Naibu Waziri: Msaidieni Rais Samia Utekelezaji Anwani za Makazi

Sep 13, 2016
49
23
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi, Kundo Mathew amewaomba Wakuu wa Mikoa yote nchini kuendelea kutekeleza zoezi la Anwani za Makazi katika mikoa yao ili kukamilisha zoezi hilo ifikapo Mei 22, 2022.

Akizungumza leo mkoani Songwe wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Operesheni Anwani za Makazi inayoendelea kutekelezwa nchini kote ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Februari 8, 2022, ambapo alielekeza utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ufanyike kwa Operesheni na ukamilike ifikapo Mei, 2022 chini ya Uratibu wa Wakuu wa Mikoa.

“Naomba muendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa vile lengo la kukamilisha utekelezaji wa mfumo huu ndani ya muda ulioelekezwa ni kuwezesha Watanzania kupata manufaa yatokanayo na mfumo lakini pia kuwezesha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti, 2022 kufanyika kwa ufanisi. Kwa msingi huo, ni wazi kwamba tunalo jukumu kubwa mbele yetu ambalo lazima tulikamilishe na tutakuwa tumeweka alama kubwa katika historia ya maendeleo ya Taifa letu.” Alisema Naibu Waziri Kundo.

Aidha, aliongeza kuwa kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika ambapo mpaka sasa utekelezaji wa jumla wa Operesheni Anwani za Makazi umefikia wastani wa asilimia 86 kwa nchi nzima, na hivyo kuwapongeza Wakuu wa Mikoa yote nchini.

Vilevile, Naibu Waziri Kundo ameupongeza Mkoa wa Songwe kwa namna alivyotekeleza zoezi la Anwani za Makazi na kushauri mkoa huo kuongeza jitihada ili kukamilisha zoezi hilo ndani ya muda uliopangwa.

“Kwa kuangalia utekelezaji wa jumla unaojumuisha majukumu yote, Mkoa wa Songwe unaonesha kutekeleza kwa asilimia 82.7 kutokana na kutokamilika kwa kazi ya kubandika au kuandika namba za nyumba na kusimika nguzo zenye majina ya barabara. Taarifa inaonesha kuwa vibao vilivyobandikwa ni 15,484 kati ya 254,312. Hali kadhalika nguzo zote zilizosimikwa katika mkoa huu ni 27 tu. Hivyo basi, tujipange vizuri na kuongeza nguvu hapa ili tukamilishe Operesheni kwa ukamilifu” Alisisitiza Naibu Waziri huyo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Omary Mgumba alisema kuwa mkoa wake utahakikisha unakamilisha utekelezaji wa Anwani za Makazi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za Anwani za Makazi.

Mwisho.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom