NADHANI KTK MAKALA HII KUTAKUWA NA BAADHI YA MAJIBU YA MASWALI YAKO, NA PENGINE CHANGAMOTO FULANI KWAKO, X-PASTER, NA WENGINE:
Kiswahili kweli lugha ya ajabu!
2008-01-12 09:13:41
Na Moses Ismail
Ilianza kama `kitimbi` fulani hivi, tulikuwa tumekaa maskani Kariakoo, nje ya mlango wa kuingilia kwenye ghorofa moja, tulikuwa watu sita, `wahindi` wawili na `waswahili` wanne. Tulikuwa tunapiga soga la kawaida.
Mara akatokea mzee mmoja wa makamu, muuza matunda, alikuwa na kapu lake lenye maembe, mastafeli, mapera na jamii nyingine ya matunda ambayo kwa kawaida huwa anatembeza na kuwauzia `wahindi`.
Alipofika mahali tulipokuwa tumekaa, kwenye benchi, akamwelekea moja kwa moja mwenzetu mmoja mwenye asili ya kihindi, akasimama mbele yake na kumuuliza; ``mama iko?``
Huyu mwenzetu anayeitwa Hafidhali Datoo, akamwangalia yule mzee kisha kwa sauti ya mshangao akamuuliza; ``nini?`` yule mzee akarudia tena; ``mama iko?``
Hapo inaonyesha Hafidhali akawa ameelewa kile alichoulizwa na mzee yule, lakini kwa namna fulani inaonekana hakupenda swali lile, kwa sauti ya juu na inayoashiria kukerwa akamuuliza yule mzee;
``Mama iko ndio nini?``, mzee wa watu akataharuki, hakuwa na la kusema akabaki ana wayawaya.
Bila kusubiri, Hafidhali akamwambia;
``Uliza \'mama yupo?\', mama iko ndio nini?``, bila ya kutaka maongezi zaidi akamwambia;
``Nenda juu, mama yupo.`` Mzee akaondoka na kapu lake la matunda na kupanda ngazi akielekea ghorofani.
``Kituko` hiki kikazua mjadala nyuma, mmoja wa rafiki tuliokuwa naye pale, Bw. Amir Aziz, akaanza kusema; ``yaani mswahili kafundishwa Kiswahili na mhindi!, kweli maajabu!``
Hafidhali hakukubaliana na hoja ya Bw. Amir, akamwambia; ``tatizo lenu watu wengine mnadhani lugha ni rangi ya mtu, mie nakwambia wewe Amir huniwezi kwa Kiswahili, tukipewa mtihani wa Kiswahili hapa lazima nikuache kwa maksi nyingi.``
Ni kweli, kwa kuwafahamu watu hawa wawili naamini kwamba kama watapewa mtihani, basi Hafidhali atashinda, atashinda kwa sababu mbali ya kuwa na asili ya Kihindi, lakini ni mtu anayeijuwa vizuri lugha ya Kiswahili na anaizungumza kwa ufasaha, amezaliwa na kukulia Zanzibar, na inaonyesha alipata nafasi ya kuishi na `waswahili` wanaojua Kiswahili haswa!
Kutoka hapo akili yangu ikanituma kufanya udadisi, kujua kwamba hivi `mswahili` wa kweli anaweza kupimwa kwa rangi ya ngozi yake au kwa namna anavyozungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha?
Kwa kutaka kufahamu hilo, masikio yangu yakaanza kuwa wazi kwa kila neno ninaloongea na mtu kwa lugha hii, na kwa muda mfupi sana niligundua kuwa watu wengi nilioongea nao Kiswahili hawakuwa wanazungumza Kiswahili bali walikuwa wanazungumza lugha inayosikika na kueleweka masikioni, ni kama Kiswahili lakini si Kiswahili.
Kwa mfano, nilikutana na mdogo wa rafiki yangu, nilijua fika kuwa kaka yake (yani rafiki yangu) amesafiri lakini kwa makusudi nikamuuliza kama kaka yake yupo.
``Hayupo.`` akanijibu.
``Yuko wapi?`` nikamuuliza tena.
``Kaondoka nyumbani,`` akanijibu.
Ingawa nilifahamu, kwamba ile kauli yake ya `kaondoka nyumbani` ilikuwa ina maana ya `amekwenda nyumbani`, lakini niuliza swali jingie kwa makusudi, ``Kaenda wapi?``.
Yule kijana akadhani sikumwelewa, akasema kwa msisitizo; ``kaondoka nyumbani, Iringa.``
Laiti ningeamua kuleta ubishi, tungekesha tukiulizana swali hilo hilo moja, kwa sababu kwa lugha fasaha ya kiswahili yule kijana hakuwa amenijibu ipasavyo, jibu sahihi kwangu lilikuwa `kaka amesafiri, amekwenda nyumbani`, lakini kwa jibu lile la \'kaondoka nyumbani`, ilikuwa kama `dogo` ananipa taarifa kuwa kaka yake ameondoka nyumbani kwao na hajui alipo.
Mgongano za namna hii upo sana mtaani, kuna mifano mingi inayoweza kuelezwa kuleta sura halisi, chukulia mfano huu; unakutana na rafiki yako na unamweleza kuwa siku iliyopita, jana, ulikwenda kwake lakini hukumkuta sasa unataka kujua alikuwa wapi? Jibu linaweza kuwa; \"ah, jana nilikuwepo sipo.``
`Nilikuwepo` ni neno linaloonyesha kuwa msemaji \'alikuwepo\' mahali fulani kwa muda uliopita, `sipo` lina maana ya msemaji anasema `hayupo` mahali fulani kwa muda uliopo sasa mtu anapoyachanganya maneno hayo mawili kuelezea kutokukutwa kwake nyumbani kwa siku iliyopita, jana, inachanganya!
Kiswahili pia huyumba kwa wasemaji kutumia maneno yanayolazimishwa kuishia na `ga` au `je`, kwa mfano, unaweza kumuuliza mtu kama anakula chakula fulani, kwa hofu kwamba isiwe chakula hicho hali na wewe ndio unakusudia kukipika, utasikia anasema; ``ah, makande mie nakulaga sana``.
Katika lugha sahihi ya Kiswahili, neno `kulaga` halipo, kuna neno `kula`, neno sahihi la Kiswahili kwa mtu anayetaka kutumia neno `kulaga`, ni neno hili; `huwa nakula`, sio `nakulaga`.
Maneno yanayowekewa `je` mwisho wake na kuleta lugha nyingine isiyo Kiswahili ni mengi, kwa mfano, unaweza kuwaeleza watu kwamba kwa idadi yao waliyo, haiwezekani kwenda safari moja kwa kupanda farasi mmoja, utasikia mtu anakuuliza; ``sasa twendeje?``.
`Twendeje` sio neno sahihi katika Kiswahili, neno sahihi ni \"twende vipi?``.
Lakini ni nini hasa kilichosababisha hadi `waswahili` kutofahamu lugha yao kwa ufasaha?
Mzee Kasim Said Shaha, yeye anafikiri kuwa ni kwa sababu ya muingiliano wa lugha ya asili ya mtu na lugha hii ya Kiswahili. Anasema:
``Watu wengi wanaoongea Kiswahili huwa wanachanganya lugha hii na lugha zao za asili, hili ni tatizo na hapo ndipo tunapopata maneno kama `nakwendag` au \'nakulaga`, na hili haliwezi kuepukika kwa sababu watu wengi wanaozungumza Kiswahili wanakizungumza kama lugha yao ya pili.``
Hii inawezekana kuwa ni moja ya sababu, lakini inashangaza kuona kwamba sababu kama hii inajitokeza wakati Kiswahili kimekuwa kikitumika kama lugha ya kufundishia mashule, je ina maana kwamba jitihada hizi hazijafanikiwa kuwafanya watu wajue Kiswahili fasaha?
``Hapana,`` anasema Mwalimu Lutha Shelikinga, mwalimu wa shule moja ya Msingi mkoani Tanga, Mwalimu huyo anafafanua:
\"Unajua mara zote lugha inayofundishwa darasani huwa ni lugha ya kitaaluma, ingawa kinachotumika ni Kiswahili, lakini kinakuwa ni kile cha taaluma, kama Jografia itakuwa na maneno yake, Sayansi nayo hivyo hivyo, na lipo somo la Kiswahili kama somo la kawaida.
``Tatizo kwenye somo hili ni kwamba wanafunzi wengi wanasoma ili wakariri, iwe methali au semi wanazisoma kwa lengo hilo tu ili wafaulu, na wengi wanaliacha somo hilo mwalimu anapotoka tu darasani, wakirudi mtaani wanakutana na lugha zao zile zile.``
Kwa mtazamo wake, Mwalimu Shelukinga anaona kuwa lugha hii kama lugha nyingine kongwe duniani lazima itabadilika toka kwenye asili yake na kuingia katika mkondo wa lugha `ya kisasa` kutokana na wazungumzaji wanavyoitumia.
``Sio rahisi leo hii kuona watu wanazungumza lugha ile ya kina Shaaban Robert, na ukizungumza lugha hiyo watu hawatakuelewa, na hapo umuhimu wa mawasiliano hautakuwepo,`` anasema Mwalimu Shelukinga ambaye bado anakubalina na kuwepo kwa haja ya kuilinda lugha asili lakini kwa njia za kukubaliana pia na mabadiliko.
``Nafikiri kama watu watasisitizwa kuelewa kuwa hatuna neno `kwendaga` bali tuna neno \'kwenda\' itakuwa vyema, na kama mkazo utawekwa hapo ili kulinda ufasaha wa lugha, hilo litakuwa jambo jema, lakini maneno mengine ya `kienyeji` lazima nayo yatapata nafasi ya kuingizwa katika lugha,`` anasema.
Hiki ndicho Kiswahili, lugha ambayo kila anayeona anaijua sana hupata wakosoaji na akaambiwa haijui, na wewe msomaji unapomaliza makala hii ningefurahi kama utapitia makosa ya lugha yaliyomo na kunitumia kwa anuani hii;
ismail_moses@operamail.com
·
SOURCE: NIPASHE