Naam, mambo yakizidi bubu huzungumza!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Mambo yakizidi bubu huzungumza!

Juvenalis Ngowi
Tanzania Daima

NATIMIZA sehemu ya wajibu wangu kwa kuanza kumwomba Mola wangu aniongoze na kuniangaza kwa namna ya pekee ninapowakilisha wazo langu jepesi kwa wasomaji wa safu hii.
Yeye ndiye mweza wa yote na haishangazi tunamuita Mwenyezi, Muweza. Huyu ndiye aonaye hadi kwenye uvungu wa mtima wa mtu na hata vilivyofichwa na kufunikwa chini ya busati, yeye anaviona.

Juma hili nimeshangazwa na habari kuhusu rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa. Wengine humuita Mzee wa Utandawazi. Huyu si tu alikuwa mwanafunzi wa darasani wa Mwalimu Nyerere, lakini alikuwa chaguo na kipenzi chake wakati akigombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995.

Mkapa ninayemfahamu ni bingwa wa takwimu, ni mtaalamu wa kufikisha ujumbe aliokusudia. Anafahamu kuchagua maneno atakayotumia na sikushangaa nilipoambiwa kitaaluma rais huyu mstaafu ni mwanahabari.

Sifa zake hazifanani hata chembe na habari ninayoizungumzia. Kwamba alikataa kujitetea au walau kutoa maoni yake kuhusu shutuma na tuhuma zilizoelekezwa kwake.

Kukataa peke yake kusingenishangaza. Ila inapodaiwa eti alikataa kwa kuwa amestaafu siasa, nashindwa kuelewa. Ubongo unakataa kuikubali sababu hiyo.

Angekataa kwa sababu ana hiari ya kujitetea au kukaa kimya hilo ni jambo jingine.

Kwamba ameona tuhuma hizo hazina uzito wa kujibiwa, ingeweza ikawa sababu. Lakini hii ya kusema amestaafu siasa si sababu ya kufanya wapembuzi yakinifu wafunge mdomo.

Mosi, tuhuma zilizotolewa sio za kisiasa. Kwa rais mstaafu huyu ziliwahi kuelekezwa tuhuma nyingi. Walianza waliomtuhumu kufanya biashara akiwa katika ofisi kuu nchini. Wakahoji hakukuwepo mgongano wa masiahi? Wengine wakaanza kuyakumbuka maneno ya Mwalimu kwamba Ikulu ni mahali patakatifu. Rais mstaafu akakaa kimya kabisa. Rais aliye madarakani naye akawaasa wanaochokonoa mambo hayo wamwache mzee wetu apumzike. Asiulizwe swali. Na imeshasemwa wazi kwamba hatachunguzwa.

Baada ya hapo zikashuka shutuma nyingine zinazoenezwa na kambi ya upinzani kuhusu rais huyu mstaafu na wenzake kadhaa. Hapa wengine walijitokeza kujibu tuhuma.

Wengine wakajiapiza kwenda kujisafisha mahakamani. Wengine wamebaki kimya.

Nisingetegemea kwamba rais mstaafu naye angejitokeza aseme anakwenda kujisafisha mahakamani. Lakini pia sikutegemea aseme anabaki kimya kwa kuwa amestaafu siasa.

Tuhuma zilizotolewa si siasa. Ni tuhuma zinazogusa uchumi wa nchi. Nituhumu zinazogusa watu walio katika nafasi ya utendaji.

Hata kama zinatolewa katika majukwaa ya kisiasa na wanasiasa bado zinabaki ni tuhuma zinazohoji uadilifu wa mtu au watu.

Hiyo si siasa hata kidogo. Tuhuma za kufanya biashara akiwa katika ofisi takatifu si siasa.

Ni hoja ya kuangalia kama kuna msuguano wa masilahi ya nchi kwa upande mmoja na ya mtu au watu binafsi kwa upande mwingine. Ni hoja ya kuangalia kama sheria, taratibu, desturi, mazoea na kanuni za maadili zimekiukwa au vinginevyo. Hiyo si siasa.

Lakini hata ingekuwa siasa, haina maana kwamba baada ya kustaafu hapaswi kuwajibika kwa matendo yake. Inawezekana vitabu vya sheria vimemzungushia wigo wa kutowajibika kwa aliyoyafanya akiwa mamlakani, bado kuna uhalali wa kimaadili utaendelea kudai majibu sahihi kwa kila kilichofanyika. Kustaafu hakufuti rekodi iliyoandikwa nyuma. Kustaafu hakufanyi kiu ya maswali iliyoibuka izimwe.

Kustaafu hakufuti makosa wala hakubadilishi haki ya kujua kama yote yako vema.

Lakini kiu ya mwanadamu ya kujua ni kubwa na kwa kawaida uvumilivu una kikomo ndio maana waswahili wakawa na msemo wao kwamba bubu akizidiwa husema.

Watanzania waliofahamika kuwa watulivu na tusiopenda kuchokonoa mambo hasa ya “wakubwa”, wamebadilika. Hii ni dalili kwamba bubu anakaribia kusema. Idadi ya mambo yanayohojiwa inaongezeka. Idadi ya tuhuma bado ni ndefu kwa watu mbalimbali.

Watu wameanza kutumia njia za mitandao kusambaza habari mbalimbali. Tumesikia wananchi wakiwazomea viongozi wa juu wa serikali katika matukio kadhaa. Huku ndiko kusema kwa bubu.

Tumeona maandamano japo madogo ya wafanyakzi wakidai nyongeza ya mishahara.

Tumeshuhudia watu wengi wakipinga uamuzi wa Bunge kumsimamisha Zitto Kabwe. Bubu wamefikia mahali sasa wanaanza kusema. Nani alijua jambo kama la Zitto lingeweza kubadili hali ya siasa za nchi hii?

Ikiwa mambo kama haya yanatokea halafu wananchi wanajibiwa kwamba “nimestaafu”, tujue bado tunapalilia tatizo.

Tumesoma kwenye vyombo vya habari kuhusu madai ya Butiku.

Ingawa madai hayo ni ya kisiasa, ni muhimu yapatiwe pia majibu kama kuna nia ya kweli ya kukinusuru Chama Cha Mapinduzi, lakini na taifa pia kwa ujumla. Ni vyema mtu ajue kama kinachosemwa ni kweli au uongo. Kama ni kweli tujue kama ni sahihi au la. Kukaa kimya ni kuacha ombwe ambalo hakuna hakika litajazwa na nini.

Hapo ndipo tatizo lililopo, maana chochote kinaweza kutokea kulijaza.

Lakini hoja nyingine pia ni ikiwa wananchi hawana haki ya kujua mambo yanayowahusu kwa sababu mhusika amestaafu siasa.

Kimsingi wananchi ndio waajiri wa rais. Kutoka kwake madarakani hakupaswi kuzuia waajiri wake wasihoji namna alivyofanya kazi waliyompa. Kama alifanya vyema sawa.

Ikiwa alifanya vibaya anapaswa kuwajibika hata kama si kisheria basi walau kimaadili. Shutuma zinaporoshwa kutoka upande mmoja, wadau wote wana haki ya kufahamu ukweli au uongo wa shutuma hizo.

Anayeshutumiwa ana nafasi nzuri zaidi ya kutoa maelezo ya upande wake kabla hatujajumlisha moja na moja kupata mbili.

Kustaafu siasa bado hakuondoi haja hii ya msingi ya kutaka kujua kama rais mstaafu aliyatumia vyema madaraka yake au la.

Lakini kwa anayepima joto la uelewa wa wananchi kwa sasa atajua kwamba kinachoendelea sasa si siasa.

Wananchi wameambiwa kuhusu maisha bora. Wamepigiwa magitaa kwamba Tanzania yenye neema iko njiani. Lakini wakati huohuo zinasambaa habari kwamba tunapoteza fedha nyingi au rasilimali nyingi kwa njia isiyo halali.

Wananchi wanaanza kuelemewa na maneno yenye matumaini ambayo hata hivyo sasa yanaanza kubadilika. Bubu anaanza kuzidiwa na taratibu anaanza kusema!

Mtu mweledi hupambanua mambo. Tanzania ina watu wengi wa jinsi hii. Wana macho wanaona. Wana akili wanatafakari. Wanaweza kutambua alama za nyakati. Hivyo wanapouliza hawafanyi dhihaka. Rasilimali za taifa si suala la siasa. Ole wetu kama uchumi tumeufanya kuwa hoja ya kisiasa. Kama ni hivyo, Tanzania yenye neema na maisha bora kwa wote. Wakati bubu wanataka kusema, wakubwa wanasema wao wamestaafu!



Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0784 265 072 au barua pepe: kevinmakyao@hotmail.com
 
Mkapa bado mwanasiasa, ajibu tuhuma

Ndimara Tegambwage
Tanzania Daima

SITAKI Benjamin William Mkapa, yule rais mstaafu, aseme asiulizwe juu ya lolote linalohusu utawala wake kwa madai kwamba amestaafu.

Sitaki aseme kwamba hataki vyombo vya habari na wadadisi wamjadili au wamfuate, au wafuatilie yale aliyotenda akiwa madarakani.

Hii ni kwa sababu Mkapa hajastaafu siasa na hawezi kustaafu siasa. Kwa mujibu wa katiba na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkapa bado ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Ni Halmashauri Kuu ya chama hicho inayotunga na kusimamia sera zinazotawala hivi sasa. Akiwa mjumbe, bado ni mwanasiasa wa nafasi ya juu.

Hatua ya rais aliyestaafu kuendelea kuwa mjumbe wa vikao vya juu vya chama chake ambacho bado kinaendelea kushika utawala, ina maana kwamba bado anaheshimika na kuthaminiwa.

Ina maana ubongo wake bado unahitajika katika kukuza, kulinda na kuimarisha utawala wa chama hicho; uwe mzuri au mbaya.

Ina maana Mkapa bado ni tegemeo, kwa kiasi kikubwa, la chama chake katika kurithisha fikra, kuzalisha mpya na kuandaa viongozi wapya wa kukiendesha chama hicho.

Si hayo tu. Aliyofanya Mkapa ndiyo nguzo ya yanayofanyika leo, ndani ya chama chake na ndani ya serikali. Hii ina maana kwamba kuna mwendelezo wa aliyofanya; naye anaendelea kuyanawirisha kwa njia ya ujumbe katika vyombo vya chama kilichoko ikulu.

Hapa Mkapa hawezi kusema wala kusemewa kwamba amestaafu siasa. Ndiyo hasa anaanza siasa; na mara hii akiwa na mali na muda zaidi wa kukisaidia chama chake.

Wanaomfuata Mkapa, kwa maswali au kwa hoja, hawajakosea. Akiwajibu kuwa amestaafu siasa, tutamtilia shaka kama kweli akili yake ingali sawa baada ya kustaafu urais na uenyekiti. Tutasema kapungukiwa.

Wakitokea wanaomsemea kuwa amestaafu siasa kwa hiyo aachwe kudadisiwa, hao tutasema ama hawajui watendacho au wametumwa kufanya bwabwaja na wanalipwa kwa kupiga kelele; lakini wanadharauliwa na anayewatuma kwani yeye anajua ni wajinga tu.

Hii ni kwa kuwa Mkapa bado ni mwanasiasa. Na katika siku chache zijazo anaweza kuteuliwa kubeba sh 6.5 bilioni za "kiongozi bora wa Afrika" kwa mujibu wa watoa nishani ya Mo Ibrahim.

Hiyo ni tuzo ya kisiasa. Naye Mkapa, pamoja na kushutumiwa kwa muda mrefu sasa, kwa kukiuka maadili ya utawala akiwa ikulu na kuwekwa orodha ya "mafisadi," amekaa kimya ili kauli zake zisisikike na kurekodiwa na labda kuathiri nafasi yake katika kuwania tuzo hiyo.

Mkapa anaendesha Mfuko wa Mkapa wa kupambana na ukimwi . Viongozi wa Tanzania wanajua vema kwamba walisukumwa na nchi wafadhili kuingiza ukimwi katika ajenda za taifa na hiyo ikawa ajenda ya kisiasa kwa kila jukwaa.

Anachofanya katika taasisi yake ni mwendelezo wa jukwaa la kisiasa na utekelezaji wa azima ya kisiasa ambayo Rais Jakaya Kikwete anaendeleza pia kwa kuhimiza upimaji wa afya.

Mkapa angali anapata marupurupu yake ya kisiasa hadi mwisho wa uhai wake. Juu ya hayo, imetungwa sheria ya kumlinda rais mstaafu na hata kuzuia asikejeliwe. Ni siasa tupu. Ni siasa hadi kifo.

Hata bila kutaja siasa, Mkapa ni "mtu wa umma." Nafasi aliyofikia; ile ya mwenyekiti wa taifa na rais wa nchi, inamweka jukwaani kwa kila mmoja kumjadili, kumdadisi na kumchunguza kama kweli alistahili au alibambikwa tu.

Lakini hapa kuna sababu nyingine ya kumfuata Mkapa. Ametoka ofisini. Wengine wameingia. Sasa sharti wadadisi wajue ameacha nini pale, kwa njia ya tabia na mwenendo wa kisiasa na mfumo wa utawala.

Mkapa alifanya biashara akiwa ikulu kwa kutumia muda wa wananchi. Mkapa alihudumiwa na vyombo vya fedha na vingine bila shaka kwa kasi ya "wanaohudumia rais" na siyo mteja wa kawaida. Rais alijua na alinyamazia ufisadi uliotendwa chini ya utawala wake.

Mkapa ni mtuhumiwa mbele ya mahakama ya wananchi kupitia njia mbalimbali za kumwasilishia mashitaka; kwa mfano vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.

Hivi majuzi, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amemtuhumu Mkapa kwa kubinafsisha CCM kwa matajiri, kushindwa kuongoza chama hicho na kubadili kanuni zake bila kufuata taratibu.

Yote haya ni kutaka Mkapa aseme. Ajibu. Ili Watanzania waanze kujiweka tayari kukabili utawala ulioingia ikulu na kuzuia usifanye vituko, vitimbi na ufisadi; mambo ambayo yanaongeza mzigo kwa wananchi na hata kuchafua roho zao.

Kimya cha Mkapa, siyo tu kinaonyesha jeuri na ubabe, bali kinadhihirisha amekabidhi yaleyale yanayolalamikiwa kwa wale waliochukua nafasi yake.

Kama hivyo ndivyo, basi huo ni msiba mkubwa. Kama sivyo, wananchi wanatarajia hata Rais Kikwete ashirikiane nao kudai majibu kutoka kwa Mkapa juu ya tuhuma zinazomwandama.

Kama alivyo Ali Hassan Mwinyi, Mkapa bado ni mwanasiasa. Mema na mabaya yake bado yanamfuata hata nje ya ofisi. Asipotaka kujibu tuhuma atahukumiwa kama anavyoonekana. Na hivyo ndivyo alivyo.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614672; barua pepe: ndimara@yahoo.com; blogu: www.ndimara.blogspot.com
 
Lbda tafsiri ya kustaafu ni kuacha kuwa rais ila kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM hiyo siyo kazi ya siasa.

Hapa Mkapa anatuonyesha kitu kipya kuwa wale wanaoingia kamati kuu na halimashauri kuu z\a ccm kumbe kule hawaendi kufanya siasa ila ni wastaafu wa kisiasa.

Nakosa kupata tafsiri sahihi ya maneno yake kuwa amestaafu siasa...

Wenye ubongo mpana jaribuni kutafuta maana ya haya maneno siyo mepesi kama watu wanavyotaka kuamini kuwa ndivyo yalivyo, unastaafu siasa ile hali wewe ni mjumbe wa kamati kuuu? ama kweli huu ni msemo wenye maana pana zaidi.
 
Hii ni Tanzania ndugu yangu hataacha kushangaa hapa bongoland!

Kuna mtu alishauri kutangaze maovu kwenye vyombo vya habari za nje. Labda inaweza kusaidia.
 
BUBU kazungumza , ila tatizo kakuta anayezungumza naye ni kiziwi hapo matokeo yanakuwaje?
 
Nadhani angekuwa Uingereza au Marekani angesema amestaafu kutoka kwenye "active politics", lakini bongo anawadharau watu anaona kuwa ni wavivu wa kufikiri
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom