Na Vijana CCM Nao Ni Wazee! ( Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Na Vijana CCM Nao Ni Wazee! ( Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Mar 31, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Mar 31, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa, (


  "HAYO malumbano ni ya kwao, sisi hatuyajui, wala hatutaki kuyajua. Tunashughulika na kutekeleza Ilani tu… maneno maneno kama hayo hayatuhusu”, anasema John Chiligati, Katibu Mwenezi wa CCM.


  Simba anapozeeka na kukaribia kufa huanza kupoteza uwezo wa kuona, kunusa na hata kusikia. Lakini, kuna moja ambalo simba ana hakika nalo, kuwa ameacha simba watoto. Kizazi cha simba kitaendelea.


  Chiligati anasema hayajui yanayotokea ndani ya UVCCM na malumbano yanayoendelea. Hapa kuna mawili; kama ni kweli hayajui ni tatizo, na kama anayajua na kuamua kutingisha mabega na kujifanya hayaoni wala kuyasikia ni tatizo kubwa zaidi. Kwa vile, Umoja wa Vijana wa Chama ni moja ya viungo muhimu kwenye mwili wa chama.


  Maana, katika maisha haya ya kisiasa, vijana ndio nguzo na uhai wa chama chochote kiwacho. Inakuwaje basi, chama kinachozeeka kinapozungukwa na ’vijana wazee’? Uhai wa chama hicho utakuwa hatarini.


  Si na juzi hapa, vijana wa CCM walikutana kule Dodoma. Tunaambiwa kuwa vijana wamewasha moto ndani ya chama chao. Nilijua, kuwa kwenye ukumbi ule wa White House walipokutana vijana wa CCM alikuwamo Mzee Kingunge Ngombale- Mwiru.


  Ukimwondoa Mwalimu , nikiri, kuwa Mzee Kingunge ni mmoja wa Watanzania walionifanya niipende siasa na aliyechangia tangu utotoni mwangu, katika kujenga misingi yangu ya kiitikadi kwenye Ujamaa na Kujitegemea. Hakika, Kingunge Ngombale- Mwiru ni hazina ya kiitikadi, si tu kwa CCM, bali kwa Taifa.


  Naam. Mkutano ule wa vijana ulipokwisha kule Dodoma nikamwuliza mjumbe mmoja aliyekuwamo mkutanoni; ” E bwana we, nimesikia Mzee Kingunge mmechagua kuwa Kamanda wenu wa vijana Kitaifa, amesemaje kwenye hotuba yake ya shukrani?


  Nikaambiwa, ilianzia kwenye salamu. Kingunge aliposalimia; ”Kidumu Chama Cha Mapinduzi!” akaitikiwa; ” Kidumu Chama Tawala! ” Ikasikika ’ ajua’, kutoka kwa Mzee Kingunge. Akaawambia; mmekosea kwenye kuitikia salamu. Hamtakiwi kujibu ”Kidumu Chama Tawala!” Jibuni “Kidumu!”


  Maana, kwa mujibu wa maelezo ya Mzee Kingunge, CCM haiwezi kuwa chama tawala siku zote. Na kuna maeneo ya nchi hii kwa sasa ambapo CCM si chama tawala. Akawauliza vijana wale; “ Sasa ina maana mkifika huko mtaacha kujibu salamu ya Kidumu Chama Cha Mapinduzi!?


  Mpaka hapo Kingunge amedhihirisha jambo moja muhimu, kuwa umri uko wa namna mbili. Kuna umri wa miaka na umri wa kifikra. Ndiyo, kuna wanaozeeka kifikra hata kama bado ni vijana. Na kuna wazee ambao kifikra bado ni vijana sana pamoja na umri wao mkubwa. Kingunge katika hilo alionekana kuwa kijana zaidi. Ameonyesha kwenda na wakati kuliko vijana wale.


  Na nikaambiwa, kuna mahali mjumbe mmoja mkutanoni alitoa hoja ya umri wa mwana-CCM kuhesabiwa kuwa kijana uongezwe. Katika kujadili lile, Mzee Kingunge akasema, ”Hakuna tatizo katika mtu kuleta hoja yake, lakini kuhusu hili la mipaka ya umri wa kijana muangalie hata katika nchi nyingine wenzenu wanafanyaje.” Mzee Kingunge akawa ameua hoja ile ya kijinga kwa kutumia busara zaidi.


  Na hili la vijana wa vyama na umri linahitaji makala yake, inakuja. Haiwezekani katika dunia hii ya sasa mtu mwenye miaka 40 na zaidi bado anang’ang’ania ndani ya jumuiya ya vijana ya chama chake.
  Mtu mzima huyo anafanya nini ndani ya jumuiya ya vijana?


  Hebu fikiri, hivi leo kijana wa miaka 20 akiwa mtundu anaweza kupata mtoto wake wa kwanza, na mtoto wa kijana huyo akiwa mtundu, naye anaweza kupata mtoto wake wa kwanza akiwa na miaka 20. Sasa basi, hapo mzazi mwenye miaka 40 atakuwa na mjukuu, ataitwa babu.


  Yumkini, kwenye jumuiya zetu hizi za vyama kukawa na wanaoitwa babu. Ndiyo, wana wajukuu. Hawa walistahili kuwa kwenye Jumuiya za Wazazi au Wanawake za vyama vyao. Nimeahidi, kuwa hili la vijana na umri nitaliandiakia makala yake.


  Turudi kwenye mkutano ule wa vijana wa CCM. Nimeambiwa, kuwa Mzee Makamba aliwekwa kiti moto. Kuna waliomshutumu kuwa kachangia CCM kupoteza majimbo. Niseme, kuwa Mzee Makamba wanamwonea bure. Alipaswa kupongezwa badala ya kukaangwa.


  Hivi nani katika CCM hiyo asiyejua kuwa karibu wajumbe wote wa Sektretariati ya chama hicho walikuwa majimboni kupigania ubunge. Pale Lumumba alibaki Makamba. Labda Makamba hakuona jimbo la kwenda kupigania, ndilo kosa lake? Makamba ni kama ’fan-belt’- mkanda wa pangaboi kwenye injini ya gari yenye matatizo. Injini ya CCM ina matatizo. Na hayakuanza Awamu hii ya Kikwete.


  Malumbano haya na mlolongo huu wa matamko ya vijana wa CCM kila Mkoa hayatakisaidia chama chao kwa sasa. Bila kufahamu, vijana wa CCM, badala ya kumsaidia Mwenyekiti wao, wanamdhoofisha katika kutekeleza majukumu yake ya kichama na Kiserikali, tena kwa kasi. Na tatizo nilimeshalisema, kuwa vijana nao ni ’ wazee’.


  Kuna wanaojipanga kwa 2015. Kuna wanaojipanga kuwania U-NEC mwakani. Kuna wanaovizia U-DC na vyeo vingine. Vijana- Wazee wa sasa wamekaa kimaslahi zaidi, si ya chama, bali ya kimakundi na zaidi yao binafsi.


  Kikwete anasemwa kuwa mpweke kisiasa, tumeanza kuelewa. Uchaguzi uliopita ukawa mtihani mgumu kwa Kikwete na chama chake. Na katika vita ya uchaguzi wa kisiasa Sektariati ya chama ndiyo ’ War Room’- Chumba cha Vita.  Unafanyaje wakati Mwenyekiti wa chama yuko vitani anapigania Urais na wajumbe wa Sekretariati ya chama nao wanapigania majimbo yao? CCM wana bahati. Idadi ya majimbo waliyopoteza ingekuwa kubwa zaidi kama wapinzani wao wangejipanga vema.


  Na siasa ni mchezo wa makosa, si wa bahati. Ndiyo, ni kama kandanda. Wanaokosea ni wale wasemao; ’ Footbal is a game of chance’- Kwamba kandanda ni mchezo wa bahati. Hapana, kandanda ni mchezo wa makosa. Ushindi unapatikana kutokana na makosa ya timu pinzani. Yaweza kuwa makosa ya kimkakati au ya mchezaji mmoja mmoja.


  Kuna kosa CCM wamelifanya na wanaendelea kulifanya; CCM imeanza kupoteza sifa muhimu ya mwanasiasa na chama cha siasa. Kuwa karibu, kuyasikiliza, kuyaelewa na kuyafanyia kazi matatizo ya watu wa kawaida walio wengi.


  Na kuna wakati Benjamin Mkapa aliwaambia wazi wana CCM wenzake kule Dodoma, kuwa kihistoria, TANU na CCM imekuwa kimbilio la wanyonge. Mkapa akabainisha, kuwa CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara. Hili ni kosa la kisiasa.


  Yaweza kuwa kazi bure kwa CCM kuwaparamia CHADEMA. Hakuna anayewasomba wananchi kwa malori kwenda kwenye maandamano na mikutano ya CHADEMA. Mpinzani mkubwa wa CCM kwa sasa ni wananchi, umma. CCM ijitathimini, basi.


  Na nilipata kuandika, kuwa kama Chama Cha Mapinduzi kina nia ya kupunguza kupotea kwa imani ya umma kwa chama hicho, basi, kutahitajika, si tu kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya muundo wa Serikali na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi, bali kufanyika kwa mabadiliko makubwa yenye kishindo.


  Kuna watakaopuuza, lakini, kuna ukweli, kuwa tuhuma za ufisadi zimekipaka na zinaendelea kukipaka matope mno CCM. Kwenye macho ya umma, chama hicho kimechafuliwa na tuhuma hizo za ufisadi. Kuna wana CCM leo wanajiuliza kama wavae sare za chama au la wapitapo mitaani. Maana, kuna Watanzania walioanza kuchukia rangi za chama hicho. Wanazihusisha na ufisadi.


  Na matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana yawe ni fundisho kwa chama tawala. Kama CCM inataka kubaki kwenye mioyo ya Watanzania wengi, kuwa na uhalali wa kubaki madarakani, basi, ina lazima ya kujipambanua kwa vitendo kutoka kwenye yote makubwa yenye kuhusiana na ufisadi na maovu mengine. Ibaki kuwa kimbilio la wanyonge. Isifike mahali, chama kikajikuta katikati ya mgogoro na umma. Hilo laweza kuharakisha mazishi ya chama yasiyo na kisomo.  MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
   
Loading...