Naishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa msamaha wa mwaka mmoja kulipa mapato kwa vijana wanaoanza biashara ili wakue kimtaji

Lucas Mwashambwa

JF-Expert Member
Jul 28, 2022
15,213
9,642
Ndugu zangu mimi kama kijana nakiri kuwa nina uzoefu wa biashara hasa inayohusu mahitaji ya nyumbani kama vile sabuni, mafuta, sukari, chumvi, na mahitaji mengine mengi, kwa kuwa nimewahi kusimamia uuzaji wa bidhaa tajwa katika maduka ya ndugu zangu.

Nakiri kuwa biashara ina changamoto nyingi sana unapokuwa unaanza, mpaka ije isimame vizuri inahitaji umakini mkubwa sana wa kiusimamizi na kimahesabu, maana bila hivyo unaweza kukuta unafunga biashara ndani ya nusu mwaka na kubaki huna kitu mikononi.

Pili kwa biashara za mahitaji ya nyumbani faida yake huwa ni kiasi kidogo sana kwa kila bidhaa inayokuwepo dukani, jambo ambalo mwingine ambaye hajawahi kukaa dukani kufanya biashara akikuta duka limejaa sana anaweza kufikiri unapata faida ya mamilioni, jambo ambalo siyo sahihi.

Kwa kuwa ukweli ni kuwa faida yake ni ndogo na ndiyo maana unakuta mtu anashindwa hata kununua chakula mgahawani kwa kuwa anajua anakula mtaji wake na unakuta hajauza sana kwa siku husika. Ndiyo maana unaona watu wakiletewa vyakula kutoka majumbani mwao ili wasile mitaji yao.

Tatu ni ukweli usiopingika kuwa kwa sasa kuna vijana mitaani waliomaliza vyuo vikuu lakini hawajaajiliwa popote pale licha ya kuwa na vyeti vyao visafi. Hiii yote ni kutokana na kuwa nafasi za ajira ni chache ukilinganisha na uwingi wa wasomi waliopo.

Hapa pongezi za kipekee napenda kumpatia Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa ajira nyingi mara tu alipoingia madarakani kama Rais lakini pia kuimarisha sekta binafsi ili iweze kuchangia katika uzalishaji wa fursa za ajira kwa vijana pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kibiashara.

Hivyo nilikuwa naiomba serikali ya Rais Dkt. Samia kuona uwezekano wa kutusaidia vijana ili katika mwaka ule wa kwanza ambapo kijana anataka kufungua biashara yake, basi aweze kusamehewa kulipa mapato ili kumsaidia kukua kimtaji na kuanza kulipa mapato mwaka unaofuata.

Mwaka huu mmoja utamsaidia kijana kujifunza na kuyazoea mazingira yake ya kibiashara, kuzoeleka na kupata wateja pamoja na kuongeza mtaji wake na bidhaa zake, kwa kuwa biashara mpya ni changamoto kupata wateja haraka haraka hasa kwa kuzingatia kuwa unakuwa mgeni na umewakuta wengine ambao tayari wanafahamika sokoni na walishajijengea majina yao kibiashara.

Jambo hilo litatoa hamasa kwa vijana wengi kufungua biashara zao na kupunguza mzigo kwa serikali katika kuwatafutia ajira, lakini pia litaongeza wigo mkubwa wa walipa kodi wapya na kuchochea uchumi kwa vijana hasa kwa kutambua ukweli kuwa vijana ndiyo wanakuwa wanaanza maisha halisi tofauti na yale ya vitabuni na kwenye vyeti.

Kwa kufanya hivi serikali itakuwa ni sawa na kumlisha vizuri ng'ombe wake kwa kumpa maji safi, pumba, majani mazuri na ndipo umkamue. Hapa ni lazima upate maziwa mengi na yenye samli ya kutosha kwa afya ya mfugaji na familia yake.

Kundi la vijana wasomi na wasiyo wasomi Tanzania ni kubwa sana ambalo linapaswa kutazamwa kwa jicho la kipekee, kwa uangalizi maalumu, kwa msaada wa kipekee, kwa moyo wa huruma, upendo na ukarimu kwake.

Kundi hili linapaswa kubebwa katika mikono ya viongozi wetu muda wote, linapaswa kulindwa na kupiganiwa kwa nguvu zote, linapaswa kupewa kipaombele katika mipango na mikakati ya serikali kibajeti na kisera, linapaswa kusikilizwa na kupewa maneno ya faraja na matumaini wakati wote.

Kundi hili la vijana halipaswi kukatishwa tamaa na yeyote kwa maneno ya aina yoyote kutoka kwa kiongozi yoyote, hili ni kundi linalochemka damu muda wote hata wakati wa baridi damu yake inachemka, hivyo ni lazima lisaidiwe na kupewa fursa za aina zote zinazopatikana hapa nchini, ni lazima mipango yote ya kiuchumi iliguse kundi hili, ni lazima bajeti zote ziliguse kundi hili,Ni lazima huduma zote zilifikie kundi hili.

Maana kundi la vijana ndiyo taifa lenyewe, ndiyo viongozi wenyewe wa leo, baadaye na kesho, hivyo ni lazima waandaliwe vyema, wapikwe vyema katika nyanja zote, wawe na uzoefu na maarifa ya kutosha ili hata siku wakipata uongozi wayajue maisha halisia ya mitaani, wajuwe nini maana ya kujiajiri na changamoto zake, wajuwe nini maana ya kilimo na adha ya kilimo, wajuwe nini maana ya uwekezaji na changamoto zake na wawe tayari kusaidia wenzao kufika walipofika.

Vijana wakiwa na amani taifa zima lazima litamalaki amani na upendo, furaha na mshikamano, umoja na ushirikiano.

Naamini Dkt. Samia na serikali yake wataliangalia suala hili na kuangalia namna ya kusaidia kuwalea na kuwakuza vijana kijasiriamali na kibiashara katika adhima nzima ya kulijenga taifa letu na kuhakikisha kila mtu anaguswa na ukuaji huu wa uchumi wetu.

Mwisho nampongeza tena Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa namna anavyofanya kazi vyema ya kututumikia watanzania na namna anavyotujali vijana wote kwa kutoa fursa mbalimbali za ajira kama ambavyo mpaka sasa ametoa ajira zaidi ya elfu 42 katika sekta zote, zikiongozwa na secta ya elimu na afya.

Lakini pia tumeona namna serikali yake ikitoa mikopo mingi kwa vijana kupitia halmashauri zao pamoja na ujenzi wa miradi mbalimbali Inayochipua ambayo nayo imekuwa ikitoa fursa za ajira kwa vijana.

Kazi iendelee, mama ametufikia na kuwafikia Watanzania kwa utumishi wake uliotukuka wa kugusa maisha ya watanzania wanyonge wasito na sauti.

Lucas Hebel Mwashambwa,,kijana mzalendo na mpenda nchi yangu: 0742-676627.
 
Leo ndio umeandika point sana hasa pragragh za mwanzo ambazo mimi pia naunga mkono hoja,lakini mkuu hizo paragraph za uchawa ndio zimeharibu maana nzima ya ulichoandika.
 
Tunaomba updates Mheshimiwa Rais ametangaza kama ulivyo omba vp kuhusu manispaa na leseni zao za biashara?
 
Tunaomba updates Mheshimiwa Rais ametangaza kama ulivyo omba vp kuhusu manispaa na leseni zao za biashara?
Naishukuru Sana serikali kwa uamuzi wake wa kishujaa na hatua ambayo imeichukua ya kufanya Kama ambavyo nami nilikuwaga Nimeomba kuwa ifikirie Jambo hili
 
Leo ndio umeandika point sana hasa pragragh za mwanzo ambazo mimi pia naunga mkono hoja,lakini mkuu hizo paragraph za uchawa ndio zimeharibu maana nzima ya ulichoandika.
Onbi langu lilishakubaliwa na serikali yetu sikivu ya mh Rais wetu mpendwa mama Samia suluhu Hassani
 
Back
Top Bottom