anayoishi mtu hawezi kumlinganisha na baadhi ya viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wakionesha kujijali wao badala ya jamii.

Aidha, Bw. Mdoga aliwapongeza wapinzani nchini kwa kuanika baadhi ya mambo likiwemo hilo la BoT, ila akasema wanapoendelea kuanika mabaya ya nchi yao, wafanye kwa usiri mkubwa badala ya kuendelea kulipua mambo ambayo yanalidhalilisha Taifa na kuondoa sifa kubwa ambayo iko nje.

Aliwataka Watanzania kuvuta subira hadi Dkt. Balali atakapopona badala ya kuendelea kumtuhumu wakati akiwa mgonjwa, kwani alisema upo uwezekano wa kukosa ukweli wa mambo iwapo Dkt. Balali mwenyewe atashindwa kuonekana.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom