Nadharia 30 za Ufisadi

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,460
39,928
Nimefungua email yangu na kukutana na email hii. Simfahamu mtunzi ingawa amejitaja kuwa ni "mwanaharakati, anayesomea Uongozi huko Ohio). Ninaiweka hapa neno kwa neno, na tuone kama nadharia zake hizi zina ukweli au zina ukweli kidogo na kama nyingine hazina ukweli wowote ule. Haya wakosoaji wajengaji karibuni! M. M.

NADHARIA THELATHINI KUHUSU UFISADI:
UNAVYOJITENGENEZA, KUJILINDA, NA NAMNA YA KUPAMBANA NAO.

Nadharia hii imeandikwa baada ya kutafakari matukio mbali mbali duniani yaliyotokea katika vipindi mbalimbali vya historia. Nadharia hii inajaribu kuchambua ufisadi pamoja na adhari zake na namna ya kupambana nao. Mwandishi alipoandika nadharia hii hakusoma kitabu au kazi ya mtu yeyote; wala hakuandika kwa mtiririko maalumu; bali alijaribu kutafakari na kuyaandika mawazo yake kama yalivyojitokeza ili kuchokoza mjadala, utafiti, au mchango zaidi kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wasomi, wataalamu wa sayansi ya jamii, na wahanga wa ufisadi. Lakini pamoja na kwamba nadharia hii ni ya awali, naamini inaweza kuwasaidia wana jamii kuufahamu kidogo ufisadi ulivyo na kufikiria namna ya kujipanga kupambana nao. Kwa watafiti na wasomi, itakuwa ni nafasi nzuri ya kuchambua zaidi, kutafiti na kuelimisha jamii zaidi juu ya adui huyu mkubwa wa mwanadamu.

1. Ufisadi ni aina fulani ya tabia inayojitengeneza ndani ya moyo wa mtu mwenye asili ya uchoyo na ubinafsi.
2. Ufisadi huanza kidogo kidogo katika maisha ya watu, hasa wale wanaopenda daima kuweka maslahi yao binafsi mbele zaidi kuliko ya wengine.
3. Kama haupigwi vita mapema katika jamii, ufisadi unakua na kujieneneza; na kasi ya kukua kwake inaongezeka kama kuna watu wanaoshabikia ‘mafanikio’ yanayotokana na ufisadi huo.
4. Ufisadi ulioachiliwa (ama kwa sababu ya hofu, kuoneana aibu, au vinginevyo) hujiimarisha kwa kujitengenezea mtandao wake mwenyewe.
5. Mtandao wa ufisadi usipovunjwa mapema hukomaa na kutengeneza tabaka la mafisadi katika jamii, ambao hutafuta namna ya kuhalalisha ‘matunda’ ya ufisadi wao.
6. Mojawapo ya njia inayotumika kuhalalisha matunda ya ufisadi ni kusaidia katika jamii, kutoa michango katika jamii au vyama, kuwekeza katika biashara, kusaidia wanasiasa kushinda uchaguzi, au kuingia serikalini; na ikibidi husaidia mafisadi wenzao kuingia kwenye siasa au shughuli nyingine muhimu.
7. Wakati wote, tabaka la mafisadi huteteana kwa siri, lakini wakishajiona wamekomaa hukosa aibu hivyo huteteana kwa wazi. Na kwa hiyo fisadi mmoja hawezi kumwadhibu fisadi mwingine isipokuwa wamekosana katika mambo au maslahi yao
8. Ufisadi uliojitengenezea tabaka huwa ni ngome ngumu kuivunja, kwani unatafuta mbinu zote kujilinda, kujitanua, na kujihalalisha.
9. Ufisadi uliokomaa hauna huruma, aibu, wala staha. Na unakuwa mkali kwa wale wanaojaribu kuupiga vita.
10. Mbinu kubwa ya ufisadi ni kusema uongo, kutumia vitisho, au kutumia nguvu yoyote ilioyokaribu nao (ya kipesa, kicheo, kichawi, kisilaha, kisiasa, kijeshi, kikabila, n.k.).
11. Mbinu ya uongo ikishindwa, vitisho vinatumiwa, vitisho vikishindwa nguvu hutumika kutetea maslahi yao.
12. Ufisadi ukipigiwa sana kelele na wananchi, unajipaka chokaa nyeupe kwa nje na kujifanya unaongoka, na hivyo kuwahadaa wananchi; kwa namna hiyo ufisadi hautenganishwi na unafiki.
13. Unafiki wa mafisadi una mbinu tatu. Mbinu ya kwanza ni ya kujisafisha kwa juu juu pasipo toba la kweli. Hilo lisiposaidia, mbinu ya pili hutumika ambayo ni kuwachafua watu wengine waliosafi ili kuiaminisha jamii kuwa kila mmoja ni fisadi hivyo wasifuatwefuatwe. Hilo lisipofaa, mbinu ya nyingine hutumika ambayo ni ya kuwachafua baadhi ya mafisadi wenzao wachache, na hasa waliobainika, ili watolewe kafara na wengine wapate kupona. Mbinu zote zikishindikana, mafisadi wanaweza kudhuru watu ili kujitetea.
14. Mtandao wa ufisadi unaweza ukawa wa sehemu moja kijiografia; au ukasambaa nchi nzima, na hata kuchukua sura ya kimataifa. Na unapovuka mipaka kuingia nchi nyingine, unatumia hila ya kuhadaa na kuwalainisha watu mashuhuri wa nchi au sehemu husika.
15. Kama jamii ya wapenda HAKI na KWELI isipojizatiti na kupambana na ufisadi, na ukiachiwa utawale jamii kama unavyopenda, matokeo katika jamii yanakuwa ni mabaya sana. Jamii inakuwa mtumwa wa ufisadi, na mafisadi wanakuwa kama wafalme wa kudumu.
16. Ufisadi unajidhihirisha katika sura mbalimbali kama vile rushwa kubwa na ndogo, ukandamizaji wa wanyonge, unyonyaji, kikundi kimoja kunyanyasa kingine, ubabe wa kiuchumi au kisiasa, biashara haramu (kama vile ya utumwa, madawa ya kulevya, bidhaa feki, biashara ya magendo, n.k.), uporaji wa mali na haki za wengine, demokrasia bandia, utawala mbovu, udikiteta, ajira mbaya kama vile ya watoto, n.k.
17. Baadhi ya matokeo mabaya ya ufisadi ni kuongezeka unyonge na umasikini; kuporomoka maadili; chuki za kitabaka, kisiasa, kikabila, au kivikundi; vita vya wenyewe kwa wenyewe; mauaji ya kikabila, kikoo, au kisiasa; kukosa kuaminiana katika jamii, ukoloni wa sura mbali mbali, maisha ya wasiwasi, n.k.
