damnz
Member
- Feb 25, 2016
- 15
- 95
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), limetangaza ufunguzi rasmi wa Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System (CAS)) kwa mafunzo yanayoratibiwa na Baraza kwa mwaka wa masomo wa 2016/17. Mfumu huo, utatumika kuratibu maombi ya kujiunga na mafunzo ya Astashahada (Cheti), Stashahada (Diploma) na Shahada ya kwanza (“Bachelor Degree”).
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maelekezo na Msaada kwa Taasisi wa NACTE, Dk. Adolf Rutayuga amesema kuwa, kwa mwaka wa masomo wa 2015/16, Baraza liliratibu udahili wa wanafunzi katika vyuo mbali mbali kwa kozi za astashahada (Cheti) na stashahada (Diploma) kwa mafunzo ya afya na ualimu yaliyoidhinishwa na Baraza. ameongeza kuwa, Baraza pia lilishirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, kuratibu udahili wa wanafunzi katika vyuo mbali mbali kwa kozi za shahada ya kwanza kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System (CAS)).
“Mifumo hii miwili ilifanyika kwa ufanisi mkubwa na uliwawezesha waombaji kudahiliwa. Mifumo hii ya udahili imekuwa na mafanikio yafuatayo: Kudhibiti udanganyifu katika udahili uliotokana na baadhi ya waombaji kutumia vyeti vya bandia, kuwapunguzia waombaji gharama za kuomba udahili katika vyuo mbalimbali, kuondoa uwezekano wa mwombaji udahili mmoja kudahiliwa zaidi ya mara moja na kuwanyima waombaji wengine nafasi, kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za waombaji udahili kwa ajili ya kufanikisha mipango ya elimu nchini, na kuwawezesha waombaji udahili kujiunga na mafunzo kwenye taasisi zinazotambuliwa na Serikali,” alieleza.
Dk Rutayuga alieleza kuwa, kwa kutambua mafanikio ya udahili wa pamoja yaliyopatikana, Serikali ya kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, imeamua kuwa maombi yote ya udahili kwa ajili ya mafunzo ya Astashahada (Cheti), Stashahada (Diploma) na Shahada ya kwanza (Bachelor Degree) yafanywe kupitia kwenye Mfumo wa Pamoja wa Udahili (CAS).
Amefafanua kwamba. Baraza linautangazia umma kuwa, kuanzia mwaka wa masomo 2016/2017 udahili wa kozi zote nchini utafanywa kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS) unaosimamiwa na NACTE, Vyuo Vikuu na taasisi za Elimu zote nchini Tanzania zinazotoa mafunzo ya Cheti na Diploma kutodahili wanafunzi nje ya mfumo wa udahili wa Pamoja kuanzia mwaka wa masomo 2016/17.
“Tunapenda kutoa taarifa pia kuwa, maombi ya kujiunga na kozi za Cheti na Diploma yataanza kupokelewa rasmi kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja kuanzia tarehe 4 Machi 2016, saa sita mchana. Baraza pia litaanza kupokea rasmi maombi ya kujiunga na kozi za Shahada (Degree) kwa wahitimu wenye Diploma kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja kuanzia tarehe 4 Machi 2016, saa sita mchana,”
Kwa maelezo zaidi ya jinsi ya kuomba mafunzo kwa kutumia Mfumo wa Pamoja wa Udahili (CAS), alisema Baraza linashauri waombaji watembelee tovuti ya Baraza ambayo ni www.nacte.go.tz
TANGAZO MUHIMU KUTOKA NACTE: WAJULISHE WOTE
TANGAZO MUHIMU TOKA NACTE: KUFUNGULIWA KWA MFUMO WA PAMOJA WA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI
(NACTE)
TAARIFA KWA UMMA
KUFUNGULIWA KWA MFUMO WA PAMOJA WA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), linapenda kuutangazia Umma na wadau wote wa Elimu nchini, kuwa mfumo wa Udahili wa pamoja yani Online Central Admission System (CAS), umefunguliwa rasmi tarehe 4 Machi, 2016, saa 6 mchana, kwa kupokea maombi kwa mwaombaji katika kozi mbalimbali, ikiwemo ngazi ya,Astashahada, Stashahada na Shahada kwa mwaka wa masomo 2016/17. Mfumo utajumuisha kozi zifuatazo;
1. Astashahada na Stashahada
2. Shahada za Elimu ya Juu
Mwombaji wa Astashahada na Stashahada anaweza kuomba kwa ajili ya eneo moja au zaidi katika maeneo ya taaluma yafuatayo;
1. Biashara na Utalii, mfano; Uhasibu, Meneja rasilimali watu, Wanyama pori, Mipango.
2. Sayansi shirikishi, mfano; Kilimo, Uhandisi, Mifumo ya mawasiliano, Usanifu majengo, Mifugo.
3. Afya, mfano; Uganga, Maabara, Ufamasia, Uuguzi
Ada ya maombi ni kama ifuatavyo;
1. Kwa eneo la Afya ada ya maombi ni Tshs 30,000/=.
2. Kwa eneo moja kati ya maeneo mengine yaliyobaki, ada ni Tshs 20,000/=
3. Kwa zaidi ya eneo moja la taaluma, mfano; Afya pamoja na Ualimu, ada ni Tshs 30,000/=, muombaji anaruhusiwa kuchagua maeneo yote.
4. Kwa waombaji wa Shahada za Elimu ya juu, ada ya maombi ni Tshs 50,000/=
Mwisho wa kutuma maombi haya ni tarehe 31/05/2016.
Imetolewa na:
Baraza la Taifa la Elimu yaUfundi
4 Machi, 2016
Chanzo: MaswaYetuBlog