18. Kwa mantiki hiyo, ufisadi sio kitu cha kuchekea kabisa (hata kama unafanywa na ndugu wa kuzaliwa). Ni janga, aibu, na hatari kwa jamii au nchi yeyote ile. Pia ni ugonjwa mbaya unaoua kabisa maadili ya jamii, kwa maana vizazi vipya vinakosa mifano mizuri ya kuiga; pia vinakosa maongozi sahihi, licha ya kukosa haki zao za msingi na msaada wa kweli.
19. Lakini jamii pia lazima ifahamu kuwa ufisadi uliokomaa hauwezi kujiondoa wenyewe, maana unajikita kama ufalme mdogo ndani ya jamii. Ili kupambana nao, umoja wa wananchi, nguvu, busara, na maarifa yanahitajika.
20. Ufisadi hauwezi kupigwa vita na mafisadi, bali utapigwa vita na watu walio safi, wapenda maendeleo, haki, na kweli. Mwenye madoa ya kifisadi akipigana na mafisadi ataumbuliwa; ndio maana si rahisi kwa asiyesafi kupambana na mafisadi.
21. Vita ya kupambana na ufisadi inatoka ndani ya moyo wa dhati wa mpenda haki, amani, na maendeleo ya watu; inahitaji uvumilivu, ni vita ya muda wote, haitafuti mafanikio binafsi.
22. Vita ya kupambana na ufisadi inahitaji viongozi safi, wenye maono safi, wenye uadilifu, wanaoweze kuelezea umma malengo yao na kuhamasisha haki na kweli, na wanaoonyesha mfano wa kweli kupitia maisha yao wenyewe.
23. Vita ya kupambana na ufisadi sio lele mama, ina hitaji kujitolea kwa hali ya juu. Lakini matunda yake ni mazuri, yanaleta faraja kwenye jamii, na yanadumu kwa muda mrefu.
24. Kila mwana jamii aukemee ufisadi wakati wote na mahali popote anapouona, pasipo kujali kama ungemletea yeye faida fulani.
25. Viongozi wa taasisi zote za jamii, serikali, kidini, na kitaaluma wapige vita ufisadi wa namna zote, na wahamasishe watu wao kuupiga vita ufisadi. Wanapofanya hivyo wajisafishe kwanza ili wawe mfano kwa wananchi wao wenyewe.
26. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa kusaidia wananchi katika vita hii, kwa kuendelea kufichua vitendo vya ufisadi, kuandika taarifa kwa busara, na kuhamasisha haki, kweli, na uadilifu katika jamii.
27. Inawezekana kupambana na kuushinda ufisadi, unyonge, na umasikini kama wanajamii wakimaanisha na wakikusudia kujiletea maendeleo ya haki na kweli.
28. Ikumbukwe kuwa ufisadi hauwezi kujiondoa wenyewe; wala malalamiko tu na kusimanga mafisadi haviwezi kuuondoa ufisadi. Wala ushabiki tu wa juu juu hauwezi kuuondoa ufisadi. Kinachohitajika ni juhudi na nguvu za dhati na za pamoja kati ya wananchi na viongozi wao, pamoja na taasisi za dini na zile zinazotetea haki za watu.
29. Kwa kuwa ufisadi unatumia mwanya wowote na hasa udhaifu fulani katika jamii, ni vema kuhakikisha kuwa maeneo yote ya kijamii yanaboreshwa (kama vile sheria za nchi na serikali za mitaa, kanuni na taratibu za taasisi, utendaji wa vyombo vya kusimamia haki na sheria, utawala bora, utendaji wa vyombo vya habari, demokrasia na ushirikishwaji umma, maadili ya viongozi, n.k.)
30. Ili kusaidia vizazi vijavyo, elimu na itolewe kuanzia ngazi ya shule za msingi. Elimu hiyo ilenge kuwasaidia vijana kuwa waadilifu, kuuchukia na kupambana na ufisadi. Kama vile tunavyopambana kulinda mazingira yetu, ni lazima kupambana pia kulinda jamii zetu na utu wetu. Mazingira ni muhimu, lakini ni kweli pia kuwa utu wetu ni muhimu zaidi. Maana utu wetu ukiharibiwa, na jamii ikiharibiwa na ufisadi, je mazingira hayo yatamsaidia nani?

Imeandikwa na mtanzania - mkereketwa wa haki na kweli, mwanafunzi wa uongozi, Ohio, Marekani.
 
Maneno mazito haya, nampongeza ndugu huyu kwa kukaa chini na kuumiza kichwa kuangalia sababu za ufisadi na pia kutoa mbinu za kupambana nao, hii ni dalili nzuri kwamba kuna Watanzania wanaojua Matatizo yetu na sasa kwa kutumia nafasi/uwezo walionao wanaiamsha jamii

nampa tano mwanaharakati huyu
 
Hii nadharia safi sana, unaonaje MKJJ umuombe ruhusa ili uipeleke kwenye magazeti ya TZ, kama raiamwema au Tanzania Daima.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom